Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kama Mbunge wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini naendelea kuishukuru Serikali kwa suala la mbolea ya ruzuku, tunaishukuru mno Serikali. Hatua hii imesaidia mambo kadhaa:-
(i) Kupunguza makali ya bei;
(ii) Kuhamasisha wananchi kuongeza mashamba kwa maana ya eneo la kulima; na
(iii) Kuongeza uzalishaji/mavuno kwa maana ya high productivity.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna changamoto kadhaa kwa mawakala, makampuni, TRA na namna ya usambazaji wa mbolea za kufika vijijini japo hadi ngazi ya kata.
Mheshimiwa Spika, mawakala wanakabiliana na changamoto ya kwanza kutoka kwa baadhi ya makampuni, kwa mfano kwa Kampuni ya Yara inamtaka wakala kulipa fedha yetu pamoja na ile ya ruzuku hali ambayo inamnyima wakala nguvu ya kimtaji kuweza kusambaza kwa haraka na kwa ukubwa. Baadhi ya makampuni hayana masharti magumu, wapo ambao wanataka tu commitment ya wakala kwa kutaka tu aweke deposit ya kiasi fulani cha fedha baada ya hapo wanaendelea kufanya kazi na wakala na mbolea inafika kwa mkulima kwa wakati. Kwa nini Yara wasiwe flexible, Yara ni giant company, ni matarajio yangu kuwa ingeunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwa na masharti rafiki kwa mawakala. Binafsi nawaona Yara kama wahujumu wa jitihada za Serikali.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu Serikali iwape maelekezo Yara, wawe na masharti nafuu kwa mawakala, wao Yara ni wanufaika wa mfumo wa mbolea ya ruzuku, lakini pia ni wanufaika kibiashara ndani ya Tanzania, kwa nini wasiwe na moyo mwema wa kui-support Serikali katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, kuhusu issue ya TRA, wakati waingizaji wa mbolea kwa maana ya makampuni wanauza mbolea kwa bei ya soko na mawakala wa pembejeo wanauza kwa bei ya ruzuku, TRA imekuwa ikiwasumbua linapokuja suala la kodi. Hii inatokana na ukweli kwamba kunakuwa changamoto za kimahesabu baina ya mawakala na maafisa wa TRA, kwa maafisa wa TRA kutokutambua mfumo wa dijitali wa TFRA Agro-dealer Tools na hivyo mawakala kujikuta wakipigwa faini na TRA kwa kuonekana kuwa wana manunuzi makubwa kuliko mauzo.
Mheshimiwa Spika, shida ni kwamba Maafisa wa TRA hawatambui kwamba wafanyabiashara hao wananunua mbolea kwa bei ya juu kwa maana bei ya soko na kuuza kwa bei ya ruzuku ambayo ni bei ya chini, hali ambayo inasababisha kuonekana wana manunuzi makubwa na mauzo kuwa madogo. Kwa sababu hiyo kuna kila sababu Serikali kwa maana Wizara ya Kilimo kukaa na Wizara ya Fedha ili kuweza ku-harmonize suala hili. Wote tunamtumikia mwananchi mmoja, tuwe na uelewa wa pamoja. Tusiwaumize mawakala licha ya kuwa hii ni biashara, lakini kwa kiasi fulani ni huduma.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa mbolea inafika ngazi walau ya kata, kumekuwa na changamoto ya gharama za bei ya nauli ya mbolea kukosa uhalisia kwenye kufika ngazi ya kata, kwa mfano umbali wa kilometa 40 gharama za kusafirisha mfuko mmoja wa mbolea ya kilo 50 ni shilingi 300 hali inayosababisha mawakala kufanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine kushidwa kupeleka mbolea vijijini na wakulima kulazimika kufuata mbolea maeneo ya mjini kwa umbali mrefu na hivyo kuongeza gharama. Nashauri wataalam watusaidie namna ya kukabiliana na changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusu maghala, kutokana na uwepo wa mbolea ya ruzuku na kutokana na ukweli kwamba bado hatujawa na maghala makubwa na ya kisasa, nashauri ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula na hasa nafaka tutumie sekta binafsi katika kujenga maghala makubwa na ya kisasa, Serikali peke yake haitakaa iweze na kama itaweza basi itachukua muda mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kilimo cha parachichi; Kata za Wambi, Rungemba, Bumilayinga, Sao Hill na Isalavanu wananchi wameitikia wito wa kulima parachichi na wenzetu wa Kibidula wamekuwa msaada sana ku-support huduma za ugani na kuwatafutia soko wakulima wa nje yaani out growers. Nashauri Serikali kuwaunga mkono wananchi na Kibidula hata kwa kuwasaidia kufanya kilimo cha mkataba ili kulinda haki za pande zote mbili.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mara kadhaa suala la soko limekuwa changamoto, nashauri watu kama hawa wa Kibidula kupewa kila aina ya support na ushauri kwa sababu walau hawa ni mkombozi linapokuja suala la soko kuyumba.
Mheshimiwa Spika, pili, nafahamu kuwa kuna miradi ya RISE na Agro-connect, naomba awamu ijayo tuitazame barabara ya changarawe kupitia Skimu ya Umwagiliaji ya Mtula, Matanana, Kisada kutokezea Nyololo, eneo lote inakopita kuna shughuli za uzalishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda kwa maana ya parachichi, itasaidia sana kufikisha mazao sokoni kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, tatu, Mheshimiwa Waziri Bashe na timu yake wamekuwa wakifanya kazi kubwa kiasi wamefanya Watanzania kuona kuwa kilimo is no longer a theory issue, but real. Hata hivyo, yako maeneo ni kikwazo, kwa mfano wenzetu wa TRA, Bandari na TANROADS/mizani, hasa kwa mazao ya mbogamboga na matunda, pamekuwepo na ucheleweshaji wa mizigo kwa sababu zisizo za msingi, huwezi kumsimamisha mtu ambaye amebeba kontena la parachichi kisa tu sijui risiti ya EFD ya transport, sisemi kwamba sheria zivunjwe la hasha, bali kuna maeneo tutumie common sense, gari limesajiliwa, dereva ana leseni, kwa nini usiache gari liwaishe mzigo sokoni na huyu dereva au mwenye gari umpige faini hata online kama ambavyo wamekuwa wakifanya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu bandari, nashauri pamoja na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha bandari yetu, pawepo jitihada za makusudi kuwa na eneo maalum kwa ajili ya kusafirishia mazao ya mboga mboga. Hivi sasa wasafirishaji kwa mfano wa parachichi wanategemea Bandari ya Mombasa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu BBT na visima 67,000; jambo hili limekuwa na mixed feelings kwa sababu ya uelewa, nashauri Serikali isichoke kuelimisha kuwa hii ni program up to 2030 maana kuna watu wanadhani hii ni one year project, nashauri Wabunge na Watanzania kwa ujumla waelimishwe kwa lugha rafiki, in humble manner, maana wapo watu wanaamini kuwa tayari Wizara ina mabilioni ya fedha kumbe so far ni pledges.
Mheshimiwa Spika, napongeza pia kupanua wigo wa BBT kupitia ile programu ya visima 67,000, nayo ni muhimu sana ifahamike kuwa ni programu ya kutoka sasa hadi 2030, vinginevyo ama kwa kutoelewa au kwa nia ya kupotosha watadhani kwamba programu hii ni kwa this financial hii ya 2024/2025. Kwa hiyo nashauri maelezo yajitosheleze na Serikali wasichoke kufafanua.
Mheshimiwa Spika, mwisho, nawashukuru sana kwa Mradi wa Umwagiliaji wa Mtula.
Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kusema kilimo chetu, maisha yetu.