Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu ndani ya Bunge lako hili Tukufu. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Mama, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya kwenye Taifa letu. Pia nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi ya Kata ya Mavanga, Mheshimiwa Rais aliona taarifa mtandaoni ya mtoto ambaye alikuwa amevimba sana tumbo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa alimchukua alimpeleka hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu, akalipia gharama zote. Bahati mbaya mtoto yule alifariki na aliweza kugharamia kusafirisha mwili na mazishi. Napenda kutumia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Ludewa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Kitendo alichokifanya kimetoa somo kubwa sana kwa Viongozi wa Ludewa na Viongozi wa Mkoa wa Njombe, kwa hiyo nashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri na kwa hotuba nzuri. Nilijua kwamba Wizara imegawanywa kwa hiyo hotuba yake itakuwa na kurasa chache lakini cha ajabu nimeona ana kurasa 260. Hii ni ishara kwamba Wizara hii ni nyeti sana.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake ukisoma ukurasa wa 10 Mheshimiwa Waziri amelieleza Bunge lako, naomba kumnukuu, kwamba; “Sekta hii ni ya tatu kwa kuchangia fedha za kigeni kupitia mauzo ya huduma kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Katika kipindi cha kuishia mwezi Februari, 2024, Sekta ya Uchukuzi ilichangia Dola za Marekani bilioni 2.4 ya fedha za kigeni ikiwa nyuma ya mauzo ya dhahabu na biashara ya utalii. Kwa hiyo hii inaashiria kwamba Wizara hii ni Wizara nyeti sana.” Kwa hiyo kwa kusoma hii na kutokana na umuhimu wa Wizara hii natamka kwamba naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, niende sasa kule jimboni kwangu. Nina kata nane ambazo zimezungukwa na Ziwa Nyasa, kuna Bandari pale Lumbila, Kilondo inaitwa Ifungu, Lupingu, Nsisi lakini vile vile kuna Bandari ya Manda na Lupingu.
Mheshimiwa Spika, meli hii ya MV Mbeya II inapokuwa inasafiri ikiwashusha wananchi wa pale Ifungu, wanatumia muda mrefu sana kufika Kijiji cha Nsele. Lakini vile vile ikishusha wananchi wa pale kituo cha Kata ya Lifuma, Kijiji cha Nsisi wanatumia muda mrefu, zaidi ya masaa mawili kutembea kufika makwao. Kwa hiyo kufuatia hili, nilipokwenda kwenye ziara wananchi wale waliomba sana Serikali iweze kutuma wataalam wakaangalie eneo lile la Nsele. Ni kijiji ambacho kina wananchi wengi na eneo lile la Lifuma ili waone kama wanaweza kuweka kituo cha kushusha abiria maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, vile vile sasa hivi tumeambiwa kwamba meli haifanyi safari zake kwa sababu ziwa limejaa sana. Yale maeneo ya kupita abiria pale Itungi na pale Kiwira hawawezi kusogea mpaka pale kuikuta meli ilipo. Kwa hiyo ningependa sana kuiomba Serikali iweze kufanya uchunguzi eneo la Matema Beach kwa sababu lile eneo lipo juu, ili ikiwezekana wakati wa dharura abiria na mizigo waweze kutumia eneo lile la Matema. Kwa sababu uwepo wa meli hii kwenye Ziwa Nyasa ulikuwa ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi. Nina takwimu za mwaka 2022/2023, meli hii iliweza kusafirisha kwenye Ziwa Nyasa wananchi elfu 72.9, lakini vile vile mizigo tani 12,000 ziliweza kusafiri. Kwa hiyo hii ni ishara kwamba meli inapokuwa haipo wananchi wanapata adha kubwa sana. Niombe sana hilo liweze kufanyika.
Mheshimiwa Spika, kuna ile meli ambayo ilikuwa inaitwa MV Songea, ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 43 za mizigo. Meli ile inahitaji fedha chache sana ili iweze kukarabatiwa, kuwekwa zile mashine mpya lakini furniture mle ndani na kupaka rangi tu lile jumba lake. Meli hii inaweza ikasaidia kama mbadala wa ile meli ya MV Mbeya II. Zikiwa zinapishana tutaongeza huduma kwenye Ziwa Nyasa. Kwa hiyo ningeomba sana Wizara hii waweze kuiangalia ile meli kama wanaweza wakaikarabati iweze kusaidia wananchi.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, aliweza kuwatuma wataalam kutoka TPA kwenda kukagua Bandari ya Manda na ikaonekana lile jengo la abiria, gati la kushushia mizigo na abiria pamoja na ofisi vinatakiwa vijengwe upya. Kwa hiyo ningeomba sana Wizara iweze kuharakisha. Katika hili watume wataalam pale Manda ili waweze kufanya uthamini ili wananchi ambao wanaondoka wajue na walipwe haki yao waweze kuachia eneo la bandari.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niende sasa kwenye eneo la reli. Ukanda ule wa Liganga na Mchuchuma una madini ambayo logistics za kuyatoa pale kuyapeleka bandarini ni changamoto kubwa kidogo. Tuliahidiwa kuwa kuna reli itajengwa kutoka Mtwara hadi Bamba Bay tawi Mchuchuma na Liganga. Nishukuru Serikali imeshatoa fedha na mkandarasi yuko pale Bamba Bay ameshaanza kujenga bandari. Tulikwenda pale na Mheshimiwa Naibu Waziri, tulishuhudia kazi inaendelea. Kwa hiyo, tunaomba na hii reli iweze kukamilika mapema ili sasa ule mzigo wa chuma na makaa ya mawe iwe rahisi kuweza kusafirisha na Mheshimiwa Profesa Kabudi amesema hapa nimemsikiliza kwa makini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halikadhalika ile reli ya TAZARA kuanzia pale Makambako waone uwezekano wa kulisogeza tawi liende kule Mchuchuma na Liganga na ikiwezekana iweze kuunganishwa hadi huku Ihumwa Dodoma, tuiangalie nchi hii kwa miaka mia moja au zaidi ijayo. Kwa hiyo, watumwe wataalam waangalie ni wapi reli hii inaweza ikaunganishwa kutoka pale Makambako mpaka Liganga na Mchuchuma, lakini vilevile ikiwezekana ije iunganishwe na SGR ili mizigo ya kule iweze kwenda katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusafirishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru pia nimeona Uwanja wa Ndege wa Njombe umeingia kwenye bajeti.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)