Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja hii iliyopo mbele yetu ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo. Naungana pamoja na Wabunge wenzangu kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kuruhusu kuendelea kuweka fedha nyingi katika hii Wizara ya Kilimo akitambua kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kumpongaza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika hii sekta ya kilimo katika kuwasaidia Watanzania. Kama tunavyofahamu kwamba kilimo, kwanza kinachangia kwa nafasi kubwa katika uchumi wa nchi yetu, lakini kilimo vilevile kinachangia kwa nafasi kubwa katika ajira ya nchi yetu. Kwa hali hiyo tuna kila aina ya sababu ya kusaidia kilimo na ndiyo maana tunasema kilimo ndiyo uti wa mgongo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia leo kati ya changamoto kubwa tuliyonayo katika nchi hii ni changamoto ya ajira, yaani vijana wengi wanamaliza shule za msingi wanaingia kwenye soko la ajira, wanamaliza vyuo wanaingia kwenye soko la ajira, lakini kwa bahati mbaya sana kwa sababu ajira ni pungufu au ni chache wanahangaika katika namna ya kupata ajira. Hata leo unaangalia wapo vijana wengi wanaamua kutoka vijijini kuja mjini, hii si kwa sababu nyingine ni kwa sababu tu hatujawatengenezea mazingira hasa ya kilimo ya kuwawezesha waendelee kuishi kule vijijini.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme tu kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alionesha njia hasa kwa mwaka jana pale alipoanzisha ule Mpango wa BBT. Kusema ukweli mimi binafsi nilifarijika sana na niliona kwamba ule mpango ungeweza kusaidia ajira kubwa kwa vijana wetu, lakini ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu ile nguvu aliyoiweka mwaka jana aliyoanza nayo, kwa hali halisi siyo nguvu aliyoiweka mwaka huu. Naamini kwamba hilo limetokea kwa sababu ya changamoto alizokumbana nazo katika ule mpango mzima wa BBT.

Mheshimiwa Spika, nimpongezee tu kwamba walau alithubutu na anaendelea kupambana. Ni vizuri tukaona namna nzuri zaidi tunavyoweza kuiboresha ile BBT kwa sababu tukifanya hivyo itawezesha vijana wengi zaidi kujiajiri hasa katika hii Sekta ya Kilimo. Niseme, mwaka jana kati ya changamoto ambazo zilitokea ni kwa sababu vijana wengi walichukuliwa kwa njia ya kupitia mtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ulikuwa unamkuta kijana yupo Dar es Salaam aliona ombi aka-apply na akabahatika kupata nafasi, lakini hawakuwa wale walengwa halisi. Sasa kwa safari hii ambacho nimshauri Mheshimiwa Waziri kama kweli tunataka kupunguza tatizo la ajira na tunataka kuongeza tija ya kilimo hasa kwa hawa vijana wetu ambao wanamaliza vyuo, wanamaliza shule na hata wale wa darasa la saba ambao wanaingia mtaani kwa kuanza maisha, tuliboreshe kwa kuunganisha kilimo pamoja na watu wetu wa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa). Wakitangaza tu kwamba leo kuna nafasi ya kuchukua wale vijana wanaotaka kuingia JKT, yaani nafasi labda 50 za wilaya, vijana wanaoenda pale ni zaidi ya vijana 1,000 wanaenda pale wanajipanga, kwa sababu wanahangaika ili waweze kupata nafasi ile. Hiyo inaonesha kwamba ni kwa kiasi gani vijana wengi hawana ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nadhani Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kama tunataka kuwasaidia hebu aingie mkataba na wale JKT, wao wafanye kazi ya kuwatambua wale vijana, kuwaweka kambini, kuwatunza na kuwasaidia katika yale mafunzo yote ya kilimo. Yeye huku atoe mtaji baada ya kutoa mtaji na aone namna ya kuwawezesha mtaji pamoja na utaalam. Tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo, basi ni rahisi kuchuja wale vijana ambao wapo tayari kwa ajili ya kilimo, wakapata mafunzo ya ukakamavu, wakapata mafunzo ya kilimo na wakasimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo baada ya ile miaka miwili, mitatu naamini kwamba, watakuwa wamezalisha kiasi kikubwa na kutokea hapo sasa ni rahisi wakapewa mitaji. Kwa sababu mafunzo wameyapata sasa wakapewa mitaji, tena mitaji ile kwa kiasi kikubwa watakuwa wameizalisha wao wenyewe. Tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo sasa, kwa sababu mahitaji ya chakula ni makubwa, leo ukiangalia mfano zao kama la mpunga nchi zote zinazotuzunguka ukienda Kenya, Uganda, Rwanda na kila mahali mchele una soko kubwa; kwa sababu mabonde tunayo makubwa yanayoweza kusaidia hiki kilimo, basi inakuwa ni rahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, niseme yaani Mheshimiwa Waziri leo akija pale Mara, tukaenda tukazungumza na wale watu wa JKT Rwamkoma; kwa sababu mabonde yapo mengi kwa nini tusifanye pale tu-cite example, ambacho mimi naamini kwamba mfano ule lazima tu utafaulu na ukishafaulu, basi tuone namna ya ku-implement katika nchi nzima, kuliko hivi ambavyo tunawaacha vijana kila leo ukipita mpaka saa nane za usiku hawana kazi wanacheza pool. Ukipita vijana wanasema Mheshimiwa hatujaamka, Mheshimiwa hatuna ajira na wakati kuna mahali ambako tunaweza tukawaficha wale vijana tukawaweka na maisha yao yakaweza kuendelea. Kwa hiyo kama Serikali au Mheshimiwa Waziri atalichukua hilo wazo basi tunaweza kuona namna ya kuli-implement na likatusaidia kupunguza ajira kwa ajili ya vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, lipo hili suala la Ushirika. Tunatambua kwamba, ushirika una manufaa mengi na una faida nyingi, kwa sababu watu wengi leo hata pale anapolima, akitaka kwenda benki anajikuta hana dhamana ya kuwafanya waweze kupata mkopo. Kwa hiyo, watu wengi kila wanapojaribu kusimama hawawezi kusimama, si kwa sababu nyingine lakini ni kwa sababu hawana zile security za kuweza kupeleka benki kwa maana ya nyumba na security nyingine ili waweze kupewa mikopo, lakini kupitia ushirika maana yake ni kwamba, watu wengi itakuwa rahisi kupata mikopo na wakaendesha maisha.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika Ushirika wa Tanzania ule unaoendelea ni ule ushirika wa Vyama vya Wafanyakazi huo unaendelea. Huu ushirika mwingine kila unaposimama unaanguka. Sasa hili nataka tu kumwomba Mheshimiwa Waziri kwamba, wala tusiende mbali tuangalie tu kwa wenzetu wa Kenya hapa, ushirika karibu katika kila angle unakuta kama ni hawa watu wenye magari daladala, wapo katika ushirika wanaendelea vizuri, ukikuta watu wanauza maziwa, wapo katika ushirika, ushirika wao wa maziwa unaendelea vizuri. Ni vizuri na sisi hapa kwetu … (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Manyinyi, kengele ya pili ilishagonga.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika ni kengele ya kwanza, labda kama mmechanganya tu. (Kicheko)

SPIKA: Mbili zimeshagonga.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, basi nimalizie tu kwamba, nadhani kuna haja ya kuona namna ambavyo tunajifunza hata kutoka kwa wenzetu, halafu tukauleta huo ushirika na naamini kwamba, utawasaidia watu wetu na maisha yataendelea.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi/Kicheko)