Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na moja kwa moja namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa afya na uzima vinavyotuwezesha kuendelea kuwatumikia wananchi waliotuchagua.

Mheshimiwa Spika, nataka kuanza kwa kusema kwamba kuna kazi kubwa sana imefanywa na Wizara ya Uchukuzi ambayo sisi wote katika maeneo mbalimbali hapa nchini tumeiona na kwa kweli tunawapongeza sana kama Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kazi hiyo. Tunapozungumza habari ya Reli ya SGR, tunapozungumza habari ya bandari zetu, tunapozungumza habari ya viwanja vya ndege kikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ambacho kinaendelea kukarabatiwa na kujengwa baadhi ya majengo, kazi inaendelea. Zaidi ya yote nishukuru sana kwa Wizara hii kutusaidia katika Chuo cha Hali ya Hewa wamefanya ukarabati mkubwa, wamekifanya kiwe cha kisasa zaidi, hongera sana na tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kabla ya kusema yale ninayoyakusudia nataka Wizara iyatazame, ninukuu maneno ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoyatoa mwaka 1976 wakati ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliagiza mchele kutoka nje. Mwalimu akaulizwa na waandishi wa habari, Mwalimu naona mmeagiza chakula, mmeagiza mchele ina maana Tanzania ina upungufu wa chakula? Mwalimu akasema hapana hatuna upungufu wa chakula bali tuna upungufu wa mchele kwa sababu wapo Watanzania hasa wakiwemo Wazaramo ambao kama hawakula wali hawajisikii kama wamekula, lakini wangetaka kula viazi, wangetaka kula mihogo wangetaka vyakula tunavyo vingi ila tuna upungufu wa mchele.

Mheshimiwa Spika, ninachokusudia ni nini? Ni kwamba ninapozungumza mambo ambayo nataka Wizara iyatazame sikusudii kusema kwamba Wizara hii haijafanya mambo mengi na makubwa isipokuwa hayo ninayoyakusudia yana upungufu hayajafanyika kwa kiwango kinachotakiwa. Kwa hiyo, wamefanya kazi kubwa, lakini meli katika Ziwa Tanganyika bado ni msalaba wanaoendelea kuubeba. Ziwa kubwa kama Ziwa Tanganyika linalotuunganisha na Nchi ya Zambia, DRC Congo na Burundi mpaka sasa halina meli hata moja inayomilikiwa na Wakala wa Meli inayofanya kazi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, Nchi ya DRC Congo, takwimu zilizotolewa na Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki inaonesha kwamba karibu 85% ya vitu vyote vinavyotumika katika nchi hiyo wana-export kutoka nje, lakini nchi ya kwanza inayofanya biashara kubwa na Congo ni China, inayofuata ni Afrika ya Kusini, inayofuata ni Zambia, inayofuata ni Kenya. Sisi ambao tuna mpaka na DRC Congo ni nchi ya saba kwa kufanya biashara na DRC, hii kwa kweli tumejipotezea nafasi kubwa ya kuinua nchi yetu kiuchumi kwa kukosa meli kwenye Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Waziri tumekutana katika nyakati mbalimbali pamoja na Wakala wa Meli, wametupa maelezo hatua mnazokwenda nazo…

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Aida Khenani.

TAARIFA

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba pamoja na kwamba hatuna meli mpya hata moja, hata zilizokuwa zinahitaji ukarabati sasa ni miaka nane hazijakarabatiwa. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa kwa mikono miwili na huko ndiko ninakoelekea kwamba wakati wanahangaika na meli ya mizigo na meli kubwa ya kisasa ya abiria 600, hebu waturudishie Meli ya MV Lihemba na Mwongozo kwa haraka. Najua hatua wanazozichukua kwa kuwa wametupitisha kwenye hatua wanazozichukua na tunajua wapi walipokwama. Leo sina mpango wa kushika shilingi ya Waziri kwa sababu najua wapi alipokwama na najua hatua anazozichukua, namwomba aongeze kasi katika hatua hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumze ni ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaotaka kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege Kigoma. Jambo hili nililizungumza kwenye Wizara ya Ardhi na sasa nalizungumza tena kwenye Wizara husika. Kwa kweli, jambo hili linatuletea mgogoro mkubwa sana, kama mnavyofahamu kipindi hiki kina mvua nyingi, wananchi wameharibikiwa maeneo yao lakini wanashindwa kuyaendeleza, hata choo kimevunjika, mtu anafikiria najenga choo inawezekana kesho nitaondolewa kwa sababu tayari evaluation ilikwishafanyika na inajulikana nitalipwa kiasi gani, nikianza tena kuingiza pesa huku, pesa zangu zitakuwa zinapotea.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, ni mtu makini na sisi tukisikia huko kwetu Profesa tunajua Profesa ndiye mbobezi wa mambo yote. Sasa nimwombe Profesa na bahati nzuri amepewa kijana chapakazi kumsaidia kufanya kazi, Naibu Waziri wake hebu wasaidie kuhakikisha hii kero ambayo iko kwa wananchi wetu inaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema mwanzo kwamba leo sikusudii kusema mambo mengi kwenye Wizara hii, najua wapi walipokwama kwa Meli ya Lihemba na Mwongozo, itakapofika bajeti ya Wizara ya Fedha nitasema mengi na hapo nafikiri patanisaidia zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)