Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu, Wizara ya Nishati na Madini. Nakushukuru wewe kwa kazi nzuri unayoifanya, pia nimshukuru Mungu kwa kutupa nafasi hata kufika mahali hapa siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mungu zaidi kwa jinsi ambavyo alimwongoza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumchagua Profesa Sopeter Muhongo katika Wizara hii ya Nishati na Madini. Profesa hakika unaitendea haki sana Wizara hii. Pia niwashukuru wale wote ambao ni Watendaji Wakuu, Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa REA Tanzania, Dkt. Lutengano Mwakahesya, Mkurugenzi wa Geothermal Tanzania na Watendaji wengine wote katika nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo mchango wangu nielekeze zaidi nikianza na umeme wa vijijini (REA). Mpango huu wa umeme vijijini hakika mwaka jana wengi wetu tumeokoka sana katika mpango huu wa REA. Tumeokoka kwa sababu pamoja na kwamba siyo vijiji vyote vimepata, naamini katika awamu hii ya III vijiji vingi vitapata umeme huu. Nikija katika Jimbo langu la Busokelo, Busokelo ni miongoni mwa Majimbo ambayo tumenufaika na mpango mzima wa REA. Pamoja na kwamba kuna changamoto za hapa na pale, kuna baadhi ya maeneo kama Lupata, ukienda Isoko, ukienda Mpata, ukienda na maeneo mengine ya Kilimansanga bado umeme huu haujafika lakini tuna imani kwamba vijiji 30 vilivyosalia, tunaamini katika mpango huu wa awamu ya III vitapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la mpango wa umeme vijijini, kwa vile vijiji ambavyo vilikuwa awamu ya pili, tunaomba watendaji pamoja na wahusika wote vikamilike kabla ya Juni ili wananchi wale kwa sababu tulishawaaminisha kwamba watapata umeme, na walituamini, tunaomba kabla ya Juni kwisha waweze kupatiwa huo umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la madini. Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo imebarikiwa sana katika nchi yetu ya Tanzania. Tuna madini ya aina nyingi sana, ukienda kule Chunya utakuta kuna gold, ukienda huku Ileje utakuta kuna madini, ukienda Kyela makaa ya mawe, ukija Busokelo, kwa hiyo tuna madini ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na madini aina ya calcium yanayopatikana pale Mlima wa Panda Hill. Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake haya madini sijayaona hapa, lakini naamini kwamba atatuma timu yake waweze kufanya exploration na extraction kule, basi wananchi wale watafaidi sana haya madini kwa sababu tunaamini hata utengenezaji wa mbolea aina ya NPK inatokana na madini hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, nikisoma kitabu cha hotuba na Waziri ameandika vizuri sana, very technical, ukurasa wa 62 kuna madini aina ya niobium, madini haya pia Mbeya yanapatikana na kazi kubwa ni kutengeneza vifaa vya elektroniki ikiwemo pamoja na engine za ndege tunaita jet, lakini pamoja na kutengenezea vitu mbalimbali, mambo kama kompyuta na simu. Kwa hiyo, tunaomba kama yataweza kuendelezwa, pamoja na kwamba upembuzi yakinifu ulishafanyika na utafiti umefanyika, sasa kazi kubwa iliyobaki ni kwamba yaanze kufanyiwa kazi kwa maana ya kuchimbwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha hotuba yake hapa atuambie kwamba ni lini hasa rasmi wananchi wa Mbeya, katika maeneo ya Panda Hill, Mbeya na Tanzania kwa ujumla watanufaika na haya madini ili waweze kuinua uchumi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika suala la geothermal (jotoardhi). Geothermal ni umeme ambao unatokana na nguvu ama joto lililoko ardhini na Busokelo tumebahatika kuwa na sehemu inayopatikana hiyo geothermal. Kwa hiyo naomba nimshukuru Waziri kwanza kwa sababu nakumbuka siku ile alikuja, alifika katika eneo hili la Mto Mbaka na alituahidi kwamba mara tu baada ya uchunguzi ama baada ya utafiti kukamilika mwezi wa Septemba wataanza kuchoronga visima vya huko, kwa hiyo tunaomba asitusahau.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba pamoja na timu yake ya wataalam waje katika eneo hili kwa sababu wananchi wakati tunahimiza kwamba wasifanye maendeleo yoyote kwa sababu hili eneo litakuwa ni sehemu mojawapo ya kuzalisha umeme na sisi tutakuwa tunauza maeneo mengine, walisikiliza ile kauli kwa sasa hivi wanasubiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo geothermal pekee tu, katika Jimbo la Busokelo pia tuna gesi aina ya carbondioxide. Hii gesi imeanza kuchimbwa tangu mwaka 1984, lakini kwa bahati mbaya hata hivi sasa ninavyoongea tuna viwanda viwili, kimoja kipo Kanyelele na hii gesi inatoka Kijiji cha Mpata, lakini pia kuna kiwanda kingine karibu na Tukuyu Mjini kwa ajili ya gesi hii na gesi hii inatumika zaidi katika masuala mazima ya kwenye soda, kwenye bia na maeneo mengine ambayo yanasababisha vitu visioze wala visiharibike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya, kwa makampuni ambayo yamewekeza kule, kuna kitu tunaita social responsibility kwa maana ya jamii inayozunguka, huwa hawafaidiki na gesi hii. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, kwa nguvu zako zote pamoja na watendaji wako wote kuisimamia vizuri gesi hii aina ya carbondioxide kwa sababu wananchi wanaona yanakwenda magari na kurudi kuchukua, lakini hawaoni wananufaikaje na hii gesi. Hii ni changamoto kubwa sana, kwa sababu nakumbuka kipindi tunaomba kura ni miongoni mwa mambo ambayo yalitusababisha tupate wakati mgumu sana. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri alizingatie hilo atakapokuwa anajumuisha hotuba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na suala hilo, ukienda Kata ya Lufilyo kuna madini ambayo yanapatikana kule kwa ajili ya kutengenezea marumaru na ukiangalia Tanzania nzima hii, mara nyingi sana tuna-rely kwenye marumaru za ku-import kutoka China lakini kule kuna madini ya kufanya hivyo. Katika Kijiji hiki cha Kikuba, Kata ya Lufilyo, kuna maji ama maporomoko ambayo yanaweza yakasababisha umeme wa Hydro Electric Power kwa maana ya umeme wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, tunaomba wataalam ama watafiti waanze kuja kuchungulia kule kwa ajili ya kuleta wataalam ili waweze kutuambia ni kitu gani pengine baada ya hapo kitafuata ili wale wananchi wasiangalie tu yale maji yanakwisha pasipo faida yoyote, naamini tukiwekeza katika umeme itatusaidia sana kama nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la matumizi ya umeme. Mara nyingi sana tunasema umeme; naishauri Serikali tuanze kutoa elimu kwa jamii kwamba umeme huu siyo kwa ajili ya kuwasha taa, siyo kwa ajili ya kupiga pasi tu, siyo kwa ajili ya kuangalia TV ama runinga, tufikiri katika uwanja mpana hasa kwa maana ya kuleta viwanda vidogovidogo, vile vya kuchakata hata kwa mikono yao. Nafikiri umeme utakuwa na faida sana na REA hii itakuwa na faida sana kwa wananchi kama tutaanza kutoa elimu ya namna hiyo. Maana wengi wetu wanafikiri kwamba umeme ni kwa ajili ya kuwasha taa na pengine kuangalia vitu vingine, lakini kumbe umeme ni zaidi ya matumizi hayo. Nafikiri elimu hii ikiwafikia na kama Wizara watakuwa na mipango ya kutoa elimu hiyo kwa jamii itapendeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie suala zima la Serikali kuhusika asilimia mia moja katika kuwekeza kwa maana ya nishati ya umeme. Umeme ni gharama kubwa sana, tunaomba Serikali kwa jinsi ambavyo wameshaanza kutafuta wadau wengine waendelee hivyo hivyo. Hakuna Taifa lolote duniani ambalo kwa nguvu zao wenyewe wanaweza wakajitosheleza katika nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri nilipata nafasi ya kutembea Mataifa mengine duniani, kama Ujerumani, utakuta nyumba moja ya familia moja inakuwa na vyanzo vitano vya nishati ya umeme; utakuta kuna maji, utakuta kuna solar, utakuta kuna umeme wa upepo utakuta kuna umeme wa biogas, geothermal na kadhalika, hata ukikatika umeme wa aina moja, basi umeme wa aina nyingine ule una-take up, hivyo katika nchi yetu pia tuanze kufikiri katika mfumo huo, tusi-rely tu katika vyanzo vya umeme wa aina moja, kwa maana kwamba kuna gesi halafu pia kuna umeme wa maji, lakini pia tuanze kufikiri zile energy ambazo ni renewable kwa maana ya kwa mfano geothermal.
Mheshimiwa Naibu Spika, geothermal is an energy ambayo inakuwa renewable, inaweza ikazalisha umeme na kuzalisha na kuzalisha, lakini tuki-rely katika umeme wa maji, sisi wote ni mashahidi hapa, kwa sababu wakati mwingine, kama kipindi cha miaka miwili iliyopita nchi yetu ilikuwa katika janga kubwa, kwa hiyo umeme ama mabwawa ambayo tunategemea yalikuwa hayatoi maji sawasawa kama vile ambavyo tulitegemea. Pia tukija katika gesi, gesi ile ukisha-extract hatutegemei tena kwamba itaendelea kuwepo vilevile kwa miaka na miaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niunge mkono Wizara hii na hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana.