Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nianze mchango kwa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe kwa kazi nzuri sana ambayo ameifanya. Mheshimiwa Bashe amewatendea haki wakulima wa nchi hii na kwa sasa kilimo siyo cha mazoea tena, ni kilimo biashara. Niendelee kumpongeza Naibu Waziri wa Kilimo, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara na Taasisi kwa kuleta mageuzi katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, nitachangia mambo yafuatayo nikianza na Tume ya Umwagiliaji. Napongeza kazi nzuri inayofanywa na Tume hii na ongezeko la bajeti.

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Iringa tunayo miradi ya umwagiliaji ambayo ni ya muda mrefu sana. Ushauri wangu, Tume sasa ifanye upembuzi yakinifu ili kuweza kukamilisha miradi ya muda mrefu kabla ya miradi mipya haijaanza ili pia kupunguza gharama, sababu miradi ikichukua muda mrefu gharama zinaongezeka. Pia kuna miradi ambayo haifanyiwi ukarabati na kusababisha miradi hiyo ianze kujengwa upya. Naomba kujua vigezo vinavyotumika katika hii miradi ya umwagiliaji kwa sababu kuna baadhi ya mikoa ina miradi mingi na mikoa mingine hakuna.

Mheshimiwa Spika, kuhusu zao la parachichi, naipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na mkakati maalum wa zao hili, tunaamini kuwa wananchi wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini tunakwenda kuwa dhahabu, naamini sasa mkakati uliowekwa kwa ajili ya kuondoa changamoto hizo itakwenda kuzimalizika kabisa hasa kuhusiana na miche bora ya ruzuku, masoko ya uhakika kwa wakulima hasa kwa maeneo yasiyo sehemu na ku-pack na kuhifadhi matunda haya ili kuyapeleka sokoni.

Mheshimiwa Spika, pia napongeza mpango mzuri unaofanywa na Serikali wa kuwa block farm kwa ajili ya kilimo cha parachichi, ni jambo jema japo lazima kuwepo na usimamizi na mpango mzuri wa uratibu kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, kuhusu zao la pareto, zao hili linalimwa na wakulima wa Nyanda za Juu Kusini ukiwemo Mkoa wa Iringa na kuna wakulima wanalima kilimo cha mkataba. Naomba kujua mkakati wa kusaidia Kiwanda cha Pareto kilichopo Mafinga Wilaya ya Mufindi ili kuweza kuchakata zao hili ili kuweza kuleta manufaa kuliko kusafirisha maua ya pareto.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya wakulima kutofikisha mazao sokoni kwa kipindi cha mvua ya masika; hii ni changamoto kubwa sana hasa kwa wakulima wetu wa Mkoa wa Iringa, sababu barabara nyingi zinazotoka mashambani ni za TARURA hazipitiki kabisa na wakulima wetu wanalima mazao ya mbogamboga na matunda kama nyanya, vitunguu, njegere, kabichi na kadhalika. Mazao haya yanaoza mashambani kwa sababu hakuna magari yanapita kwenda kuchukua bidhaa hizo, sasa nini mpango mkakati wa kuwasaidia wakulima hawa sababu wengi wao wamechukua mikopo benki? Wanateseka sana.

Mheshimiwa Spika, napongeza mpango mzuri wa kuwawezesha vijana na akinamama kwa Mradi wa BBT, ni mradi mzuri sana na utasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira kwa vijana wengi na akinamama nchini. Tunaomba ikiwezekana halmashauri zote wapatiwe mradi huu na pia kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwezekana mikopo ile inayotolewa na halmashauri ya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu iwe pia ya kilimo ili Wizara isaidie utaalam tu.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, nampongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia, mama yetu kipenzi kwa kuona umuhimu wa kuendelea kuongeza pesa kwa Wizara hii ili kuwatendea haki wakulima ambao ni zaidi ya 80%.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.