Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye bajeti kuu. Namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuamsha salama na anaendelea kutupa uhai. Nataka kuipongeza Wizara kwa kutuletea bajeti nzuri, bajeti ambayo inajenga matumaini ya Watanzania. Yapo mambo machache ningependa niyaseme ili tuone jinsi ambavyo tunaweza kuboresha bajeti yetu na vile vile tuweze kupata maendeleo kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo moja ninalotaka kuchangia ni uzalishaji wa cement katika nchi yetu. Tangu mwaka 2015 tumeona uzalishaji wa cement katika nchi yetu ukiongezeka kutoka metric ton milioni 3.0 mpaka kufikia metric ton million 6.5 mwaka jana. Hii ni hatua kubwa kwa sababu cement ina mchango mkubwa sana katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu. Tunaipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri yaliyovutia uwekezaji katika nchi yetu na kukuza uzalishaji wa cement katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukipongeza hivi tunaanza kuona dalili ambazo zinaweza kuvuruga mambo mazuri tunayoyaona kwenye sekta hii. Mwaka jana mwezi Oktoba, kampuni mbili kubwa za kimataifa moja inayojulikana kama Skansen International ambayo ni subsidiary ya Heidelberg Cement ambao wanamiliki Twiga Cement na Kampuni ya African Mauritius International ambao ni wamiliki wa hisa kwenye Tanga Cement walitoa a cogent statement kwamba Skansen wanaenda kumiliki 68.33% ya Tanga Cement na umiliki huu ulikuwa na thamani ya bilioni 137. Sasa tangu mwaka jana mwezi huo Oktoba kumekuwa na sintofahamu kwa wadau waliopo katika sekta hii, wakisema kwamba umiliki huu wa hisa unaenda kuvuruga unaenda kuwa ni kinyume na sheria yetu. Unaenda kuleta mazingira ya ushindani usio sawa kwa sababu inaenda kuiwezesha Skansen kuweza kumiliki soko la cement nchini kwa 47% kinyume na sheria zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa ndipo tulipo na hofu na hasa sisi watu wa Tanga kwa sababu Tanga Cement ni muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Tanga, lakini vile vile ni ukweli kwamba Tanga Cement ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Tanga Cement kwa Tanga ni mwajiri muhimu sana kwa watu wetu, kwa hiyo sisi hatuko tayari kuona sekta hii inatikisika kwa sababu Tanga ni wahanga wa kupoteza ajira kwa sababu ya mambo ya namna hii. Viwanda vingi vimefungwa Tanga baada ya hisa zake kumilikiwa na watu wengine na matokeo yake tukapoteza ajira. Tumeona baadhi ya viwanda umiliki wa hisa ulipobadilika viwanda vile vimefungwa mashine zimeondolewa kule Tanga zimeenda kuwekezwa kwenye mikoa mingine. Kwa hiyo kwetu sisi hili ni jambo kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiuchumi na kwa usalama wa nchi yetu, nyinyi wote hapa ni mashahidi, ukitokea mtikisiko kidogo tu kwa wazalishaji hawa wa cement, tunaona jinsi ya ambavyo bei ya cement katika nchi yetu inapanda na inaleta kilio kikubwa kwa watu wetu. Sasa kama tunakwenda kuruhusu mmiliki mmoja amiliki 47% ya soko yeye peke yake, kinyume na sheria ya nchi yetu nadhani siyo sawa, kwa sababu ikitokea siku moja mtu huyu anayemiliki 47% akaamua asizalishe kwa sababu tu hajatekelezewa mambo fulani nchi yetu itakuwa kwenye matatizo. Najua jambo hili liko Fair Competition Commission lakini linachukua muda kushughulikiwa, Waziri wa Fedha aingilie kati, jambo hili lipatiwe ufumbuzi haraka ili nchi yetu isiingie kwenye matatizo. Waziri wa Fedha anajua, mapato anayoyapata kutokana na sekta hii tusiruhusu sekta hii ikaingia mtikisiko utakaotusababishia kukosa mapato kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni kwenye eneo la Vyuo vya VETA, naipongeza sana Serikali, nami kwa niaba ya watu wa Mkinga naishukuru Serikali kwa kutujengea Chuo cha VETA. Chuo kile kitaleta ukombozi mkubwa sana kwa watu wa Mkinga, Mheshimiwa Naibu Waziri alipotembelea Mkinga tuliahidiwa kwamba ikifika mwezi Julai, vyuo vile vitakuwa vimekamilika ujenzi wake na itaanza kudahili na leo hii amesema hivyo hivyo. Hata hivyo, kwa sisi tunaojua kinachoendelea site tuna wasiwasi kwa mambo mawili, kwanza kuna uhaba mkubwa sana wa Walimu kwenye vyuo hivi, sina uhakika kama tumejiandaa vizuri kuhakikisha vyuo vyote hivi vitapata Walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kasi ya ukamilishaji wa vyuo hivi na kupeleka vifaa vya kufundishia bado hatuoni kwamba mwezi wa Julai itafanikiwa. Tunaiomba Serikali iongeze kasi katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni Mfuko wa Mafuta na Gesi, taarifa zinaonesha kwamba Mfuko ule sasa tumekwishakusanya zaidi ya bilioni 295.5, lakini fedha hizi haziisaidii TPDC kuendelea kuwekeza kwenye sekta hii, lakini vile vile kuweza kufanya utafiti. Hii ni kwa sababu ya matakwa ya sheria. Wakati tunapitisha sheria ile matarajio yetu ilikuwa kwamba tutapata mapato makubwa ndani ya kipindi kifupi, lakini ukweli siyo hivyo. Ili tuisaidie TPDC ifanye majukumu yake ya utafiti na iweze kufanya biashara ya mafuta, tunaishauri Serikali twendeni tukafanyie marekebisho Sheria ile ili TPDC iweze kupata mtaji kutoka kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa TPDC naelewa, kipindi ambacho TPDC ilifanya kazi kubwa ya utafiti ni kipindi ambapo ilikuwa inafanya shughuli ya biashara ya mafuta. Baada ya kuondoa shughuli ya biashara ya mafuta kule TPDC, kasi ya utafiti kwa TPDC imekuwa ndogo kwa sababu fedha ilizokuwa inapewa ni chache. Twendeni tukaisaidie TPDC hasa kipindi hiki ambacho kuna sintofahamu kwenye Sekta ya Mafuta duniani ili TPDC iweze kutukomboa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)