Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia jioni ya leo. Kipekee nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuniwezesha kusimama hapa ili kuchangia katika Bajeti hii ya Uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameweza kuweka mkazo na kipaumbele katika kuboresha na kuendeleza sekta hii ya uchukuzi. Ameboresha miundombinu, lakini pia huduma za uchukuzi zimeboreshwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nisiache kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Sekta ya Uchukuzi imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo na kujenga huduma ya uchumi imara katika Taifa letu. Sisi wote ni mashahidi, miradi mikubwa ya kimkakati inaendelea katika Sekta hii ya Uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikianza na SGR. SGR inafanya kazi nzuri, tumeona tayari wameanza majaribio ya SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma. Haya ni maendeleo makubwa sana kwa nchi yetu. Tukio hili ni la kihistoria kwa sababu na sisi tumevuka na tumekuwa katika Nchi za Afrika zenye SGR, lakini ambayo ni ndefu kuliko zote Barani Afrika ni SGR ya Tanzania ambayo ina kilometa 2,100. Sisi tunapaswa kujivunia na kumpongeza sana Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Nchi jirani kama Ethiopia mpaka sasa wana kilometa 700, Kenya wana kilometa 700. Kwa hiyo, sisi Tanzania tunamshukuru Mungu kwa hatua hii kubwa tuliyofanya. SGR hii imefanya majaribio, sasa iende ikaanze kazi na huduma zitolewe na wananchi waweze kufurahia SGR yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, nawaomba sana wanaohusika katika SGR, katika ujenzi wazingatie mabadiliko ya tabianchi kwa sababu wakati mwingine yanaenda kutukwamisha na sisi hatutaki SGR yetu ipate matatizo yoyote katika usafiri.
Mheshimiwa Spika, naendelea na bandari; katika uboreshaji wa huduma za bandari tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tumeona ni namna gani ameweza kuwekeza pia hapa kwenye bandari. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana kaka yangu Mbossa kwa kazi kubwa anayoifanya. Vijana hawa wameaminiwa na Mheshimiwa Rais na wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Spika, tunaona gati zinajengwa, lakini si hivyo tu, wanapoenda kufanya hii kazi tunaomba tuishauri Serikali zile fedha za wharfage ambazo hata wenzangu wamesema sana ziweze kubaki pale TPA na ziweze kuboresha miundombinu. Miundombinu hiyo itasaidia TRA waweze kukusanya kodi yao kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia siku ya leo ni kuhusu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Tanzania. Niwapongeze sana TAA, sisi kwetu Kilimanjaro tunawapongeza sana kwa namna ambavyo waliona umuhimu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Waziri, Naibu Waziri na wote wanaofanya kazi katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kule Kilimanjaro tuwanapongeza sana kwa sababu, wameweza kuiondoa KADCO iende kukaa chini ya TAA. Hayo ni mapinduzi makubwa sana, tunawaongeza sana Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Ili hii Taasisi iweze kufanya kazi zake vizuri na kutoa huduma bora zaidi kwa abiria na mizigo. Nashauri waweze kuleta ile Sheria hapa, ifanyiwe marekebisho ili iweze kupata zile fedha zinazotokana na tozo ya huduma za abiria (passenger service charges) iweze kubaki katika taasisi hii ili iweze kujitegemea kwa sababu sasa inaitegemea sana Serikali. Kwa hiyo, naomba kushauri jambo hili lizingatiwe ili taasisi hii iweze kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea hapohapo, sisi kule kwetu Moshi tunaendelea kuwashukuru kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kiwanja chetu cha Moshi ili kiweze kupanuliuwa, tunaomba sasa Taasisi hii au Wizara iweze kuangalia ni namna gani inaweza kulipa fidia kwa wale watu wenye zile nyumba sita ambao wana hati pamoja na zile tatu ambazo hazina hati ili sasa waweze kupanua runway na kuweka taa. Hapohapo iweze kuboreshwa kutoka, ndege ambayo inatua pale kwa sasa itakuwa ina abiria 40 tu, lakini pakiboreshwa kwa namna hiyo panaweza kutua ndege yenye watu zaidi ya 70. Tunaomba jambo hilo liweze kuzingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naenda kwenye ATCL. Naomba kwa kipekee sana nimpongeze sana Engineer Matindi kwa kazi nzuri anayoifanya. Sisi wote ni mashahidi, ATCL inafanya kazi nzuri na mpaka sasa tunaweza tukasema kwamba Tanzania tumepiga hatua kubwa sana kwenye usafiri wa anga. Leo tuna ndege 16 zikiwemo ndege za mizigo, hii ni hatua kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunampongeza Mheshimiwa Rais katika uwekezaji unaoendelea katika Kampuni hii ya Ndege. Leo wakati wanatambulisha hapa tumeona Marubani wanawake. Naomba nichukue nafasi hii kuipongeza sana Taasisi hii kwa namna ambavyo inaona umuhimu wa wanawake na kazi nzuri wanayoifanya wanawake. Tulimwona ndugu yetu, dada yetu Neema ameendesha ndege ile kwa masafa marefu na mpaka amefika Tanzania salama. Ni kiasi gani wanawake wanaendelea kuaminiwa na nampongeza sana Engineer Matindi kwa namna ambavyo anaona ni namna gani wanawake wanaweza kufanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeona wahudumu wa ndani ya ndege, waliokuwa hapa leo wako katika viwango vya Kimataifa; ni bora sana, nawapongeza sana ATCL. Si hivyo tu, tunaona namna mtandao wa safari za ATCL unavyoendelea kukua hapa nchini na nje ya nchi, niwapongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siku hii yangu ya leo, nimesoma katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimesilikiza pia Hotuba ya Kamati. Nimesikia wamesema maneno mengi sana mazuri, lakini kipekee niwapongeze kwa kazi nzuri sana waliyoifanya. Hata hivyo, nina jambo moja ambalo nataka kushauri. Naomba kuishauri LATRA kwa maana imesema katika vipaumbele vyake ni kudhibiti usafiri, kuimarisha usalama, udhibiti na utoaji wa huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa niliyoisikia wamesema vizuri sana kuhusu mabasi na usafiri mwingine, lakini sikusikia wakisema kuhusu pikipiki. Naomba tujiulize sisi kama viongozi tulioko hapa ndani tunajua kabisa usafiri wa pikipiki ndiyo unaotumika sana kwa sasa hivi. Inaweza kuwa mtu asiseme lakini kiukweli pikipiki zinatuokoa sana. Niliwahi kuchelewa airport, kilichoniokoa ni bodaboda. Nasikitika sana katika taarifa hii sijaona ni namna gani wamejipanga kuwanusuru vijana wetu wanaoangamia kwa ajali za bodaboda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda MOI, asilimia kubwa ya vijana wako pale ambao wamepata ajali. Kuna Gazeti la Nipashe ambalo lilitoka Februari 7, lilikuwa limeandika MOI imezidiwa na wagonjwa ambao wanatokana na ajali za bodaboda. Hili ni jambo la Taifa kuliwekea macho, ni jambo ambalo wanatakiwa kuliangalia vizuri. Kipindi kilichopita sisi tulikwenda Rwanda kwenye michezo. Wote tuliokuwa pale tulijionea wenzetu wanavyofanya kazi nzuri ambapo bodaboda wamepewa elimu na wanafuata sheria za barabarani. Tunaomba sasa jambo hili liangaliwe na lizingatiwe vizuri ili kuokoa maisha ya vijana wetu na waweze kupata ajira.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)