Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hoja hii iliyopo mezani. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta mageuzi katika Sekta hii ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki kinachofanyika kwenye sekta ya kilimo ni maono sahihi ya Mheshimiwa Dkt. Samia katika kushughulikia matatizo ya Watanzania ambayo yamekuwa yakiikabili nchi yetu kwa muda mrefu. Hili ndiyo jawabu sahihi la kushughulikia matatizo ya ajira kwa vijana wa Kitanzania. Mageuzi katika sekta ya kilimo ni jawabu sahihi la kushughulikia upungufu wa fedha za kigeni ambalo limekuwa likizikumba nchi nyingi za Afrika kwa sababu tutaongeza mauzo ya nje na tutaongeza fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuwekeza kwenye sekta ya kilimo cha kisasa ni jawabu sahihi la kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja kwa sababu kilimo ndiyo sekta inayoajiri Watanzania walio wengi. Kwa hiyo huu ni uelekeo sahihi na sisi kama Wizara ya Fedha tutafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba fedha ambazo zinatengwa na Bunge lako Tukufu zinawafikia wenzetu wa Wizara ya Kilimo ili waweze kutekeleza miradi hii ambayo itaenda kuleta mageuzi kwenye maisha ya Watanzania hasa vijana ambao sasa wamekwenda kwenye shughuli hizo za kilimo.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kufanya mawasiliano na taasisi nyingine kwa sababu kilimo ni jambo ambalo linafanywa kwa kiwango kikubwa na Sekta Binafsi. Tunazialika na sekta nyingine na taasisi nyingine na nyingi zimeshaonesha utayari wa kuja kushirikiana na sekta yetu ya kilimo ili kuweza kuhakikisha kwamba kuanzia kwenye uzalishaji mpaka kwenye toleo la mwisho, vyote vinakuwa vinafanywa kwa njia ya kisasa.

Mheshimiwa Spika, kwa maslahi ya muda, niguse pia jambo ambalo ulinipa nafasi ya kuchangia pale mwanzoni. Jambo hili tumelipokea na kama ambavyo Mbunge ameongelea kwamba Benki Kuu walishatoa maelekezo kwa Umoja wa Taasisi za Kifedha. Mpaka imeenda Benki Kuu tayari huo ulikuwa ni mchakato ambao ulikuwa unahusisha kufanyia kazi jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unajua utaratibu wa utungaji wa sheria ya aina yoyote ile una mchakato wake, una mchakato wa kushirikisha wadau ili iweze kufika mpaka hatua ya mwisho ya kuitunga sheria. Sasa katika hatua hiyo ambayo imeshafika ni hatua nzuri. Kitu kitakachosalia tulipokee sisi kama Serikali. Litapita mikono ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baada ya hapo kama yatakuwa yameshashughulikiwa maoni yote ambayo yametolewa na wadau ambapo tayari tumeshapata mojawapo ni lile linalohusisha Benki Kuu pamoja na Umoja wa Mabenki yaani ile association ya mabenki. Baada ya hapo Serikali itatoa jawabu lake kuhusu utaratibu wa hatua za kisheria ambazo huwa unakuja Bungeni. Kwa hiyo naomba Bunge lako liridhie kwamba tumelichukua, tutamaliza consultation ya ndani ya Serikali, tutamaliza consultation ya wadau na baada ya hapo taratibu za kiutungaji wa sheria zitaweza kufuatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie, kuna baadhi ya michango iliyokuwa imetolewa inayohusu BBT. Ukienda nchi ambazo zimeendelea, nchi ambazo tulikuwa sawa huwa tunatolea mfano, Vietnam pamoja na nchi nyingine ambazo wamepiga hatua kubwa sana kwenye masuala ya kilimo. Sehemu walipoanzia ilikuwa ni kuipeleka nguvu kazi iende kwenye kufanya kazi hizo.

Mheshimiwa Spika, kilimo hakiwezi kikawa ni shughuli ya wazee, hakiwezi kikawa ni shughuli ya wastaafu kwamba mtu akishastaafu ndiyo anasema anataka kwenda kulima. Hatuwezi tukapiga hatua kwa kufanya hivyo. Ni lazima tufanye orientation na hivi tulivyofanya ndiyo njia sahihi. Hatuwezi tukaanza mara moja kwa kila kitongoji, hatuwezi tukaanza hivyo. (Makofi)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, tunaanza kwa miradi na tutapiga hatua. Baada ya muda hiyo ndiyo itakuwa standard ya utaratibu tunaolima hapa nchini.

SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mafuwe.

TAARIFA

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka kumpa kaka yangu kwa mchango wake mzuri taarifa kwamba ni kweli tunapaswa kuwekeza kwenye kilimo, lakini bajeti hii inayopita imekwenda kwa 53% tu. Maana yake tulipaswa hasa Wizara yake ingetusaidia, fedha zingeenda ili kilimo sasa kiwe ni kilimo cha vijana, waweze kufanya kazi na miradi iweze kutekelezwa, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Taarifa hiyo unaipokea?

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yake kwa sababu inahamasisha fedha ziende kwenye miradi, lakini naomba tu nitoe taarifa kwa Watanzania kwamba mwaka huu tumeathiriwa sana na mafuriko. Kwa kweli mradi usingeweza kuendelea eneo kama Rufiji. Usingeweza kuendelea maeneo kama Manyara, kusingeweza kuendelea na maeneo mengine ya aina hiyo. Sipingani naye na sisi kama Wizara na Mheshimiwa Rais mara zote anatuambia tusikae na fedha Wizarani, anatuelekeza fedha ziende kwenye miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sipingani naye isipokuwa kwa kweli si mradi ule tu, tumeathiriwa sana na masuala ya mafuriko na sio tu kwamba miradi imesimama, miradi imeathiri pia miundombinu mingine. Ukiambiwa uchague kati ya kupeleka mradi uendelee au ukawafukue watu waliofukiwa na nyumba zao, utapeleka fedha kufukua watu kwanza. Kwa sababu lazima ufukue watu kwanza na uwape makazi ndiyo upeleke fedha kwenye miradi ya maendeleo. Kwa hiyo hiki ni kipaumbele wala hakitabadilishwa na mafuriko, la mafuriko ni la dharura tu, tutaendelea na utekelezaji kama kawaida, ndiyo maana tumeiongeza bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilichokuwa namalizia naona na kengele imeshagonga. Nilichokuwa namalizia ni kwamba, Watanzania tunatakiwa tuvuke, huwa tuna bidhaa nzuri sana kwenye maonesho, ukioneshwa mazao yaliyopo kwenye sherehe za maonesho zile yanakuwa bora sana. Hivyo hivyo na kwenye mifugo, yanakuwa bora sana. Anachokifanya Mheshimiwa Rais anataka vile ambavyo huwa tunavionesha kwenye Maonyesho ya Nanenane na Sabasaba, iwe ndiyo standard ya production ya nchi. Hapo ukishakuwa na mazao ya aina hiyo unaweza ukauza popote kule na nchi ikawa the world largest producer na exporter wa zao hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii itaanza na miradi kama hii ambayo Wizara ya Kilimo inafanya. Kwa hiyo Wizara ya Kilimo wapo kwenye njia sahihi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tumekutengea na ofisi pale Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuhakikisha hii miradi haikwami, mara zote tunashirikiana ili tuweze kuhakikisha mambo yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)