Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii kuchangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo. Kabla sijakwenda katika mchango wangu, niungane na Wabunge wenzangu wote kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo amekuwa akizifanya hususan katika Wizara ya Kilimo, kwa kweli tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amewatendea haki wakulima wa nchi hii kwa kipindi cha miaka mitatu tangu ameingia madarakani. Mheshimiwa Rais ameyatenda haya kwa vitendo na kila Mbunge hapa ni shahidi. Tunayoyasema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu moja, karibu kila jambo ambalo Mheshimiwa Rais alilisema amelitekeleza kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo hili linatupasa sisi sote tuendelee kumuunga mkono na kumpa moyo ili aendelee kuwatumikia Watanzania kwa miaka mingine mitano inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu wa pili wa kumshukuru ni Waziri wangu Comrade Hussein Bashe. Mheshimiwa Bashe ni kiongozi, ni mzalendo, ni mchapakazi na ni moja ya Mawaziri wanaotaka kuona matokeo. Mimi binafsi ukiacha kwamba ni kiongozi wangu ni role model wangu katika mambo mengi sana hususan ya kiuongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yote unayoona leo Waheshimiwa Wabunge wanayashuhudia, msukumo wa Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kiwango kikubwa, mimi huwa namwambia yeye ni Waziri Mtendaji, anafanya kwa moyo mkubwa sana. Niwaambie Watanzania, tuna mtu sahihi na mwelekeo anaotupeleka ni sahihi kabisa. Ndiyo maana leo kilimo tunaiona kabisa ni game changer katika uchumi wa nchi yetu; kila mmoja anaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, timu nzima ya Wizara ya Kilimo na Menejimenti. Kama kuna Wizara inafanya kazi vizuri as a team work, Wizara ya Kilimo inaongoza. Nayasema haya hata Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda, kama kuna Wizara tunafanya kama team work, kila mmoja anashirikishwa kwenye kila hatua Wizara ya Kilimo tunafanya. Tunawashauri wengine waje kujifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kumshukuru zaidi Mheshimiwa Rais kwa ongezeko la bajeti. Tangu anaingia madarakani kutoka shilingi bilioni 294 katika mwaka wa fedha 2020/2021 mpaka leo tunapozungumzia, bajeti ya shilingi trilioni 1.248 mwaka wa fedha 2024/2025. Mheshimiwa Rais ana maono, anataka kubadilisha uchumi wa kawaida wa mwananchi wa Tanzania kupitia Sekta ya Kilimo. Katika fedha hii ambayo leo Wizara ya Kilimo tunaiomba, shilingi trilioni 1.06 inakwenda katika miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unaona kabisa kwamba tunataka kufanya kilimo chenye kumnufaisha mkulima wa kawaida, ndiyo maana tunasema hivi, ukiangalia hata kwenye bajeti ya umwagiliaji, ongezeko la bajeti wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani mwaka wa fedha 2020/2021 ambayo ilikuwa shilingi bilioni 45, leo tunazungumzia zaidi ya shilingi bilioni 410.

Mheshimiwa Spika, lengo la Mheshimiwa Rais anataka Tanzania tupeleke kilimo kinachotegemea maji na wala si kilimo kinachotegemea mvua. Mheshimiwa Rais anataka Mtanzania wa kawaida anayejishughulisha na shughuli za kilimo alime mwaka mzima, yaani awe na vipindi zaidi ya viwili vitatu ambavyo anaweza kukaa shambani akajiongezea kipato cha kawaida. Hii itatuletea faida kubwa sana katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matarajio yetu ni kwamba miradi yetu ya kilimo itakapokuwa imekamilika, tunaamini tuta-double export value ya mazao yetu, tutaongeza kipato cha mkulima mmoja mmoja na contribution katika GDP ya Taifa itaongezeka mara dufu kwa sababu matokeo ya kilimo huwa yanalipa moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wizara ya Kilimo tunaamini katika tafiti. Ndiyo maana unaona leo Wizara ya Kilimo tumeongeza fedha katika taasisi zetu zinazofanya tafiti na malengo yetu makubwa ni kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini na sio kuagiza kutoka nje ya nchi. Ndiyo maana leo moja ya kazi kubwa wanayofanya TARI ni kufanya tafiti ya mbegu mbalimbali nchini na hiyo kazi inaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Spika, sisi Wizara ya Kilimo tunaamini kilimo ni biashara kama biashara nyingine, ndiyo maana sasa hivi ukiona hata katika ajenda yetu ya 2030 tumeandika moja kwa moja kilimo ni biashara. Mkulima yeye anapolima asiwe tu ni yule mtu ambaye anategemea kilimo kama sehemu ya kujipatia chakula cha kawaida, lakini iwe ni sehemu ya kujipatia fedha zake zitakazomsaidia katika shughuli nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tunaamini katika kilimo kinachotegemea maji na wala sio mvua. Ndiyo maana wataona ukipitia katika Kitabu chetu cha Bajeti, tunapitia mabonde yote, tunayafanyia usanifu wa kina ili Watanzania wanaoishi katika maeneo hayo waweze kufanya shughuli za kilimo katika mwaka mzima ambao utakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, tunaamini katika kuongeza tija katika kilimo, ndiyo maana sasa hivi unaona moja ya jukumu kubwa tulilonalo Wizara ni kuhamasisha wakulima wetu waongeze tija katika kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tunaamini katika kilimo cha kisasa. Ndiyo maana Wabunge wanaona tunafanya mambo makubwa yakiwemo modernization of agriculture hususan katika mechanization. Kuleta vifaa vipya vya kisasa, kilimo cha kidijiti ambacho kitakwenda kumsaidia mkulima wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na vipaumbele vingi kama Wizara ikiwemo utafiti na uzalishaji wa mbegu. Tumeongeza usambazaji wa mbolea, hata Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo langu la zamani la Momba Mheshimiwa Condester, alipokuwa anazungumzia, sisi kama Wizara tunakiri kwamba zipo changamoto ndogondogo ambazo tutaendelea kukabiliana maana yake mnapokuwa katika kutengeneza road map lazima panatokea changamoto.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo changamoto kama alizozieleza Mheshimiwa Mbunge zipo, lakini sio kwa kiwango kikubwa. Ndiyo maana vingine nitamshauri tu Mheshimiwa Mbunge apitie bajeti yetu pale. Masuala ya BBT asome aone mipango ambayo Wizara ya Kilimo tumejaribu kuiainisha pale ili kuweza kuwasaidia Watanzania wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu tumewekeza nguvu sasa hivi katika kutoa huduma za ugani. Hili tunalifanya kwa sababu tunaamini kilimo kinahitaji wataalam watakaokwenda kuwasaidia wakulima wa chini. Sisi lengo letu tunataka tumsaidie mkulima wa chini, tunataka kumsaidia mkulima wa Katikati, lakini hatuwezi kumuacha mkulima mkubwa katika nchi hii ilimradi ni Mtanzania. Hata mwekezaji yeyote anayekuja, sisi kama Wizara ilimradi anaongeza tija katika Sekta ya Kilimo, Wizara tupo tayari kumsaidia wakati wowote. Hayo ndiyo malengo makubwa ambayo sisi tupo nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tuna jukumu kubwa la kuongeza wigo wa masoko kwa wakulima wetu kwa sababu ukiongeza tija bila kuhakikisha unakuwa na masoko ya uhakika, maana yake wakulima watafanya kazi kubwa na mwisho wa siku mazao yao yanaweza kuharibika kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, ukiacha ya kwamba watu wanaozalisha mazao ya nafaka kama mahindi na mpunga, hawa soko lao la kwanza litakuwa ni NFRA. Jukumu moja la Wizara tulilonalo sasa hivi ni kuongeza wigo wa uhifadhi wa chakula kufikia tani 500,000, lakini malengo yetu tunataka tufikie tani 3,000,000 kwa mwaka, NFRA awe na uwezo wa kuhifadhi chakula hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ni malengo makubwa, yanahitaji wenye vision kubwa, wenye msimamo wanaoweza kutekeleza. Hili jukumu sisi tunaliweza, haliwezi kutushinda na tukafikia malengo ya Mheshimiwa Rais ambayo anataka Tanzania ya baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu mbolea, changamoto ndiyo zimekuwepo, lakini kwenye mbolea ninyi nyote ni mashuhuda katika mwaka uliopita. Sasa hivi sisi kama Wizara kupitia kampuni yetu ya TFC tunataka kuanzisha blending facilities kwa kushirikiana na Sekta Binafsi ili sehemu ya uzalishaji wa mbolea uwe unafanyika hapa nchini. Hili linafanyika kwa sababu ni maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi tunalitekeleza kwa sababu lipo katika mpango. Sasa hivi tunavyozungumza tupo katika mchakato wa kupata mzabuni ili sasa kutengeneza blending facilities ambazo zitaweza kusaidia uzalishaji wa mbolea hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo ni malengo ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyaweka kwa Watanzania ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo tunaweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la utafiti wa jumla tumeendelea kufanya hivyo, kuhakikisha mazao yote yakiwemo mazao ya kimkakati na yale mazao mengine, kwa sababu Wizara ya Kilimo tunasimamia mazao 89 na kati ya hayo 89 kuna mazao ya kimkakati yakiwemo mazao ya kibiashara; sasa jukumu letu sisi kama Wizara ni kuhakikisha kwamba tunakwenda na mazao yote, ikiwemo kuyapa kipaumbele mazao yale yanayoiingizia Serikali fedha nyingi za kigeni.

Mheshimiwa Spika, jukumu hilo tunalifanya kwa uaminifu mkubwa na Watanzania wakiendelea kutuamini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ana passion ya moja kwa moja kwenye kilimo. Ninyi wote ni mashahidi, hakuna uwekezaji mkubwa kwenye kilimo uliowahi kutokea katika vipindi vyote vya uongozi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya. Kwa hiyo tunawaomba Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono, wapitishe bajeti yetu ili sisi kama Wizara twende tukatekeleze yale yote yaliyopo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapindizi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo amekuwa akiyatoa kwa sisi watendaji na kwa Watanzania wote, pamoja na Bunge lako Tukufu ili haya tunayoyasema yaweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, niwaondoe shaka Waheshimiwa Wabunge, kwamba miradi yote ambayo tumeahidi itatekelezeka kwa sababu tuna mahusiano ya karibu na Wizara ya Fedha na wamekuwa wakituahidi kuleta fedha na wanafanya hivyo, isipokuwa pale zinapotokea changamoto za kawaida.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru kwa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)