Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Bajeti Kuu ya Serikali. Kimsingi nina vitu viwili tu leo ambavyo napenda kuviongelea. Cha kwanza, nizungumzie pendekezo la bajeti yetu kupunguza asilimia 10 ile iliyotengwa kwa ajili ya akinamama, vijana na wenye ulemavu. Kimsingi hizi fedha mwanzo zilikuwa hazitoshi, mfano nichukulie kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini, Halmashauri yetu, makusanyo yetu pale hayazidi Shilingi Bilioni moja, ni around Shilingi Bilioni moja kwa hiyo, tunawatengea hawa watu Shilingi milioni zisizozidi 100 na kimsingi maombi yanakuwa zaidi ya Shilingi milioni 500 kila mwaka. Kwa hiyo, imekuwa ni usumbufu mkubwa wa Mbunge kusumbuliwa, tunaomba utusaidie kupata mikopo na viongozi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo kwa hili pendekezo la Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu kana kwamba zile Shilingi milioni 100 tulizokuwa tunazitoa sasa zinakwenda kuwa Shilingi milioni 50, kimsingi kwa hii si sahihi. Niungane na Wabunge wenzangu wengi ambao wamekataa pendekezo hili, Wizara ione namna ya kufikiria upya. Kuwapunguzia hawa watu ambao tulitaka kuwa-empower ni kuwarudisha nyuma. Kwa hiyo, naamini kabisa kama ndugu yangu Aweso huwa anasema hakuna sikio ambalo haliwezi kusikia vinywa vya watu wengi, naomba niungane na Wabunge wengi ili viwe vinywa vya watu wengi na Waziri akapate kuja na kitu cha mbadala na kuliahirisha hili pendekezo lake. Hapa hapa pia nipende kuongezea kitu kwenye hii hii asilimia 10. Kimsingi halmashauri nyingi endapo wakikopesha zile Shiingi milioni 100 mfano, kwenye halmashauri yangu, yale marejesho huwa yanarudi halmashauri kama other source. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, badala ya kuboresha ule mfuko zile fedha zinarudi tena halmashauri kwa hiyo, kila mwaka inaendelea kuwa ile Shilingi milioni 100. Ningependa kuwe na account special kwa ajili ya hii fedha, kama mwaka huu zikiwa Shilingi milioni 100, yale marejesho ya mwaka huu na ile Shilingi milioni 100 ya mwaka unaofuata isiwe tena Shilingi milioni 100. Kwa hiyo, baada ya miaka 10 miaka mingapi ile fedha itakuwa nyingi mikopo itaongezeka, lakini pia watu ambao tunawahudumia wataongezeka. Kwa hiyo, naomba tulifanyie kazi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipende kushauri halmashauri zetu kuongeza jitihada kubwa kusimamia fedha hizi. Fedha hizi zilikuwa zikitolewa kwa madhumuni mazuri kabisa, lakini usimamizi wake ni mdogo. Cha kwanza, tuombe hawa watu ambao wanapatiwa hizi fedha hivi vikundi vifanyiwe screen ya kutosha, tuhakikishe tunawapa watu sahihi, wenye biashara sahihi ili hizi fedha ziweze kurudi kuweza kuboresha huu Mfuko na kukopesha watu wengi zaidi. Hilo lilikuwa jambo langu la kwanza nililosema nichangie siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nataka kuchangia kwenye Mradi wetu unaitwa TACTIC. Huu ni mradi kwa ajili ya kuboresha Miji yetu 45. Kwanza niipongeze Serikali kwa mradi huu, naamini ukikamilika utaboresha kwa kiasi kikubwa miji yetu na nashukuru Mungu, Mji wangu wa Korogwe ni kati ya miji hiyo ambayo inakwenda kuboreshwa kwa mradi huo. Hata hivyo, huu mradi una changamoto. Huu mradi ni wa miaka mingi, lakini hadi leo haujafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kucheleweshwa kwa mradi huu kunatupa changamoto kubwa sisi wa Jimbo kutoka kwenye miji hiyo, mathalani kwenye Mji wangu wa Korogwe, huu mradi unakwenda kugusa kata zangu saba kati ya kata 11 nilizokuwa nazo. Kwa hiyo, kwenye kila kata kwenye Jimbo langu nimeahidi kujengwa kwa barabara, nimeahidi kujengwa kwa mitaro kupitia fedha hizi, lakini hadi leo miaka mingi huu mradi bado haujafanikiwa, kwa hiyo inatupa changamoto kubwa Wabunge wa maeneo hayo kufanya siasa zetu. Mfano mradi huu unaunganisha Kata yangu ya Mtonga, Kata ya Mgombezi, Kata ya Bagamoyo, lakini mradi huu huu unaunganisha Kata ya Manundu, Kata ya Masuguu na Kata ya Magunga pamoja na mradi huu uko kwenye Kata ya Majengo. Kwa hiyo, ni asilimia 70 ya kata zangu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokamilisha miradi hii wanatupa changamoto sisi Wabunge ambao kila siku tunaahidi. Kuna kata ambayo haijawahi kupelekewa barabara ya lami tumeahidi zaidi ya miaka miwili kwamba watapatiwa barabara ya lami kupitia mradi huu lakini hadi leo huu mradi haujafanyika. Tumwombe Mheshimiwa Waziri, kama kuna changamoto kwenye utekelezaji wa mradi huu basi atuambie, au arudi kwenye hii miji kuwaambia kwamba utacheleweshwa kwa kipindi gani ili tusiendelee kuwa waongo kila siku. Kwa hiyo, naomba Waziri akija kuhitimisha atuambie kwamba huu mradi utakamilika wakati gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine inayotupata Wabunge ambao tuko ndani ya mradi huu, bajeti ikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo huwa sisi tunapewa fedha pungufu. Mfano, mwaka jana tulipewa karibu Shilingi milioni 500, baadaye watu wengine wakaongezewa Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya miradi ya barabara, lakini sisi badala ya kupewa Shilingi 1,500,000,000 tulipewa Shilingi Bilioni moja tu kwa ajili tuko kwenye huu mradi wa Miji 45. Kwa hiyo, tunaendelea kupata shida ya kuambiwa mradi upo lakini hadi leo mradi haujafanyika. Kwa hiyo, nimwombe Waziri akija kuhitimisha atuambie nini hatima ya mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho ambacho napenda kukiongelea leo, kwanza nimpongeze Waziri mwenye bajeti kwa mikakati mikubwa aliyoiweka kukabiliana na ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha hasa kwenye sehemu ya magari pamoja na mafuta. Sehemu hii naomba nichangie kidogo, tuna taasisi yetu tunaita TEMESA, hii taasisi imekuwa kati ya taasisi ambazo zinaiongezea hasara Serikali badala ya kuipunguzia. Hii taasisi kila mmoja anajua changamoto zake, kila Mbunge hapa ukimwambia TEMESA iendelee kuwepo au isiwepo kila mtu atakwambia hii isiwepo. Sasa sioni kwa ajili gani Waziri hadi leo tunaing’ang’ania taasisi kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hii taasisi haipo karibu wilaya zote iko Mikoani. Kwa hiyo, magari yakitaka kutengenezwa yatoke wilayani yaende mkoani. Mfano, gari inakwenda kufanyiwa service ya kilomita 3,000, lakini kuna gari inatembea zaidi ya kilomita 1,000 kwenda kufuata service ya kilomita 3,000. Kwa hiyo, sioni sababu ya hii taasisi kuendelea kuwepo. Naamini kuna ndugu zetu wameajiriwa pale, lakini hatuna budi, watatafutiwa tu sehemu nyingine za kwenda, hii taasisi ni mzigo mkubwa kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yako umesema unaenda kupunguza idadi ya magari ya Serikali, sasa sijui hii TEMESA ikiendelea kuwepo itakuwa inahudumia magari gani? Kimsingi hawana uwezo, hawana karakana, hivyo vitu ukivipeleka TEMESA kesho unavikuta vimepelekwa kwenye gareji bubu kwenda kutengenezwa. Kwa hiyo, tunapeleka TEMESA, lakini wao wanaenda kulipia, kwa ajili gani iendelee kuwepo? Kama unataka iendelee kuwepo, basi yeye awe kama Msimamizi kuangalia quality ya hizo service zinazotolewa, lakini siYo TEMESA kuendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nilikuwa na hayo machache kutokana na muda naomba niishie hapa. Ahsanteni sana na ninaunga mkono hoja (Makofi)