Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii muhimu na ya kihistoria ya shilingi trilioni 1.2. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uzima, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Taifa letu na miradi kedekede aliyotuletea ndani ya Jimbo la Hai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kweli nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Bashe, kwa kweli kiti kimepata mwenyewe kwa namna ambavyo anakimbizana na miradi na kwa namna ambavyo anasimamia sekta hii pamoja na wasaidizi wake, Mheshimiwa Naibu Waziri, kule kwetu tunamwita Mzee wa Makeresho, sasa amalize na lile Bwawa la Makeresho ili kazi iende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia kaka yangu Naibu Katibu Mkuu, ndugu yangu Gerald kwa kazi kubwa anayoifanya. Nimpongeze pia Mkurugenzi wa Umwagiliaji, ndugu yangu Ray kwa kazi nzuri pia anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza tangu nimekuwa Mbunge leo ndiyo namsikia Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Taifa, kwa kazi aliyoifanya, nitaeleza baadaye. Kwa mara ya kwanza nilikataa humu humu kwamba sitampongeza mpaka atakapokuwa amemaliza matatizo ya ushirika. Sasa kwa kuwa ameanza kazi hiyo vizuri na yeye nampongeza pamoja na watumishi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sababu ya kuipongeza taasisi hii na wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Mwaka jana walinipa miradi mingi sana Mheshimiwa Waziri kule Hai na watu wa Hai wakashukuru sana, lakini bado haijakamilika na haijakamilika kwa sababu pia hawajaletewa fedha. Fedha walizoombwa zimekuja kwa 53%, sasa hizo nyingine ziko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu Mheshimiwa Waziri, miradi ile ime-troam, walitwambia inafanyiwa feasibility nimeiona. Bwawa la Borutu nimeliona hapa, Makeresho nimeona, Kikafu chini angalau wameitangaza jana, nampongeza sana na namshukuru sana kwenye hili. Mwera na Kalali wameyatangaza. Bwawa la Bwana Mganga bado, Bwawa la Mtambo kule kwenye Skimu ya Mtambo wameitangaza, nawashukuru sana; Ismaili bado hawajatangaza, lakini ilikuwa kwenye bajeti na Longoi Mapacha bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara aliyoniahidi mwaka jana ya kutoka Kwa Sadala kwenda Longoi ambayo inakuja kwenye Soko la kwa Sadala na ikizingatiwa Soko la kwa Sadala tayari Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameshatupatia shilingi bilioni 11.2. Sasa nimshauri Mheshimiwa hii miradi viporo aitangaze, nitamsaidia kwenda kudai. Mimi nakodisha tu mabasi matatu ya hao wananchi wa Hai, tunakwenda pale Hazina tunaimba nyimbo za ukombozi na Mheshimiwa Mwigulu atatoka tu ili atupe hizi fedha. Kwa hiyo yeye atangaze, asiogope, kazi ya kwenda kuzidai nitamsaidia, kwa sababu yeye jukumu lake ameshalifanya? Asipoitangaza hii miradi maana yake hana justification ya kuidai. Yeye atangaze halafu aone namna nitakavyomsaidia kwenda kuidai hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nimshukuru sana kwa jambo la kihistoria ambalo amelifanya kuhusiana na mradi wetu wa lile Soko la Mula. Sasa na hili lisiwe tena akaweka huku likavuka mwaka, hili likiwezekana tukishapitisha bajeti yake hapa, na tunapitisha hii bajeti; atangaze kujenga hili soko la kisasa, namna ya kudai nitamsaidia, nitamsaidia vizuri kwenda kudai kule Hazina, tutakwenda kushinda pale siku tatu tunaimba nyimbo za ukombozi mpaka watoe hela. Kwa hiyo nimtie moyo na nimwombe aendelee kufanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nililosema hapa ni kuhusu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania. Nimepiga kelele sana na ushirika na lengo nililokuwa nataka twende kwenye ushirika ni hapa tulipofika. Leo Wilaya ya Hai na nachukua nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Ushirika wa Wilaya ya Hai pamoja na Afisa Ushirika wa Mkoa wetu, hongereni sana, wamenielewa Mheshimiwa Waziri. Kwa mara ya kwanza tumesaini mkataba hadharani tena umeandikwa kwa Kiswahili. Tukachukua ule mkataba tukawapa vijana wetu walioko Dar es Salaam, tukawapa wananchi na ukatangazwa kwa uwazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaenda kufanya ziara na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Taifa kwenye chama kimoja baada ya kingine na mwisho tukaenda kusaini mkataba mchana kweupe, vyombo vya habari vikiwepo, wananchi wakiwepo. Hiki ndicho tunakitaka siyo ile biashara eti Mrajisi wa Ushirika anakwenda peke yake na watu wake wawili kusaini mikataba ya hovyo. Sasa niombe, najua shamba la Silver Bay mkataba unakaribia kwisha, najua kule Makoa bado, najua na maeneo mengine yanakuja, utaratibu uwe ni huo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mashamba ni ya kwetu watushirikishe. Ndugu yangu amesema hapa kwamba sheria inatubana, sheria inasema tusiwaingilie, lakini tusinyimwe haki yetu sisi kama viongozi kujua. Nashukuru sana Wilaya ya Hai sasa hivi Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji wanakwenda kwenye vikao. Huo ndio ushirika tunaoutaka, wa uwazi na ukweli ili turudi kule tulipotoka ambapo ushirika uliweza kusomesha watoto wetu, ushirika ukajenga Chuo cha Ushirika Moshi, ushirika ukajenga barabara ya kwenda Kyalia kwa lami na kwamba fedha ya ushirika ndiyo imetunyanyua sisi. Kwa hiyo tunapolilia ushirika watuelewe na lengo letu lilikuwa ni hapo. Hongera sana kwa Mrajisi wa Ushirika kwa kazi kubwa aliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kushauri kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri amefanya kazi nzuri sana, kwenye indicator zote za kupima performance amevuka. Nilikuwa naangalia upatikanaji wa chakula, nimeona amevuka, ameweza, chakula kwa ajili ya kula kipo, sasa aanze kuwaza kuhusu chakula kwa ajili ya biashara. Tutoke huko sasa tuanze kufanya biashara ya kilimo ya uhakika na siyo hii tunayoifanya. Kwenye hili anaweza kutengeneza zones, kwamba kama ukanda huu wanakuwa ni wataalam wa kulima zao fulani awape indicator za performance watu wake, awape vigezo, bwana wewe kwenye wilaya fulani, Wilaya ya Hai wewe ni mtaalam wa mbogamboga, wewe ni mtaalam wa kilimo cha kahawa, tunataka tani kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mkuu wa wilaya akimegemewa kipande chake na kwa bahati nzuri wako hapa, na Mkuu wangu wa Wilaya Amiri Mkalipa yuko hapa na sisi Hai tupe. Malengo yawe kwamba nenda kazalishe kwa tani kadhaa, mambo ya umwagiliaji, hili eneo hili la umwagiliaji lilipo hapa la hekta 727,000 ni ndogo sana kwake. Amekwishapewa mashine za kuchimba visima huko, akipambana kwenye hili tukawa na eneo lote la umwagaliaji ambalo limepata maji, ana uwezo wa kuwaambia wataalam walioko kule kwamba nendeni mkatuzalishie. Kama ni mahindi kwa tani kadhaa, kama ni maharage tani kadhaa ili tuwe na chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, precautions mwaka jana hapa nililizungumzia tena eneo hili. Hivi wanaposema kwamba tuna chakula tani kadhaa huwa wanaweka na chakula cha mifugo? Kwa sababu leo Mheshimiwa Waziri wanapozalisha wanasema wana mahindi yanayotosheleza mahitaji ya chakula, lakini hawaweki kwamba mahindi hayo hayo ndiyo yanayokwenda kutumika kutengeneza chakula cha kuku, ndiyo yanayotumika chakula cha mifugo. Sasa lazima waweke wakijua kabisa mahitaji halisi ya Watanzania ni yapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa haraka haraka kwa sababu kengele imegonga, naomba sana habari ya mbolea tafadhali ije kwa wakati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Saashisha, naomba uhitimishe…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: …pamoja na mbegu, nimeona wameweka hapa, watusaidie, kwenye hizi mbegu kuna mbegu nyingine feki, zimeanza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, mengine nitaandika kwa maandishi, nitawasilisha na ahsante sana. (Makofi)