Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nianze kwa kuunga mkono bajeti hii nzuri sana na ya kihistoria katika nchi yetu. Nitachangia kwenye maeneo matatu, eneo la ushirika, eneo la soko la mazao na eneo la ongezeko la bajeti yetu ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini wa ushirika. Nchi yetu hii imepitia katika historia ndefu sana kuhusiana na suala hili la ushirika. Kuna mahali ushirika ulifanya vizuri sana, lakini kuna mahali ushirika ulipoteana kweli kweli. Leo hii nafurahi kwa uwepo wa Waziri, Mheshimiwa Bashe angalau sasa kama nchi, wote kwa pamoja tunazungumza vizuri kuhusu ushirika. Nakumbuka wakati tunaanza Bunge hili baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa hawataki kusikia kuhusu suala la ushirika, lakini leo hii wote tunakwenda kwa pamoja kuhusiana na suala la ushirika. Niseme kiukweli kabisa upele umepata mkunaji na mkunaji mwenyewe ni Mheshimiwa Bashe. Hapa niungane na usemi ule wa Kiswahili wanasema mzigo mzito mkabidhi nani? Mnyamwezi, yule pale. Amekabidhiwa mzigo na ameufanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna hii Tume yetu ya Maendeleo ya Ushirika na jukumu mojawapo la hii Wizara ya Kilimo ni kusimamia maendeleo ya ushirika. Sasa katika utaratibu wa uratibu na utekelezaji wa ushirika hivi karibuni pametokea na maelekezo kwamba hawa wana ushirika wajibu wao ni moja kwa moja kwenye Tume ya Ushirika. Ni jambo zuri japo kwa mtazamo wangu tulikuwa na Sera hii ya Ugatuaji, kwamba haya mambo sasa yafanyike kule chini. Sasa unaposema watu hawa wa ushirika wajibu wao uwe moja kwa moja kwenye Tume naona unaenda tofauti na suala hili la ugatuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye ushirika, kwenye kilimo tuna Maafisa Kilimo Wilayani, tuna Mkurugenzi pale Wilayani lakini tuna Wakuu wa Wilaya kule wilayani. Kwa bahati mbaya sana kupitia hili neno la kusema huyu afisa ushirika wajibu wake uko moja kwa moja kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, wako baadhi ya hawa maafisa ushirika hawatoi heshima, wanatoa kiburi na maneno ya dharau kwa hizi taasisi ambazo ziko pale chini zinazosimamia kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako maafisa ushirika wanasema mimi siwajibiki kwa mkurugenzi, ataniambia nini? Mimi siwajibiki kwa mkuu wa wilaya, Mbunge ataniambia nini? Maneno haya si mazuri na kama kweli na sidhani kama ni nia ya Wizara ya Kilimo kuwafanya hawa maafisa ushirika kuongea lugha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeona kuna marekebisho ya sheria. Kama eneo mojawapo tunapaswa kuliangalia ni eneo la lugha hizi, lugha hizi zinawapa jeuri hawa maafisa ushirika, hawana nia nzuri ilhali ushirika unakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie kwamba ushirika ndiyo fimbo ya mnyonge, ushirika ndiyo fimbo ya sisi wanyonge, hivyo tuunganishe nguvu ili twende mbele, lakini tukiuharibu kwa maneno ya hawa maafisa ushirika hatimaye tutapoteana na hatutaona tija kwenye ushirika. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Bashe, hizi lugha zinakwaza wale ambao tumewapa jukumu la kusimamia hiki kilimo kule chini. Huwezi kuniambia mimi siwajibiki kwa mkuu wa wilaya, sasa unawajibika kwa nani? Huwezi kuniambia mimi siwajibiki kwa mkurugenzi na nikwambie kwenye maeneo mengine wana nguvu kweli kweli hawa maafisa ushirika, wana nguvu kweli kweli kiasi cha kumfanya mkurugenzi asifanye chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri atoe maelekezo, ikionekana kwenye sheria kuna namna yoyote basi waje na kanuni ili hawa watu wawajibike. Mbona tuna TARURA pale ambao wana heshima nzuri sana kwa mkuu wa wilaya pamoja na halmashauri na wengine ambao wamegatuliwa haya madaraka na wanafanya vizuri? Kwa nini maafisa ushirika waoneshe kiburi cha namna hiyo? Hilo lilikuwa eneo mojawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo soko. Nimeona jitihada nzuri ya wizara kama jukumu lao la kuratibu na kutafuta masoko wanalifanya vizuri. Sasa iko shida na hofu kwenye baadhi ya mazao likiwemo zao hili la mahindi. Sisi wakulima wa Mbinga tumelima vizuri sana, tumelima vizuri mwaka jana, tumelima vizuri mwaka juzi na tumelima vizuri mwaka huu. Tuishukuru Serikali kwa miaka hii miwili nyuma mazao yetu yaliuzika vizuri sana, lakini hivi ninavyoongea bado wakulima wana mazao ya mwaka jana, hayajamalizika kuuzwa; lakini bado mazao ya mwaka huu yameshakomaa na baadhi ya wakulima wameanza kuvuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo iko hofu, kwamba masoko ya nje ya nchi yetu yamezuiwa. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aondoe hii hofu kwa wakulima, kwamba ni kweli yamezuiwa? Kwa nini mazao haya hayauziki? Nimeambiwa sijui kuna procedure, procedure nyingi. Kwa hiyo niombe, kama ni kweli shida ni procedures, basi tuziondoe hizo procedures au tuzirahisishe ili mkulima huyu aliyelima apate tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa kwamba, wakulima wetu hawa wanakimbilia kulima mazao wakiona yananunulika, yasiponunulika hawalimi na wasipolima nchi yetu itaingia kwenye shida zaidi maana njaa itatupata. Niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa awaambie wakulima wa Mbinga kwamba hajazuia mpaka wowote. Wakulima hawa wawe huru kuuza mazao yao; eneo la pili hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo lingine ni kuhusu hili ongezeko la bajeti. Naishukuru sana Serikali kwa nia njema kabisa hii ya kuongeza bajeti. Tumeshuhudia hapa kwamba huu ni mwaka wa tatu mfululizo bajeti inaongezeka. Tulitoka kwenye bilioni 200 tukaja kwenye bilioni 900 na leo hii tupo kwenye trilioni 1.2. Hongera sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita, hongera sana kwa Mheshimiwa Rais kwa nia hii njema ya kumkomboa mkulima, lakini hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. Najua hizi fedha haziji hivi hivi, zinakuja baada ya yeye kuonyesha mipango ya namna gani anakwenda kuzitumia, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida hii taarifa inafurahisha sana kusikia kwamba bajeti imeongezeka, lakini inasikitisha kusikia fedha zilizoenda huko kwenye Wizara hadi leo tumeambiwa kuwa ni 53% tu, hii ndiyo ilikwenda Wizara ya Kilimo. Mimi ni shuhuda mzuri sana nimeona mipango mizuri ya Mheshimiwa Waziri hapa, ni mizuri mno, hata wenzangu wamesema. Tunampimaje Mheshimiwa Waziri ikiwa amekuja na mipango mizuri ya kuisaidia nchi hii, ikiwa amekuja na mipango mizuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, kwamba akitoe kilimo kutoka hatua tuliyokuwanayo kwenda hatua nzuri zaidi halafu fedha haiendi? Jambo hili siyo zuri, siyo zuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaitaka Serikali itoe fedha kwa namna tulivyopitisha hapa Bungeni. Haiwezekani mipango hii ikaenda kutekelezeka? Hapa ningeomba waziri anapokuja kuhitimisha aniambie Mradi wangu wa Umwagiliaji Litumbandyosi unakamilika lini? Nimepekua pekua hapa siuoni sasa sijui ndiyo huu umeondoshwa kwa sababu ya hii ya kibajeti ama la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Benaya, muda wako umekwisha.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)