Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu, hoja ya Wizara ya Kilimo. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuongoza nchi yetu, lakini kwa fedha nyingi ambazo anazipeleka katika miradi ikiwemo Wilaya ya Kakonko. Ametuletea fedha nyingi kwenye miradi ya afya, elimu na hata kwenye kilimo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Bashe na wasaidizi wake ikiwemo pamoja na Katibu Mkuu na wataalam wote, wanafanya kazi nzuri, wameandika historia ya nchi hii kwenye Wizara ya Kilimo. Nawapongeza sana kwa kazi hiyo nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafahamu Watanzania kwa asilimia kubwa ni wakulima, lakini wananchi wetu wanategemea kilimo. Serikali imefanya kazi kubwa kuboresha kilimo kwa hatua ambayo tunapongeza, lakini yapo maeneo kadhaa ambayo yanahitaji kuangaliwa. Kwangu mimi, moja ni upatikanaji wa wataalam wa kilimo. Wataalam wa kilimo kwenye maeneo yetu hawatoshelezi, naomba sana wataalam waajiriwe na wapelekwe katika maeneo yetu na wakienda katika maeneo yetu ya kijijini ambako kilimo kinafanyika waende watoe elimu kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna uwezekano wataalam wakawepo, lakini hawafikishi elimu kwa wakulima, niombe wataalam waajiriwe, lakini waende kwa wananchi kutoa elimu juu ya kilimo bora ikiwa ni pamoja na wao wenyewe kuonesha mfano kwa kuwa na mashamba katika maeneo ya vijijini ili wananchi wetu waweze kujifunza kutoka kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utoshelevu wa pembejeo; kwangu kwenye utoshelevu wa pembejeo nitazungumzia mbegu ambazo wenzangu pia wamezungumza. Mbegu hazipatikani kwa wakati, mbegu hata zikipatikana hazitoshelezi, kwa nini? Kwa sababu uzalishaji wake ni mdogo sana na upatikanaji wake ni mdogo sana na hivyo hata bei inakuwa siyo rafiki. Niombe yaanzishwe mashamba ya kutosha ya kuzalisha mbegu kwa ajili ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwetu sisi Kakonko ardhi tunayo, Mheshimiwa Waziri aje Kakonko tutampatia ardhi kwa ajili ya kuweka mashamba ya kuzalisha mbegu katika mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, alizeti na kadhalika. Nina hakika kwetu Kakonko tukija kupata wataalam hawa, wakaja katika maeneo yetu ule uzalishaji wa mbegu kwa sababu mashamba yapo, wataalam wapo nina hakika yatatusaidia wananchi wetu kuweza kuboresha kilimo chao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri aliyoitoa, ukurasa 30 anasema kwamba hadi Aprili mwaka huu upatikanaji wa mbegu ulikuwa ni tani 68,474.67 ambayo ni sawa na 54%. Maana yake ni kwamba wananchi wa nchi hii, wakulima wa nchi hii wanazalisha au wanafanya kilimo chao wakiwa na mbegu kwa 46% tu, maana yake nusu ya mbegu inayohitajika nchini haipo. Kwa nafasi hii niwapongeze wakulima wa nchi hii ambao wanazalisha na kulisha nchi hii, lakini wakiwa na upungufu wa 46%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge wenzangu wamesifia Wizara kwa kupeleka mbolea katika maeneo yao. Kwetu sisi Kakonko ni tofauti, mbolea hatuipati kwa wakati, lakini hata ikipatikana inapatikana kwa kiwango kidogo sana na niombe, Mheshimiwa Waziri Bashe tulishaongea, shida tuliyonayo sisi hatuna wakala wa usambazaji wa mbolea katika Wilaya ya Kakonko. Anayetusaidia kusambaza mbolea katika Wilaya ya Kakonko ni yule anayetumika Wilaya ya Kibondo.
Mheshimiwa Spika, nitoe ombi maalumu, nafahamu zipo taratibu za kumpata huyo wakala ikiwa ni pamoja na uchumi wake, lakini kwa Wilaya yetu ya Kakonko fedha kwa wafanyabiashara wetu kuna uwezekano ikawa kidogo, kuna uwezekano wasiweze kufikia vile viwango vinavyotakiwa. Niombe Mheshimiwa Waziri aangalie na atupatie majibu atakapokuwa anatoa taarifa. Lini tutapata msambazaji wa mbolea katika Wilaya yetu ya Kakonko? Ili tuwe na uhakika wa kupata mbolea kwa wakati lakini kwa utoshelevu wake.
Mheshimiwa Spika, zao la muhogo; zao la muhogo ni zao ambalo ni la kutegemewa kwa biashara katika Wilaya yetu ya Kakonko, lakini na Mkoa wote wa Kigoma. Wilaya ya Kakonko tunategemea zao la muhogo kama zao la biashara. Muhogo kwa Wilaya ya Kibondo ni zao la biashara, hivyo hivyo Wilaya ya Kasulu, Buhigwe, Kigoma hadi Uvinza lakini zao hili halijaweza kupewa kipaumbele. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tuliangalie zao hili la muhogo kwa Mkoa wetu wa Kigoma kama zao pekee kwa ajili ya kuongeza uchumi wa wananchi wa Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo mambo kadhaa ambayo yanahitaji kufanyika katika eneo hilo. Zao hilo halina bei ya kutosheleza, zao hilo halina mbegu ya kutosheleza, kwa hiyo nashauri mambo yafuatayo:-
(i) Serikali ihakikishe zao la muhogo kutoka Mkoa wa Kigoma linapewa kipaumbele kwa kutafutiwa soko la ndani na nje ya nchi;
(ii) Kuendelea kufanya utafiti ili tuweze kupata mbegu bora ambazo zitaongeza uzalishaji kwa lengo la wananchi kuzalisha kwa kiwango kikubwa zaidi; na
(iii) Serikali itengeneze mazingira kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wafanyabiashara wa kati kuweza kuanzisha viwanda ambavyo vitaongeza uzalishaji, lakini kuongeza thamani ya zao hilo katika mkoa wetu na kwa nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ipo changamoto nyingine kwa upande wa kilimo, wakulima wanalima kwa uzoefu wa mazingira yao, udongo haupimwi. Niombe sana, imezungumzwa katika hotuba ziongezwe juhudi za ziada kuhakikisha kwamba udongo unapimwa. Mwaka jana mimi mwenyewe nilikuja hapa nikatoa taarifa kwamba nimetumia mbolea lakini haikutoa matunda kwenye eneo langu. Wataalam walivyokuja kupima kulinganisha mbolea niliyonunua na kutumia na udongo uliopo havikuwa sawa. Kwa hiyo maana yake nilitumia mbolea ambayo haifai kulingana na udongo ule, kwa nini? Udongo ule haukuwa umepimwa. Kwa hiyo niombe Wizara ichukue mawazo ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba udongo unapimwa ili wananchi wajue udongo uliopo katika shamba unafaa kwa mbegu ipi na unafaa kwa mbolea ipi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudie tena kuwapongeza Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwa nchi nzima ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Rais. Tunazidi sisi kuwapa moyo kuhakikisha kwamba wanafanya kazi, wanaongeza bidii katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)