Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kuhusu bajeti Wizara yetu ya Uchukuzi. Kipekee nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya kwenye Taifa letu. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana ikiwemo kuhakikisha kwamba majimbo yetu yanaendelea kupata fedha pamoja na kuzisimamia Wizara zetu tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Waziri wa Uchukuzi pamoja na Naibu Waziri na Watendaji wake wote pamoja na Wakurugenzi mbalimbali wa taasisi zetu zote za Wizara ya Uchukuzi. Pia nakupongeza wewe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Tunaona unafanya kazi nzuri na uko smart. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, nataka nichangie maeneo machache sana, kama maeneo mawili tu. Eneo la kwanza ni eneo ambalo pia dada yangu Mheshimiwa Mwanaisha hapa amejaribu kuchangia. Pia nitachangia sehemu ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa na katika taarifa ya Kamati imesemwa sana, wakati Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Miundombinu anahitimisha, amezungumza juu ya tozo ya wharfage ambayo inakusanywa na TRA. Labda tutafute kwanza nini maana ya tozo ya Wharfage. Tozo hii ni tozo inayotozwa kwa mizigo pale bandarini kwa ajili ya uendeshaji na kuboresha bandari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo hii ninajua mwaka 2017 ilibadilishwa kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati, na kukusanywa na TRA. Najua wazi kwamba enzi hizo mifumo ya bandari haikuwa mizuri na ndiyo maana ilisababisha kubadilisha na badala ya kukusanywa na TPA, basi ikaanza kukusanywa na TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uteuzi makini wa Mkurugenzi wa TPA, kaka yangu Mbossa. Ni Mkurugenzi makini, ni mchapakazi. Nina imani kubwa kwamba atakwenda kusimamia vizuri haya ambayo tunayazungumza. Kwa uteuzi huo unanishawishi sasa kuishauri Serikali kurudisha tozo hii iendelee kukusanywa na TPA ili ifanye kazi ambazo zimekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwanaisha ametuambua hapa kwamba fedha hizi hazitumiki zote kama ilivyokusudiwa, kwamba kwenda kutumika katika uendelezaji wa bandari zetu. Tunaomba sasa, kama Mwenyekiti wa Kamati alivyoshauri, fedha hizi sasa watu wa Uchukuzi wakae na Waziri wa Fedha, wakae na watu wa Fedha ili wakubaliane kwamba fedha hizi zirudi zianze kukusanywa na watu wa TPA ili waweze kuendeleza bandari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuona makusanyo yanaongezeka, tunahitaji kuona Bandari ya Mwanza, Mtwara pamoja Tanga zikitengenezwa; na pia tunahitaji kuona gati zinaongezeka. Kwa nini? Inawezekana sasa hivi tunasema mizigo ni michache, ni kwa sababu tunakalisha meli muda mrefu, kwa sababu hatuna gati nyingi za kutosha kuweza kushusha mizigo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu wanaona bora waende Mombasa au sehemu nyingine kushusha mizigo yao kwa sababu ya uharaka, lakini tukiwa na magati mengi tutaenda kushusha mizigo kwa wakati na zaidi tutaenda kufanya pato la TPA liongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo TPA peke yake, kuna uhusiano mkubwa kati ya wingi wa mizigo itakayoshushwa pale TPA na makusanyo ya TRA, kwa sababu kama mizigo mingi itashushwa TPA, na kama mizigo mingi itapitia bandari yetu ya Dar es Salaam na bandari nyingine maana yake sasa TRA na wenyewe wanaenda kupata fedha nyingi watakazokusanya kulingana na mizigo utakayoenda kuipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni wakati sasa wa kuendelea kutafakari ili tuwasaidie hawa watu wa bandari tuwarudishie hizi fedha waweze kufanya ukarabati, waweze kutafuta wakandarasi, waweze kuboresha miundombinu ya bandari ikiwemo gati namba 12 mpaka 15, imesemwa hapa, kina cha gati namba nane mpaka namba 11, Bandari ya Mwanza, Bandari ya Mtwara kama nilivyosema, na maziwa makuu yakiwemo Nyasa pamoja na ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia advantage nyingine itakayo patikana maeneo haya baada ya fedha hizi kukusanywa na bandari yetu kwa maana ya TPA, watakapokusanya fedha hizi advantage watakapoingia mikataba ya uendelezaji wa bandari kwa maana ya wakandarasi watawalipa kwa wakati. Wakiwalipa kwa wakati, mantiki yetu sasa tunaenda ku-solve tatizo ambalo tumeendelea kuwa nalo la kulipa interest kwa wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sasa hivi tunalipa interest kubwa kwa wakandarasi kwa kucheleweshewa malipo kwa sababu ya mlolongo mrefu, kwa sababu ya fedha kuwa kidogo ambazo zinatokana na bandari, lakini sasa hivi tukiwaruhusu wakusanye, watumie vizuri tuwape target. Kazi yetu Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi ni kuwapa target hawa watu wa bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapeni target za nini kifanyike katika mwaka husika ili waweze kutimiza yale malengo, nasi tuwahoji baada ya muda husika ambao tutakuwa tumejipangia kuwahoji sasa, kwamba tulikubaliana hii fedha tumewapatia, mmekusanya ninyi wenyewe, tulikubaliana mjenge gati namba 12 mpaka 15, tulikubaliana mwendeleze Mwanza bado hamjaendeleza, tupeni sababu. Kwa sasa hivi hatutawahoji kwa sababu namna wanavyopata fedha, wanapata kidogo ikilinganishwa na uhalisia wa zile fedha za tozo ya wharfage zinavyokusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nishawishike sana kuishauri Wizara ya Fedha, kuishauri Wizara ya Uchukuzi sasa mkubaliane mapato haya sasa yaanze kukusanywa na TPA ili sasa TPA waweze kufanya kazi kubwa, ikizingatiwa kwamba sasa hivi mapato ya wharfage yalikuwa asilimia 50, yamesemwa kwenye taarifa na yote sasa yanakusanywa na TRA. Yale makusanyo ambayo yalikuwa yanakusanywa na TPA yalikuwa yanakusanywa asilimia 50 na sasa tayari DP World ameshaingia kwenye uwekezaji, anakusanya zaidi ya asilimia 35. Sasa TPA wanabakiwa na asilimia 15 ambazo hazitoshi kwenye kuendeleza bandari, hazitoshi kutengeneza miundombinu ya bandari ikiwemo hata na mawasiliano ya TRC pamoja na bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani sasa ile mizigo ikishashushwa iingie moja kwa moja kwenye treni ili iweze kusafirishwa. Bwana Kadogosa yupo hapa najua, watakuwa na mawasiliano ya karibu na watu wa bandari ili miundombinu ya reli iwasiliane pale bandarini iwe ni kushusha na kuweka kwenye treni na kusafirisha. Tutapata mapato aina mbili; tutapata mapato ya TPA na pia tutapata mapato ya reli na kusababisha nchi yetu kuendelea kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nichangie ni ujenzi wa uwanja wa ndege pale Simiyu. Tumeshaachia eneo na wananchi tayari wameshapisha eneo la ujenzi, lakini mpaka sasa tunavyozungumza bado hawajalipwa fidia. Tunaomba sasa mweke kwenye mpango wa kulipa fidia wananchi ambao wamepisha maeneo yao kwa muda mrefu kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege pale Bariadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa waweke kwenye mpango, tunatamani kuona ujenzi wa kiwanja cha ndege pale Simiyu unaanza mara moja. Advantage yake ni nini? Watalii watashuka pale Bariadi, na uchumi wa Bariadi utaongezeka, Simiyu kwa ujumla uchumi utaongezeka na pia pale Lamadi kwangu uchumi utaongezeka kwa sababu watalii watapita pale kuelekea lango la Serengeti na wananchi watazidi kupata kipato. Kwa hiyo, tunaomba sana iwekwe kwenye mpango ili tuweze kuwa na uwanja wa ndege pale Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba sasa Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi pamoja na Mkurugenzi wa ATCL nimemwona hapa, Bwana Matindi, ni aibu leo tunazungumza eti hakuna ndege ya kutoka Dodoma kwenda Mwanza. Haiwezekani! Hatuna ndege ya kutoka Mwanza kuja Dodoma! Hiyo ni aibu bwana. Tunatamani kuona tunapata ndege ya kutoka Mwanza kuja hapa Dodoma, tunatamani kuona ndege ya kutoka Dodoma kwenda Mwanza, hata kama ni siku tatu kwa wiki zinatosha. (Makofi)

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWEMYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Fyandomo.

TAARIFA

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nataka kutoa taarifa kwa mchangiaji kwamba hata Mbeya tunahitaji ndege ya kutoka Mbeya - Dodoma, Dodoma - Mbeya kulingana na watu walivyo wengi wanaotokea Mbeya wanazunguka mpaka wafike Dar es Salaam na ndege ndiyo warudi Dodoma. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Simon, unaipokea taarifa?

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Niongeze, na kutoka Dodoma kwenda Kilimanjaro. Kwa hiyo, haya maeneo ni ya kimkakati, Mkurugenzi Matindi naomba uyachukue haya. Natamani kuona wiki ijayo tunapata ndege kutoka Dodoma kwenda Mwanza, Dodoma kwenda Kilimanjaro, Dodoma kwenda Mbeya kama ilivyokwisha kusemwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)