Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Hotuba ya Wizara yetu ya Uchukuzi. Nami naanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli kwa kuona umuhimu wa Sekta ya Uchukuzi na kuitenganisha na Wizara ya Ujenzi. Hebu fikiria sasa mambo yote haya tunayoyajadili kama yangekuwa kwenye Wizara moja ingekuwa namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuja leo mbele yetu anaomba karibu shilingi 2,700,000,000,000 ili aweze kwenda kutekeleza kwa kiasi kikubwa uwekezaji mkubwa ambao ukiangalia sekta ambazo anazisimamia na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, utaona wazi kwamba ndiyo zinashika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchukuzi; sisi katika Kamati ya Miundombinu tumepita katika meli, TRC tulipanda treni hapa mpaka Dar es Salaam, tumeshakagua Bandari TPA, tulienda kule tukaona Mamlaka ya Hali ya Hewa na rada. Hapa kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kweli niwapongeze sana wanafanya kazi nzuri. Juzi tumeona taarifa ya HIDAYA na kwa kweli watu wakazingatia kweli HIDAYA anakuja, HIDAYA anakuja; Wazee wa Mtwara na Lindi huko wakaomba dua, wakatambika. Naona kufika huko Kilwa sijui wapi HIDAYA akapotea, lakini kapotea wakati huo huo sisi wengine tumepata athari za upepo wa huyo HIDAYA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa pole kwa wananchi wangu wa Jimbo la Kilombero na Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Jana tulipata hali ngumu sana, leo kidogo maji yameanza kupungua na mpaka sasa hivi Mlabani kuna watu 135, Katindiuka 35 na Ifakara 120. Tayari maombi yetu nimeshayawasilisha kwa viongozi wetu wa mkoa, wanayafanyia kazi, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, RAS na kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama ili kuona namna gani tunapata msaada wa nguvu zaidi na mimi Mbunge wao nipo pamoja nao, nitaelekea huko kwenda kuwapa pole. Natoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa DC, Dunstan Kyobya, Kamati ya Usalama ya Wilaya kwa kazi kubwa ya uokoaji na mpaka sasa hivi hatujapata kifo chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchukuzi nashukuru Wizara ya Uchukuzi na mwaka jana nilisema hapa sana kuomba ufufuaji wa Reli ya Kilosa kwenda Kidatu. Naishukuru Serikali kwa sababu nimeona fedha angalau za consultation zimetengwa karibu shilingi bilioni nne ambapo reli ile itafufuliwa kutoka Kidatu kwenda Kilosa na kutakuwa kuna stesheni Kidatu, kutakuwa na stesheni pia Kilosa ya kubadilisha kontena. Katika kujenga uchumi wa nchi yetu kwamba tunaweza tukaweka kontena katika Bandari ya Dar es Salaam ikafika Johannesburg, South Africa. Serikali sikivu hii naishukuru sana. Pamoja na hapo nilichomekea katika TAZARA kwamba, Ifakara ni Mjini na tuliomba kipande cha lami cha kutoka TAZARA kuunganisha katika Stendi ya Kibaoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia Wizara kwa sababu nililalamika kidogo kuhusu Airport yangu ya Ifakara inajaa maji, DG wa Airports (Viwanja vya Ndege) akaniambia ananiletea wakandarasi. Ameleta wamechimba mitaro, wamepunguza kidogo hali ya maji kujaa na aliniahidi wanaweza kuweka lami kidogo na kujenga banda la kupumzikia abiria. Kutokana na hayo nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nichomekee tu kidogo kutokana na taarifa ya Mheshimiwa Waziri aliyoisema ya Idara zake zote za Wizara, inaonesha wazi kwamba nchi yetu inakwenda vizuri katika uwekezaji. Hapa katika bandari, kwa mfano amesema tuna bandari 693, bandari zilizosalimishwa ni 131, sasa hawa wanaopotosha kwamba kuna bandari zimeuzwa ni bandari gani? Nimesoma taarifa ya Waziri, nimerudia mara mbili, mara tatu sijaona mahali popote ambapo bandari imeuzwa au inawekezwa na mtu mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema hivyo kwa sababu nimeona juzi, nimeona jana Morogoro, nimeona Iringa wapo viongozi wa kisiasa wanarudia kupotosha, kumharibia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi. Natumia nafasi hii kumshukuru sana Comrade Abdulrahman Kinana kwa ufafanuzi wake wa jana kuhusu hoja zote zinazohusu uwekezaji wa Sekta ya Wizara yako. Katika kuharibu, yaani kuna mtu katika kila mkoa akienda anarudia, mama huyu kauza bandari, kila akienda na sasa hivi kashindwa hoja kaachana na Mama Samia ambaye anamsikiliza tu, kaenda hadi kwa watoto wake, siku hizi anamtaja na Abdul kila anapokwenda kwa uwongo tu ambao hauna maana yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo kwenye Ujumbe wa Kamati ya Miundombinu. Bandari ya Dar es Salaam ina magati 11 na magati yote 11 hayajatolewa kwa mwekezaji mmoja na hawatoki nchi moja, wale wawekezaji wawili. Utasemaje Bandari ya Dar es Salaam imeuzwa kwa Waarabu, sijui kuna ardhi imeuzwa kwa Waarabu? Ni upotoshaji ambao kwa kweli hautusaidii chochote, tunaendelea kuchangia hapa kumpa moyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan afanye kazi kubwa. Kelele zilikuwa mwaka jana, halafu tunapowekeza katika mambo haya ya uchumi hii kusema sema kuna watu wamegoma, sijui kuna watumishi wataandamana, sijui nini, tunaharibu uwekezaji wa nchi yetu, tunajiharibia wenyewe tuachane na tabia hizi. Kama tunataka kura tuombe kura kwa busara siyo lazima kuzusha mambo ya uwongo uwongo, mtu unaongea maneno yamepinda na ukitembea hunyooki, tabu tupu. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia ametulia anajenga nchi yetu vizuri, kwa nini tusimuunge mkono? Tuseme tunaongea kwa maneno ambayo hayafai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili la msingi wenzangu wamesema hapa na kauli za Wabunge ni wazi kuwa zinathibitisha kwamba Wabunge wote wanataka hii wharfage irudi ikusanywe na TPA. Nataka kusisitiza hapa na nilivyokuwa naangalia meaning (maana) ya wharfage wanasema ni accommodation provided at the wharf for the loading or storage of the goods. Sasa kama wharfage maana yake ni hii, Wabunge wote wamesema hapa na mimi nataka kusisitiza sekta yoyote ukiangalia hapa makusanyo makubwa tunayopata tunapata katika bandari zetu tulizosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Kamati ya Miundombinu tumezunguka wote huku tunakosoa bandari, uwekezaji ongezeni kasi, Dar es Salaam kuna foleni unganisheni na reli, kontena ziondoke mjini, foleni ipungue Dar es Salaam. Hawawezi kama hawana fedha, 50% ya mapato ya wharfage haikusanywi na wao. Sasa hivi wameshafunga mfumo mzuri wa mapato ambao unaitwa Real Time Revenue Collection Data, warudishiwe hii. Wizara walete Sheria Na. 17 ya mwaka 2004 iliyoboreshwa mwaka 2019 kupitia Sheria Na. 7 Kifungu cha 67(1) ili Bunge hili lipitie libadilishe lipeleke fedha hizi. Shilingi bilioni 50 kila mwezi zinatolewa Bandarini Dar es Salaam zinapelekwa Hazina na huko wanaweza wakazipangia kazi nyingine yoyote na hazirudi kuboresha bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo tukiboresha bandari yetu kama sehemu inayotupa mapato makubwa; kauli ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba tukiwekeza vizuri katika bandari tutapata 50% ya bajeti ya nchi yetu itaweza kufikika na kufikiwa. Kwa hiyo, naomba sana jambo hilo tulifanyie kazi kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, amesema Morogoro tuna Kiwanda cha Ndege na kweli kipo pale, matajiri ambao wapo humu waje wanunue ndege Morogoro, yaani kuna ndege za watu wawili wawili. Waje pale, walete order, waweze kununua ndege, tunatengeneza ndege kweli siyo uwongo. Waje pale waone kwa namna gani tunaweza kuboresha sekta yetu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba kuzungumzia madeni; najua Mheshimiwa Waziri ulishasema mara kadhaa kwamba maendeleo ni mchakato, ni process. Mheshimiwa Waziri hata tukikukaba koo hapa huwezi kufanya yote kesho asubuhi, lakini kwenye madeni wajaribu katika Wizara yao kuweka vipaumbele. Kamati tulienda kule Mtwara tulikutana na kampuni iliyojenga Airport ya Mtwara na ma-sub contractors walikuja pale chini wanalia machozi zaidi ya karibu miaka miwili yule Beijing Construction hajalipwa na wao chini huku hawajalipwa na wana mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda huko Shinyanga, tumeenda Mwanza kuna wakandarasi wanalalamika kwamba hawajalipwa. Nafikiri hatuwezi kulipa wote, basi tuchague wachache ambao tunaweza tukapunguza madeni yao, tukalipa ili kuifanya sekta hii iweze kwenda vizuri, vinginevyo nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana. (Makofi)