Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namwomba Mwenyezi Mungu nikiwa nazungumza, taarifa zisiwe nyingi sana kama yaliyompata Ndugu yangu Kunambi hapa. Ila kama kuna mtu ana taarifa ya kujenga, itakuwa ni vizuri, lakini mwenye taarifa ya kuchelewesha muda, basi Mwenyezi Mungu ashughulike na yeye. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia hoja hii ya Wizara ya Fedha ambayo ni hoja ya Serikali kwa ujumla kwa maana ya Wizara zote. Kuna mtu mmoja aliwahi kuishi miaka 500 kabla ya Kristo, alisema hivi: “Watu huangamia kwa kukosa maarifa (my people perish for lack of knowledge).” Halafu mwingine aliishi miaka 500, anaitwa Suleyman Bin Daud, yeye alisema: “Watu wangu wanaangamia kwa kukosama maono (my people perish for lack of vision).” Kwa hiyo, hawa watu wote wawili; aliyesema watu wanaangamia kwa kukosa maarifa, na aliyesema watu wanaangamia kwa kukosa maono, wote walikuwa sawasawa. Kwa hiyo, kukosa maono kunaangamiza na kukosa maarifa kunaangamiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu gani imenifanya niseme hivi? Kujenga Taifa ni sawa na kujenga nyumba. Huwezi ukajenga nyumba bila ramani. Itajengwa, lakini baadaye utakumbuka palipopaswa kuwa na dirisha sasa halipo. Tunapokuwa tunajenga Taifa la Tanzania, tunahitaji maono ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni nilijaribu kuchangia hapa kwa habari za maono, ikaonekana kana kwamba nasema tu, lakini maono yapo. Naongelea maono ya muda mrefu; maono ya miaka 50, maono ya miaka 60, maono ya miaka 100 ya Tanzania ijayo. Hicho ndicho ninachotaka kuongea. Ninapotaka kuongea, kiongozi anatakiwa aone mbali kuliko wengine. Kiongozi anatakiwa aone kabla ya wengine na kiongozi anatakiwa aone sana kuliko wengine. Katika kuona, lazima tuwe na maono ya muda mrefu ya nchi yetu Tanzania ili tuweze kuijenga kutokea mbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nina maana gani nikisema maono ya muda mrefu ya nchi yetu? Tunaweza kusema hivi kwa mfano, ndani ya miaka 50 ijayo, kila barabara ya Tanzania iwe ya lami, ni maono yetu. Natoa mfano, ndani ya miaka 50 ijayo iwe barabara ya TARURA au TANROADS iwe ya lami. Tukasema ni maono yetu ndani ya miaka 50 ijayo Tanzania kila nyumba ya Mtanzania iwe na nyumba, maji na salama. Natoa mfano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kusema kwa mfano, ndani ya miaka 50 ijayo asiwepo Mtanzania anayekaa ndani ya nyumba ya majani au nyumba ya matembe kama ndugu zangu Wagogo. Tukasema, ndani ya miaka 50 ijayo kila Wilaya iwe na Hospitali ya Rufaa; ndani ya miaka 50 ijayo kila Wilaya iwe na University ya Serikali; ndani ya miaka 50 ijayo, nchi yetu yote iwe imepimwa; tukasema ndani ya miaka 50 ijayo, tuwe na mipango ya energy ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hicho ndicho kinaitwa maono ya muda mrefu ya nchi. Hicho kinawasaidia, tukisema ndani ya miaka 50 ijayo, kila Wilaya iwe na uwanja wa mpira na Academic Institution ya ku-train watoto wetu; ndani ya miaka 50 ijayo tuseme asipatikane mtoto anayeshindwa kusoma chuo kwa sababu ya kukosa pesa. Tunaweza kuiona nchi yetu kwa mbali sana na tukapanga mipango yetu kwa mbali sana. Hicho ndicho mimi nakiona ni maono ya nchi ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokosa maono ya nchi ya muda mrefu, tunakuwa na maono na mipango mifupi mifupi, tunajikuta tumepoteza direction. Nasikitika kusema kwamba na ndiyo sababu huwa tunakumbwa na jambo kubwa la kukosa institution memory. Kwa mfano, inapotokea regime moja inamaliza, inaingia regime nyingine, kwa sababu ya mtazamo wa regime inayokuja ni tofauti na ile, inabidi viongozi wengi sana wabadilike, ni kwa sababu inaonekana kana kwamba maono mapya yanaingia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tungekuwa na maono ya Taifa ya muda mrefu, regime zingekuwa zinaingia kutekeleza maono hayo hayo kwa kutumia style tofauti. Kwa mfano, tukisema ni maono ndani ya miaka 50 kuhakikisha kila Wilaya ina Hospitali ya Rufaa, regime inayokuja itatimiza maono hayo kwa kutumia sarakasi zake. Itatimiza kwa haraka au kwa muda mfupi, kwa kutumia mbinu inavyofikiri ni njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie jambo moja. Maono ya muda mrefu it is a development instrument ya nchi yenye kuilinda nchi ikae katika msingi unaotakiwa. Madikteta wote duniani walishinda uchaguzi wa kidemokrasia kuanzia Bokassa mpaka Hitler walishinda uchaguzi wa kidemokrasia, isipokiwa walikuwa hawana governing tool ya kuwafanya wabaki kwenye maono yale ambayo wananchi walijipangia. Wakatoka nje na nchi zao zikaharibikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, kama iko zawadi tunatakiwa kuipa nchi hii, ni kuipa maono ya muda mrefu sana. Nini maana yake? Watoto wanaosoma shule, wanaona kwa kuwa ndani ya miaka 50 kila Wilaya inatakiwa kuwa Hospitali ya Rufaa, watoto wataona soko la Udaktari lipo; ma-nurse wataona soko la u-nurse lipo. Wanapoona ndani ya miaka 50 kila Wilaya itajengwa University, wajenzi wanaona soko la ujenzi lipo, watu wa rangi wataona soko la rangi lipo, watu wa mabati wataona soko la mabati lipo kwa sababu wanaiona nchi yao kutokea mbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata Ilani za Uchaguzi zinakuwa zinaongelea maono ya nchi, Mitaala ya Elimu inakuwa inaongelea maono ya nchi. Watoto wanaweza kuiona nchi yao katika three D kwa mbali na wakaamua hatma yao leo wakikua wanajua kwamba nchi yao itakuwa ya namna fulani ndani ya miaka 50. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mipango hii ya muda mfupi tuliyonayo ni mizuri, lakini haiwezi kujenga nchi imara. Investments zote zinazoweza zikawa sustainable zikaijenga nchi, ni zile zilizowekwa kwa muda mrefu, wafanyabiashara wakaziona, halafu wakafanya maamuzi leo, na maamuzi yale yaka-prevail ndani ya miaka 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kule Mtwara, ilipoibuka miradi ya gesi zikajengwa Hoteli nyingi, ziko pale Mtwara. Leo Hoteli hizo hazina watu wa kulala. Kwa nini? Kwa sababu focus tena ime-change. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa natoa ushauri kwamba kama tunataka kuipa nchi hii zawadi kubwa, tuipe maono ya muda mrefu; miaka 50, miaka 60 na maono hayo yanaweza kubadilishwa kutegemea na ulemwengu unavyobadilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa kule Uholanzi nikataka kuita taxi kama tunavyoita kwetu hapa. Wakasema sasa hivi wanafanya mpango wa taxi ambazo hazina dereva. Unaita kwa kutumia simu yako, inakuja haina dereva, unaingia ndani, unaandika namba ya simu ya nyumba unayokwenda, inakupeleka mpaka nyumbani kwa mtu. Dunia ijayo madereva tulionao hawa hatutakuwa nao, dunia ijayo marubani wa ndege tulionao hawa hatutakuwa nao, dunia ijayo kuna roboti Wanasheria. Tunatakiwa tuione dunia ijayo kwa mbali sana ili kama nchi, tujipange kwenye mitaala yetu ya elimu ili watoto wetu waweze ku-handle dunia ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, pamoja na Serikali kwa ujumla; kazi ya Mbunge ni kuishauri Serikali. Nashauri tutafute namna ambayo tunaweza tukaipa nchi mipango ya muda mrefu sana ili watoto wasipate depression kwa kutokujua Tanzania ijao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)