Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema ambaye ametupa zawadi hii ya uhai na uzima kuweza kusimama leo hapa katika kuendeleza majukumu yetu haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya kulitumikia Taifa letu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalendo wa Dkt. Mama Samia, uchapaji kazi wake, utu wake unaonesha nia yake thabiti kabisa katika kuwatendea haki Watanzania na kuleta maendele makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa, Waziri wa Uchukuzi kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya yeye na timu yake, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yao yote kwa utendaji mkubwa kuendelea kusimamia miradi mikubwa katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ambayo inasimwamiwa na Wizara hii ni mikubwa na ya kimkakati, ambayo inagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania hasa wa chini. Ukiangalia mradi wa SGR, ukiangalia mradi wa utengenezaji na uundaji wa meli na vivuko mbalimbali, ukiangalia mradi wa ufungaji na ununuzi wa rada mbalimbali, miradi hii yote na mingine ambayo sijaitaja ni miradi mikubwa ambayo inakwenda kugusa maisha ya Watanzania mmoja mmoja, hususan maisha ya Watanzania wa kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia, Taifa hili pamoja na dunia sasa hivi inavyoendelea, Mamlaka za Hali ya Hewa nchini pamoja na dunia kwa ujumla ni mamlaka ambazo zinafanya kazi nzuri sana. Tunaona mabadiliko mbalimbali ya hali ya hewa ambayo majanga yameendelea kuja katika maeneo mbalimbali ya dunia, lakini tunaona mvua kubwa, na upepo mkali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ya kuwepo mamlaka kama hii ya hali ya hewa kuweza kutoa tabiri za kila siku, tabiri za siku kumi kumi na tabiri za misimu, kuweza kuonesha ni kitu gani kinatokea, kitu gani kitakuja kwenye masuala haya ya hali ya hewa, ni dhahiri kwamba na tunakubaliana kwamba kwa kweli maisha ya watu na mali zao yanaweza kuwa hatarini, lakini kwa sababu ya uwepo wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini na kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya, tunaona kwamba mali za wananchi zinaokolewa na maisha ya wananchi kwa kiasi kikubwa sana wanajitahidi katika kuokoa mamlaka hii ya hali ya hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza kuhakikisha kwamba huduma hizi za hali ya hewa zinaendelea kuimarika ni lazima kuwepo na mikakati madhubuti kuhakikisha kwamba mamlaka hii inakuwa sustainable na huduma zake zinapatikana kila siku na zinakuwa endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma hizi za hali ya hewa haziwezi kuwa endelevu na haziwezi kuwa sustainable kama hakuna fedha za uendeshaji mamlaka hii. Tulipitisha hapa kwenye Bunge la Kumi na Moja, Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa, lakini Sheria ile imeunda kanuni mbalimbali ikiwemo Kanuni ya Cost Recovery ya huduma ambazo Mamlaka ya Hali ya Hewa inazitoa, lakini hadi leo Kanuni hizi za Cost Recovery bado hazijapitishwa rasmi na kuweza kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wadau wengi ambao wanahitaji kutumia huduma hizi za hali ya hewa, lakini pia kama watahamasishwa naamini kwamba, wanaweza kulipia huduma hizi ambazo wanazitumia na kuifanya mamlaka yetu hii kuimarika na kutoa huduma bora zaidi. Bado hadi leo Kanuni hizi za Cost Recovery za Mamlaka ya Hali ya Hewa, hazijapitishwa rasmi kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba, utendaji wa Wizara hii kwenye jambo hili ni wa upande mmoja na upande mwingine ni Wizara ya Fedha, lakini tunatambua kwamba, Serikali ni moja na wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, jambo hili alisukume, aende akasimamie pale kwa Waziri wa Fedha, ili liweze kufikia kikomo, mamlaka hii iweze kujiendesha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Chuo cha Hali ya Hewa pale Kigoma. Kila siku tunazungumza namna ya kuboresha chuo hiki ili kiweze kutoa huduma hasa kwa nchi ambazo zimetuzunguka. Huduma hizi za hali ya hewa ama taaluma hii nchi nyingi hawana, lakini sisi nchi yetu tunatoa taaluma kupitia Chuo kile cha Kigoma na UDSM. Bado huduma zinazotolewa pale zipo chini kabisa, hazina ubora na ndio maana nchi nyingi ambazo zimetuzunguka hawapendi kutumia kile chuo chetu kwa sababu, bado huduma ni duni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipata fedha hizi na Serikali ikawekeza zaidi pale kwenye Chuo cha Hali ya Hewa ni hakika kwamba, chuo kile kitapata wanafunzi wengi kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambazo zinatuzunguka na kutoka duniani kwa ujumla kwa sababu, sasa hivi Mamlaka yetu ya Hali ya Hewa inaendelea kujitangaza na imeendelea kuaminika kidunia. Ndio maana Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Dunia kwenye lile Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na hali ya hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi hii hakupewa tu kwa sababu, iligombaniwa na wagombea wengine kutoka nchi mbalimbali na tuliweza kuzishinda nchi kubwa ikiwemo Afrika Kusini, Urusi, Seychelles na nyinginezo. Hii ni kwa sababu, tayari Taifa letu linaaminika, mamlaka yetu inaaminika kwa huduma pamoja na kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie hizi Kanuni za Cost Recovery ni lini zitaweza kukamilishwa? Pia, ni upi mpango madhubuti ambao upo wa kuweza kukiboresha Chuo chetu cha Hali ya Hewa Tanzania ambacho kipo Kigoma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la ATCL. Tunaipongeza sana ATCL, inafanya kazi nzuri katika kulitumikia Taifa letu. Tunatambua kwamba, kuna vituo vimeongezeka na tangu mwaka juzi tumekuwa tunasikia mara nyingi tu hadithi na ahadi za kwamba, ndege za ATCL zitafika katika Uwanja wa Ndege wa Pemba na lakini hadi leo hii tunasikia matangazo mbalimbali yanatolewa, lakini hatujui ratiba hasa ya ndege hii kufika Pemba ni lini itaanza? Mwaka jana tuliahidiwa Mwezi Agosti itaanza, Mwezi Agosti umepita. Mwaka huu pia tumeahidiwa, lakini hadi leo hatujui ratiba ya ndege hii ya ATCL kufika pemba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba, kufika kwa ndege kule Pemba kutanyanyua uchumi wa watu wa Pemba, kutainua uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na pia, itaboresha huduma za ATCL. Tunaomba sana na tunatamani sana ndege hii iweze kufika Pemba kutoa huduma mbalimbali ambazo zinapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo natamani kulizungumza, ikiwemo huduma ya meli katika ukanda wetu wa pwani. Sisi watu wa pwani uchumi wetu zaidi unategemea Bahari. Bila kuwa na usafiri wa meli zitakazoweza kuhudumia maeneo ya ukanda wote wa pwani, Pemba, Unguja, Lindi, Mtwara na Tanga kwa kweli, uchumi wetu utaendelea kudumaa. Ukituwekea meli ambayo itaweza kutoa huduma, basi itachangamsha na pia, itaongeza uchumi wa maeneo haya ambayo nimeyataja, hususani ukanda wetu wa pwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)