Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote katika Wizara hii, kwa kazi nzuri sana inayolenga kuleta mapinduzi ya kilimo nchini. Hongera sana wanastahili sifa.

Mheshimiwa Spika, wameweka nguvu nyingi sana kwenye kuboresha na kupanua kilimo cha umwagiliaji ili wakulima waweze kulima, kumwagilia na kuwawezesha kulima na kuvuna mwaka mzima. Natambua juhudi zinazolenga kuboresha kilimo cha kahawa nchini, hususan Mkoa wa Kagera. Mkoani Kagera kahawa ni biashara na ni siasa. Niwaombe ziwepo juhudi za makusudi ili bei ya kahawa iendelee kupanda ili mkulima aweze kunufaishwa na kilimo chake.

Mheshimiwa Spika, Mkoani Kagera kilimo cha vanila kilianza kwenye miaka ya 80 hivi. Viongozi wa mkoa walihamasisha na watu wengi wakaingia kwenye kilimo cha vanila. Wananchi wamekuwa wakinufaika na kilimo hiki, wamesomesha watoto, wamenunua pikipiki, wamejenga nyumba kutokana na mauzo ya vanila.

Mheshimiwa Spika, huko nyuma Shirika la Mayawa ndio waliendeleza hiki kilimo kwa kutoa elimu, huduma za ugani na masoko. Miaka ya hivi karibuni Mayawa ilipata changamoto na kuacha kabisa kununua vanila. Wapo wakulima ambao yapata miaka mitatu au minne hawajalipwa fedha zao walizouza vanila. Mwaka jana alijitokeza mnunuzi mmoja, akaomba kununua, mkoa ukampa kibali, akanunua na akapotelea kusikojulikana bila kuwalipa wakulima hadi leo. Kuna kilio kikubwa sana cha wakulima wa vanila.

Mheshimiwa Spika, nimeshamfuata Mheshimiwa Waziri mara kadhaa kuhusu kilimo cha vanila, hata Wabunge wa Kagera wengine nao wameongelea vanila, lakini hatujui Serikali wana mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa vanila ili waweze kupata soko la uhakika. Ni kweli bei ya vanila kidunia imeshuka, lakini hata kahawa kwa miaka kadhaa bei ya kahawa iliporomoka, lakini waliendelea kuwa na soko na hivyo kilimo kiliendelea.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana Waziri aliniahidi kuwa anakuja mnunuzi wa vanila na atajenga kiwanda pale Maruku, lakini Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kwenye hotuba yake ya bajeti sikusikia neno hata moja kuhusu kilimo na mkulima wa vanila. Kwa mwaka huu wa 2024, msimu wa kuvuna vanila unaanza Juni – Julai, je, hawa wakulima maskini wa vanila watauza wapi? Je, sisi wawakilishi wa wananchi tukirudi mkoani tuwaeleze nini wakulima hawa? Je, Serikali wanawasaidiaje wakulima wa vanila Kagera na wanawapa matumaini gani?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.