Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na pia namshukuru Mungu kuwa mchangiaji wa kwanza kwa siku hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya mchango wangu, nina mambo machache ya kusema ambayo ni ya kuipongeza Serikali na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu, mambo haya pamoja na kuwa ni ya kitaifa, lakini yanagusa maisha ya wananchi wenzangu wa mafinga. Baadhi ya mambo haya nitayataja kwa haraka kwa sababu ya muda na ni mambo yanayostahili kupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kiti kilishaongoza hapa ndani kwamba, vyovyote iwavyo hatutaruhusiwa kuruka sarakasi au kupiga magoti, kwa hiyo, mimi na wananchi wenzangu wa Mafinga, kesho saa 4:00 tumeamua kwa dhati ya mioyo yetu kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa haya ambayo nitaenda kuyasema hapa ambayo ametufanyia watu wa Mafinga. Sisi watu wa Mafinga maisha yetu ni misitu. Tumeona katika bajeti ya Serikali, baada ya kilio cha muda mrefu, hatimaye sasa VAT imeondolewa kwenye mti, jambo ambalo zamani hata mti ulikuwa unatozwa VAT. Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini kwa wananchi wetu wa Mafinga? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale watakapoenda kwenye shamba la Sao Hill, kama ana bill ya kulipa shilingi milioni moja ambapo angelazimika kulipa 1,180,000, sasa 180,000 ni ahueni, itaenda kuongezeka kwenye mtaji. Pia, hata cess, kadhalika tumeondoa kutoka tano hadi tatu. Maana yake ni kwamba tumempunguzia mzigo pia mfanyabiashara wa mazao ya misitu, na Halmashauri nayo tumeibakizia kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la kilimo, sisi ni wakulima. Tumeona katika hotuba ya Mheshimiwa Bashe, zaidi ya shilingi bilioni 150 zitaenda kutolewa kama ruzuku kwa ajili ya wakulima wetu. Hili ni jambo la kupongeza sana kwa sababu linagusa maisha yetu na uhai wa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa pia niombe kwa Mheshimiwa Bashe, sisi watu wa Mufindi, pamoja na kilimo ambacho tutaenda kuanza mwezi wa Kumi na Moja, sasa hivi tukishavuna tu mwezi wa Saba, tunarudi mabondeni kwenye kilimo maarufu tunakiita kilimo cha vinyungu. Nacho tutaomba hiyo mbolea ya ruzuku, pale mwaka wa fedha utakapoanza basi taratibu zianze kwa haraka ili nasi tunapoenda kulima kile kilimo cha vinyunguni, ambacho kinasaidia sana kujazia kama kunakuwa na upungufu wa chakula, basi tuanze kunufaika na kufaidika na matunda mema ya Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, tumepata mradi wa miji 28, ambao ni mradi wa maji ambao tulizungumza hapa Bungeni zaidi ya miaka saba. Wiki mbili zilizopita nasi Wabunge wa miji 28 tulialikwa pale Ikulu, wakandarasi wameshapatikana, wameshasaini, wanaingia kazini. Maana yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupata mradi huu, maana yake ni kwamba, akina mama wa Rungemba, Kitelewasi na Matanana, muda ambao walikuwa wanaupoteza kwenda kutafuta maji, sasa watatumia muda ule kufanya shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, yako mambo mengi ya kusema pale Mafinga, ndiyo maana nimesema tumeamua kwa sababu ya muda, sisi wana-Mafinga kesho pale Mafinga tutafanya shughuli maalum ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake. Yako masuala ya nguzo ambayo ilikuja taharuki kwamba zitanunuliwa nje ya nchi, lakini baadaye tumekaa na Mheshimiwa January Makamba, tumekubaliana na Serikali, nguzo zitanunuliwa hapa hapa nchini na maisha ya wananchi wetu yataenda kupata ahueni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile haitoshi, katika miundombinu, naipongeza sana Serikali, tumeona Barabara ya Mafinga – Mgololo. Pamoja na Serikali kuwa na sera ya kuunganisha mikoa kwa mikoa, lakini Serikali imeona umuhimu wa barabara hii kwa sababu za kiuchumi; barabara ya Mafinga kwenda Mgololo na Nyololo mpaka Mtwango ambayo itasaidia sana kusisimua uchumi wa Taifa letu, na pia uchumi wa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 35, ameeleza umuhimu wa kuwa na viwanda na vijana wafanye kazi saa 24. Nami naiomba Serikali, nimesema kwa miaka mitatu, minne, watu wa Mafinga tunaomba, watu ambao tunaishi kandokando ya barabara kuu kama Ruaha Mbuyuni, Tunduma, Mikumi, na Korogwe kwa shemeji zangu, turuhusiwe kufanya biashara saa 24. Hii Mheshimiwa Waziri nakuomba iwe kama ni sheria au kanuni au mwongozo. Kwa sababu, as it is now, tunafanya biashara saa 24 kwa kudra za kiongozi aliyepo eneo linalohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi tuna Mkuu wa Mkoa, Queen Sendiga, mwelewa sana, tuna Mkuu wa Wilaya, Saad Mtambule, mwelewa sana, tuna OCD mwelewa sana, walau anasema, jamani kusiwe na vurugu watu wafanye biashara wajiachie. Akija kiongozi ambaye sio mwelewa, kwa sababu hakuna sheria wala kanuni wala mwongozo, inakuwa tafrani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali itoe kama ni mwongozo au kanuni kwamba, baadhi ya maeneo watu wafanye biashara saa 24. Duniani kote watu wanafanya kazi kwa shift. Kama ulivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye viwanda unataka watu wafanye biashara saa 24. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais kupitia ile Royal Tour tunaamini kwamba kutaongezeka watalii wengi sana. Bajeti yetu asilimia 11.2 inategemea mikopo na misaada. Sasa kuna huu mradi wa Regrow, huu mradi wa kuendeleza utalii Kusini. Mradi huu ni fedha za mikopo kutoka Benki ya Dunia. Ni mradi ambao Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais, tarehe 12/2/2018 tuliuzindua pale Iringa. Mojawapo ya manufaa ya mradi huu ni kuboresha sekta nzima ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumza sasa mradi huu una miaka mitano, utekelezaji wake unaenda ukisuasua. Kwa mujibu wa kalenda ya utekelezaji, ilitakiwa kufikia sasa hivi iwe imeshatumika wastani wa Dola milioni 111, lakini mpaka sasa hivi kuna maeneo ya kuboresha. Kwa mfano, ku-upgrade viwanja vya ndege, kujenga barabara na kuimarisha mafunzo. Sasa katika mbuga zetu ikiwemo Mbuga ya Ruaha National Park, haya mambo yote yakifanyika, hata mimi wananchi wangu wa Mafinga watauza mbao, watauza milunda, watauza nguzo kwa watu wanaojenga mabanda kule kwenye National parks. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kwa miaka mitano unaenda ukisuasua, lakini bad enough huu ni mkopo. Kwa hiyo, tunapochelewa kuutendea haki maana yake hatupati returns kwa wakati, maana yake tutakuja kulipa mkopo ambao tumejichelewesha sisi wenyewe. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Maliasili na Utalii inayohusika na jambo hili, sasa lifanyike kwa speed. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kengele imelia, nimelisema sana suala ambalo kama Taifa tunaweza kunufaika na mifuko inayotoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mheshimiwa Rais alienda Glasgow akashiriki ule Mkutano wa Mazingira na akapata nafasi ya kuzungumza, akayaambia Mataifa makubwa kwamba tunaomba muheshimu ahadi zenu. Kwa sababu, Mataifa makubwa ndiyo wanaoongoza kwa kuharibu mazingira. Sisi huku tukipanda miti Mafinga, Mufindi na kwingineko, tunasaidia katika haya mambo ya carbon emission. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kifuko ambayo inatoa fedha. Sisi kama Taifa, juzi alisema Mbunge wa Kiteto, ni taasisi mbili tu, nami nazipongeza; NEMC na CRDB ndizo ambazo zinanufaika na hizi fedha. Hizi fedha nyingi ni grants wala siyo mikopo. Tupate hizi fedha, tunaweza kujengea miradi ya umwagiliaji kule Mafinga. Wananchi wetu tunaweza tukawapa miche zaidi ya kupanda tukakabiliana kwa namna moja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho au la pili kutoka mwisho ni hizi mamlaka za udhibiti. Kuna hizi taasisi, regulatory authorities; Mheshimiwa Mkapa Mungu amlaze mahali pema; Serikali ya Awamu ya Tatu iliona kuna umuhimu sana, nchi inayoendelea huwezi ukaacha mambo yawe holela holela, lazima uwe na vyombo vya ku-regulate hali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa vyombo hivi vingi unavikuta viko chini ya Wizara ambazo vyenyewe vinahusika kuzi-regulate. Tuna SUMATRA, LATRA, EWURA, TASAC, naomba mkasome literature za mambo ya regulatory authority. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, hivi vyombo vinapaswa viwe independent. Kama haviwi chini ya Ofisi ya Rais, basi viwe chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili vipate ile nguvu kweli ya ku-regulate. Leo hii huyu regulatory authority, huyu huyu anawajibika kwa Katibu Mkuu fulani au kwa Waziri fulani. Kama tuko open minded, tunataka kuisaidia nchi, hebu tutengeneze utaratibu hizi regulatory authorities zipate uhuru unaotosheleza ili kweli ziweze kufanya kazi hiyo ya ku-regulate uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, nawashukuru sana wote na wale ambao watakuwa wako tayari kuungana nami kesho Mafinga, karibuni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mungu awabariki na Mungu abariki Taifa letu. (Makofi)