Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii uliyonipa sasa kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Naomba radhi leo sauti yangu imekuwa ya mahaba zaidi, kwa hivyo mtanistahimili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa roho safi na kwa sauti kubwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi anavyosimamia kazi yake ya kuiongoza nchi yetu, mpaka hapa tulipo tunaenda vizuri. Mheshimiwa Dkt. Samia anaweza, tena anaweza sana na tungependa kusema asijali, madebe matupu hayaachi kutika, ndiyo dunia, lakini yeye anawaka na anaweza vizuri, na Mungu atamsimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu za pili naomba ziende tena kwa Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kuchagua hii timu ambayo Mheshimiwa Waziri Hussein Mohamed Bashe, Naibu Waziri Mheshimiwa David Silinde na Katibu Mkuu Mweli na timu nzima. Hii timu ni kabambe na safi kwa mapambano, nafikiri itaipeleka nchi yetu tunakokufikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia ameweza kututoa kule tulikokuwa, na sasa kuna ongozeko la bajeti kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021 kufikia shilingi trilioni 1.248 mwaka 2024/2025. Nani kama Mama Samia? Hii ni bajeti kubwa kwa kilimo kwa kujua kwamba bila mapinduzi ya kijani, hatuwezi kufika popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ya mauzo nje yameongezeka kutoka dola milioni 1.2, trilioni 2.5, mpaka dola bilioni 2.3 sawasawa na fedha za Tanzania shilingi trilioni sita. Vilevile mapato yanayotokana na mazao ya malighafi ya kilimo yamefikia shilingi za Tanzania trilioni sita. Hii ni kazi kubwa sana iliyofanyika kwa umahiri wa Mheshimiwa Waziri wetu. Vijana hawa ambao nami pia nina mkono, kwa sababu Mheshimiwa Hussein Bashe nimemlea, Mheshimiwa David Silinde nimemlea na kama mtu anapinga apinge hapa mbele ya Bunge hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nataka kuzungumza kuhusu mbegu asilia. Nashukuru sana Wizara kwa jitihada inazochukua kwa uhifadhi na utafiti wa mbegu hizi. Bajeti hii kwa kweli pia imetenga fedha za kuimarisha jengo la uhifadhi wa mbegu. Sasa Wizara isaidie kuharakisha mchakato wa kupitia sera ya mbegu ili kuwezesha hizi mbegu kutambulika kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Wizara kutenga bajeti kwa wakati ili kusimamia mbegu za wakulima pamoja na utafiti, hasa kwa vile ukitilia maanani kwamba mbegu hizi zinapotea kwa kasi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu za asili ni urithi wetu wa asili, kwa hiyo, lazima tuhakikishe zinaendelea kuweko na kustawi. Pengine zitakapokua vizuri zaidi na sisi tutauza huko na zitatuongezea kupata fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ninalotaka kuzungumzia ni kilimo ikolojia hai. Nawapongeza sana Wizara kwa ushirikiano na asasi zisizo za Serikali kwa kuhakikisha kwamba tumekuwa wa kwanza katika Afrika Mashariki na Afrika chini ya Sahara, kuwa na Mkakati wa Kilimo Ikolojia Hai. Naomba tufahamu kwamba mfumo wa kilimo duniani umeanza kuelekea kwenye kilimo ikolojia hai. Tujue hata hao Ujerumani, ndiyo kwanza wamepitisha mkakati sambamba na sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapongeza juhudi zinazoendelea kwa ushirikiano kuhakikisha kwamba kilimo hiki kinaeleweka na mpango kazi mkakati unaendelea kufanyiwa kazi. Tunategemea katika bajeti hii kutatengwa pesa kwa ajili ya utekelezaji kwenye maeneo ya uhamasishaji, (sensitisation) hasa kwa sisi Waheshimiwa Wabunge kufahamu zaidi nini kilimo ikolojia hai ili tuweze kufanya maamuzi kwa namna gani mtu atumie kilimo kipi, kwa sababu tumeona pia katika kilimo hiki tunaweza kutumia samadi zetu wenyewe. Kwa hiyo, zitapunguza gharama ya kununua mbolea, au kupigania mbolea au kuomba mbolea iuzwe robo, kilo au nusu kilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakuwa tunakwenda zaidi kwenye mfumo ule ambao pia kwa mazao hayo imefahamika duniani kwamba yanapata soko zaidi. Tunaomba Wizara pia katika kupitia bajeti hii, itoe ruzuku kwa sababu wako vijana ambao wamejitolea kutengeneza viuatilifu kwa kutumia hayo hayo mambo ya kilimo hai. Kwa hiyo, Wizara iwaone na kuwapa support vijana hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nataka kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Hussein Mohamed Bashe kwa jinsi alivyosimamia hizi Bodi za Mazao. Napongeza kwa sababu bodi hizi zimeweza kufanya kazi kwa manufaa ya wakulima. Kwa mfano, bei ya cocoa imeweza kufika kutoka kilo 3,000 mpaka kilo 34,000 katika soko la dunia. Huu ni msingi mkubwa, kwa hiyo tukikazania hizi bodi hata kwenye mazao mengine, basi wakulima wetu wataendelea kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kama kuna mtu anabisha hapa kama kilimo siyo muhimu kwa sababu naamini wote hapa tunakula ndiyo maana tuko hivi. Bila kula huwezi. Kwa hiyo, kilimo ni uti wa mgongo kama alivyosema. Kwa hiyo, kila namna tutakayoweza nchi hii tujitahidi kilimo chetu kiwe mbele tuweze kupata mazao zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naweza kushauri Serikali iweze kushirikiana, yaani Wizara hii ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Viwanda na Biashara kuongeza thamani katika mazao. Kwa mfano, kuna watengenezaji wa chocolate kule Kyela wanaita Mababu Chocolate wamejiongeza na wanauza chocolate zinauzwa dunia nzima. Kwa hiyo, tunaweza kupata zaidi. Wizara hizi zishirikiane ili kuwapa wananchi wale ambao wanajitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nataka kuzungumzia hii dhahabu ya kijani (parachichi) ambayo kwa kweli sometimes imeshatokea habari kwamba parachichi zinarudishwa kwani zimeonekana zina viuatilifu sumu. Kwa hiyo, tuwe makini zaidi. Vilevile kama tungeweza kutenga eneo maalum kama vile Njombe, tukasema huku tutalima parachichi za kilimo ikolojia hai ili kuepusha na kukuza thamani kwa sababu parachichi zinahitajika sana na parachichi zetu zina thamani kubwa. Kwa hiyo, naomba ushauri huo utiliwe maanani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hayo, mimi naridhika kabisa na utendaji wa Waheshimiwa Mawaziri hawa. Nasema tu tuendelee kuwapa ushirikiano na nchi yetu itapanda kutokana na kwamba tumeweza kuongezewa bajeti kubwa kama hii. Kwa hiyo, mwakani tutapata zaidi ya hapo. Wote nataka mniombee dua nirudi tena humu Bungeni mie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuwasilisha. (Makofi)