Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mungu kwa neema na baraka zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nakupongeza wewe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge letu. Naona koti hilo limekaa mahali pake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua mbalimbali inazozichukua ili kuhakikisha kwamba rasilimali zetu zinatumika vyema kuboresha uchumi wa Taifa letu. Kipekee pia naipongeza Kamati yangu ya miundombinu kwa taarifa nzuri yenye maoni yanayokidhi haja ya kuboresha sekta zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imepanga sekta ya bandari ichangie kwenye pato la Taifa kwa kiwango cha asilimia saba ifikapo mwaka 2025/2026. Pia Mamlaka ya Bandari inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuzingatia mpango kabambe wa mamlaka wa mwaka 2020 – 2045.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya miradi hiyo imeelezwa vizuri na mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri, kama vile upanuzi wa gati namba nane mpaka 11. Vilevile ujenzi wa matenki ya kupokea na kuhifadhi mafuta pamoja na ujenzi wa gati namba tatu ya kuhudumia makasha katika Bandari ya Tanga. Utekelezaji wa miradi hiyo yote unahitaji fedha za kutosha, ikizingatiwa kuwa washindani wetu miundombinu waliyonayo au gati walizonazo ni mara mbili ya gati zilizopo Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuzungumza hapa ni kwamba bila ya Mamlaka ya Bandari kuwa na vyanzo vya kutosha vya mapato kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii yote, hakika malengo tuliyojipangia kwa sekta hii ya bandari ya kuchangia asilimia saba katika pato la Taifa haiwezi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, popote pale duniani, mapato yatokanayo na wharfage ambayo ni mapato yanayotokana na mtumiaji wa meli katika kutumia miundombinu ya bandari, duniani kote fedha hizi zinatengwa kwa ajili ya kuboresha na kujenga miundombinu ya bandari. Vivyo hivyo nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Bandari Namba 17 ya Mwaka 2004 imekitaja chanzo hiki cha mapato (wharfage) kwamba ni chanzo cha mapato cha Mamlaka ya Bandari chenye lengo la kuboresha miundombinu ya bandari zetu. Kwa mujibu wa tamko lililotolewa mwezi wa Agosti, 2017, bandari ilisitisha kukusanya mapato yale. Kwa mujibu wa sheria ambayo ilikuja kuundwa mwaka 2019 Sheria Na. 7, iliipa Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya fedha zile zinazotokana na wharfage na kuziweka katika akaunti maalumu iliyoko BOT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi kwa mujibu wa taarifa zilizopo, hazitumiki ipasavyo kwa uhitaji tulionao wa kuboresha miundombnu yetu, na ikizingatiwa kwamba tayari gati zilizokuwa zimekamilika sasa hivi zinatumika na DP World, ina maana Mamlaka ya Bandari Tanzania inahitaji kuongeza gati nyingine zaidi kwa ajili ya ufanisi na kuongeza shehena kwa ajili ya mustakabali mpana wa sekta ya Bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za wharfage ni almost 50% ya mapato yote ya Mamlaka ya Bandari Tanzania. Kwa sasa hivi bandari inatumia asilimia 50 ya mapato mengine yatokanayo na bandari ili kuendeleza miundombinu mbalimbali pamoja na kuiendesha Mamlaka ya Bandari Tanzania, fedha ambazo zimekuwa chache na hazitoshi kutimiza amza ya Serikali ya kuchangia katika pato la Taifa kwa takribani asilimia saba ifikapo mwaka 2025/2026. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa fedha hizi zimewekwa kwa mujibu wa sheria, kwamba ni mapato ya bandari kwa lengo la kuendeleza miundombinu yetu ya bandari, nasi sote ni mashahidi kwamba tunahitaji sekta ya bandari ifikie malengo yake ili nchi yetu iweze kunufaika na advantage ya kijiografia kwa kuwa na miundombinu bora ya bandari na meli kubwa ziweze kufika katika bandari zetu. Kwa hiyo, suala la kuboresha miundombinu ya bandari ni suala ambalo haliepukiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba, nami ninashawishika, na ninaungana na maoni ya Kamati yangu, Kamati ya Miundombinu kubadilishwa kwa sheria ya Mamlaka ya Bandari Tanzania ili kuiwezesha Mamlaka ya Bandari Nchini kuweza kukusanya mapato yale yatokanayo na wharfage ili iweze kuboresha miundombinu ya bandari zetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba mapato haya yatokanayo na wharfage, kabla ya kupelekwa kule BOT yanaingia kwanza kwenye akaunti fulani za biashara halafu ndipo yanapelekwa kule BOT. Kwa taarifa zilizopo ni kwamba fedha hizi zinaanza kutumiwa na TRA kabla hazijafika kule kwenye akaunti maalumu iliyowekwa. Maana yake ni kwamba inakwenda kinyume na taratibu zilizowekwa kwa matumizi ya fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile utakuta fedha hizi labda zimekusanywa shilingi bilioni 500, lakini kabla hazijaingia kwenye akaunti iliyopangwa iliyoko BOT, fedha zile zinapunguzwa na utakuta zinaingizwa kwenye kiwango ambacho siyo halisi katika makusanyo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashawishika kuishauri Serikali kuhakikisha kwamba sheria inabadilishwa na Mamlaka ya Bandari inakusanya fedha hizi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ili kuboresha miundombinu ya bandari zetu nchini na ili kuongeza shehena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo naomba nizungumzie kuhusu passenger service charge ambayo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa ICAO (International Civil Aviation Authority) inazitaka mamlaka zote za viwanja vya ndege kuwa na chanzo cha mapato, na passenger service charge ni miongoni mwa chanzo cha mapato ambapo tunalipia shilingi 10,000/= tunaposafiri ndani ya nchi na dola 40 tunaposafiri nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, chanzo hiki cha mapato kilibadilishwa kwa mujibu wa sheria na kinakusanywa na TRA, na kwamba mamlaka inayohusika na viwanja vya ndege mpaka iombe TRA. Tumeona hali halisi ya viwanja vyetu vya ndege nchini kuwa haikidhi haja kuendana na kasi ya ongezeko la watalii wetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawiwa kuishauri Serikali kuhakikisha kwamba kwa kuwa sheria zinabadilishwa, passenger service charge irudishwe na kukusanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania. Vivyo hivyo pamoja na wharfage, sheria ibadilishwe ili iweze kukusanywa na Mamlaka ya Bandari Tanzania ili kufikia azma ya Serikali ya kuchangia kwenye pato la Taifa asilimia saba na vilevile kuongeza shehena na kwenda na kasi ya ufanisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)