Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kukushukuru wewe kwa dhati kwa kunipa fursa ya kuja kuhitimisha hoja. Pili, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao. Hoja yetu imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 48. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, ndugu yangu Silinde. Namshukuru sana kwa support anayonipa na ushirikiano anaonipa Wizarani. Namshukuru sana na namuahidi kuendelea kufanya naye kazi kwa karibu, kwa sababu ya historia yetu mimi na yeye. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kila wakati kunipa Naibu Waziri ambao tuna historia ya pamoja ya muda mrefu. Namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, natumia nafasi hii kukishukuru chama changu, Chama Cha Mapinduzi. Nakishukuru sana chama na jana walikuja hapa baadhi ya viongozi wa Sekretarieti ya Chama Taifa na baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu, kuangalia na kusikiliza mwenendo wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo. Nawashukuru sana na nitaendelea kuhakikisha kwamba Ilani ya Uchaguzi inatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru Katibu Mkuu na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo, ahsante sana kwa support wanayonipa kama Waziri na kuendelea kuwatumikia Watanzania. Nawashukuru Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Waziri wa Kilimo hana wakulima ofisini, hana wakulima Dodoma. Nawashukuru sana wakuu wa wilaya walioko katika maeneo mbalimbali, wanaosimamia shughuli zetu za kilimo kila siku. Nataka niwaahidi, tarehe 7 na 8 tutakuwa na semina ya pamoja ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Sisi Wizara ya Kilimo katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha za kusimamia shughuli za kilimo ambazo tutazipeleka moja kwa moja kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ili asimamie shughuli za kilimo katika ngazi ya wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna Mradi wa P4R, nataka niwahakikishie wakuu wa wilaya wote wa nchi hii na wakuu wa mikoa, kwamba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Ofisi ya Wizara ya Kilimo itawapa support zote wanazohitaji ili kuhakikisha wanasimamia miradi na shughuli tunazopeleka katika ngazi ya wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kumshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Tabora. Sijui kama yupo hapa, ndugu yangu Chacha, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkuu wa Mkoa wa Tabora hivi ninavyoongea amekamata Maafisa Ushirika wa Halmashauri watatu, kawaweka ndani. Amekamata watendaji na amekamata Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi. Naendelea kuwapa moyo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kwamba yeyote anayehujumu shughuli, miradi na efforts za wakulima katika ngazi ya wilaya katika nchi hii wana mamlaka waliyopewa na Mheshimiwa Rais, watumie mamlaka waliyopewa. Hatutaruhusu nguvu zinazopelekwa na Serikali na Bunge lako Tukufu kuidhinisha pesa halafu watu wachache wakafaidike na jasho la wakulima. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, hawa wamekamatwa kwa kufanya ukangomba wa tumbaku. Namshukuru sana Chacha na Wizara ya Kilimo iko pamoja naye. Aliyebaki ni Meya wa Jiji la Tabora ambaye aliiba mbolea za wakulima, yuko mtaani. Kiongozi yeyote hana immunity, hata kama ni ndugu yangu atakayehujumu rasilimali za Serikali zinazopelekwa katika Sekta ya Kilimo, Serikali iwachukulie hatua na isiwe mambo ya kukamata watu wadogo. Tumekubaliana kwamba hili ni jambo la kufa na kupona. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo nataka niseme, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, namshukuru kwa dhati. aliponiteua kuwa Waziri wa Kilimo, aliniuliza swali dogo tu, kwamba unadhani matatizo ya kilimo ya nchi hii ni nini? Nikamwambia Mheshimiwa Rais, ni public investments; fedha ya umma kuwekeza kwenye maeneo ya msingi, wakulima si wavivu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha ya umma inapowekezwa na tunapojenga mazingira mazuri ya sekta binafsi kufanya kilimo, kwa sababu wakulima ni sekta binafsi; hii dhana ya sekta binafsi kusubiri kudhani ni mtu mwenye suti na briefcase na anaongea Kiingereza siyo sahihi. Sekta binafsi ya nchi yetu inaongezwa na wakulima wadogo wadogo wa nchi hii, hawa ndio drivers wa sekta binafsi ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili uweze kutathmini fedha za umma zinazowekezwa unatakiwa uangalie mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kitu cha kwanza, je, ukuaji wa sekta hiyo mnayopeleka fedha za umma kuna ukuaji wa aina yeyote? Kitu cha pili mnatakiwa mjiangalie, je, kuna ajira zinatengenezwa? Kitu cha tatu, efforts zenu mnazozifanya zina mahusiano na tumbo na mifuko ya hao watu mnaowapelekea hizo fedha?

Mheshimiwa Spika, mwaka 2021, Bajeti ya Wizara ya Kilimo ilikuwa ni shilingi bilioni 294. Export yetu kwa wastani ilikuwa kati ya dola milioni 800 mpaka dola bilioni 1.2. Kwa maamuzi ya kufungua mipaka, kuondoa ukiritimba, kupeleka mbolea ya ruzuku na kufanya efforts mapato yetu ya forex yameongezeka kutoka dola bilioni 1.2 mpaka dola bilioni 2.3. Wala siyo maeneo ya kutisha, ni maeneo yale yale ambayo wakulima wetu wadogo wamekuwa wakifanya efforts na sisi tunafanya jitihada za kuwasaidia kufungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mauzo ya mazao yanayoitwa oil seeds yameongezeka mpaka kufika dola milioni 743 katika msimu wa kilimo uliopita. Horticulture imefikia dola milioni 265, legumes zimefikia dola milioni 338 na traditional crops zimefikia dola milioni 509. Serials, kwa mara ya kwanza tumeruhusu tu-export mahindi na mchele katika nchi hii, imefikia dola milioni 448. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la kujiuliza, hizi dola zipo kwa wakulima? Hawa wakulima wadogo wanazipata? Hii ndiyo kazi tunayotakiwa kuifanya sisi waliotupa dhamana. Jambo la kwanza tunalolifanya na naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wa korosho, ahsanteni sana kwa support wanayotupa katika mabadiliko tunayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe mfano mdogo wa zao la korosho na mwone namna ambavyo kama hatutoamua pamoja, juhudi za Mheshimiwa Rais zitaishia hewani, kama hatutaamua pamoja kufanya haya mabadiliko. Nataka nitoe mfano, mkulima wa korosho akivuna korosho na kuipeleka mnadani, kwa mwaka jana, natumia msimu uliokwisha, halmashauri zinapata kati ya tani 310,000 tulizozalisha kutoka tani 180,000 ya miaka miwili iliyopita. Hii ni kwa sababu Mheshimiwa Rais alitoa ruzuku ya pembejeo bure na kuwapa wakulima wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka wakati tunachukua hii hatua ilionekana ni muujiza, tukawa tunalaumiana sana, tukawa tunapiga kelele na sasa leo ile kelele haipo kwa watu wa korosho. Tunajadili namna ya kuujenga mfumo wa ruzuku ili mkulima aweze kufaidika. Halmashauri zimepata shilingi ngapi? Mwaka jana halmashauri zimepata bilioni 14 kama cess. Ushuru kwa Bodi ya Korosho ni bilioni sita, ushuru kwa TARI ni bilioni sita, tozo za ushirika ni bilioni 24, tozo za maendeleo kwa ajili ya zao ni bilioni 26, tozo za taasisi zingine za umma zinazopata kutokana na kilo moja ya mkulima, ni bilioni 12, export levy ni bilioni 96. Jumla ni bilioni 186. Hizi ni fedha zimechukuliwa kutoka kwa mkulima, tumechukua sisi. Ni lazima tufanye reform. Tumemwomba Mheshimiwa Rais ruzuku ametupatia na kwa hiyo ni lazima tufanye reform. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu ni kuhusu cartel. Nataka niwape, wao ndio Waheshimiwa Wabunge, mnaona hizi fomu mbili? Hizi karatasi mbili na hii nimechukua karatasi ya Kampuni inaitwa Harmony Agro Limited. Wanapoweka lile dude la kulala usiku lile, debe; mnunuzi anaingiza karatasi mbili kwenye ile bahasha. Karatasi moja anaandika bei kabisa, karatasi nyingine inakuwa empty. Usiku ufunguo mmoja anao afisa ushirika, ufunguo mwingine anao kiongozi wa ushirika. Wanaitana usiku, wanakaa wanafungua sanduku. Wakimaliza kufungua sanduku wanampigia simu Hussein, katani ameandika 2,000 ndiyo bei ya juu, na wewe umeandika 1,980. Unaonaje uandike 2,010 halafu sisi utatupa shilingi 30?
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa amejaza hizi katarasi mbili; na we have enough evidence, Bunge hili likiwa tayari nitawawekea, ninazo video, tume-record vikao vya siri. Sasa kinachofanyika, kwa kuwa tumeshakubaliana tunaitoa ile karatasi ya bei halali uliyoweka tunaweka sasa ile bei tuliyokubaliana saa nane usiku. Halafu na sisi tumepeana shilingi 30, 40, 50. Kwa uchunguzi wa Kamati, sijui ile Kamati yangu kama iko hapa, hata mmoja; nawashukuru sana; wamefanya hii kazi kwa miezi mitatu, wamekutana na resistance kubwa sana katika ngazi za wilaya. Nilijua kwa sababu kuna ajali za kisiasa, niliwaambia kila wanakofanya mkutano, wahakikishe wana-record kwa siri na kwa dhahiri. Average waliyochukua watu wa cartel ni kati ya shilingi 40 mpaka shilingi 60. Over 20 billion shillings wamegawana hawa watu. Hatuwezi kuruhusu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Mheshimiwa Mulugo, sijui kama yupo; tumezuia mnada wa ufuta uliokuwa ufanyike siku tatu zilizopita huko Songwe. Eti wamekubaliana mnada au debe liwekwe leo halafu lifunguliwe baada ya siku tatu. Nimemwambia Mheshimiwa Chongolo na RAS wake, tumekubaliana TMX inakwenda.

Mheshimiwa Spika, wakulima wa nchi hii siyo wajinga, wanajua bei ikianguka na bei ikipanda. Yule pale Mheshimiwa Kinanasi, yule pale, amepiga kelele kuhusu cocoa kwa muda mrefu. Sauti yake ikabaki ya kwake peke yake. Leo cocoa imefika shilingi 30,000 katika Wilaya ya Tukuyu na Kyela. Cartel ya wizi ya cocoa ilihusisha watumishi wa umma, politician and every leader. Hatuwezi kuruhusu hili. Aidha, ni afadhali tumwambie Mheshimiwa Rais asilete fedha kwenye kilimo na apeleke kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumekwenda naye Kagera tukaenda kufanya mkutano wa kahawa; Waheshimiwa wabunge wa Karagwe na kwingine wako hapa; leo kahawa iliyokuwa inanunuliwa shilingi 700, its almost 3,000 shillings kwenye open market. Tumeenda kufanya nini? Tumeenda kubadili mfumo, tumebadili mfumo. Tatizo siyo mfumo wa ushirika, tatizo lilikuwa ili kiongozi wa ushirika aibe ni lazima Afisa Ushirika wa Wilaya ashiriki kwenye wizi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Katani na wenzake, Serikali iko determined. Tutakwenda ku-confront the big elephant in the house. Nimemwambia Mkurugenzi wa TMX, yuko hapa, yuko ndani ya Bunge hili; Ofisi ya TMX na mfumo wa TMX wanahamishia Mtwara na Lindi. Nimemwambia Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho atoe jengo, tutaweka kompyuta, tutaanza bidding pale openly na tutaanzisha mfumo wa kuweka minimum price. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaanza na ufuta, tunakwenda mbaazi na baadaye tunakwenda kwenye korosho. Wakulima hawa kama bei wanaiona wamekaa hivi, wanaona washindani wanashindana, wana haki ya kukataa bei kwa sababu zao litakaa ghalani, halili wali wala halitaki chai. Tunakwenda ku-confront, najua na tunafahamu kuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili, nimeongelea kuhusu tozo. Cha kwanza, mbele ya Bunge lako Tukufu, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mkurugenzi wa COPRA mwenye mamlaka kwa mujibu wa sheria kusimamia mazao yasiyokuwa na bodi, ameanza kazi. Nataka niseme hivi, mmeona hii kwenye korosho nimetaja zaidi ya shilingi bilioni ngapi, zinazorudi kwa mkulima, Mheshimiwa Rais mwaka jana alivyoruhusu export levy 50 percent irudi. Mwaka huu tumeshakubaliana na Mheshimiwa Mwigulu, yule pale kwamba export levy 100% inarudi kwenye korosho, yote ni hela ya wakulima na Mheshimiwa Rais ameshaidhinisha hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni hivi, halmashauri zinapokea cess halafu kule chini kuna watu wanaitwa watu wa kwenye kata wanamkata tena mkulima shilingi 20 ya kata kila kilo, jumlisheni. Acha hizi nilizozitaja, kuna shilingi 20 tena kila kilo ya kata, shilingi 20 ya wilaya jumla ni 40 na ya mkoa shilingi 10, hivyo jumla hamsini. Ukipiga hesabu kwa tani laki tatu ni 15 billion shillings wanachukua tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halmashauri imeshachukua cess inatosha. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia anapeleka madarasa, maji, umeme na barabara. Kupitia Bunge lako Tukufu na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, yuko hapa, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika yuko hapa na Mkurugenzi Mkuu wa COPRA yuko hapa; ni marufuku kuchukua tozo tofauti na tozo zilizowekwa kwa mujibu wa sheria, marufuku. Ni mwisho kwenye ufuta, mbaazi, korosho kuchukua shilingi 20 ya kata, shilingi 20 ya wilaya na shilingi 10 ya mkoa, hakuna. Tutapunguza shilingi 10 kutoka kwenye Bodi ya Korosho na tutapunguza shilingi 10 kutoka kwenye Bodi ya TARI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge wameongelea Stabilisation Fund, namshukuru Mheshimiwa Rais, tulivyompelekea wazo la kwenda kuanzisha Agricultural Development Fund, akaidhinisha, Agricultural Development Fund tumeipitisha kwenye sheria ya mwaka jana na ina function kubwa tatu: -

(i) Stabilisation;

(ii) Infrastructure Development; na

(iii) Kusaidia mifumo ya Irrigation na Digitalisation.

Mheshimiwa Spika, ilivyoidhinishwa na Mheshimiwa Rais, tukatakiwa tuanzishe vyanzo vya mapato ambavyo tutachukua kutengeneza kwenye Agricultural Development Fund. Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesaini kanuni kama miezi miwili iliyopita. Tunaenda kuanzisha Mfuko wa Kuendeleza Kilimo katika nchi hii, mfuko huu utakuwa na jukumu la stabilisation. Moja ya kazi ya stabilisation ni pale ambapo bei labda zimeanguka katika Soko la Dunia na mkulima anatakiwa kulindwa kutokana na bei hiyo.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wameshauri tutengeneze Mifumo ya Mjengeko wa Bei, tunayo mifumo kwenye tumbaku, tunao mfumo mzuri kwenye pamba, tutaenda kutengeneza kwenye korosho na mazao mengine ili tuwalinde wakulima. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge waturuhusu kama Serikali, watupe nafasi tutakapokuja kusoma bajeti ya mwaka kesho, kutakuwa kuna tengo lililo wazi la Mfuko wa Kuwalinda Wakulima katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeshaweka legal framework, tunatengeneza vyanzo ili mfuko huu uwe sustainable, tunauanza, hiyo safari itatuchukua muda lakini lazima tuijenge na ni jambo la kisera. Nataka niwaambie wakati tunaanza ruzuku ya mbolea, Taasisi za Kimataifa zote zilitupinga zikatuambia it’s not sustainable, leo ukienda Europe wana-subsides wakulima wao. Wanawa-subsides kwenye equipment, wanawa-subsides kwenye inputs wanawa-subsides kwenye price, why not us? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua ya kuwapunguzia wakulima gharama za uzalishaji na hii ni sehemu mojawapo ya stabilisation. Kwa sababu, stabilisation ni aidha uifanye kwenye price ama uifanye kwenye cost of production, Rais kafanya nini? Tumeanza ruzuku ya mbolea hapa, ilikuwa tunaona kama ni jambo gumu, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu naamini zipo changamoto, changamoto haziwezi kwisha, zitakuwepo tu. Tutaendelea kukabiliana na hizi changamoto moja baada ya nyingine ili tuweze kuzipunguza na tuweze kumlinda mkulima kama inavyotakiwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mawazo yao tunayapa thamani na tunayasikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka niseme ni kwenye zao la pamba, Wabunge wameongelea hoja ya mbegu, wameongelea suala la bei ya pamba na kuongeza thamani. Tulivyoanzisha maranja ya korosho tulisema 2026/2027, nchi hii hatutaki ku-export raw cashew nuts, tunataka korosho ibanguliwe. Serikali imepeleka fedha cross to ten billion mwaka huu na tutaendelea kupeleka mpaka tukamilishe ile infrastructure, lakini priority tutawapa local, hakuna dhambi, Serikali kutumia kodi ya nchi yake kumwezesha Private Sector Local wa kwake na Sekta hii ya Kilimo tunafanya, tunaanza maranje na hiyohiyo model tunaipeleka kwenye pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeshachukua hekari 156 ambazo tunazifanya Mkoa wa Simiyu, Serikali inaenda kupeleka umeme, tunapeleka maji, tunapeleka barabara, lakini vilevile tunaenda kujenga shades na kujenga warehouses. Niwaombe Ginners, wao watakuwa priority ya kwanza, nitumie Bunge lako Tukufu hili kuwaambia, yeyote atakayekuja kwenye hicho kituo na kuweka Kiwanda cha Cotton Twine ambazo ni kamba tutakazozitumia kwa ajili ya kufungia zao la tumbaku, tuta-save importation ya seven million dollar, sisi tutampa off taking agreement ya miaka mitano kulinda uwekezaji wake pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe tuache ku-export ma-robot tuanze kuongeza thamani, tumekubaliana na Bodi ya Pamba tunachukua hii hatua na tutaanza kuifanya na tutawekeza.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka niliseme ni kuhusu mazao ya horticultural (ndizi na parachichi). Tumefanya tathmini Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini kuangalia uwezekano wa kulitumia zao la ndizi, Kigoma na Kagera kuweza kuondoa watu kwenye umaskini. Jambo kubwa ambalo tumegundua sisi tumekuwa kila siku tunataja magonjwa mnyauko, sijui nini, tunamfundisha mkulima ng’oa miche, halafu Serikali inachukua hatua gani?

Mheshimiwa Spika, cha kwanza tunajenga maabara mbili kubwa za tissue cultural. Moja tunaiweka Maruku nyingine tunaiweka Kaskazini katika Kituo chetu cha Utafiti cha Arusha na pale ndiyo itakuwa Centre of Excellency kwa ajili ya multiplication ya miche ya ndizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha pili tunachokifanya, tumeamua kuichukua Wilaya ya Rombo, tunaifunga Wilaya ya Rombo, tutang’oa migomba, tutapanda variety moja kwa ajili ya export na tutaweka miundombinu ya umwagiliaji kwa hao wakulima, linawezekana. Tumeshaanza na namshukuru boss wangu wa zamani, Waziri amekubali ku-take the risk ili tuanze hiyo safari ya pamoja ni lazima tuwekeze, matokeo hayawezi kutokea kesho, yatatuchukua tu muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua matamanio ya Watanzania wote, wakulima wa nchi hii na Waheshimiwa Wabunge ni kuona matatizo yote yanaisha leo. Niwaombe patience, hizi hatua tutakwenda nazo polepole, tutatatua tatizo mojamoja na tutavuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni parachichi, parachichi na Horticultural ndiyo Sekta inayokua haraka katika Sekta zote za kilimo. Inakua kwa wastani wa asilimia saba. Tuliwaacha wakulima wameenda. Serikali inafanya nini kuanzia mwaka ujao wa fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha kwanza, tunawapelekea vifaa kwa ajili ya kufanya irrigation kwenye mashamba yao. Tunaenda kuwa-support wale wenye eneo ambalo kuna mito midogomidogo, tutaweka mabwawa madogo, tutawapa pump, tutaweka pipes ili waweze kumwagilia kwenye miti yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha pili tunachokifanya, tunajenga common use facility, ukienda Wilaya ya Rungwe mazao yanapotea, tumeshaanza, tunajenga mbili, moja Iringa nyingine Rungwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha tatu tunachokifanya, namshukuru Waziri Dkt. Mwigulu, tumeenda kuongea na African Development Bank. Tunaweka kitu kinaitwa Agricultural Special Processing Zone (Vituo vya Kuchakata Mazao ya Horticultural) tunaanzia Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini lakini tuna-link na bandari. Tunalalamika hapa kila siku parachichi yetu inasafirishwa na Wakenya, ni kwa sababu bandari zao zina miundombinu. Rais Dkt. Samia katuruhusu, tunachukua dola milioni 100 kuanzia mwaka ujao na sasa hivi tumeshatoa one million dollar kwa ajili ya feasibility study.

Sasa hivi namsubiri kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ndani ya miezi miwili, mitatu atasaini huo mkataba ili hizo fedha tuanze kujenga common use facility ambayo itatumika kwa ajili ya sorting, grading, packing na processing. Halafu tunaweka core chain facility kwenye eneo la Dar es Salaam pale Kurasini. Haya hayawezi kutokea over night yatachukua muda, lakini niwatie moyo wakulima wa parachichi, tumeweka fedha mwaka huu, tunawapa ruzuku ya madawa bure ili waweze kupambana na vidudu vinavyoathiri parachichi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nililotaka niliongelee kidogo katika mkutano wako, nimpe dada yangu Mbunge wa Mbarali uhakika, tukimalizana na Highland Estate, shamba lile ni la wakulima wadogo, tutawagawia wakulima wadogo, tutahakikisha wanapata haki yao wale ambao wanafanyishwa kazi za kuwa vibarua katika ardhi yao, tutahakikisha Mbarali Highland Estate Farm tutakubaliana naye na kumlipa haki zake zote, hatutamdhulumu tutahakikisha linakuwa shamba la wakulima wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, mechanisation, siku zote tumekuwa tukisema wakulima wanunue matrekta, ni mzigo kwa mkulima wa heka moja kumwambia nenda kakope milioni 70 benki kwa riba ya asilimia hizo zinazofahamika halafu alime kwa trekta? Rais Dkt. Samia tulivyoenda India akaagiza tutengeneze mpango wa Serikali kununua jumla ya trekta 10,000 kwa kipindi cha miaka mitano. Tunaanza sasa hivi, mwaka huu tunaanza kujenga mechanisation centre, sisi tunapeleka trekta na vifaa vyote wakulima watakodi pale kwa bei ambayo Serikali itaiweka ya ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaanza na mechanisation centre 10 katika maeneo ya uzalishaji na Mbarali ni mojawapo ambapo tutaweka, kwingine ni Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Ruvuma tutaziweka hizi mechanisation centre. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tutafanya hivi kwa mikoa yote ya uzalishaji kasoro Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge wameongelea issue ya upimaji wa afya ya udongo. Wakisoma Hotuba ya Wizara ya Kilimo tumesema tumeshapima mikoa 17, imebaki mikoa nane. Sasa hivi, kwenye bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya kumalizia mikoa nane, maana yake mikoa yetu 25 ya Tanzania Bara yote itakuwa imepimwa na kupata soil profile ya mikoa yote. Hatua itakayofuata ni kuzalisha ramani za kila mkoa kuonyesha namna ambavyo udongo wake ulivyo.

Mheshimiwa Spika, tumeshachukua hatua sasa hivi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, tumeshaleta vifaa vya kupimia afya ya udongo katika halmashauri 142 na hii ni huduma ya bure. Ombi langu kwao wanapoenda kukaa kwenye Mabaraza ya Madiwani wamuulize Afisa Kilimo na Mkurugenzi mwaka huu umepimia wakulima wangapi, afya ya udongo na kuwapa certificate? Zile certificate zina lugha mbili, Kiswahili na Kiingereza. Inaeleza kuhusu zao unalofaa kulima, mapungufu ya nutrients kwenye eneo lako na unatakiwa utumie virutubisho gani na baada ya hapo kama Serikali tutapiga marufuku aina za mbolea ambazo hazikidhi mahitaji ya udongo wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa ni kuhusu Vituo vya Utafiti na Vituo vya Kufundishia. Hili naomba niliongee polepole wanielewe, ni hivi Mwalimu Nyerere alivyoanzisha Vituo vya Utafiti pembeni alijenga Vituo vya Kufundishia na Mwalimu alijua anaowafundisha ni wakulima, baadaye tulibadili Sera, tukaamua kuvigeuza ni sawasawa na Sokoine University na CBE, tukawa tunasomesha watu Diploma, Certificate, Advance Diploma wanaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara imeamua jukumu la kusomesha Certificate, Diploma, Advance Diploma atabaki nalo kaka yangu Profesa Mkenda. Wizara ya Kilimo, sisi tunaenda kufanya retraining ya Extension Officer walioko kwenye halmashauri, tutawarudisha madarasani mle ndani, tunawa-train kama yeye yuko Kusini anaenda Naliendele, atafundishwa kuhusu korosho, atafundishwa kuhusu mbaazi, atafundishwa kuhusu ufuta na mahitaji ya ikolojia iliyoko Naliendele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, tutaanza kuwafundisha wakulima ili tuwapatie elimu kuhusiana na ikolojia zao na warudi vijijini. Wakulima hawataki kufundishwa mambo makubwa na kizungu kingi, wanataka waambiwe mbegu ya mahindi bora ni hii, unapanda hivi, mbolea unaweka kwenye stage hii, simple language kazi hiyo itafanywa na Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nimalizie tu jambo moja. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tumeanza safari hii ya mabadiliko, tunawekeza kwenye irrigation. Matokeo ya irrigation yanaweza yasitokee kesho yatatokea muda ujao. Naamini mwelekeo tuliochukua kama nchi ni mwelekeo sahihi sana. Hakuna hata siku moja kwenye kilimo mahali popote ambapo matokeo ya kilimo yametokea kwa urahisi ni uwekezaji wa muda mrefu na Serikali hii imechukua hatua hiyo. Wakulima wa mahindi, NFRA anakuja kununua mahindi wasiwe na hofu, tutaanza kununua mahindi siyo muda mrefu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani ni kengele ya mwisho hiyo. Ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, naomba iidhinishiwe kukusanya Maduhuli ya jumla ya shilingi bilioni 10.6 kupitia Fungu 43 na Fungu Na.5. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 7.0 zitakusanywa katika Fungu 43 na shilingi bilioni 3.6 kupitia Fungu Na.5.

Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara ya Kilimo inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 1,248,961,680,000 kupitia Fungu 43, Fungu Na.5 na Fungu 24 kwa mchanganuo ufuatao:-

Mheshimiwa Spika, Fungu 43; shilingi 824,069,158,000, kati ya fedha hizo shilingi 700,318,469,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na shilingi 123,000,750,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo shilingi 69,894,933,000 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 53,000,000,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo ya Wizara, Bodi na Taasisi.

Mheshimiwa Spika, Fungu Na.5; shilingi 403,783,833,000, kati ya fedha hizo shilingi 331,899,223,000 ni fedha za maendeleo na shilingi 71,000,000,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida; kati ya hizo shilingi 64,000,000,000 ni kwa ajili ya OC na shilingi 7,000,000,000 kwa ajili ya payee.

Mheshimiwa Spika, Fungu 24; shilingi 21,108,000,000, kati ya fedha hizo shilingi 20,000,000,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo shilingi 11,954,614,000 ni mishahara ya watumishi na shilingi 8,325,459,000 ni matumizi ya OC. Aidha, fedha za ndani kiasi cha shilingi 828,626,000 zinaombwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)