Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Pandani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai na uzima na pumzi yake nikaweza kusimama katika Bunge hili Tukufu leo hii. Pia nakushukuru wewe kwa kunizawadi nafasi ya pili katika kuchangia bajeti kuu ya Serikali kwa siku hii ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yote nakumbuka katika kumbukumbu zangu nilivyokuwa nikichangia mchango mwaka 2021 nilimwambia kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu sitampongeza mpaka pale atakaporudi tena ili nione mpango ule tulioupanga 2021/2022 umefikia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako, naomba niondoe ahadi yangu kwa kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa ule mpango uliopita, kwani umezidi ile asilimia 70 niliyosema. Hongera sana pamoja na wasaidizi wako wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika mpango huu na nianze kwa kuizungumzia asilimia kumi. Mpango huu ni mzuri sana na umekaa vizuri kuliko ule uliopita, lakini endapo tutaitoa asilimia tano kwenye asilimia kumi itakuwa tumeharibu, wala itakuwa hatujatengeneza ule mpango. Kwa sababu tunaweza kupunguza pale ambapo tayari tumekidhi haj ana hatuwezi kupunguza sehemu ambayo bado ina uhitaji. Katika asilimia kumi, bado tuna uhitaji mkubwa wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliamini pengine mpango wa mwaka huu tutakuwa na asilimia 20 badala ya asilimia kumi. Sasa tukisema asilimia kumi hii tuende tukaipunguze, Hapana. Naomba Mheshimiwa Waziri atafute namna kwenda kuwawezesha Wamachinga; tunawapenda na tunawajali pia, lakini siyo kwa kupunguziwa asilimia kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili niende kwenye elimu bila ada, niipongeze Serikali wamefanya jambo la maana sana, lakini bado kama hatukuendelea na utaratibu mzuri hii kuondoa ada tu haitosaidia kwa sababu utitiri wa michango ndiyo unaotuumiza wazazi na siyo ada. Endapo kwamba tutaweka vizuri michango yetu kwenye hii elimu ya juu kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita basi tutakwenda vizuri huku tukiwa tumeshaondoa hii ada, lakini tukiendelea na mfumo huu huu wa michango mfululizo bado tutaendelea kusikia vilio vya wazazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja kwa vile mimi ni Balozi wa Mazingira niende kwenye mazingira na nitaizungumzia hewa ya ukaa. Duniani sasa hivi kilio kikubwa kwenye uharibifu wa mazingira ni hewa ya ukaa na nikiangalia katika bajeti ya mazingira bado ni ndogo sana kuweza kuhimili hii hali. Sasa ushauri wangu kwa Serikali hapa, hewa ya ukaa inasababishwa sana na viwanda vyetu, ifikie muda tupate fungu moja kwa moja katika hivi viwanda viingie kwenye Mfuko wa Mazingira ili kuweza kuikabili hii hali fedha iliyopangiwa mazingira ni ndogo sana hatuwezi, mazingira tuna kampeni ya upandaji wa miti kwa kuweza kulihimili suala hili la mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu kwenye kingo za bahari, bado bahari inaendelea kula ardhi zetu, kingo ambazo zimejengwa bado ni chache, tukiliingiza na hili la hewa ya ukaa bado fedha ni chache mno, hebu tujitahidi, hata kama ni kuja na sheria viwanda viweze kutoa fungu moja kwa moja. Nasema hivi kwa sababu sisi tumetembelea viwanda vingi, mimi nipo kwenye Kamati ya Uwekezaji, Viwanda na Mazingira, sijaona sehemu ambayo kiwanda kimepangiwa fungu linaloingia moja kwa moja kwenye mazingira. Wachafuzi wakuu kwenye mazingira, hawa watu wa viwanda wanahusika moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo nilizungumzie suala la mwani. Nalizungumzia suala la mwani nikiwa ni mdau mmojawapo wa mwani kwa sababu katika Jimbo langu asilimia 90 wanategemea kipato kupitia mwani. Hata hivyo, wafanyabiashara wa mwani ndiyo wanaofaidika kuliko wakulima wa mwani. Mkulima hafaidiki na chochote, nataka nikupe hesabu ndogo ambayo nimeipata kutoka kwa wakulima wangu wa mwani. Shamba moja la mwani linatumia kamba vipande 200. Ukipiga hesabu kipande kimoja cha kamba ni Sh.2,000 x 200 = 400,000, hii ni kamba tu. Katika kilimo cha mwani tunategemea pia vipande vya miti, kule kwetu tunaita pegi, lakini Naibu wa Fedha anaweza kunisaidia hata vipigi tunavitumia, ni msemo sahihi kwa kule kwetu, umeshanifahamu? Korija moja ya hivyo vipande ni Sh.10,000. Ili shamba likamilike katika standard yake linahitaji korija tano za vipande ambapo ni sawa na Sh.50,000, ambapo ukijumlisha na ile Sh.400,000 inakuwa Sh.450,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, twende sasa katika uvunaji, tuangalie huyu mwananchi anafaidika na nini? Hafaidiki na chochote kile kwa sababu kama mwani utastawi vizuri shamba moja unavuna kilo 230 tu, kilo moja ya mwani mkavu ni Sh.700, kitu ambacho mwani mkavu kilo moja ni saw ana mwani mbichi kilo nne. Kwa hiyo mwani mkavu kilo moja ni mwani mbichi kilo nne ambao ni Sh.700. Hebu piga hili mara 230 ya mwani mbichi atapata kilo ngapi? Nilivyofanya nilipata 57.5, nikizidisha mara Sh.700 anapata Sh.40,250, hapo alishatumia Sh.450,000. Jamani bado ni kilio kikubwa sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalisema kwa huzuni, Serikali tuingilie kati, twende tukatafute masoko, tutafute wawekezaji na bado mwani huu hauliwi katika kiwango standard, wakulima wetu hawana elimu ya hili zao. Nchi nyingi zimefaidika kutokana na mwani, kwa nini Tanzania tushindwe? Kama tunatafuta vyanzo vya mapato hiki ni kimojawapo. Kama tutaliboresha hili zao likaingia kwenye zao la Taifa kama ilivyo karafuu kule Zanzibar, basi ndivyo itakavyokuwa mwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali bado tuliingilie kati hili zao. Nashukuru Wizara ya Mazingira kupitia Mfuko wa Mazingira, Mheshimiwa Jafo anafahamu, walitujengea kaushio moja la mwani kule Makangale, lakini bado tuna uhitaji sana kwa sababu niwaambie mwani ni chakula, unatumika kama mbogamboga kama zilivyo mbogamboga nyingine, mwani unaweza kutengeneza juice, tena una juice nzuri sana, kama jana Mheshimiwa Omar alisema leo niwaweke wazi kila alichokimaanisha ukinywa juice ya mwani ni sawa na umekunywa juice ya tende. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo twende tukawekeze kwenye mwani bado tuna mahitaji sana kwenye mwani. Tukiwawezesha wakulima wa mwani, basi tutapiga hatua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ahsante sana. (Makofi)