Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara ambayo kama nyingine ni catalyst, basi hii ndiyo msingi na ndiyo mustakabali. Kwa sababu ukiangalia katika nchi zinazoendelea au nchi kama za kwetu, kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo kinaajiri watu wengi na kilimo ndiyo kinagusa. Ukiweza kuchechemua na kukuza kilimo kama inavyostahili, utakuwa umegusa watu wengi tofauti na Wizara nyingine pengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize ni kwa kiwango gani tumeweza kulima? Ni kwa kiwango gani tumeweza kusimamia dira, dhima, mienendo na matarajio? Mheshimiwa Bashe ameeleza vizuri sana, napitia dira yake amesema, “Tujilishe sisi na tuwalishe wengine” ambayo ndiyo Dira ya Wizara. Nataka kumwuliza ni kwa kiwango gani tumejilisha sisi na tumewalisha wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu ziko wazi, ameeleza kwamba kilimo kimeongezeka. Hizo ni takwimu ambazo zipo ambazo kilimo kimetoka 3.3% kwa mwaka 2020, kuja 4.2. mwaka 2022. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika uchangiaji wa Pato la Taifa tunaona kwamba kuna slight change kutoka 26.2% kuja 26.5%, lakini pia na ajira na vitu kadha wa kadha pamoja na namna ambavyo kimekua au fedha zinavyoongezeka katika kuuza nje: Sasa swali, je, tumefika tulikotaka kwenda? Tumefika kwa kasi tunayoenda nayo? Kuna kitu hakiko sawa? Ni wapi tunapaswa kuongeza nguvu? Haya ni maswali ambayo nayauliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, amesema tumeongeza kilimo, leo tumezalisha kutoka tani 17,000 kuja zaidi ya tani 20,000, mkaonyesha kwamba ongezeko ni slight change, lakini katika hilo ongezeko ni asilimia ngapi? Akaeleza kwamba ni asilimia mia moja na nimeandika hapa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kwa takwimu ambapo asilimia inayoongezeka unaona kwamba haijawa tofauti sana na mwaka 2023 ambayo ilikuwa ni 114%. Leo tunaenda asilimia kama 120% ambayo unaona kwamba siyo ongezeko kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi concern yangu imekuwa tusiishi kwa kula tu, kwamba mmesema tunazalisha kwa ajili ya kulisha nchi tu, lakini surplus ikiwa ni tani 4,000,000 na kadhaa, unaona kwamba ni kiwango kidogo sana kutoka tani 16,390 mwaka 2023/2024 na ziada ya tani 4,000,000 na kuendelea. Takwimu zinaeleza kwenye hotuba yake, lakini unaona kwamba ni mchango mdogo sana ambao unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huo mchango mdogo, ni juhudi gani zimejitokeza? Nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeona akieleza matarajio ambayo amekuwa nayo, ni matarajio makubwa tu ya kuongeza kilimo, akieleza kwamba kipaumbele chake cha kwanza ni kuongeza productivity.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia wakaonyesha productivity imekuwa ni ndogo kwa miaka iliyopita na hasa ukilinganisha tunavyozalisha na tunavyovuna ni vitu viwili tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona kwamba nguvu kubwa wakulima wanaitumia kwenye kuzalisha, wanaitumia kwenye kulima eneo kubwa, lakini output yake inakuwa ndogo. Nimechukua mifano hapa kadha wa kadha, na mfano mdogo katika mpunga, katika ekari moja tulikuwa tunapata tani 1.25, lakini kumbe estimate tungeweza kupata tani nne na hapo hatujafika. Ukiangalia korosho ambayo sasa katika ekari moja unapata tani 0.5, lakini matarajio ni kwamba tunaweza kupata katika ekari moja zaidi ya tani mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, kahawa katika ekari moja leo tunachokipata ni 0.3 wakati unaweza kupata mpaka 1.5 per acre. Unaona kwamba nguvu bado ipo, lakini sasa ni kwa nini hatuwezi kuzalisha vya kutosha? Jitihada zinaonyesha zitapatikana kwenye mbegu kwamba tukipata mbegu bora tunaweza kuzalisha kwa ubora, lakini sasa unaona mbegu bora bado zinazalishwa kidogo. Ameonyesha kwamba, sasa mbegu ambazo leo zinapatikana ni tani zaidi ya 68,000 lakini estimate tunapaswa kupata tani zaidi ya 127,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua shida yetu ni nini? Ni kwa nini hatuzalishi zaidi? Tunaweza kuwa tunalima eneo kubwa, lakini kama tuna mbegu ambazo hazina tija, matokeo yake yanakuwa ni madogo. Kwa hiyo, sasa tunajua tukiwekeza zaidi kwenye kuzalisha mbegu zilizo bora, hata output itakuwa ni kubwa. Kwa hiyo, kile ambacho mnalenga kukifanya kitakuwa kimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini wakati mwingine vipaumbele havikamiliki? Ni kwa sababu wakati mwingine bajeti inayokuwa imetengwa haiendi. Sasa ukiangalia bajeti, tukija kwenye ku-scrutinise bajeti, tunaona imeenda kwa 53% point something takribani 54%. Tumekuja hapa tukapanga kwamba mnapeleka zaidi ya shilingi bilioni 900 na kadhaa lakini zilizoenda hazijatimia. Unaona bajeti ya maendeleo, bajeti ya matumizi (OC) bado ni hela ambazo haziendi kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama bajeti haitoshi, tunategemea output au productivity, au mazao yenye kuwa na tija! Bila shaka hatuwezi kupata kwa wakati. Moja kati ya kipaumbele kingine, mkasema ni ajira zenye staha. Ameeleza vizuri Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza sasa hivi. Kusema ukweli jembe la mkono siyo ajira yenye staha. Jembe la mkono ni ajira inayomtesa mkulima, anatumia muda mwingi, nguvu nyingi, kazi nyingi, akili nyingi lakini productivity na anapata nini kwa kweli hairidhishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahitaji kuweka hela ya kutosha, tunahitaji kuweka nguvu ya kutosha ili kuona tunapata hiyo output pamoja na kuimarisha upatikanaji wa masoko. Hili hususan niliongelee mfano kwenye suala la kilimo cha vanilla. Wakazi wa Mkoa wa Kagera waliingia kwenye kilimo cha vanilla kwa nguvu kubwa sana, lakini wameishia kutapeliwa na bado matumaini hayakuwepo ya kutosha ya kuhakikisha tunapata soko la vanilla yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii naomba wakati wa kumalizia Mheshimiwa Waziri atoe kauli, ni nini hatima ya wakulima wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanapata soko la hilo zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuongelee Mkoa wa Kagera na mikoa mingine ya pembezoni, walianzisha masoko ya kimkakati na hapa nataka Mheshimiwa Waziri aeleze, nami nitashikia shilingi. Nini hatma ya masoko ya Murongo, Tarime na Mutukula pamoja na maeneo mengine ambako kuna fedha ya Serikali. Fedha iliwekwa na masoko yametelekezwa. Nitashika shilingi hususan kujua hatima ya masoko hayo ambayo yangeweza kuchechemua upatikanaji wa masoko ambayo leo ndiyo tunayaongelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulima ni kazi ya wakulima, lakini upatikanaji wa masoko sasa ni kazi ya Serikali kwa sababu ninyi mna network, mna uwezo, mnaweza kuwasaidia wakulima kufikia hiyo azma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuimarisha matumizi ya TEHAMA. Ni kwa kiwango gani wananchi wanaweza kupata taarifa ya soko? Ni kwa kiwango gani wananchi wanaweza kuuza kutoka kwenye maeneo yaliyopo na pia kulima kidigitali? Tumeona juhudi kadha wa kadha ambayo ni pamoja na kuboresha mbegu na Maafisa Ugani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wameeleza hapa, nami nataka niliongelee kuhusu uhaba wa Maafisa Ugani. Unawezaje kuboresha kilimo bila kuwa na watu on the ground ambao wanaweza kusimamia kuhakikisha wakulima wanazalisha na kupata tija tunayoitaka? Wameeleza kwamba upungufu ni zaidi ya 30% na zaidi, upatikanaji wake ni 35%. Unaweza uka-equate ukajua upungufu ni kiasi gani. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini bado tuna kazi kubwa hasa post-harvest loss, mazao mengi yanapotea wakati wa kuvuna. Pia kutenga 10% ya National Budget kwenda kwenye kilimo. Hiyo ndiyo Maputo Protocol walivyoongelea. Ni kwa kiwango gani tunaenda kufikia hapo? (Makofi)