Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kupata fursa hii na nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kabisa kwa Wizara hii, kwa kazi kubwa na nzuri ambazo wametufanyia Wanambarali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati jana kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe anasoma bajeti yake yenye kurasa 307, neno Mbarali limetamkwa mara 27. Ukiachilia miradi ambayo iko kwenye table zile mbalimbali. Hii ni namna gani inaonesha Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetutendea haki Wana-Mbarali. Ilikuwa ni kiu ya miaka mingi kwa Wanambarali, kuona Serikali yao inawasaidia kuhakikisha inatengeneza miundombinu ya umwagiliaji ili bonde hili sasa tuwe na kilimo kilicho na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiangalia mambo ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya kwa Wilaya yetu ya Mbarali kwenye Sekta hii ya Kilimo, Wanambarali tutaandika historia ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wino wa dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti inayoenda kuisha sisi Wana-Mbarali tumepata miradi nane ya umwagiliaji. Mheshimiwa Rais ametutengenezea miradi nane ya umwagiliaji ambayo mpaka sasa wakandarasi wako site, shilingi 98,200,000,000 zimeshuka pale Mbarali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini hivi ninavyozungumza mabwawa nane wanatafuta mkandarasi mshauri ili aende kuchimba Mbarali. Kubwa zaidi jana baada ya kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, wanakwenda kuongea na mwekezaji ili shamba moja la mwekezaji lirudi kwa wananchi, wakulima wadogo wa Mbarali ambao wamekuwa wakifanya kazi ya vibarua kwa muda mrefu, waende kupata maeneo ya kufanyia shughuli zao. Kwa kweli, tunayo haja ya kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu baada ya kukamilisha miradi hii, tunaamini kabisa Mbarali itakwenda kutulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi. Wana-Mbarali 90% ni wakulima, kikubwa tulichokuwa tunataka Wanambarali kuwa na kilimo chenye tija. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameonesha kuithamini na kuijali Mbarali kwa muda mfupi aliopokea kijiti. Leo kuna wazee wa Mbarali wamenipigia wanasema Dkt. Samia Suluhu Hassan, vahongije sana. Kwa lugha hii ya Kisangu tafsiri yake ni kwamba Wana-Mbarali tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Bashe na timu yake, Mheshimiwa Rais hakukosea kuiteua hiyo timu. Wanafanya kazi njema, wamekuwa wanakipenda kilimo na wanapenda wakulima wa Taifa hili, kwa kweli nawapongeza sana, wanafanya kazi njema sana. Kipekee nimpongeze kaka yangu Mndolwa amekuwa ni msaada mkubwa kwenye mambo ya umwagiliaji Mbarali, nimpongeze sana na tunaendelea kumpa ushirikiano wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kikubwa ninachoomba Mheshimiwa Bashe, pindi mazungumzo na mwekezaji yatakapokamilika, tunaomba mashamba haya yakagawiwe kwa walengwa, wakulima wadogo wa Mbarali, isitokee tena ma-giant wachache wakajimilikisha. Ili tija ile ambayo Mheshimiwa Rais anayo kwa wakulima wale wadogo ambao hawana uwezo wa kukodi mashamba, kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya vibarua, leo wakapate ardhi, wakafanye shughuli yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tunatambua kazi kubwa ambayo wanaendelea kufanya, ni muhimu sana kaka yangu afungamanishe sekta yake na sekta zingine ambazo zinaingiliana na wakulima. Kwa mfano, sasa hivi kilio kikubwa cha wakulima nchini ni ushuru, lazima awalinde wakulima hawa kwa wivu mkubwa, ashirikiane na TAMISEMI kutoa mwongozo wa namna ya upatikanaji wa ushuru kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano sasa hivi pale Mbarali, wakulima kilio chao simu zinazoingia sasa hivi ni mkulima anatoka shambani, kwenda kupeleka mazao yake nyumbani anatakiwa alipe ushuru. Hapo hapo akitoka nyumbani, anakwenda kulipa mashineni ushuru, akiwa anataka kuuza ushuru, hii ni kinyume na sheria iliyopo ya ushuru. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kwa sababu hata Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa ufafanuzi hapa Bungeni, lakini bado huko hali inaendelea kuwa mbaya. Kwa hiyo, nimwombe Waziri alichukue hili kwa uzito unaostahili kwa sababu wakulima wanatumia gharama kubwa, wakati wa ushuru tusiende tukawakata ushuru mara mbili mbili, siyo sawa na Mheshimiwa Rais alitamka anataka kodi ambayo itakuwa ya amani na ukweli ili tuendelee kubarikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine hata wakulima wa Mbarali wanakumbwa sana na mikopo ya kausha damu, tena kule kinachofanyika kwa sababu taratibu za kupata mikopo kwenye benki bado ni changamoto, mkulima mdogo hawezi kupata mkopo na akipata mkopo hauwezi kumtosheleza. Maximum heka moja ya mpunga mpaka imalize kila kitu, siyo chini ya milioni moja mpaka milioni moja na nusu. Leo hii mkulima mwenye heka tano hata akipewa milioni mbili haiwezi kumsaidia, Wanachofanya, wanakwenda kukopeshwa pesa ili wakivuna wapeleke mpunga, kitu ambacho kinawaua wakulima wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimwombe Waziri aendelee kuboresha maslahi ya upatikanaji wa fedha kwa wakulima, hasa wale ambao hawana dhamana. Benki hizi wakulima wanaoweza kupata mikopo ni wale ambao tayari wanazo dhamana na wana uwezo mkubwa kidogo, lakini kwa wakulima wadogo bado tuna changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, vilevile kwenye suala la kufungamanisha na maeneo mengine, sisi Mbarali kwa safari hii, mbolea zilifika lakini wakulima walipata shida sana kuzifikisha mashambani, barabara zetu za vijijini hazipitiki. Kwa hiyo, tunaomba wanapokuwa kwenye mipango lazima aangalie sekta nyingine ambazo zitachangamsha vilevile kilimo. Leo una mipango mizuri, Dkt. Samia, alikuwa na mpango mzuri sana mbolea zifike kwa gharama nafuu, lakini kutoa mbolea pale walipoziacha mpaka kufika huko mashambani ile nafuu ambayo Mheshimiwa Rais anaiweka inapoteza tija kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuombe ndani ya Serikali, Wizara na Wizara nyingine waone namna maeneo haya ambayo, kilimo kinaendelea waweze kuangalia vichocheo vyote na sekta zote ambazo tutaweza kumrahisishia huyu mkulima aweze kuwa na kilimo chenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimwombe Waziri kwamba, natambua pamoja na miradi inayoendelea, tuna miradi mingine na scheme nyingine kama 11 ambazo zipo kwenye Mpango wa Serikali. Tayari mshauri mkandarasi ndio wanamtafuta. Niombe sana zoezi hilo lifanyike haraka ili mwaka ujao wa fedha tuone miradi hii ikiwa kwenye bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, napenda nishukuru sana kwa kazi kubwa ambayo Wizara hii imeifanyia Mbarali na Wana-Mbarali tunashukuru sana, kwa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ametufanyia. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)