Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Haji Ameir Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii leo ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi. Kwanza kabla ya yote, nijumuike na wenzangu kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anatimiza ahadi na vilevile kuleta uwekezaji mkubwa sana katika nchi yetu hii hasa katika Wizara ya Uchukuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Makame Mbarawa pamoja na Watendaji wake wote wa Wizara. Tatu, kwa kipekee kwa maana hizi ni pongezi za kipekee nampongeza Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye jana alitoa hotuba yake nzuri sana pale Jakaya Kikwete na kila ambaye hakuweza kwenda pale aitafute ile hotuba ya Makamu Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi kwa sababu kazungumza mambo ambayo ni mazuri sana pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nije katika hali ya mashairi, kule kwetu Zanzibar kuna wimbo ambao mara nyingi huwa unaimbwa sana na ni wimbo wa kimapinduzi na wimbo huu ni maarufu sana. Leo sitoweza kuimba isipokuwa nitasema yale mashairi. Ni wimbo ambao ni maarufu sana, mashairi yale yanasema hivi: “Walisema hatuwezi, waje watutazame”. Wakati huohuo kukawa na kibwagizo kingine, “Walisema uongozi, kwetu hautosimama”. Sasa niingize shairi la tatu, “Mama Samia kiongozi, imara amesimama.” Hayo ndiyo mashairi ambayo kwa leo itakuwa kama ni kibwagizo kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije katika mtazamo wa Waswahili. Waswahili nao wana maneno yao ambayo ni maarufu sana huwa wanasema kwamba: “Usimtake bubu kusema, ukimlazimisha kusema, siku atakayokuja kusema, maana yake utakuja kuadhirika. Usimlazimishe kipofu kusikia, siku utakapokuja kumlazimisha kusikia, utakuja kuadhirika au utakuja kwenda mbio”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo kubwa la kuzungumza kwangu hapa ni kuchangia bajeti...

SPIKA: Mheshimiwa Amour, nadhani ulikusudia kusema kiziwi.

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Spika, ndiyo kiziwi. Lengo kuu la kuchangia bajeti hii, kwanza kabla ya kusema lolote naunga mkono hoja ya Taarifa ya Bajeti ambayo imetolewa na Wizara ya Uchukuzi kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi iliyofanywa katika Bajeti ya Uchukuzi ni kazi ambazo ni kubwa sana. Hizi kazi zilizofanywa ni kazi za ahadi ambazo ameahidi Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ambayo ameapishwa. Kwa maneno ambayo aliyasema: “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee”. Bahati nzuri Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mtangulizi wake aliachiwa kazi nyingi sana ambazo hapo nyuma zilikuwa katika asilimia ndogo sana, lakini kwa sasa hivi kila mmoja anaona na mwenye macho haambiwi tazama. Kazi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kazi hizo zilizofanywa kupitia Wizara ya Uchukuzi kwanza, niangalie katika Taasisi yao moja ya TRC. TRC ambayo ina kazi iliyoachwa nadhani kwenye 30%, lakini kwa sasa hivi hakuna asiyeona kwamba Shirika la Reli (TRC) ambalo limefanya kazi kubwa sana ya kujenga ile Reli ya Standard Gauge, hatukutarajia kwamba ndani ya miaka miwili hii au mitatu ambayo kakaa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan; treni ile kwa sasa hivi itaweza kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Kwa kweli hiyo ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuangalie upande wa TPA, napo pamefanyika mapinduzi makubwa sana. Tukiangalia kwa namna ambavyo alivyoichukua kipindi chake kutoka kwa mtangulizi wake, mimi siyo mtu wa mahesabu lakini kila siku tunasikia kwamba mapato ya TPA sasa hivi yamekua kwa asilimia kubwa sana. Kwa wale Wabunge wenzangu ambao huita kwa mabilioni, nadhani mimi nitaita kwa matrilioni sitosema kwa mabilioni. Kwa hiyo, nawapa hongera sana TPA, TRC na TASAC kwa namna ambavyo wametimiza ahadi ya kuikamilisha ile Meli ya Hapa Kazi Tu. Pia, ile meli imeleta taswira nzuri sana kama ni moja ya maendeleo ambayo yatakuwa yamefanywa katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia suala la TMA kwa mujibu wa radar zilizowekwa pale maana yake napo kunastahiki sifa ambazo ni kubwa sana na yote hayo yapo kutokana na uongozi bora, uongozi mzuri wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, vile vile kuna mambo ambayo lazima tuyaseme. Kuwepo kwa miundombinu ya reli, ndege na meli ni moja ya mambo ambayo yataweza kuchangia kwa kiasi kikubwa sana katika uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwanza tufahamu wazi kwamba kutakuwa kuna zile fursa za kijamii kwa sababu kila kitu kitakuwa kimerahisishwa kwa namna yake. Kitu ambacho naiomba Serikali yangu Tukufu, haya mambo yote huko nyuma tulikuwa nayo, mashirika ya reli tulikuwa nayo, ndege tulikuwa nazo na mambo mengine mengi tulikuwa nayo, lakini kuna vitu vinaonekana kwamba labda pengine Watanzania tunakosea, tunakuwa na mambo mazuri sana, lakini hatimaye utaona kitu kimoja kimoja kinaanza kudondoka.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali yangu Tukufu, kuna mambo matatu ambayo ni mambo muhimu sana kwa kile ambacho tunakifanya. Kitu cha mwanzo tuwe na uongozi bora katika zile taasisi ambazo zinasimamia vitu vyetu vyote kama vile reli na ndege; ni lazima tuwe na uongozi ulio bora.

Mheshimiwa Spika, la pili ni operation; namna ya kuziendesha zile, maana yake tuwe na watu ambao wanaweza kusimamia katika hali nzuri sana. La tatu, linaloweza kugonga watu wote ni suala la maintenance. Tutakuwa na treni nzuri sana, tutakuwa na ndege nzuri sana, tutakuwa na mitambo mizuri sana lakini bila maintenance za kila wakati maana yake baada ya miaka mitano ama 10 tunaweza kuja kujihesabu tunarudi nyuma.

Mheshimiwa Spika, siku zote hizo tumezungumzia suala la bajeti zetu hizi hapa na tunapitisha mafungu mengi sana. Kwa kweli Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa, maana tunapopitisha yale mafungu tunapitisha kwa pamoja, lakini wakati mwingine inakuwa ni vichekesho sana, Waheshimiwa Wabunge sote tunakuwepo hapa wakati Mafungu yanapitishwa sote tunasema ndiyo, lakini unakuja baadaye kunakuwa na baadhi, wanakwenda kulaani huko nje kwamba lile fungu gani au kwamba kumefanyika kitu gani.

Mheshimiwa Spika, inavyotakiwa sisi viongozi ambao tupo hapa Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunatakiwa tumsaidie Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kila kitu ambacho tunakipitisha hapa. Kama tunakipitisha hapa katika bajeti zetu maana yake tunakipitisha kwa umoja wetu. Kama tunakitenda ndani ya Bunge letu hili, tunakitenda kwa umoja wetu. Maana yake ni kwamba sisi tunakuwa kama ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nasema kwamba, kama nilivyosema awali kwamba naiunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na ahsante sana. (Makofi)