Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumpongeza Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe kwa hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Ni hotuba nzuri yenye taarifa na takwimu muhimu za kutuwezesha Waheshimiwa Wabunge kujadili na kushauri Serikali kuhusu sekta hii muhimu ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Tume ya Umwagiliaji; Tume na Wizara zimeanzisha miradi mingi kwa wakati mmoja na imeshindwa kukamilisha hata mradi mmoja tangu Mwaka wa Fedha 2022/2023. Hivi sasa Tume inatekeleza miradi 780 ambapo kati ya miradi hiyo 17% ni miradi ya tangu Mwaka wa Fedha 2022/2023.

(i) Mradi wa Ujenzi la Bwawa katika Kijiji cha Mwaukoli, Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu; ujenzi ulitarajiwa kuanza Juni Mosi, 2023 na kukakimilika Juni Mosi, 2024, lakini hadi sasa mradi huu uko katika hatua ya kumpata mshauri elekezi, miaka miwili iliyopita.

(ii) Skimu 25 za umwagiliaji zinazoendelea na ujenzi (Kiambatisho Na.1), wastani wa utekelezaji ni 30% na miradi mingine iko kwenye hatua za usanifu na mingine kutangazwa zabuni na hakuna mradi hata mmoja uliokamilika.

(iii) Miradi 30 ya skimu za umwagiliaji zinazoendelea na ukarabati (Kiambatisho Na.2), wastani wa utekelezaji wa miradi ni 32% na mradi mmoja uko kwenye hatua ya kumpata mkandarasi, hakuna mradi uliokamilika.

(iv) Mabwawa 14 ya umwagiliaji yanayoendelea na ujenzi (Kiambatisho Na.3) ambayo wastani wa utekelezaji ni 40% na hakuna mradi uliokamilika.

(v) Miradi 711 ya skimu na mabwawa ya umwagiliaji (Kiambatisho Na. 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10) ambapo miradi hii iko kwenye upembuzi yakinifu na usanifu, manunuzi ya kumpata mshauri elekezi, hatua ya kusaini mikataba, hatua za manunuzi ya ujenzi na miradi michache ambayo ujenzi umeanza.

(vi) Fedha zilizotengwa na kuidhinishwa na Bunge katika kipindi cha miaka hiyo miwili ni shilingi bilioni 631.85 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya skimu na mabwawa ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Waziri atuambie ukweli nini sababu ya kusuasua kwa miradi hii hadi leo miaka miwili hakuna mradi uliokamilika hata mmoja. Pia mwaka jana nilihoji hapa Bungeni sababu za kubadilishiwa matumizi fedha za umwagiliaji takribani shilingi bilioni 200 na bila ridhaa ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, kuhusu utoaji wa mbolea ya ruzuku, wanufaika wa mbolea ya ruzuku; katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 wananchi 3,389,951 walijiandikisha kupata mbolea ambapo kati yao wananchi 2,551, 239 hawakupata mbolea sawa na 75% pamoja na kwamba walikuwa na sifa zote za kupata mbolea ya ruzuku. Licha ya kuripotiwa kuwa na bakaa ya mbolea ya tani 326,344. Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 wakulima waliosajiliwa katika mpango wa mbolea ya ruzuku walifikia 3,910,556. Hotuba ya Waziri haijaeleza idadi ya wanufaika wa mpango wa mbolea ya ruzuku katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Waziri atuambie sababu za kuwafikia wakulima 25% tu huku idadi kubwa ya wakulima wakikosa mbolea ya ruzuku, ruzuku ya mbolea inayotolewa na Serikali ni haki ya wananchi wote wenye mahitaji. Jambo hili tumelilalamikia hapa Bungeni mwaka jana lakini hatuoni hatua za Wizara za kuhakikisha wakulima wote wanapata mbolea. Hawa wananchi waliokosa mbolea wanaendeshaje shughuli zao za kilimo? Ruzuku ya mbolea ni kwa ajili ya kundi fulani la wakulima?

Mheshimiwa Spika, kuhusu utoaji wa fedha kugharamia mpango wa mbolea ya ruzuku katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, TFRA na Wizara ya Kilimo walinunua mbolea ya ruzuku yenye thamani ya shilingi bilioni 480 wakati bajeti iliyoruhusiwa na Bunge ilikuwa ni shilingi bilioni 150, hili ni sawa na ongezeko la 220%. Wizara ilipata wapi kibali cha kununua mbolea ya ruzuku zaidi ya shilingi bilioni 330 ya kiwango kilichoruhusiwa na Bunge. Waziri atoe maelezo ya kutosha kuhusu suala hili kwani hana mamlaka kisheria kubadilisha matumizi ya vifungu na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, kuhusu usimamizi wa bei elekezi ya mbolea ya ruzuku, ili kupata tija katika utoaji wa mbolea ya ruzuku, ni lazima bei zinazotangazwa ziwe halali, wakulima wamudu bei hizo na fedha za umma zitumike kihalali. Pasipo usimamizi imara na kuwepo bei elekezi (indicative price) ruzuku inayotolewa haiwezi kuwanufaisha wakulima kwani bei zitaendelea kuwa juu na kuwepo madai hewa ya waagizaji na wasambazaji wa mbolea.

Mheshimiwa Spika, kukosekana msingi wa mjengeko wa bei na hivyo kwa sehemu kubwa bei inatokana na matamko ya wafanyabiashara, TFRA na Wizara kuacha kutumia mfumo wa BPS katika kuagiza na kusambaza mbolea nchini na hivyo kuondoa ushindani na manufaa ya ununuzi wa pamoja (economies of scale). Katika mwaka wa fedha 2022/2023 manunuzi ya kutumia mfumo wa BPS ulikuwa 6.3% tu.

Mheshimiwa Spika, BPS inataka kufanya uhakiki wa bei katika masoko mbalimbali (due diligence) ili kushindanisha wazabuni kwenye soko lenye bei nafuu na kuagiza kwa pamoja ili kupata bei nzuri. Hivyo kwa mazingira haya huwezi kushusha bei ya mbolea hata kama utatoa ruzuku.

Mheshimiwa Spika, kuhusu usimamizi dhaifu wa bei elekezi, pamoja na kuwepo bei elekezi, lakini baadhi ya wauzaji na wasambazaji wa mbolea hawazingatii bei elekezi iliyotangazwa na TFRA, imethibitika kuwa wauzaji wengi wa mbolea (Agro Dealers) katika LGA zaidi ya 80% wanauza kwa bei kubwa tofauti na bei elekezi iliyowekwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, suala la ufuatiliaji wa dhaifu wa bei katika soko la dunia, karibu kila mwezi bei ya mbolea ilikuwa ikishuka, lakini bei ya mbolea hapa nchini ilibaki vilevile hadi Machi, 2023.

Mheshimiwa Spika, utoaji wa mbolea ya ruzuku una tija ndogo kwani unawafikia wakulima 25% tu, pia kuwepo kwa bei kubwa zisizo na uhalisia na matumizi makubwa ya fedha za umma unaopelekea kuharibu mipango mingine ya Serikali. Bado naamini kuwa kama kungekuwa na usimamizi makini wakulima wengi wangepata mbolea tena kwa bei nafuu na mzigo kwa Serikali ungekuwa mdogo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji na usambazaji wa mbolea; mwaka jana nililalamikia juu ya matumizi ya mfumo wenye changamoto nyingi ikiwemo kukosa usalama (security) na kuruhusu kufanyika multiple scanning, pia kuwepo kwa mbolea fake/mbolea bandia, wakulima kuuziwa mchanga badala ya mbolea, kuuziwa mbolea iliyokwisha muda wa matumizi, utoroshaji nje ya nchi na kuliingiza Taifa kwenye hasara kubwa. Haya yote yanafanyika Waziri na TFRA wapo na hatujaona masahihisho yoyote kukabili changamoto hizo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uzalishaji wa mbolea ya ndani ya nchi; pamoja na nchi yetu kuwa na uzalishaji mkubwa wa mbolea ya samadi, mboji na uzalishaji wa viwanda vya ndani, lakini kwa sehemu kubwa tunaagiza mbolea kutoka nje ya nchi, Wizara haina mkazo wowote wa kuongeza matumizi ya mbolea za asili na pia viwanda vya ndani ikiwemo Kiwanda kipya cha ITRACOM ambapo umepelekea kuongeza uzalishaji wa mbolea na kufikia tani 114,224. Waziri atueleze ni kiasi gani cha mbolea ya ndani kimenunuliwa kupitia mfumo wa ruzuku ya mbolea? Nini mkazo wa Serikali wa kuongeza matumizi ya mbolea za asili?

Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo ya madeni; Wizara imelipa madeni kwa mawakala wa pembejeo za kilimo na wazabuni wa pamba kiasi cha shilingi bilioni 64.5, madai ya mwaka wa fedha 2015/2016 ambayo yamehakikiwa na kukubaliwa mwaka wa fedha 2023/2024. Je, kwa nini madeni ya Mwaka wa Fedha 2015/2016 yafanyiwe uhakiki na kukubaliwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 takribani miaka kumi iliyopita, kupitia Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG), amekuwa akifanya uhakiki wa madeni ya nyuma na kukamilisha kazi hiyo tangu mwaka 2017. Waziri atakapokuja kuhitimisha bajeti yake aweke wazi orodha ya watu waliolipwa fedha hizi ili kuweka uwazi wa matumizi wa fedha za umma. Awali tuliambiwa baada ya uhakiki yalibainika madeni mengi hewa ambayo yalifutwa na Serikali. Ni jambo linalofikirisha madeni ya miaka kumi kufanyiwa uhakiki leo na kukubaliwa kwa malipo ni lazima tujiridhishe Waheshimiwa Wabunge ili eneo la madeni lisije kutumika kama uchochoro wa kufuja fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, kuhusu zao la pamba, bei ya pamba kuwepo makato makubwa ya fedha yasiyo na uhalali kwa kisingizio cha ununuzi wa pembejeo. Mfano, wakulima wa pamba katika msimu wa kilimo wa 2022 walikatwa kiasi cha shilingi 400 na mwaka 2023 walikatwa shilingi 300 kwa kila kilo waliyouza. Makato yanayokatwa kupitia Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Pamba katika kununua mbegu, viuatilifu na vinyunyizi ni makubwa na kwa kiwango kikubwa yanaathiri bei ya mkulima na kumtia hasara kubwa, kwani gharama za kilimo ni nyingi, sio mbegu na viatilifu tu, bali kuna kupata shamba, kulima, kupanda, kupalilia zaidi ya mara nne, kupulizia dawa, kuvuna, kuuza, kusafirisha, kuhifadhi kwenye ghala na kadhalika ambako kote kunahitaji gharama.

Mheshimiwa Spika, bei ya kilo moja ya pamba ni shilingi 1,360 halafu mkulima anakatwa shilingi 300 kwa kila kilo moja sawa na 22% kulipia pembejeo. Kwa maelezo ya aina yoyote suala hili halikubaliki, badala ya kuwainua wakulima tunawatia umaskini. Pamoja na kikao cha wadau kilichokutana Machi, 2024 ambacho amekinukuu Waziri katika Ibara ya 339 ya hotuba yake, makato haya hayakubaliki na kuna haja ya kupanua mjadala kwa kuwashirikisha wakulima wenyewe kutoka kila wilaya na Mabaraza ya Madiwani, mfano Baraza la Madiwani la Meatu na Baraza la Madiwani la Bariadi walipinga makato hayo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ununuzi wa pamba kupitia kampuni moja usiruhusiwe kwa kuwa utaenda kuua ushindani ambao utapelekea kuporomoka kwa bei na usumbufu wa kuuza zao hilo. Kata 40 ambazo zilikusudiwa kupelekewa matrekta ya kulimia, matrekta hayo hayajapelekwa hadi sasa na hivyo hakuna sababu ya kupeleka kampuni moja katika maeneo hayo. Hata baada ya matrekta hayo kupelekwa, mwakani utafutwe utaratibu mzuri ambao hautaathiri biashara ya zao la pamba.

Mheshimiwa Spika, kuhusu bei za mbegu na viuatilifu na usimamizi wa bei za pembejeo kwa wakulima; pembejeo hizi za kilimo zimekuwa zikiuzwa kwa bei kubwa isiyo na uhalisia mfano mfuko wa kilo mbili za mbegu ya mahindi kuuzwa kati ya shilingi 16,000 hadi shilingi 24,000 wakati mahindi ya kawaida kuuzwa kwa shilingi 1,200 kwa kilo mbili. Hakuna uthibitisho wa uhalali wa bei hizo za mbegu zinazoagizwa kutoka nje na zinazozalishwa ndani ya nchi. Kuna tishio kubwa la kupotea mbegu za asili na Taifa kuwa tegemezi kwa mbegu za kisasa ambazo zinalazimu kununua kila mwaka, mfano zaidi ya 45% za mbegu za mahindi tunaagiza kutoka nje ya nchi kila mwaka. Baadhi ya maeneo wananchi wanauziwa viatilifu fake vinavyonenepesha wadudu badala ya kuua, lakini pia viatilifu vimekuwa vikichelewa kuwafikia wakulima na hivyo kuwasababishia hasara kubwa. Inashangaza kuona mambo haya yameruhusiwa huku Waziri na mamlaka zipo zinazosimamia za TPRI, TFRA, ASA, TARI na TOSCI.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mageuzi makubwa ya kilimo tunachokiendea hatuna sababu ya kutokuwa na Maafisa Ugani katika vijiji na kata zetu zote, Serikali imalize tatizo hili kwa haraka kwa kutoa ajira mpya.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.