Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku-declare interest, mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tunapomzungumzia mchimbaji mdogo haina tafsiri ya kuturudisha nyuma kwa mchimbaji aliyekuwa akitumia excel, akitumia Kinu na nyundo kuponda mawe. Bado mchimbaji mdogo anaweza akaja kwenye uchimbaji kwa kutumia crushers za sasa hivi akatumia tekonolojia ya sasa hivi. Kwa hiyo, tukimwongelea mchimbaji mdogo, naomba kwanza tupate sura hiyo, ili tupate picha ya huyu mchimbaji mdogo ni lazima awezeshwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchimbaji mdogo akiwezeshwa tutamtoa ambaye jabari analipasua pasua na kuligeuza unga kwa kutuma nyundo na nguvu zake „kwa kutumia muscles’ hao wengi kwa sasa hivi ninavyoongea na wengi walishapoteza maisha! Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri tuwaangalie hawa wachimbaji wadogo kwa maana ya kuwawezesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mpanda niwaelezeni tu, kuna maeneo ya Dirifu, Idindi, Katisunga, maeneo haya wanapatikana wachimbaji wadogo, lakini kuna leseni kubwa imewaatamia wachimbaji hawa! Nilichokuwa nakiomba kwake Mheshimiwa Waziri, kama alivyotenga katika maeneo mengine naomba na wachimbaji hawa wadogo wa eneo la Mpanda waweze kupatiwa leseni. Tukifanya hilo tutakuwa tumewasaidia watu hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye gari kuna kitu kinaitwa shock absober. Wachimbaji wadogo tukiwapatia maeneo nao ni shock absober ya namna yake katika kupunguza suala la ajira. Katika eneo moja unaweza ukakuta kuna wananchi zaidi ya 500, mchimbaji mmoja mdogo tunapopiga kelele ya kwamba tunataka tuwainue bodaboda, machinga, mchimbaji mmoja mdogo aliyewezeshwa vizuri ana uwezo wa yeye pia kumiliki bodaboda, naye anaisaidia Serikali hii kwenye kufanya shughuli nyingine za namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, system ilivyokuwa huko nyuma tulikuwa tukiona wachimbaji wadogo wanashindana kwenye kunywa na kufanya vitu vingine, sasa hivi wamebadilika. Wachimbaji wadogo hawa wamekuwa wakijenga majumba mazuri, wachimbaji wadogo hawa wamekuwa wakiwekeza hata kwenye kilimo! Kwa hiyo, tukiweza kuwa-support maana yake tuna-support na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimweleze Mheshimiwa Waziri, ni kweli ule Mji kwa mfano, ukienda Johansburg ule mji umejengwa kwa dhahabu ya pale. Kwa hiyo, tukiwawezesha watu hawa wataijenga Mwanza, wataijenga Chunya, wataijenga Mpanda, naliomba sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpanda ina shida nyingine ya umeme, tunazungumzia habari ya kupewa power plant, lakini eneo lile Mkandarasi ni mmoja ambaye tunaambiwa ana maeneo mengi ya kufanya kazi. Naomba namna yoyote ifanyike kuhakikisha eneo hilo linafanyiwa kazi mapema kwa sababu vinginevyo mji ule tutaendelea kupata umeme wa mgao.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru ndugu yangu mmoja, Mheshimiwa Ally Saleh, wakati akichangia aliongea kitu kimoja nilikipenda sana. Alisema, tunaweza tukafanya vizuri zaidi kwa sababu tuna utulivu wa kutosha, ile point niliisikia asubuhi aliongea hapa, nami niendelee kuamini kwa utulivu huu tulionao kama nchi, tuna nafasi kubwa ya kufanya mambo makubwa. Nimtie moyo tu Mheshimiwa Waziri kwamba sasa safari hiyo bado tunayo na ni nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye eneo la tanzanite; Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri, niseme kitu kimoja, tunaomba tujiulize, mtu mmoja aliniambia hivi; ukilifahamu swali ni sehemu ya kujibu mtihani. Kama hujajua swali linataka nini huo mtihani umefeli. Kwa nini tusijiulize hawa watu wanakwenda kuuza tanzanite nje kwa sababu gani, shida ni nini mpaka wakauze nje? Tukishajiuliza swali hilo tuna nafasi kubwa ya kurudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna siku nimekwenda South Africa, nakuta tanzanite, niliona tanzanite nikachekelea nikijua hapa naenda kusikiliza habari ya nchi yangu Tanzania, lakini wale watu katika kibao, anakwambia kutana na tanzanite ambayo Mama Afrika ameizawadia Afrika, haijatajwa Tanzania! Hivi tunafanyaje ku-promote mambo haya kwa sababu tunaweza tukawa tunalaumu tu tanzanite hazitoki, hazitoki! Je, eneo la promotion likoje? Pale South Africa mtu mwingine akifikiri tanzanite ni jina tu, lakini hajui kwamba kuna neno Tanzania pale. Tumefanyaje katika eneo hilo, naomba nalo hilo lizingatiwe sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuongelea suala la vinasaba, binafsi bila kushawishiwa na mtu yeyote, sababu za msingi zilizopelekea mpaka tukapata hii kitu, hizo hizo ziendelee kuimarishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.