Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, napenda nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kusema machache kwenye bajeti yetu hii ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwanza ningependa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kutupa kheri na afya njema ya kuweza kuwatumikia Watanzania. Kipekee kuwatumikia Wanamasasi. Pia ningependa kuwashukuru sana ndugu zangu za Masasi kwa kuendelea kuniamini, kuniunga mkono, kushikamana na mimi kuhakikisha kwamba, tunaijenga Masasi mpya kulingana na kauli mbiu yetu.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Chama Cha Mapinduzi, kwa juhudi kubwa ambazo wanazifanya kuweza kushirikiana na mimi pale Masasi, kuijenga Masasi mpya na Wanamasasi wanaona. Tumekubaliana na Wanamasasi kwamba mwakani mimi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tuna jambo letu, kwa hiyo wanatuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, ningependa kuchangia sasa kwenye Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Kwanza kwenye bajeti hii, tunaona ni bajeti ambayo inajielekeza kwenye kutatua changamoto ambazo tumekuwa sisi Wabunge tunazisema kila wakati. Kwa hiyo, napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Bashe na msaidizi wake Mheshimiwa Silinde, kwa kusikiliza hoja za Wabunge na hasa sisi Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na wenzetu wa Ruvuma, hasa kwenye maeneo yanayogusa tasnia ya korosho.

Mheshimiwa Spika, kwenye tasnia ya korosho tumekuwa tukisema siku zote hapa kwamba, bei ya mkulima anayopata kule wakati wa ununuzi siyo bei halisi, haiakisi bei halisi ya dunia. Bahati nzuri miaka 21 iliyopita wakati namaliza degree yangu ya pili (masters). Nilifanya utafiti wangu ulikuwa ni kwenye mapato ya mkulima wa korosho, kwa sababu natokea kwenye mikorosho nimezaliwa huko na mimi mwenyewe nalima pia na kwamba kuna changamoto mbalimbali ambazo Serikali ikizirekebisha, basi bei ya mkulima inapanda. Tunafahamu pia kitaalam mapato ya mkulima huwa tunasema ni mapato ya mara moja kwa mwaka. Wale ni fixed income earners (mara moja tu kwa mwaka), ni mtu ambaye unatakiwa kumwonea huruma.

Mheshimiwa Spika, ni sawasawa na sisi au watumishi wa umma, tungekuwa tunapewa mshahara mara moja tu, tarehe 1 Januari unapewa kwa ajili ya mwaka mzima, sijui kama tungeweza kuishi vizuri. Kwa hiyo, tuwaangalie wakulima kwa tafsiri hiyo hiyo ni watu ambao wanapokea pesa yao mara moja tu kwa mwaka. Hivyo basi, tunatakiwa tufanye juhudi zote zinazowezekana kuhakikisha kwamba, bei yao inakua na ikiwezekana iwasaidie kwenye kutatua changamoto za maisha yao.

Mheshimiwa Spika, hili nataka niliseme wazi kabisa, naunga mkono Hotuba yote ya Bajeti na hasa uamuzi wa Wizara ya Kilimo kuja na mfumo mpya wa uuzaji wa korosho na kuachana kabisa na mfumo wa zamani ambao ulikuwa unanufaisha wachache, wajanja na ambao hawahusiki kabisa na kilimo. Matumizi ya TMX ndiyo itakuwa suluhisho, tunaamnini itakuwa suluhisho hata kama itatokea changamoto kama Mheshimiwa Waziri alivyozungumza ni majaribio, lazima tujaribu. Naamini kabisa tukiitengeneza vizuri, tukatangeneza kupitia financial modeling namshauri Mheshimiwa Waziri kwa korosho pia na mazao mengine, ile bei elekezi tusiitaje kwa kuifikiria kukaa kichwani tu, tutumie module ya kiuchumi na kifedha tuweze ku-calculate kabisa gharama halisi za uandaaji wa shamba. Nafikiri Mheshimiwa Bahati amezungumza hapa kuhusu gharama za kuzalisha mpunga.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa opportunity cost, kwa yeye kuacha kutengeneza income sehemu nyingine ameenda kulima kule, pia lazima tumwekee kitu chake kama incentives. Pia kuna profit margin ambayo anatakiwa aipate yeye kama ilivyo kwenye biashara 15% au 20% ya bei, ile base price, pia tunataka huyu mkulima aweze kutanua uzalishaji wake whether vertically kwa kuongeza productivity au horizontally kwa kuongeza area of production.

Mheshimiwa Spika, lazima tuwe na future investment, tuifuate hii, kwenye gesi na maeneo mengine tunafanya hivyo, hata hizi computer tunaletewa huku, wanafanya hivyo hivyo kwenye pricing system yao. Mwisho risk profile, hawa wakulima wana-risks nyingi, risk ya kutokuvuna, hali ya hewa kubadilika, mavuno kuharibika njiani, unyaufu, kutolipwa kwa wakati, zote hizo unazi-compile unatengenezea sasa base price, ambayo tukiichukua ile tukaingiza kwenye TMX halafu tukashindanisha kwenye mnada, naamini kabisa wakulima wa korosho watapata fedha za kutosha na kupunguza umaskini kule nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka hata iliwahi kuzungumzwa mara nyingi tu na akiwemo aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati ule ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Makamu wa Rais. Alikuwa anahoji Mkoa wa Mtwara kwa mfano, unapata karibu bilioni 600 mpaka 750 za korosho kwa kila mwaka, lakini hali ya wananchi hatuioni? Ni kwa nini hatuoni mabadiliko makubwa kwa wananchi? Ni kwa sababu kuna watu hapo katikati ambao siyo wakulima, wamejitokeza wanapata 40% mpaka 65% ya bilioni 700 zote, ambao siyo watu wa Mtwara. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, sisi Wabunge wote wa Mkoa wa Mtwara, Lindi na Ruvuma ambao tunalima korosho tumekubaliana kwa dhati kwamba amejibu hoja zote za kila siku, twende kwenye TMX. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ningependa kumshauri Mheshimiwa Waziri kuhusu suala la value chain ya mazao ikiwemo korosho, tuliangalie holistically kutoka kwenye kulima, kuvuna, kusafirisha, kutunza (storage), kwenda kwenye processing ambayo ni ubanguaji na uongezaji wa thamani na mwisho kwenda kwenye soko. Humo kote kuna watu ambao kupitia hata BBT na programu nyingine wanatakiwa waingie humo katikati. Kila sehemu tuwe tunajua kwamba, ni watu gani tunahitaji waingie kwenye eneo gani ili tuchachue mnyororo mzima wa thamani na hatimaye kuongeza uwezo mkubwa wa wananchi wetu kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kumshauri Mheshimiwa Waziri, huu Mfumo mpya wa TMX lazima tuu-promote. Tengeneza trade mission, kwenda kwenye maeneo makuu ambayo yana wanunuzi wakubwa wa korosho, tuweze ku-introduce na kupata pre-contract agreements za commitment yao na namna gani tunaweza tukawasajili wakaingia kwenye mfumo wa ununuzi ili kuwe na buy in ili tuepuke jeopard ambayo inaweza ikatokea hapo katikati kutokana na mabadiliko ya mfumo.

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho ningependa kushauri ni elimu kwa Maafisa Ugani, kuna mmoja amezungumza hapa, Maafisa Ugani wengi wamesoma agronomy, sijui ni kawaida tu, wamesoma masomo more general. Ukimpeleka kwenye korosho hajui chochote ndio kwanza inabidi wewe mkulima uanze kumwambia. Kwa mfano, katika pembejeo za korosho viuatilifu hawajui kwamba, ni wakati gani sasa uweze kupulizia sumu inayoitwa sumu, halafu baada ya siku ngapi upulizie ile inayofuatia, halafu baada ya siku ngapi upulizie sulphur, au inaanza sulphur halafu inamalizia nyingine, hawajui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni vitu ambavyo tunatakiwa tuwatengeneze Maafisa Ugani wetu tuwa-customize ikiwezekana hizi TARI institutes zitumike tu-train wawe na specialization kwenye maeneo kama Mlingano Tanga, wawe na specialization ya mazao yanayopatikana kule. TARI Naliendele Mtwara, wawe na specialization ya kule, tuwa-train on the job training ili waweze kufanya kazi vizuri ya kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo ningetamani niliseme kwenye Wizara hii ya Kilimo, namna ambavyo Wizara ya Kilimo inaweza kuchachua viwanda, huwa kawaida viwanda ni zao la kilimo. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri ashirikiane na Waziri wa Uwekezaji, Waziri wa Viwanda na Biashara ili kuhakikisha kwamba Wizara ya Kilimo ina-feed kwenye viwanda vilivyopo tuongeze ajira na mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)