Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia mpaka muda huu nikiwa na afya njema na kunipa kibali cha kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kuchangia hotuba hii ya bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Marais wangu; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuudhihirishia ulimwengu uwezo wake, umahiri wake wa kuliongoza Taifa letu. Watanzania wana matumaini makubwa kwa Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimpongeze sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ally Mwinyi kwa kazi kubwa anayoifanya kule Zanzibar. Sasa hivi ukija Zanzibar ni mafuriko ya miradi ya maendeleo. Kila sehemu ni miradi ya maendeleo maskuli yanajengwa kwa wingi sana na vituo vya afya kila sehemu. Kiukweli Mheshimiwa Dkt Hussein Mwinyi kwa upande wake wa Zanzibar na yeye anaupiga mwingi sana. Yote haya ni kutokana na ushirikiano mkubwa ambao anaupata kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli tunawapongeza sana Viongozi wetu hawa Wakuu wa Kitaifa, kazi wanayoifanya ni nzuri sana na inaleta matumaini kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nichukue nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake pamoja na timu yote ya Wizara ya Fedha kwa wasilisho zuri la bajeti, ni bajeti ambayo inakwenda kujibu changamoto za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo sasa nielekee kwenye mchango wangu na nitachangia mambo mawili; suala la kilimo cha mwani, pamoja na suala la uvuvi. Kwa kawaida duniani kote wananchi wanategemea kuendesha maisha yao kutokana au kutegemeana na rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amewajaalia katika Taifa lao, ni vivyo hivyo kwa wananchi wa Tanzania. Kwa upande wa Zanzibar kama tunavyofahamu Zanzibar ni nchi ya visiwa ambavyo eneo lake kubwa imezungukwa na Bahari kuu ya Hindi. Hapa maana yake wananchi hawa wa Zanzibar watategemea bahari kama rasilimali yao. Kwa upande wa Serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi hawa inawajengea mazingira mazuri na mazingira wezeshi katika kuhakikisha kwamba wanatumia rasilimali hii ili kuweza kujipatia kipato cha kuendeshea familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali nitagusia zao la mwani. Kama nilivyosema eneo la ardhi kwa Zanzibar ni dogo sana, hivyo wananchi hawawezi kujishughulisha na shughuli za kilimo kwa vile eneo la ardhi ni dogo, maana yake wananchi hawa wa Zanzibar hususan Pemba wamejiajiri kwenye zao la mwani kama ndivyo zao la mwani. Wananchi wa Pemba au wa Zanzibar wamelichukulia zao la mwani kama ni kilimo mbadala, badala ya kuelekea kwenye ardhi maana yake wanaelekea baharini kulima zao hili na ni zao ambalo kwa sasa limeajiri wananchi wengi. Wananchi hawa ambao wamejikita kwenye kilimo cha mwani ni wananchi wenye kipato cha chini na hususan akinamama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la mwani ni zao ambalo linalimwa na nchi mbalimbali ulimwenguni ikiwemo China, Indonesia pamoja na Philippine. Kuna aina mbili za mwani; kuna cottonii na spinosum farm. Hizi ni aina ambazo zinalimwa ulimwenguni miongoni mwa nchi zinazolima ni kama nilivyozitaja. Mwani unatumika katika matumizi mbalimbali Wabunge wenzangu wengine wameelezea vya kutosha, unatumika kama chakula, madawa, unga, mbolea pamoja hata mapambo ya nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile unatumika kiongozeo cha ladha katika vyakula, kutokana na faida hii tumeona nchi ambazo zinazalisha mwani mfano Indonesia wananchi wake wanapata faida mbalimbali, na wanaendesha familia zao kutokana na kilimo hichi cha Mwani. Kwa mfano, mnamo miaka ya 2015 katika familia moja iliweza kuzalisha takribani tani 70,000 kwa familia moja na kuweza kuingiza kipato wastani wa Dola 15,000 ambayo ni sawa na fedha ya Kitanzania 34,500,000 hiki ni kipato kikubwa sana kwa mwananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuangalie wananchi hawa wa Indonesia katika Kijiji cha Solowesi mwaka 2015 waliweza hadi kufikia familia kupata kipato cha Milioni 34 fedha ya Kitanzania hili ni pato kubwa sana, sasa ni wakati Serikali yetu kuona kwamba inalitilia maanani na kulipa umuhimu zao la mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameelezea vizuri mikakati ya Uchumi wa Bluu na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri amelielezea katika kitabu chake cha bajeti kwenye ukurasa wa 76 mikakati ya Uchumi wa Bluu, nimuombe Rais wa Zanzibar na Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba katika Sera au mikakati ya uchumi wa bluu kwa upande wa Zanzibar kipaumbele kiwekwe kwenye zao la mwani, kwa sababu ni zao ambalo limebeba wananchi walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar wananchi walio wengi wamejiajiri kwenye zao la mwani, sasa nimuombe sana Mheshimiwa Rais, miongoni mwa vipaumbele katika mikakati ya kulikuza au kukuza sera ya Uchumi wa Bluu iwekwe kwenye zao la mwani, atatusaidia sana Wazanzibar. Nimuombe sana Mheshimiwa Rais na niiombe Serikali zao la mwani wasione kwamba labda ni zao la kiwango cha chini, ni zao ambalo linaweza kuwasaidia sana wananchi na linakwenda kuwakomboa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nilivyoelezea umuhimu wa mwani wakulima wetu wa mwani wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali, miongoni mwa changamoto hizo kwanza inaonekana Serikali bado haijailipa uzito wa kutosha zao la mwani, changamoto ya pili wakulima wetu bado wanalima kienyeji hawana elimu ya kutosha juu ya zao hili, lakini kama haitoshi zao la mwani kwa kawaida linastawi zaidi katika kipindi cha mvua na kipindi cha kiangazi halistawi kutokana na temperature kuwa katika hali ya kiwango cha juu. Kama ndivyo, maana yake katika msimu huu wa mvua ambao zao la mwani linastawi vizuri zaidi, wakulima wanajitahidi kulima lakini changamoto inajitokeza wakati wa ukaushaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu zao la mwani linahitaji jua ili kuweza kukaushwa na kuweza kupelekwa sokoni. Sasa maana yake wananchi wanapolichukua zao la mwani, wanapolitoa baharini na kwenda kulikausha hatimae inanyesha mvua, na kawaida ya mwani unaponyeshewa na mvua, mara moja tu maana yake umepoteza uhalisia wake wote, na hivyo kumtia hasara mkulima. Changamoto nyingine ni suala la bei, mara nyingi wanaonunua mwani ni matajiri au kampuni na hatimaye kampuni hizi au matajiri hawa wanapanga bei ambazo wanazitaka wao, bei ambazo zinamuumiza mkulima, hizi ni changamoto ambazo kwakweli zinasababisha wakulima wetu kupata hasara kubwa na kutoweza kuona ile faida ya kilimo chao cha mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kama nilivyoelezea wakulima wetu wanaliendesha zao hili bila utaratibu mzuri, bila kutumia utaratibu wa kibiashara, bila kuzingatia kwamba labda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali sasa itujengee makaushio ili wakulima waweze kukaushia mwani wao katika kipindi cha mvua, vile vile niiombe Serikali…