Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwenye Taifa letu hili la Tanzania. Pia nipongeze Wizara ikiongozwa na Waziri, kaka yangu Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita kuchangia kwenye maeneo matatu. Ikipendeza nitaanza na madini, lakini nitazungumzia kidogo biashara na mwishoni nitazungumzia kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kwa kuzungumza yafuatayo na kaka yangu Mwigulu Nchemba naomba anisikilize vizuri katika jambo ambalo naenda kulizungumza. Wizara ya Madini, Sekta ya Madini imepita kwenye mabonde, milima mpaka ilipofika sasa na kimsingi wachimbaji wadogo wadogo kwenye Taifa hili, sasa wameanza kuonekana kama ni watu ambao hawana mchango kwenye Taifa hili, lakini ukiangalia taarifa ya mwaka jana ya Waziri wa Madini, baada ya kukaa na viongozi na wachimbaji na wadau mbalimbali katika Sekta ya Madini, tulikaa na kujadili namna bora ya kuweza kurasimisha biashara hii ya madini, kuweka mazingira mazuri kwa wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kuchangia kwenye pato la Taifa. Nakumbuka tulikubaliana baadhi ya mambo ikiwemo kuondolewa kwa VAT, lakini pia kuwajengea mazingira mazuri wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo kwenye hotuba hii nimeenda kuona hapa kuna baadhi ya maeneo kuna baadhi ya kodi imeanzishwa ambayo mchimbaji mdogo mdogo anapaswa kulipa ambayo ni asilimia mbili. Ikumbukwe kwamba Waziri wa Madini hapa alizungumza akasema, mwanzoni Wizara ya Madini ilikuwa inakusanya takribani Shilingi Bilioni 200, lakini baada ya kuweka mfumo mzuri na mazingira mazuri, mapato yalipanda kutoka Shilingi Bilioni 200 mpaka Shilingi Bilioni 500 na hao waliopandisha ni wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ameeleza hapa, amekitaja Kitengo cha GST kwamba tayari kimeweza ku-perform asilimia 16 ya kufanya tafiti katika nchi hii. Baada ya bajeti hii kupita maana yake itaenda kutekeleza asilimia 96 katika kuhakikisha kwamba inaenda kufanya tafiti katika maeneo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwa uchungu mkubwa kwamba kuna haja kubwa na hii tumeendelea kushauri muda mrefu. Hiki Kitengo cha GST kazi wanayofanya ni utafiti kama mganga wa kienyeji. Leo wachimbaji wadogo wadogo hawana uhakika na maeneo yao wanayochimba. Leo wachimbaji wadogo wadogo wanatumia ramli kuchimba madini haya na wachimbaji hawa wadogo wadogo hawana msaada wowote ambao wanaweza wakapatiwa ili wajengewe mazingira mazuri ya uchimbaji, lakini leo Serikali na kaka yangu Mwigulu Nchemba tunaenda kuanza kufikiria kuwaongezea kodi, tena kodi yenyewe inakatwa kwenye mtaji na si faida ambayo wanaipata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo unaweza ukafikiria uchimbaji ni rahisi, uchimbaji ni mgumu mno, watu hawa wanapata tabu sana. Nimwombe sana Mheshimiwa kaka yangu, Waziri, waende kukaa waangalie vizuri asilimia mbili ya kodi hii ambayo imeanzishwa kwa mchimbaji mdogo mdogo inaenda kuua Sekta ya Madini. Sekta hii imetoka mbali, imeanza kujikwamua, sasa tunataka twende kuiua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tumepambana, Mheshimiwa Waziri amepambana kuhakikisha kwamba utoroshaji wa madini unakomeshwa. Watu walielewa, kwa sababu ya mazingira mazuri tulishauri kodi ya royalty ipunguzwe, kodi mbalimbali za halmashauri ziondolewe. Sambamba na hilo tulishauri pia tukasema, katika asilimia saba hiyo iliyowekwa maana yake asilimia sita, asilimia nne iende Serikali Kuu, asilimia mbili ibaki kwenye halmashauri na halmashauri ziweze kuondoa kodi hizo huko ili kuwarahisishia wachimbaji wadogo wadogo hawa waweze kuchimba kwa urahisi zaidi na kwa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mchimbaji mdogo mdogo hana eneo la kuchimba. Leo tunazungumzia leseni nyingi zimekamatwa na watu makampuni makubwa hawana sehemu za kuchimba. Leo hii mchimbaji mdogo mdogo huyu anaenda kuwekewa kodi tena nyingine. Nimwombe kaka yangu, Mheshimiwa Waziri, Sekta hii ya Madini, wachimbaji hawa wadogo wadogo ndiyo wanachangia kwa sasa pato kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme katika sekta ambayo ilipaswa kuchangia asilimia 70 katika nchi hii ilikuwa ni Sekta ya Madini. Leo tunazungumzia asilimia 10 tu.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumpa taarifa tu mchangiaji anayeendelea kuchangia Mheshimiwa Iddi Kassim. Kwa kweli katika Sekta ya Madini ndiyo inapaswa kuangaliwa kwa umakini maana mpaka sasa hivi Wabunge tunaotoka kwenye maeneo ya madini kuna kero kubwa. Hizi tozo nyingi mno, service levy pamoja na mambo mengine mengi ikiwemo hawa watu wa GST wanapofuatwa na wachimbaji wadogo huwa ni ngumu sana hata kuwachukua kuwapeleka site kwenda hupima kwenye maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Iddi.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa hiyo na niendelee kusema tu kwamba tumeshauri kama tuna kampuni ya STAMICO ambayo tunaiwezesha kila mwaka, Serikali inaipatia bajeti, kwa nini sasa Kitengo cha GST kisivunjwe, kikawa ni tawi la STAMICO? Kwa sababu STAMICO wana mitambo, GST hawana mitambo, wanafanya utafiti gani? Kwa nini GST wasiwe tawi la STAMICO, kampuni ambayo kila mwaka tunaitengea fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri waende wakakae waangalie namna gani ya kuboresha sekta hii. Leo hii tunapozungumzia migodi mikubwa tunataja Migodi ya North Mara, Bulyankhulu, GGM, lakini STAMICO ambayo ni kampuni yetu sisi wenyewe Serikali haionekani. Kwa nini tusiende kuijengea uwezo hii kampuni yetu na yenyewe iweze ku-perform vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba kuna kodi hapa imeanzishwa na masharti yametolewa kwamba kwa yoyote yule atakayeenda kuuza dhahabu kwenye refinery, atalipa asilimia nne na kwa yoyote yule ambaye atauza nje ya refinery atalipa asilimia saba. Niseme kwamba hapa hawajapunguza bali wameongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchimbaji mdogo mdogo badala ya kulipa asilimia saba aliyokuwa anaenda kulipa, sasa anaenda kulipa asilimia 9.3. Leo hii tulishauri tukasema, tunatambua uanzishwaji wa refinery ni hatua nzuri. lakini kwa nini Serikali isilete hapa tukaweka sheria ya kwamba dhahabu yetu tunayoichakata hapa Tanzania isisafirishwe nje ya nchi mpaka iwe imesafishwa kwa asilimia 99? Tunaposema kwamba watu wote watakaokwenda kuuzia kwenye refinery watauza kwa asilimia nne na watakaouza nje ya masoko watauza asilimia saba, maana yake nini nini? Maana yake tunaenda kuwaua ma-dealer, tunaenda kuua masoko yetu ambayo tumetumia gharama kubwa kuyatengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, waende wakakae kufanya mabadiliko kwenye hili jambo, ni kwamba tunaenda kuongeza wizi wa dhahabu na dhahabu zitaibiwa kweli kweli. Hata hivyo, tusiwapangie wapi pa kuuza, tunafahamu uanzishwaji wa refinery hizi ni kutoa service ya kusafisha na siyo kununua na kuuza. Kama wao wanataka kuuza wekeni fair competition kwamba watu wote wanunue kwa asilimia nne, lakini dhahabu itakayosafirishwa nje ya nchi isiende mpaka iwe na asilimia 99, maana yake ni nini? Hawa ma-dealer nao watanunua dhahabu ile lakini pia watapeleka kwenye refinery hizo ili ziweze kusafishwa na Serikali itapata mapato yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri anielewe sana, wachimbaji hawa wanapitia mazingira magumu mno. Niombe, niombe, chonde, chonde watu hawa katika kodi hizi mbalimbali, leo tunahangaika hapa ukisema leo mchimbaji mdogo mdogo kodi anazolipa. Kwanza analipa ushuru wa shamba, royalty analipa mara mbili, akichimba mawe yake kama ni mifuko 100 anakatwa asilimia saba. Akitoka hapo akienda kwenye plant anakatwa asilimia saba. Leo hii tena wanataka kumwekea asilimia mbili, bado kuna ushuru wa shamba, karasha, mwalo na kijiji, huyu mchimbaji mdogo mdogo anapata wapi faida Mheshimiwa Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii wanaenda kuiua kama hawatachukua hatua za haraka. Sekta hii ni sekta ambayo inatakiwa ichangie pato hili la Taifa isizidi chini ya asilimia 75 kama itajengewa uwezo. Tuiunge mkono Wizara hii, tuondoe kodi ambazo zinamchelewesha mchimbaji mdogo mdogo ili naye aweze kuendelea kuchimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kuzungumzia suala zima la biashara. Mimi nimefanikiwa kuwa kidogo kwenye biashara, mazingira ya biashara ni magumu sana kwa sasa na hasa kwa hiki ambacho kinaendelea, kama tusipochukua hatua, Mheshimiwa Mbunge mwenzangu kaelezea hapa. Haya tunayozungumza ni mazuri, lakini utekekezaji wake kama utaenda tofauti maana yake tunaenda kuwaumiza sana, wafanyabiashara wanalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii utaona tunataka kwenda kupunguza asilimia nne kwa vijana, asilimia nne kwa wanawake, asilimia mbili kwa walemavu. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri fedha hizi aweke kwenye biashara na hapa ndipo tunapokosea. Naomba tutafute definition ya non-machinga. Tatizo kubwa lilipo hapa tunatakiwa tuelewe hivi machinga ni nani? Machinga ni yule anayepanga barabarani, machinga ni yule anayetembea au machinga ni nani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii utaona kupitia fursa iliyopo makampuni mbalimbali umeona watu leo wanaweza ku-organize wenyewe wakasafiri nje ya nchi kwenda kununua mzigo wakaleta. Leo hii hebu tuangalie, mtu anaenda anakopa benki fedha na mabenki haya nimwambie Waziri, kazi kubwa ya mabenki katika Taifa hili si kumtengeneza mtu ni kummaliza mtu kabisa. Hakuna mfanyabiashara ambaye amefaidika kupitia mabenki. Interest rate ya mkopo kwenye mabenki yetu ni kubwa mno. Leo hii mtu anakopa Shilingi Milioni 500 mathalani, anataka asafiri kwenda kununua nje. Kwa nini kusiwe na period time ya mtu anapokopa walau apewe mwezi mmoja?
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi huyu machinga ambaye amekua, mfanyabiashara ambaye amekua naye anataka kwenda kusafiri kuleta mzigo kutoka nje. Leo hii anapewa mkopo na mkopo ule unakatwa na kodi mbalimbali mle, unabakia kidogo, lakini pia anatakiwa siku ikiwekwa tu hela kwenye akaunti ndipo makato yanaanza…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)