Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Serikali. Nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, nimpongeze pia Naibu wake Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, niwapongeze na Watendaji wote kwa kuandaa bajeti ambayo ni nzuri sana ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu nyingi ziende kwa Mheshimiwa Rais wetu kipenzi, Mama Samia Suluhu ambaye kwa kweli amefanya mambo mengi mazuri, mambo mengi makubwa katika nchi hii hatutamsahau. Naomba kwa kweli, mimi sina la kumpa lakini tuendelee kumuombea maisha mema, tuendelee kumuombea aendelee kufanya kazi vizuri, kuwatumikia Watanzania na nchi iendelee kuwa na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imelenga makundi yote wakiwepo wakulima, tumeona ongezeko kubwa la bajeti katika kilimo zaidi ya asilimia 200, lakini imelenga pia wafanyakazi, tumeona maslahi ya wafanyakazi yamezingatiwa, vilevile katika elimu tumeona tayari Kidato cha Tano mpaka cha Sita elimu bure. Kwa hiyo, tutakuwa tuna elimu bure kuanzia Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita. Bajeti pia imegusa TEHAMA, vilevile itakuza diplomasia yetu hii bajeti, lakini vilevile utalii naona kuna ongezeko ambako tutakuwa na miundombinu katika utalii ili kuunga mkono hiyo Royal Tour kwa ajili ya Mama yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kuchangia mchango wangu kuhusiana na Serikali kupunguza asilimia Kumi inayotolewa katika Halmashauri zetu kwa mikopo ya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu. Hii mikopo ilikuwa inasaidia sana haya makundi kwa sababu kwanza iliweza kuongeza ajira na ilikuwa inaongeza pato na vilevile ilikuwa inasaidia hata heshima nyumbani ilikuwa inakuwepo, kwa sababu kinamama wengi sana walikuwa wanachangia pato katika familia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la hii mikopo labda tunaona sehemu nyingine ilikuwa labda haikusanyiki ndiyo maana mmeweza kupunguza, ni kwa sababu walikuwa wanatoa pesa kidogo kwenye kundi kubwa. Kwa mfano, kikundi cha watu 20 wanapewa Milioni Mbili kwa hiyo, tatizo lake walikuwa wanagawana tu sasa Elfu Ishirini-Ishirini kila mtu anafanya biashara anayoitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ningeomba sana hii mikopo tufanye kama wenzetu wa China. Tulivyokwenda kutembelea nchi ya China kwenye miradi ya akinamama wenzetu walikuwa wanawawezesha viwanda vidogovidogo vile vya nyumbani. Kwa hiyo, utakuta viwanda vidogovidogo vingi vya akinamama vilikuwa vinasaidia sana kukua kwa uchumi katika nchi ya China. Sasa na sisi hii mikopo tungelenga kwenye viwanda vidogo vidogo vya akinamama, tungewapatia vifaa kwa mfano mashine na teknolojia, tungeona kwamba, hawa akinamama na vijana na watu wenye ulemavu hii mikopo ingeleta faida sana katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye Mkoa wetu wa Iringa tunalima kilimo cha nyanya na pilipili, sasa kama akinamama wangekuwa na viwanda vidogovidogo vya kusindika hizi nyanya unaona hata soko la nyanya kuna wakati zinakuwa hazina soko kabisa, kwa hiyo wangesindika hizi nyanya na wangeweza kupata biashara kubwa sana. Kwa hiyo, ningeomba Serikali, pamoja na kuwa najua kwamba, Serikali ni Sikivu, itarudisha na ingewezekana ikaongeza asilimia 15 katika hii mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akinamama wengi sana sasa hivi bado walikuwa wako wanasubiri mikopo haitoshi, najua idadi ya akinamama ni wengi sana kwa hiyo, mimi naomba Serikali hii asilimia 10 irudi na ikiwezekana iongezewe ifikie asilimia 15. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na vijana pia nilikuwa naona hawa vijana wetu badala ya kuwapatia pes ana wenyewe tungeangalia. Kwa mfano, kuna vijana wamemaliza VETA kwenye vyuo vya ufundi, hao vijana wangekuwa wanapatiwa mikopo hii ya Halmashauri. Kwanza kwa mfano wangepelekewa mashine za kutengeneza tofali, wangepatiwa mashine za kutengeneza madawati, vilevile wangewaunganishia kwamba, zile tenda katika Halmashauri wangewapatia sasa hizo tenda na wangewapatia pesa ingekuwa rahisi hata kukusanyika hizi pesa na ingekuwa pesa ina mzunguko watu wengi wangeweza kukopa kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi noombe hii mikopo pia iboreshwe pamoja na kuwa itaongezeka najua, lakini iboreshwe ili vijana wapatiwe vifaa badala ya kupatiwa pesa. Vilevile kwa mfano kuna Halmashauri nyingine ni wakulima, wafugaji au wavuvi, wangeweza kutengenezewa hata mabwawa, wakapewa vifaranga, wakapatiwa chakula halafu baadae Halmashauri baada ya kuwapatia soko wangeweza kukusanya hizi pesa kwa urahisi zaidi. Kwa hiyo, hii mikopo ingesaidia sana katika kuongeza pato katika Halmashauri, lakini kwa vijana na ingeweza kuwa ina mzunguko mwepesi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti kubwa sana ya kilimo. Mimi niko katika Kamati ya Kilimo, siku zote tulikuwa tunaomba Serikali iongeze bajeti ya kilimo, kwa sababu asilimia zaidi ya Sabini ya Watanzania ni wakulima, kwa hiyo, tunajua kwamba, kuongezwa kwa pesa hii kutasaidia sana uchumi na kila mtu ataweza kuchangia pato katika nchi yake, lakini tunategemea sasa elimu kwa wakulima, tunategemea mbegu bora, tunategemea miradi ya umwagiliaji itaongezeka, kilimo kitakuwa kina tija na tunategemea Maafisa Ugani wamepewa pikipiki, sasa wataenda kuwazungukia wakulima na kupima ule udongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa, kuna mazao ambayo yana soko nje ya nchi, Serikali ingeangalia iweke mkakati kuhakikisha haya mazao yanalimwa kwa kiasi cha kutosha ili tupate soko la nchi lenye uhakika. Kwa mfano, nataka kumpongeza Waziri kutoka China ambaye mara kwa mara amekuwa akitupa data ya masoko ya mazao ambayo yanatakiwa. Kwa mfano, mwezi Oktoba mwaka 2020 Tanzania kupitia Balozi Kairuki na China zilisaini mkataba, kuhusu mkataba wa zao la soya, mahitaji ya soya nchini China ni makubwa sana, wanatumia karibu tani 100, wao wenyewe wanazalisha tani Milioni 15, wanaagiza nje tani 85 na Tanzania ni kati ya nchi 14 ambazo China wanaagiza soya. Kwa hiyo, kitendo cha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi 14 zinazoruhusu kuuza maharage ya soya China, tena bahati nzuri yanastawi katika sehemu kubwa ya nchi yetu. Kwa mfano, Soya inastawi Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Katavi, Rukwa, Iringa, Morogoro, Arusha, Manyara, Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Simiyu, Mara, Singida, Lindi, Mtwara, Dodoma na Pwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu Serikali imetoa pesa nyingi sana katika kilimo, ingeangalia sasa jinsi ya kusaidia kilimo katika Mikoa hiyo ambayo nimeitaja walime kwa uhakika ili tuweze kupata soko ambalo linatakiwa, tunakosa kupata soko kwa sababu inakuwa haitoshelezi zile tani zinazohitajika kusafirishwa. Kwa hiyo, mimi naiomba sana Wizara ya Kilimo, najua tuna vijana makini sana, Mawaziri makini wahakikishe kwamba, katika Mikoa hiyo wanatengewa pesa ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaomba kwa sababu mchango wangu ni mkubwa basi nitaachangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)