Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Uchukuzi. Ni kwamba Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi, wakati mwaka jana tunaleta ushauri kwamba igawanywe tulikuwa tuna maana kubwa sana na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kukubali mawazo ya Waheshimiwa Wabunge na kuigawa Wizara hii kuwa katika Wizara mbili ili kupunguza mzigo katika Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa Wizara hii imebeba sehemu nyingi sana, imebeba idara nyingi sana za kiuwekezaji. Kuna uwekezaji, wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo yao kwa njia ya magari, kwa njia ya bandari lakini kwa njia ya anga na kote huko ni sehemu kubwa sana kwa ajili ya kutengeneza uchumi wa nchi yetu. Sasa Mheshimiwa Rais baada ya kuigawa Wizara hii akatoa majukumu ya kazi ambazo Wizara imepangiwa kuzifanya. Nataka kuzungumza katika maeneo matatu; sehemu ya usafirishaji kwa barabara na sehemu ya usafirishaji kwa njia ya meli na ujenzi wa bandari lakini usafiri kwa ajili ya njia ya anga.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba uwanja wetu wa Dodoma sasa hivi pamoja na kuwa mdogo lakini bado hatujaufanya kuwa busy kwa ajili ya biashara. Kwa mfano, mpaka sasa hivi tulikuwa tuna ndege ya kutokea Dodoma kwenda Mwanza, hii ndege ikawa imeondolewa wakati ilikuwa inapata abiria. Na ni kama vile kuwazuia watu wa kanda ya ziwa wasikutane na wenzao watu wa Dodoma na kufanya shughuli zao za Dodoma kwa haraka. Waheshimiwa Wabunge, wote wa kanda ya Ziwa tumelalamikia jambo hili, lakini Serikali haitaki kusikiliza kilio cha Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi wanalalamika, watumishi wa Serikali wanalalamika, shughuli nyingi za Serikali ziko hapa, lakini ili uweze kufike Dodoma kwa haraka unatakiwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, unatakiwa katika Ofisi ya Waziri wa Fedha, unatakiwa Ofisi, Ofisi zote lazima uje Dodoma kutokea kanda ya ziwa. Sehemu ya karibu kwa anayetoka Simiyu, anayetoka Shinyanga, anayetoka Mara, anayetoka Kagera akitaka haraka aje Mwanza achukue ndege anawahi kufika Dodoma.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri leo hii kama hatakuja na majibu ya ndege ya Kwenda Mwanza anairudisha lini, alitueleza kwamba tukipata ndege nyingine tutapata ndege ya Mwanza. Ndege imeshakuja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kapokea ndege, Wanamwanza tumeona hilo, sasa kama hutakuwa na majibu leo, nitashika shilingi japo ni ndugu yangu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, ni suala la ndege kutokea Dodoma kwenda Zanzibar, Dodoma kwenda Arusha, Dodoma kwenda Mbeya, Dodoma kwenda Kigoma, kwa nini tunataka kuuvunja huu mji? Utakuwa lini Mji wa Dodoma? Leo mpaka mabasi yanatembea usiku, lakini sisi watu wa anga tunayo ndege yetu inayotokea Dar es Salaam - Dodoma. Wizara imetoa kipaumbele kwa ajili ya Dar es Salaam - Dodoma tu, mikoa mingine haina hadhi ya kupata ndege, hili jambo sio sawasawa, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna jambo la usafiri wa barabara, kumekuwa kuna matatizo makubwa sana hasa katika mizani zetu. Najua hii mizani iko Wizara ya Ujenzi na Waziri ana-deal na uchukuzi, lakini ni kwamba, lazima akae na Waziri mwenziwe kuhusiana na suala la mizani. Mizani imekuwa ni kero kubwa kwa madereva, mizani imekuwa ni kero kubwa kwa matajiri. Kwa mfano, gari linapakia lita 42,000 ya petrol au lita 37,000 ya diesel unaambiwa gari likifika Vigwaza limezidi kilo 50. Hao wa Congo watapitaje Bandari ya Dar es Salaam? Kwa hiyo, atakwenda anasumbuliwa kwa kilo 50 mpaka anafika Tunduma, atakwenda anasumbuliwa analipa faini mpaka anafika Rusumo, mpaka anafika Kabanga au anafika Mtukura.
Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo lazima wakae waangalie na anaambiwa dereva ayapange mafuta vizuri mzigo umekaa vibaya, umezidi mbele kilo 120. Mzigo umefungwa seal na watu wa TRA, hawaoni kama wanasumbua hawa watu majirani zetu wanaotumia barabara hizi? Watumiaji wa ndani pia imekuwa ni kero, tunamwomba Mheshimiwa Waziri aje atupe majibu ya Serikali kuhusiana na jambo hili.
Mheshimiwa Spika, suala la Port ya Kasanga, Kasanga Port kwenda Mlilo, Kasanga Port kwenda Kalemie, Kigoma kwenda Kalemie, Kigoma kwenda Uvira, Kigoma kwenda Bujumbura wanakwama wapi? Kwa mfano, kutokea Dar es Salaam mpaka Lubumbashi ni kilometa 1,870 na ukitoka Dar es Salaam mpaka Kasanga Port ni kilometa 1,200, kutokea Kasanga Port kwenda Lubumbashi kilometa 218, hawaoni kama sisi tunapoteza uchumi mkubwa?
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kilumbe Nge’nda amezungumza hapa kuhusiana na suala la biashara ya Congo, kutokea Kigoma kwenda Bujumbura kilometa 300, Kigoma kwenda Uvira kilometa 300, Kigoma kwenda Kalemie kilometa 250. Hawaoni kama uchumi wa Congo tunaupoteza? Huu uwekezaji wa bandari utakuwa una manufaa gani kwa nchi yetu? Congo kuna mizigo ya mbao, Congo kuna mizigo ya madini, Congo wanahitaji chakula kutoka Tanzania, sisi tutafanyaje biashara zetu?
Mheshimiwa Spika, tunazalisha chakula Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi na Kigoma, jamani Congo kuna biashara kubwa, sisi tunaofanya biashara na Congo ndio tunajua yaliyoko Congo. Congo wanataka mboga, dagaa na samaki lakini tutasafirishaje? Uwekezaji wa hizi bandari zote zilizojengwa kule, labda Mheshimiwa Waziri hajafanya ziara kwenye Ziwa Tanganyika aone uwekezaji uliowekezwa kule bandarini ni wa gharama kubwa hakuna mfano wake.
Mheshimiwa Spika, nakupa mfano mmoja kwa Bandari ya Mwanza, kutokea Mwanza kwenda Port Bell Kampala, Mwanza-Jinja, Mwanza – Kisumu, bandari ile tunavyozungumza haina hata crane, , hili jambo halikubaliki. Tumeenda pale na Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwenda kuona kwanza hata hii meli ya Mwanza, MV Mwanza, Hapa Kazi tu haina gati. Nimekwenda pale na Naibu Waziri wa Uchukuzi tulikuwa naye hakuna gati pale Mwanza. Meli inatakiwa ikabidhiwe mwezi huu, je, itatumia gati lipi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bandari yetu ya Mwanza tunaonewa, Bandari ile ya Mwanza hailingani na hadhi ya Mwanza. Tunaomba sana Waziri akija hapa atupe majibu lini ataboresha Bandari ya Mwanza. Hizi Bandari zetu zote zinatakiwa kufanya kazi, tunahitaji kutengeneza uchumi wa nchi hii kupitia kanda ya ziwa na sisi kanda ya ziwa ni wahanga tunapelekewa treni ya mwendokasi. Kama hatujajiandaa kutengeneza bandari, hii treni ya mwendokasi itafanya kazi vipi? Pia tuna meli ambayo mikataba yake ilisainiwa kwa ajili ya kubeba makontena ya kusafirisha kwenda Kisumu, Jinja na Port Bell Kampala, hatujui na yenyewe imekwama wapi. Sasa tunajua kwamba mipango mingi ya Serikali ni mizuri, lakini hawa wawekezaji wetu pia tunataka tujue ni namna gani wataweza kuboresha bandari yetu ya Mwanza.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nataka pia nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kuhusu suala la station ya Fella. Station yetu ya Fella mpaka sasa hivi ni kwamba inatengenezwa, lakini eneo lile pale la Fella kuna hekta mia tano. Hekta mia tano zimewekwa pale, uwekezaji ambao ulikuwa unatakiwa pale ni zaidi ya dola bilioni tano kwa ajili ya uwekezaji wa Bandari ya Fella, lakini hatuoni kazi inayofanyika pale na sisi tunategemea itafanya kazi kwa ajili ya kupokea mizigo ya Mara, Kagera na Mwanza, mizigo inayokwenda katika Nchi nyingine za Kenya na Uganda. Kwa hali hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri, naona bado anaongea huko na mimi hapa namweleza suala la Mwanza sasa inakuwa haifai namna hii, inaonekana kama labda hanisikilizi sasa.
SPIKA: Mheshimiwa Tabasam.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naam.
SPIKA: Mbunge ukiwa unachangia huongei na Waziri, unazungumza na Spika. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, lakini Waziri anatakiwa anisikilize.
SPIKA: Ukiwa unaongea naye moja kwa moja hasikii, ukiongea na mimi ndio anasikia na kanuni zinakutaka hivyo, ndio maana unasema Mheshimiwa Spika. Ukimtaja Waziri mimi nahesabu kwamba umeteleza kidogo. Kwa hiyo, wewe ongea na Spika, yeye anasikia yote, ukitaja Spika tu yeye anasikia, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naongea na Spika, lakini suala la Bandari yetu ya Mwanza... (Kicheko/Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Tabasam, sekunde thelathini malizia.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutuboreshea uwanja wetu wa Mwanza, huu uwanja wa Mwanza ulikuwa umesahaulika sana, kwa hiyo tunaenda kupata International Airport kutoka Mwanza.
SPIKA: Haya ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Nampongeza Pia Mtendaji Mkuu wa Viwanja vya Ndege Wakili Musa, Mwenyezi Mungu amjalie sana kwa kukubali kutengeneza Uwanja wetu wa Mwanza. (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mwenyezi Mungu amjalie, ahsanteni sana. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Kicheko/Makofi)