Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi nianze mchango wangu kwa kuungana na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuzungumza. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya ya maendeleo kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu leo hii nitazungumza namna gani tunaongeza wigo wa kodi (tax base) kwenye sekta ya ardhi. Hayati Baba wa Taifa aliwahi kuzungumza maneno haya; nchi yoyote ili iweze kupiga hatua ya maendeleo lazima iwe na watu, siasa safi kwa maana ya utawala bora, lakini mwisho alisema ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inakadiriwa tuna ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba takribani 945,000. Nilikuwa najaribu kuangalia na wenzetu wa Kenya, wenzetu wana ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba takribani 580,000. Lakini pia nilikuwa nafuatilia tarehe 28/04/2021 saa nne usiku nikiwa nasikiliza taarifa ya habari kwenye television ya The Citizen; Waziri wa Ardhi wa Kenya alieleza kwamba nchi ya Kenya mpaka sasa ina hati miliki milioni 11, nchi ya Kenya, yenye population ya watu takribani 48,000 sisi tunakwenda milioni 60. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ardhi yetu ni kubwa kuliko Kenya, lakini mpaka leo kupitia bajeti ya Wizara ya Ardhi mpaka sasa tuna hati miliki milioni mbili, tangu tupate uhuru, I stand to be corrected. Utaona ni namna gani tunashindwa kuwa na wigo wa kodi, tunaiacha nyuma sekta ya ardhi. Ikumbukwe maneno ya Hayati Baba wa Taifa kwamba tukiwa na ardhi, ardhi ni kila kitu. Ukizungumzia ardhi madini yapo kwenye ardhi, kilimo kipo kwenye ardhi. Leo tuna jitihada kubwa kwenye sekta ya ardhi kupitia Wizara ya Kilimo; Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anahangaika kweli ili kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inakuwa, lakini atakwama. Leo hii mkulima Mtanzania ana ardhi yake lakini haina faida, ardhi yake haimsaidii kwa sababu haina thamani. Sasa mkulima ili akopesheke mtampelekea Benki za Kilimo, benki zote lakini hawezi kukopesheka, ana heka 10; ana heka 20 ana heka 100; ardhi ili iwe na thamani lazima ipimwe, ikishapimwa inapanda thamani na inakuwa mtaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa haraka haraka nitaje faida chache za ardhi ikipangwa na kupimwa vizuri; kwa haraka haraka ili nitunze muda wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, faida ya kwanza tunakuwa na matumzi bora ya ardhi kama nchi, kila eneo linakuwa limepangwa. Pili kuiongezea ardhi thamani na kuifanya kuwa mtaji. Tatu kuziongezea mapato halmashauri zetu. Nne kufanikisha zoezi za anuani za makazi. Leo hii naona Mheshimiwa Waziri Nape amekuja na jambo jema kwa Taifa letu, postcode na anuani za makazi. Najiuliza maswali, nipo kule Mlimba kijijini, zile barabara zile asili unasema hii barabara ya mtaa, hakuna mtaa. Kwa hiyo, yote haya kwa sababu hatujaipanga na kuipima nchi yetu. Kwa hiyo, nadhani kuna kuna haja ya kuipanga vizuri na kuipima nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ndilo eneo langu la leo kwenye mchango wangu, ninaongeza wigo wa kodi yaani tax base. Nizitaje tozo za ardhi; ya kwanza ni stamp duty, ya pili ni premium, ya tatu ni land rent ambayo ni sustainable. Ukiwa na watu walipa kodi wa sekta ya ardhi (land rent) milioni 10 tu hatuhangaiki na hayo mambo mengine, sijui start there, lakini hatuhangaiki, milioni 10 tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni registration fees ambayo ni one percent na capital gain 10 percent. Sasa hizi zote ni fedha ambazo tunaziacha. Sasa nilikuwa nataka nieleze taratibu za upimaji, na hizi ni kwa mujibu wa sheria. Ili ardhi yote ipimwe lazima uanze na mpango kabambe. Leo hii naona jitihada za Serikali kuwekeza fedha kwenye halmashauri, lakini hizo fedha tukija kuzipima matokeo yake tutakuja kuona changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nchi hii tangu tupate uhuru halmashauri pekee yenye master plan ni Dodoma? and I stand to be corrected, nchi nzima halmashauri pekee yenye master plan ni Dodoma, yaani mpango kabambe master plan ni kama Katiba I stand to be corrected. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama…
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taarifa. Taarifa ya Mheshimiwa Waziri.
T A A R I F A
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kumpa taarifa msemaji, tunazo halmashauri 26 zenye master plan nchi hii na si Dodoma peke yake. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Kunambi unaipokea taarifa hiyo.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kubishana naye kwa sababu namheshimu.
NAIBU SPIKA: Siyo kubishana, huyu ndiye mwenye sekta.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupokea taarifa.
NAIBU SPIKA: Ameshaipokea taarifa.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea taarifa.
NAIBU SPIKA: Endelea Mheshimiwa Kunambi, zungumza na kiti.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na mchango wangu. Ili ardhi ipimwe ina mambo makuu matatu, ya kwanza ni mpango kabambe yaani master plan, huwezi kupima ardhi kama hakuna mpango kabambe, utapima tu upimaji wa kiholela. Lakini namba mbili lazima uwe na ramani za mipango miji, na namba tatu lazima uwe na ramani ya upimaji. Sasa maeneo haya, labda nieleze eneo hili, kabla sijaendelea naomba niende kwenye success story.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, mchango wake ni mzuri sana, na shida kubwa sana katika eneo hili la ardhi ambayo inatakiwa kusaidia sana kufungua tax base au wigo wa kodi, Dar es Salaam ni mfano tu. Pamoja na sifa zote alizozisema Dar es Salaam bado ni shida, watu zaidi ya milioni sita kuna makazi yasiyopungua milioni nne. Lakini makazi yaliyopimwa hayafiki 400,000. Shida ni kubwa, kwa hiyo mchangiaji anachangia vizuri katika eneo hilo.
NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Kunambi unaipokea taarifa. Mheshimiwa Mtemvu kaa chini.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa ya mjukuu wa Muasisi Zuberi Mtemvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye success story hapa Dodoma. Miaka mitatu, minne iliyopita Dodoma Jiji ilikabidhiwa jukumu la kupima na kupanga Dodoma. Mtakumbuka siku moja nikiwa nahudumu kama Mkurugenzi wa Jiji, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliniita ofisini nikiwa na Mstahiki Meya na Afisa Mipango Miji wangu akiniuliza ni lini utagawa viwanja kwa watumishi wa umma. Sikumuomba fedha, sikwenda benki kukopa, nilimjibu nipe miezi mitatu naenda kukabidhi viwanja kwa watumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Dodoma mpaka ninaondoka, nahitimisha utumishi wangu wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, niliacha viwanja takribani 400,000. Na nilitumia njia gani, naomba niseme kidogo, niliwaita wataalam wangu, yaani menejimenti timu, nikawaambia wanishauri. Sasa wengi walisema tupime wenyewe, nikachukua eneo la Michese viwanja 2,000 walinikabidhi viwanja hivyo kwa muda wa miaka mitatu. Nikatumia sekta binafsi, nikapima viwanja zaidi ya 390,000, kwa kutumia sekta binafsi. Sasa hii naieleza kwa sababu ni success story. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri.
T A A R I F A
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ninaomba msemaji anapozungumza asitupe story ambazo sasa hivi ndizo zinazotuletea matatizo kwa nchi hii. Akiwa Mkurugenzi wa Dodoma kama anavyosema, tulikuwa na story ya Kinondoni kuongoza migogoro, sasa hivi Kitaifa Dodoma inaongoza kwa dhuluma ambazo wamezifanya kwa wananchi. Kwa hiyo huo si mfano ambao anaweza akautolea kama success story kwenye kazi aliyoifanya. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunambi, unaipokea taarifa.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei taarifa yake. Naomba niendelee, unajua mimi nazungumza mambo ya Kitaifa. (Makofi)
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa, mwacheni Mheshimiwa Kunambi, amalize mchango wake. Endelea Mheshimiwa Kunambi.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoeleza, nazungumza hapa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikie, ninachosema nchi hii ni tajiri. Sekta ya ardhi peke yake hebu nieleze tu mathalani tuna idadi ya watu milioni sita, hati miliki milioni mbili tangu tupate uhuru. Kwa hiyo, nikasema Kenya tu hapa jirani wana milioni 11 na ardhi yao ni kilometa za mraba 580,000 tu, sisi laki tisa na kidogo. Jambo hili ni sensitive na niseme… (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa mwacheni Kunambi amalize mchango wake. Mheshimiwa Kunambi endelea.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuendelea kunipa nafasi. Nataka kusema nini, ardhi hii yaani sijui na ninasema tu kwa dhati na niliwahi sema hapa sitaacha kuzungumzia ardhi mpaka nione kama nchi imechukua hatua kuifanya nchi yetu inapimwa na tunaongeza wigo wa kodi kwenye sekta ya ardhi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na Mungu akubariki, ahsante. (Makofi)