Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti Kuu hii ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu moja kwa moja kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake nzima kwa kuandaa bajeti nzuri ambayo ni bajeti ya Watanzania wote itakayowasaidia katika sekta mbalimbali katika maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru sana Serikali kwa sababu ya kuondoa ada kwa kidato cha tano na kidato cha sita tunaomba tena Serikali iangalie tena mbele zaidi kusaidia katika Vyuo vya Kati kwa sababu kuna watoto ambao bado wakienda katika vyuo hivyo hawana uwezo wa kulipa ada katika Vyuo vya Kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita katika masuala makuu mawili, jambo la kwanza ni suala la makusanyo ya Serikali na rushwa, jambo la pili ni matumizi ya Serikali katika vyombo vya umma pamoja na mashirika yote ya umma na rushwa, hayo ndiyo mambo yangu mawili ambayo nitayazungumzia kwa ufupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukusanyaji wa mapato kumekuwepo na masuala ya watu kula njama ya kufanya rushwa, ufisadi, wizi na hujuma mbalimbali katika kukusanya mapato ya Serikali. Kumekuwepo na baadhi ya watumishi wachache ambao kazi yao kubwa ni kuchonga dili ili waweze kuhakikisha kwamba wanajipatia fedha za aibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sheria ile ya PPRA ambayo ni Sheria ya Manunuzi ya Umma kumekuwepo na tabia ya watu kukubaliana kwenye mikataba mbalimbali kwamba fanya hivi nitakufanyia hivi, hasa katika maeneo ya makadirio yanayofanywa na Maafisa mbalimbali wa Serikali hasa katika eneo la TRA hasa katika tender mbalimbali za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali kama hiyo, kama watu hawa wachache ambao hawana nia nzuri na Taifa letu wakiachiwa kuendekeza masuala ya wizi na ufisadi katika mikataba mbalimbali ya Serikali na manunuzi ya umma, bajeti hii ambayo tunaipigia kelele hapa ili ikalete tija kwenye barabara, kwenye elimu kwenye uletaji wa madawa hospitalini na kwenye maji hatutafikia malengo hayo kwa sababu watu hawa wamejikita wanasubiria tu hapa tukishapitisha wanasema, hewala! tumeshaupata tukapate kula na kunywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alipokuwa anasoma hotuba yake hapa nilimuona kama ni mtu mwadilifu sana kwa sababu alijaribu kujikita sana kupinga masuala ya rushwa; kwamba atashughulika na rushwa na wanarushwa. Mwenyezi Mungu akubaliki Mheshimiwa Waziri kama nia yako ni hiyo, na kweli naamini nia yako ni hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana pia kwamba wakusanyaji wa kodi hasa katika TRA hasa kuanzia ngazi ya mikoa ngazi ya wilaya wapewe mikataba kila mwaka katika kukusanya kodi kwa sababu ndio watakaoweza kuleta tija. Kama tukimpa kwa mwaka mmoja atakuwa anaangalia bajeti yetu, kwamba alitakiwa kukusanya shilingi ngapi kwa mwaka huo, na ameyafikia malengo hayo, na kama hajafikia ni kwa sababu gani. Hapo ndipo Wizara na Serikali itakuwa inatathimini, kwamba mtumishi huyu kweli alifanya kazi kwa uwaminifu na uadilifu. Vilevile tutapunguza rushwa na mambo yanayofanana na hayo katika kuhakikisha kwamba watu hao wamikoa na wilaya wanapewa mikataba ya kukusanya kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naungana na Wizara pale ambapo mtumishi atakuwa amefanya hujuma na akabainika kwa mujibu wa Sheria za nchi yetu kwamba amefanya ufisadi na wizi asiendelee na huo mshahara aliokuwa nao kwa sababu ameshindwa ku- maintained status quo ya kuendelea kuwa na huo mshahara. Hatuwezi kuwa na huruma na watu ambao hawana huruma na akina mama na watoto wanaoteseka bila huduma. Waondolewe hiyo mishahara ili mwingine akiona asirudie kufanya ufisadi na wizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika masuala ya matumizi. Kwenye suala la fedha za umma katika ununuzi katika matumizi ya ununuzi wa umma na mambo mbalimbali pamekuwepo pia na mchezo mbaya sana katika taasisi zote za umma. Hapo utagundua kwamba kila mwaka CAG anapoleta ripoti yake hapa Bungeni kumekuwepo na taarifa za wizi, ufisadi na mambo mengine yote machafu ya ubadhilifu katika miradi mbalimbali ya umma. Kwanini hatutaki kusema kwamba watu hawa ifike mwisho, tuseme basi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuna nia ya kuondoa rushwa katika masuala ya miradi ya maendeleo naamini ripoti ya CAG imekuwa kila mwaka ikitupa taarifa nzuri ya kutuonesha hali ya maendeleo katika nchi yetu dhidi ya watu wanaoujumu bajeti katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu hao wamekuwa wakishirikiana kabisa na mawakala na makandarasi kusema nipunguziwe bei fulani nitakupa kitu fulani; hata katika tender zile za ununuzi wa bidhaa za Serikali. Naomba hili Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa makini sana kwa sababu hapa ndipo Serikali inaposhindwa kutekeleza miradi yake. Kwa sababu, kwa mfano unakuta labda mradi ni milioni 50 lakini watu watapelekea huo mradi lutafika milioni 100. Mtu anakuwa na kampuni tatu. Kampuni ya kwanza itasema milioni 90 nyingine itasema milioni 95, nyingine itasema milioni 100, obviously kutokana na ile sheria atachukua mtu wa milioni 90 lakini uhalisia wa mradi ulikuwa ni milioni 50; hiyo ni hasara kubwa kwa Serikali ingetekelezwa zaidi ya miradi miwili. hapo napo lazima tuangalie na tuamue kwa moyo wa dhati na moyo wa kizalendo kwa sababu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, katika kuyafanya haya niliyoyasema lazima tuangalie sheria zetu hasa Sheria hii ya Manunuzi lazima irekebishwe haraka iwezekanavyo ili iweze kuleta tija katika utekelezaji na utoaji tender mbalimbali za Serikali. Kwa sababu sheria hii imekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo, naweza kusema hivyo. Haiwezekani mtu unaenda kusema the lowest bidder na highest bidder ndiyo utachukua the lowest bidder ilhali bado sheria hiyo imetoa mwanya mkubwa kuhakikisha kwamba mtu anaweza akafanya jambo hapo katikati na akaiba fedha nyingi tu kwa kutumia sheria hiyo. Naomba tuangalie hiyo na turekebishe haraka iwezekanavyo tuendane na bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, si sheria hiyo tu, pia utaona Sheria ya TAKUKURU (Prevention and Combating Corruption Act, 2007); hii sheria nayo inatakiwa iangaliwe. Kutoka mwaka 1980 mpaka 1990 ilikuwa imeonekana sheria hii imeshindwa kuleta tija, ikaunda tume ya Warioba mwaka 1996 ndiyo iliyokuja kuleta sasa hii ambayo ipo hapa sasa. Naomba sasa pia iangaliwe na irekebishwe. Makosa yote yaliyopo kwenye sheria hii ya kuzuia rushwa yapelekwe yawe ya uhujumu uchumi. Kwa sababu watu wanaoiba dawa za hospitalini, fedha za barabara si ni wauaji? Ni zaidi ya yule mhujumu uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utaona jinsi Waziri Mkuu alivyokuwa analalamika MSD; dawa moja milioni 17 inaenda mpaka milioni 100 hawa si wauwaji wanaoua watu hospitalini. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)