Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha kwa kutuwasilishia bajeti nzuri ya kimkakati, pia kipekee kabisa nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anafanya kwenye Taifa letu nasi sote tumekuwa ni mashahidi namna ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akihangaika usiku na mchana katika kutafuta fursa mbalimbali za kuzileta katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi kwamba Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana na hivi juzi tumeshuhudia akizindua filamu ya Royal Tour, filamu ambayo ndani ya muda mfupi tumeanza kuona athari chanya kwani kumekuwa na ongezeko kubwa sana la watalii katika nchi yetu, hali iliyopelekea hata Shirika la Ndege la Precision kurudisha safari zake katika hifadhi ya Serengeti, sasa hivi inaenda mara tatu kwa wiki, hii ni dalili ya kuonesha kwamba watalii wanakuja kwa wingi sana katika nchi yetu, kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe ushauri kwa Wizara kwa sababu tunafahamu Mama ameshatufungulia mlango na kutuonesha njia, ni jukumu lao sasa kama Wizara kuja na mikakati mizuri ya kuhakikisha kwamba tunakuza sekta nzima ya utalii. Jambo la msingi la kufanya kwanza ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na mitandao mizuri ya barabara inayoenda katika hifadhi zetu pia na barabara ambazo zipo ndani ya hifadhi. Vilevile tunayo kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba tunatangaza vivutio vyetu vya utalii kwani Tanzania tumebarikiwa kuwa na vivutio vingi sana vya utalii, lakini wazi bado vingi havijatangazwa na havijulikani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ninataka nitoe ushauri kwa Wizara kwamba tunafahamu kwamba nchi nyingi sana ambazo hazina vivutio vya utalii lakini zinafanya vizuri sana kwenye sekta ya utalii, tafsiri yake ni nini, tafsiri yake ni kwamba utalii siyo tu wa Wanyama, maana yake vipo vitu vingine ambavyo kama vikifanyika vitasaidia sana kuweza kukuza sekta ya utalii. Kwa hiyo, niwaombe Mawaziri watilie mkazo kwenye kuvumbua vivutio vipya vya utalii. Tunao utalii wa fukwe katika nchi yetu lakini vilevile tunao utalii wa utamaduni ambao ni muhimu sana, mimi ninaamini Serikali pamoja na Wizara ikiwekeza nguvu yake huko itasaidia sana kuweza kukuza sekta ya utalii katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie pia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa kusikia kilio cha wananchi wa Mkoa wa Songwe. Kwa muda mrefu sana tulikuwa tukiomba kupatiwa Chuo cha VETA na katika bajeti hii tumeambiwa kwamba Serikali sasa inakwenda kutuletea chuo cha VETA katika Mkoa wa Songwe. Nitoe ushauri sasa kwa Serikali kwamba kwa sababu Mkoa wa Songwe ni mpya mimi niombe kwamba wafanye utafiti ili kuweza kujua fursa gani za kiuchumi ambazo zipo ndani ya Mkoa wetu wa Songwe ili kozi zile ambazo zitaanzishwa pale ziwe ni kozi ambazo zinaendana na fursa za kiuchumi ambazo ipo ndani ya Mkoa wetu wa Songwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kumekuwa na changamoto moja ya uniformity kwamba kozi ambazo zipo Singida, kozi ambazo zipo Mtwara zinakuja zinawekwa na Songwe, lazima tufahamu kwamba mazingira ya kiuchumi yanatofautiana. Kwa hiyo ni jambo la msingi sana wafanye utafiti kujua fursa mbalimbali za kiuchumi, ambazo zipo ndani ya Mkoa wetu wa Songwe ili kozi ambazo zitaanzishwa pale ziweze kuwanufaisha vijana ikizingaitwa kwamba Mkoa wa Songwe ni lango la SADC, kwa hiyo zipo fursa nyingi sana za kiuchumi katika Mkoa wetu wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nizungumzie suala zima la asilimia 10. Wakati nikichangia bajeti ya TAMISEMI humu Bungeni, nilitoa ushauri kwa Serikali, kwamba Serikali iangalie sasa uwezekano wa kuongeza asilimia Tano ili ziwe asilimia 15, kwa ajili ya kwenda kuweka miundombinu ya machinga, hiyo asilimia tano ikaweka miundombinu ya machinga lakini asilimia kumi ibaki kwa ajili ya kuhudumia akinamama, kuhudumia vijana pamoja na makundi maalum. Ninasikitika sana katika bajeti hii tumeambiwa kwamba asilimia tano inatolewa kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Mbunge wa wanawake wa Mkoa wa Songwe ambaye wanawake wa Mkoa wa Songwe wameniamini na kunileta humu Bungeni nisimamie nakutetea maslahi yao ninasema kwamba hiki kitu siyo sawa na hakikubaliki!
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hakikubaliki kwa sababu gani, lengo la Serikali la kuleta hii asilimia kumi na mwisho wa siku tukaitungia sheria ndani ya Bunge hili, ni kuhakikisha kwamba wanawake, vijana na makundi maalum wananufaika na hii fursa ya asilimia 10. Lakini tunafahamu kwamba makundi haya matatu yana changamoto kubwa sana wanapoenda kuomba mikopo katika benki zetu wengi wanakuwa hawana hati za nyumba wengi hawana hati za viwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali ikaona yenyewe iingie kuwa mdhamini wa makundi haya matatu, vilevile tunafahamu kwamba kuna changamoto kubwa sana ya ajira katika nchi yetu, Serikali peke yake haiwezi kumaliza changamoto ya ajira, ndiyo maana Serikali ikaona iweke sasa mazingira mazuri ili vijana wawe na sehemu ya kwenda kukopa na akinamama na makundi maalum ili waweze kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niiombe sasa Serikali, tunaomba ibadili msimamo wake juu ya jambo hili kwa sababu athari yake ni kubwa. Ukiangalia takwimu za mikoa sasa hivi vikundi ambavyo vimeshapata mikopo ni vichache kila mwaka kuliko vikundi ambavyo havijapata mikopo. Tafsiri yake ni kwamba bado kuna uhitaji mkubwa sana wa hii asilimia kumi; na tulidhani kwamba ingewezekana Serikali ingeongeza hii asilimia na si kuipunguza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na sote tunafahamu kwamba mama yetu, Rais wetu Samia Suluhu Hassan, alishatuambia kwamba wanawake wa Tanzania tutamuweka madarakani mwaka 2025, na hizo kura za wanawake wa Tanzania zinatafutwa na sisi Wabunge wa Viti Maalum, sisi ndio tunaokwenda kwa wanawake wenzetu kumuombea kura Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, na moja wapo ya vitu ambavyo sisi huwa tunavitumia ni hii asilimia kumi. Ndiyo maana wakati nikichangia kwenye TAMISEMI niliishauri Serikali, kwamba iangalie sasa namna sisi Wabunge wanawake kuhusishwe katika kusimamia hiyo asilimia 10 ambayo inakwenda kwa akina mama, vijana pamoja na watu wenye ulemavu. Lengo lake ni ili iweze kuleta tija inufaishe Watanzania, na ikifika mwaka 2025, sisi Wabunge tukienda kutafuta kura za Mheshimiwa Rais kwa wanawake wenzetu, Mheshimiwa Rais aweze kushinda kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nitoe mapendekezo kwa Serikali. Ushauri wangu wa kwanza; mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, suala hili la asilimia 10 libaki kama lilivyo; asilimia nne iende kwa akina mama, asilimia nne iende kwa vijana na asilimia mbili iende kwa watu katika makundi maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuwa tunafahamu kwamba katika nchi yetu tuna majiji, tuna manispaa, na lengo la hii asilimia tano ambayo inataka kutolewa kwenye asilimia 10 ni kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu. Sasa kwa sababu lengo ni jema, niishauri Serikali, kwamba kwa sababu tunajua machinga wengi wanapatikana kwenye majiji na manispaa tofauti na maeneo mengine, lakini tunafahamu kwamba majiji pamoja na manispaa wana makusanyo makubwa kuliko maeneo mengine, kwa hiyo nitoe ushauri kwa Serikali; kwamba majiji pamoja na manispaa wao watenge hizo asilimia 15 ili asilimia tano iende kwenye kurekebisha na kujenga miundombinu kwa ajili ya machinga. Kama ambavyo wenzetu wa Dodoma wamefanya. Dodoma wamefanya, wametumia own source, na tumeona wamefanikiwa katika hilo. Kwa hiyo naamini hata kwenye majiji na manispaa nyingine zinaweza zikafanya na zikafanikiwa kwa sababu lengo ni jema, na ni kitu ambacho huwezi kujenga miundombinu kila siku, maana yake tutajenga tutafika mahali tutamaliza, wataendelea kutenga asilimia 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la tatu ambalo ninataka nishauri Serikali; sote tunakubaliana kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana hasa kwenye ukopeshaji wa hii mikopo ya asilimia 10, lakini vilevile kwenye urejeshaji wa hii mikopo ya asilimia 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii ni kubwa sana, ndiyo maana mimi nikajaribu tu kushauri kwamba Serikali iangalie kwamba na sisi viongozi ambao ndio tunakwenda kuomba kura tuhusishwe katika kusimamia hii fedha kwa sababu tunajua wahusika wanaotakiwa kupata ni akina nani.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nitoe ushauri; lengo siyo kutoa asilimia tano, haiwezi kuwa solution. Mimi nitoe ushauri kwamba Serikali sasa ije na mkakati maalum kuhakikisha kwamba hii fedha inawafikia wahusika. Ahsante. (Makofi)