Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kulingana na dakika ambazo umeniambia, umeni-pressurize kidogo. Sasa Nitajikita kwenye eneo moja la usafiri wa Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Wizara kwa kutusoma mikoa mitatu kwenye vitabu kwa miaka nane mfululizo, juu ya usafiri wa Ziwa Tanganyika. Wakati tunazungumza kuhusu Ziwa Tanganyika wote tunajua kwamba, bidhaa zinazokwenda Congo zaidi ya 60% zinatoka Tanzania. Wakati tunazungumza kuhusu Ziwa Tanganyika sote tunajua Serikali imewekeza kwenye Bandari za Kigoma, Karema, Kabwe, Kipili pamoja na Kasanga. Tumewekeza kwenye bandari hizo fedha za Serikali halafu hatuna meli ya kusafirishia mizigo. Ukikaa unafikiri, kama Waziri wa Mipango yupo, Waziri wa Uchukuzi yupo na Waziri wa Fedha yupo, shida ipo wapi katika mipango yetu kwenye nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Waziri aliji-commit hapa akasema kuna mipango ya muda mrefu na mipango ya muda mfupi. Mpango wa muda mfupi alituambia ni kukarabati meli mbili, Meli ya Mv Liemba na Mv Mwongozo, lakini mpaka leo tunapozungumza huo mpango wa muda mfupi hakuna meli ambayo inatembea. Meli mpya bado na zinazohitaji ukarabati nazo bado, tunataka Serikali ikija hapa itueleze inatuwazia nini sisi watu wa mikoa mitatu ambayo tupo kwenye Ziwa Tanganyika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inajua tunapoteza ndugu zetu kila siku kwa sababu ya usafiri ambao siyo rasmi wa Ziwa Tanganyika. Kama tunaamini Ziwa Tanganyika linaweza kusaidia uchumi wa nchi hii, ni nini kimeshindikana kuwekeza kwenye usafiri wa Ziwa Tanganyika? Kama tumewekeza kwenye bandari ni nini ambacho kinasababisha kigugumizi kuweza kupata usafiri wa Ziwa Tanganyika? Naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri mambo mawili kwa sababu, ni dakika tano; cha kwanza, waliopata nafasi ya kumshauri Mheshimiwa Rais, basi wamshauri vyema kuhusu uchumi ambao tunaweza kuupata kupitia Ziwa Tanganyika. Naamini kama amekubali kutoa fedha kuwekeza kwenye bandari, hawezi kukataa kutoa fedha kwa ajili ya usafiri wa Ziwa Tanganyika, yaani haya mambo yanakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumza hapa, kama ukarabati umechukua zaidi ya miaka nane, meli mpya itachukua miaka mingapi? Hili jambo kama Watanzania tunaotoka kwenye hii mikoa mitatu halikubaliki. Naomba Mheshimiwa Waziri, tunaona jitihada ambazo anazionesha kwenye kutusoma kwenye vitabu, leo tunataka tusikie jibu lake kuhusu Mv Liemba na Mv Mwongozo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia njema aliyotuambia ya kutengeneza kiwanda kwa ajili ya meli, tumemsikia na tumeona ameandika, tunataka tuone utekelezaji wa hilo jambo na kwa sababu, hilo jambo ni la muda mrefu, basi tuone la muda mfupi linafanyikaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliposema hapa mwaka jana, niliondoka nikaenda kuwaambia wananchi mpigieni makofi Mheshimiwa Rais tunapata meli sasa, wakapiga makofi. Sasa Waziri aje yeye mwenyewe afute haya maneno kwa sababu, yeye ndiye alisema hapa na nikaamini maneno yake. Sasa wananchi wa hayo maeneo tunataka kujua, yaani sisi kila siku ni wa kusomwa tu kwenye vitabu au inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo linahitaji dhamira tu, kwa nini maeneo mengine meli zipo? Ikiwa wanajua kabisa faida za hili Ziwa Tanganyika, kila siku tunaimba wimbo, ninapozungumza sasa ni miaka nane, kama ni dhamira basi tungeiona hata kwenye kutengeneza zilizopo. Mv Liemba mpaka leo imechukua miaka nane na vifo vingine sasa hivi wanaripoti, lakini vingine hawaripoti. Tumechoka kupoteza ndugu zetu kwa sababu ya kukosa dhamira ya dhati kwenye uwekezaji wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge ambao tunasema tutaondoka na shilingi ya Mheshimiwa Waziri asipotupatia jibu la kueleweka juu ya usafiri wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kidogo kwenye suala la TPA. Pamoja na uwekezaji ambao nauzungumza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa dakika zako zimeisha, tafadhali hitimisha.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.