Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Bajeti kKuu ya Serikali. Cha kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa bajeti nzuri, bajeti ya mfano, bajeti ambayo imebeba matarajio ya Watanzania kwa ukubwa wake. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa bajeti nzuri, bajeti ya viwango. Nakumbuka tu maneno aliyosema kwamba you will be unpopular Finance Minister. Naamini utakuwa ni popular kwa sababu bajeti kama itatekelezwa kwa asilimia 100 utakuwa umeandika historia kubwa sana kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, napenda kushukuru kwa miradi ambayo sisi wananchi wa Makete tuliomba kwenye bajeti. Miradi mingi tumepitishiwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, Makao Makuu ya Wilaya, barabara kutoka Makete kuelekea Mbeya, lakini tumepewa bwawa la umeme la Shilingi bilioni nane. Kwa hiyo, tuna miradi mingi kwenye bajeti hii imepitishwa. Kwa niaba ya wananchi wa Makete, tunamshukuru sana Rais na Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina michango yangu kwenye maeneo mawili au matatu. Eneo la kwanza ni Jeshi la Polisi. Eneo hili kuna haja ya kulifanyia kazi. Polisi wetu wanafanya kazi kubwa ya ulinzi na amani ambayo tunayo, lakini ukiangalia vote yao na fedha zao zinatengwa kwa uchache sana. Kuna mahitaji compulsory ya Jeshi la Polisi lakini bado nayo hayatimizwi kwa vigezo vile vinavyotakiwa. Kwa mfano, ukienda kwenye suala la uniform za Polisi, takribani miaka 10 sasa Polisi hawajawahi kununuliwa uniform, wanajinunulia kwa gharama zao. Leo hii tukiitwa Polisi wa Tanzania hapa wakapangwa foleni, rangi ya vitambaa vya Jeshi lao, kila mtu ana rangi yake. Sasa ni jambo ambalo kama Wizara ni lazima tulichukulie katika uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, angalia mahitaji ya nyumba za Polisi. Polisi kwa sasa kwa kiwango kikubwa wamekuwa wakiishi kwenye makazi na raia wa kawaida. Nyumba zao ambazo zilijengwa toka miaka ya 1960 hadi leo hazina hadhi tena ya kuendelea kutumika na Askari wetu wa Jeshi la Polisi. Angalia Dodoma!
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuathiri mchango wa Mheshimiwa Sanga, ambaye ni mchangiaji mzuri nataka tuweke sawa mambo hapa kwamba Jeshi la Polisi linanunuliwa uniform, na kila mwaka zinatengwa fedha kwa ajili hiyo. Labda aseme kwamba hazitoshi, lakini akisema hawajawahi kununuliwa uniform miaka 10, mtu ambaye hajanunuliwa uniform miaka 10 hali yake haiwezi kuwa hivyo. Siyo kweli kwamba Jeshi la Polisi wanajinunulia uniform. Upo utaratibu ambao unatumika. Kwa hiyo, nilitaka tuweke sawa ili mchango wake uwe mzuri zaidi, basi tuendelee. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sanga, mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Ni kweli anachokisema Mheshimiwa Waziri. Tuendelee. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilindie dakika zangu, kwa sababu nina mambo mengi ya kuchangia. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, niseme napokea taarifa yake kwamba fedha hazitoshi lakini naomba waliangalie kwa ukaribu sana hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri ni kwamba Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ni mmoja kati ya ma-senior minister ndani ya Serikali yetu. Amepita Wizara ya Katiba, Wizara ya Kilimo, Naibu Waziri wa Fedha, Wizara ya Mambo ya Ndani, haya mahitaji yote anayajua.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri mhusika.
T A A R I F A
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Naomba pia kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge. Kwanza naunga mkono taarifa ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na uniform za polisi. Niongezee na taarifa nyingine kwamba katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya mkakati wa miaka 10 ya ujenzi wa nyumba zaidi ya 51,000 za Polisi nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo sahihi kwamba fedha hizo hazitengwi, lakini niseme kwamba tunatenga kwa kadri ya hali ya bajeti inavyoruhusu. Kwa upande wa nyumba za makazi na vituo vya Polisi, vyote hivyo vinafanyika. Vile vile katika bajeti yangu nilivyoisoma mwaka huu, nilieleza kwa kina kuhusiana na mpango huo wa miaka 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sanga kuna mambo mengine ya vyombo hivi huwa hayaletwi hata na Kamati ndani Bunge kwa sababu yanamalizwa huko huko kwenye Kamati. Kwa hiyo, naomba tu uendelee na mchango wako katika maeneo mengine.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naendelea na mchango wangu. Kwenye eneo hilo, nimepokea taarifa ya Waziri wangu, kaka yangu Mheshimiwa Masauni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye hoja nyingine ambayo nilitaka nichangie. Kuna fedha ambazo zinaitwa unclaimed financial assets, fedha ambazo zinapotea bila sisi kuzikusanya vizuri. Hizi unclaimed financial assets ni fedha ambazo zinapotea kwa maana ya kwamba hazikusanywi kutokana na upotevu uliopo. Ni fedha zipi ambazo nazizungumzia?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Watanzania ambao wamefariki, kuna Watanzania ambao wamepoteza laini za simu au kadi za benki. Hizo kadi na laini za simu zina fedha. Hizo fedha zimekuwa unclaimed kwa muda mrefu. Mheshimiwa Waziri, kwenye Banking Financial Act ya Tanzania inaitaja BoT tu inaweza ikachukua fedha hizo kutokea kwenye banks, lakini kwenye eneo la Pension Funds, mobile money na insurance, fedha nyingi zimekuwa zikiishia kwenye hayo makampuni, haziendi kwenye Mfuko wa Serikali. Fedha ni nyingi ambazo zipo kwenye mikono hiyo na unaweza ukatumia fursa hiyo kwenda kutafuta hizo fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Kenya wameanzisha authority inayosimamia hayo mambo, inaitwa The Unclaimed Finance Asset Authority. Wameianzisha mwaka 2011, kufikia leo wamekusanya kiwango cha trilioni 1.2 kwa fedha ambazo zimeishia kwenye mikono ya watu. Sisi Tanzania hatujazikusanya fedha hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatafuta fedha kwa ajili ya kutatua kero za Watanzania, badala ya kutoa zile 5% kwa vijana na 5% kwa akina mama zile ambazo anataka kuzichukua kwenye asilimia 10, hapa kuna fedha nyingi sana. TFC pale ofisini kwake awaambie wamletee takwimu iliyoko BoT toka Watanzania walipoanza kutumia simu, mitandao na banks, kuna fedha nyingi ipo kule ambayo haijawahi kukusanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema mkaanzisha authority ambayo inaweza kusimamia hiki kitu tukakusanya hizi fedha nyingi ambazo zinapotea tu. Kwa sababu mtu anafariki na bodaboda leo, ameacha Shilingi 50,000/= kwenye laini yake, ameacha Shilingi 20,000/= au Shilingi 10,000/=, hakuna anayefuatilia hiyo fedha. Zinabaki kwenye makampuni ya simu. Huu ni muda muafaka sasa kutafuta fedha hii, kwa sababu sheria tuliyonayo inatambua ni banks tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni vyema mkiweza kuiboresha sheria tukaweza kuwasaidia Watanzania na hizi fedha zikakusanywa zikaenda kujenga hizo machinga complex, mahospitali zikaenda na kufanya shughuli nyingi za maendeleo kwa Taifa hili, kwa sababu zinaishia kwenye insurance companies, Pension Funds na mobile money transactions ambazo zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni mbolea. Hapa ndani limezungumzwa sana suala la mbolea. Niseme wazi, sisi Tanzania Rais ameonyesha mlango wa kuweka Shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kuweka ruzuku kwenye mbolea. Hii ni hatua ya haraka anayoichukua kwa sababu ya mtikisiko wa uchumi ambao tunapitia. Rwanda anatoa ruzuku ya mbolea, Burundi anatoa ruzuku ya mbolea, Zambia anatoa ruzuku ya mbolea, na Rais ameamua kuli-apply hili Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Waziri wetu Mheshimiwa Hussein Bashe, ameshaanza kuchukua initiatives za kurekebisha mfumo wa manunuzi Bulk Procurement kwenye Wizara yake. Mfumo huu kwa muda mrefu ulikuwa unampa mlaji mmoja tu ndio alikuwa anashinda tender. Ila changamoto anayoipata sasa, kwa sababu sisi Wabunge tukiyasema hapa haya mambo tunafuatilia Wizarani kuona mambo yanavyoenda. Sasa hivi Waziri anahangaika na kufumua mfumo wa Bulk Procurement Wizarani lakini bado kuna hatari ya kukwamakwama kutokana na wataalam wetu kumkwamisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Bunge, kwa sababu sisi ndio tumepewa dhamana ya kuishauri Serikali, namwomba Mheshimiwa Rais, Wizara ya Kilimo iangalie kwa ukaribu kwa sababu tumeiongezea fedha ya bajeti hadi Shilingi bilioni 900 kwenye mbolea kwa sababu ni suala sensitive, Waziri anahangaika kutatua changamoto ya mbolea lakini kuna siasa inayoendelea aidha kwa wanasiasa na wataalam ndani ya Wizara wanamkwamisha Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati sahihi kwa Mheshimiwa Rais kuingilia kati jambo hili ili huu mfumo uweze kufanya kazi, kwa sababu mimi nikienda Makete, wananchi wangu wanataka mbolea, tukienda Mbinga wanataka mbolea, tukienda Iramba wanataka mbolea. Mheshimiwa Rais anapambana kuweka Shilingi bilioni 150 ili mbolea ishuke bei, lakini kuna wataalam wanachezea akili ya Waziri wetu, amekwama, ame-stuck.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme kwa sababu, nina wakulima wengi nyanda za juu kusini, ndiyo tunalisha robo ya nchi hii, tunalifuatilia kila siku hili jambo tuweze kuisaidia Wizara ya Kilimo. Ili hizi fedha tulizoziongeza kwenye bajeti ziwe na tija na ziweze kuwa na faida kwa wananchi wetu, mfumo huu uweze kurekebishwa. Najua wafanyabiashara hawawezi kufurahia lugha kama hizi. Yes, I can be unpopular MP lakini niwe unpopular kwa ajili ya mbolea ya wana-Makete, niwe unpopular kwa ajili ya mbolea ya Watanzania. Waziri hawezi akawa anafanya kazi anakwamishwa na wataalam kwenye Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Rais kupitia hiki nilichokisema aweze kuchukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, Mungu awabariki sana. Ahsanteni sana. (Makofi)