Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia kwenye bajeti muhimu sana, bajeti ambayo ndiyo moyo wa uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja hii. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayofanya ya kusukuma fedha nyingi kwenda kwenye miradi mbalimbali hasa katika sekta hii ya uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu utajikita sana kwenye uwekezaji kwenye sekta ya uchukuzi. Naendelea kutoa pongezi kabla sijasema hoja yangu kwa Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa na Naibu Waziri na Menejimenti nzima ya Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa kweli mimi nipo Kamati ya Uwekezaji. Tumetembelea miradi mingi, tumeona kazi kubwa inayofanyika. Katika ziara hiyo pia tumepata fursa ya kujifunza mambo mengi ambayo yanafanyika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli uwekezaji uliyofanyika, nitaanza kwenye Sekta ya Bandari, tulipata fursa ya kutembelea Bandari ya Tanga, Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Mtwara. Serikali imewekeza fedha nyingi takribani shilingi trilioni 1.4 ambazo sisi kama Kamati ya Uwekezaji, na niendelee pia kuunga mkono hoja ya Kamati ya Miundombinu, wameeleza mambo ambayo yanashabihiana na yale sisi tuliyoyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala ambalo limefanyika kwenye Bandari ya Tanga, Dar es salaam na pale Mtwara limeleta impact gani katika pato la Taifa? Kupitia uwekezaji huu, umesababisha mabadiliko makubwa. TRA walikuwa wanapokea shilingi trilioni saba, zimepanda kufika shilingi trilioni tisa ambayo ni sawa na ongezeko la 42%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuliona uwekezaji huu umeleta tija kwa kiasi fulani, lakini tumeona shehena na alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, shehena imeongezeka kutoka asilimia hiyo 11.2 imeenda mpaka kufika shehena ya tani milioni 20. Ni achievement kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia makasha yaliyokuwa yanakusanywa mwaka ule uliyotangulia na mwaka huu yameongezeka kutoka 600,000 na sasa wanakimbilia makasha ya makontena 800,000. Huu ni uwekezaji wa shilingi trilioni 1.3 uliyofanyika katika bandari zetu zote hizi tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ninachotaka kusema? Kuna dhana imezungumzwa na Kamati ya Miundombinu, lakini kuna dhana imezungumzwa pia na wachangiaji walionitangulia juu ya hii tozo ya wharfage. Mimi na Kamati yangu tulipita tukaliangalia kwa upana wake kama Taifa tunatakiwa concentration yetu iwe wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, concertation ni kuangalia ile cash curve, ile sekta inayotuzalishia fedha nyingi kuliko kui-paralyse. Kwa mfano, tuliona kwamba kuondolewa kwa hii wharfage kuchukuliwa na TRA, kunaenda ku-paralyse uboreshaji wa bandari zetu na hii mileage iliyotoka kwenye shilingi trilioni saba kuja kwenye shilingi trilioni tisa, achievement yake hatutaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niungane na Wabunge wenzangu na Kamati katika hoja yao hii. Kuna haja sasa ya Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Fedha warudishe hizi fedha ziendelee kwa utaratibu ule ule wa zamani, tuje tu-amend hapa sheria ili sasa tuweze kupata mapato ambayo TPA itachangia kwenye mapato ya Mfuko Mkuu wa Hazina, kupitia TRA na mapato yakue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlivyopeleka pale mmetoa room; TRA inaendeshwa na Sheria ya Kodi, ikitokea kuna mtu yeyote anasema nina madai nadaiwa, au nawadai TPA na hiyo ni tax liability, TRA hawachelewi, wanaikata hiyo wharfage, wanamalizana, mtajuana huko. Kwa hiyo, hii pesa badala ya kwenda ku-invest, na kutuletea fedha zaidi, inaishia sasa huku TRA ambapo inaweza ikatumiwa vile ambavyo sivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, kaeni na Wizara ya Fedha mrudishe hii wharfage, tukaboreshe miundombinu yetu ya bandari. Leo Kisiwa Mgao pale tunaenda kujenga bandari ya kupokea tani 100,000 za makaa ya mawe pamoja na cement inayozalishwa kule Mtwara; lakini pale pomba la EACOP linaenda kuanza hivi karibuni ambapo kwanza tu katika hatua za awali TRA ilikusanya shilingi bilioni 30 kupitia bomba la EACOP, tena katika mobilization stage.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini mradi huu ukikamilika utaweza kuleta pato kubwa sana. Sasa TPA itafanyeje kazi yake kama tunai-cripple? Kwa hiyo, ni high time sasa tuanze kufikiria kiuwekezaji zaidi, tusiwe tunatamani zile fedha ambazo tunaziona, tukawekeze ili ile return on investment iweze kuleta tija katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo hayo hayo yanazungumzwa kwenye mamlaka ya viwanja vya ndege. Haiwezekani Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, nitawapa mfano, terminal three ile ilijengwa kwa fedha takribani shilingi bilioni 560, lakini kwa collection inayofanyika pale, return on investment ya hiyo fedha shilingi bilioni 560 ni ndani ya miaka nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna uwekezaji mkubwa ambao unaweza ukalipwa ndani ya miaka nane. Maana yake ni nini? Tukiwarudishia hiyo forty percent kama Kamati ilivyopendekeza, hii itaenda kuwapa nguvu na TRA watakusanya sana. Kwa hiyo, tusiwe waoga, ile sheria tulikuwa na hofu kwamba hawana uwezo, sasa hivi naamini mkiwarudishia iwe power wataenda ku-invest.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo terminal two ile tulijenga mwaka 1984 imekuwa ya kizamani, ATCL inatakiwa kuwa na hub yake ambayo tukiwapa terminal two tutapata wageni wengi. Watapita pale kwa sababu facility zetu zitakuwa nzuri, tutaongeza mapato zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naombe Mheshimiwa Prof. Mbarawa, sisi tunafanya kazi pamoja na nashukuru Waziri wangu wa Uwekezaji na Mipango yupo hapa; kama Taifa lazima tuwe na integrated planning. Leo hii nitawapa mfano tumewekeza shilingi bilioni 421 kujenga Bandari ya Tanga, lakini Bandari ya Tanga itakuwa underutilized tu, kwa sababu hakuna miundombinu inayounganisha na nchi jirani kama Burundi na Rwanda ambapo ndipo mizigo mingi inahitaji kutumia Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umbali wa kutoka Bandari ya Mtwara kwenda kufikia nchi zile ni less than kilometa 300 ukitoka Dar es Salaam kwenda Burundi na Rwanda. Kwa hiyo, wapo interested na kutumia Bandari ya Tanga na itakuwa more effective na tutawazidi competitors wetu ambao ni nchi jirani kama tutawekeza kwenye miundombinu ya Barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kutoka Tanga - Sengera inatakiwa iwe kipaumbele, lakini ile barabara ya kutoka Handeni kilometa 433, Handeni - Kiberashi kupitia Kiteto - Kondoa kilometa 433 zitawafanya na kuwavutia nchi jirani kama Burundi na Rwanda watumie Bandari ile ya Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga bandari ndogo pale, tumetangaza tender ya tani 100,000 ya makaa ya mawe, lakini kubeba makaa ya mawe kupitisha pale Kisiwa Mgao ni changamoto. Leo hii mmejenga Bandari ya Kalema, ile shilingi bilioni 47 hakuna barabara inayounganisha kuja kufika Mpanda, Bandari ya Kabwe mmeweka shilingi bilioni saba, pale hamna miundombinu ambayo inaunganisha. Kwa hiyo, ile imekuwa kama white elephant. Tumewekeza mabilioni ya fedha, lakini itabaki kuwa white elephant. Tutakuwa tumeweka fedha nyingi kwa kuwa hatuna integrated planning katika mipango yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sasa namshauri Mheshimiwa Waziri wa Mipango, mje, tuko pale Lagosa tumewekeza shilingi bilioni 15, miundombinu ya kuunganisha ili bandari ile iwe-effective, ifanye kazi na ili return on investment tuliyoiweka pale tuione hamna! Sisi kama watu wa uwekezaji tuliona jambo hili tuishauli Serikali mkae pamoja, kuna vipaumbele ambavyo mki-invest, return on investment itakuwa ndani ya muda mfupi, tutasonga mbele kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia leo hii nitaongea kuhusu Bandari ya Kasanga, Bandari ya Kalema, na Bandari ya Kabwe kwamba hamna meli. Mheshimiwa Profesa Mbarawa ni ndugu yangu, nakuheshimu sana na ni mtu unachapa kazi, lakini leo hii jioni kwenye mafungu ya shilingi tutapambana kuhusu meli katika Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyopita mlikuja na habari ya kutuletea meli ziwa Tanganyika. Kwenye meli hizo tulisema walau mbili ziamke; meli ile ya Mwongozo na Liemba, hizo imekuwa ni hadithi, na leo hapa nimeona unasoma. Sasa tunataka leo utuambie. Hizo meli kwenye ziwa hilo zina-impact kwa mikoa mitatu; Kigoma, Katavi na Rukwa, lakini sisi tunapakana na nchi tatu kule ambazo tuki-trade nazo tutapata faida za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapakana na Burundi, DRC Congo na Zambia, na wote wana potential ya market kwenye biashara. Kila bidhaa tunayouza upande wetu wa mikoa hii tukiwa na usafiri upande wa pili tutapata faida za kiuchumi. Kwanza tutainua uchumi wa watu wetu, lakini siyo kuinua tu uchumi wa watu wetu, Tanzania kama nchi itapata pato kubwa la kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika bajeti hii mambo ambayo hatutavumilia ni juu ya meli Ziwa Tanganyika. Jana tulivyokutana mahali, nilimwambia Mheshimiwa Waziri, na leo hii kwa kweli hili jambo tunakuja na msisitizo wake, tunataka lifike mwisho ili tukirudi, wananchi wasiseme mmezoea kuja kutuambia uwongo, kwamba meli inaanza mwaka huu, lakini mwaka unapita unakuja mwaka mwingine na unafuata mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Prof. Mbarawa anapokuja kuhitimisha aje na commitment ambayo itatu-convince Wabunge wa mikoa hii mitatu juu ya kurekebisha meli katika Ziwa Tanganyika, meli ya Liemba pamoja na meli ya Mwongozo wakati tukiendelea na mipango mingine mliyonayo kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)