Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Gairo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nimshukuru Waziri wa Fedha na Naibu wake na wataalam wote, na waliomshauri kutengeneza bajeti hii. Washauri wote wamefanya vizuri sana; kazi yetu sisi kama Wabunge ni kushauri, na ninajua kabisa wao ni wasikivu, watasikia zile sehemu ambazo tunashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwanza kidogo tu kuhusu masuala ya magari. Umezungumzia magari kwamba sasa income tax yake itakuwa ni 3,500,000 pamoja na mabasi makubwa, lakini najua umezungumza kwenye yale magari makubwa hujaenda kwenye yale magari madogo. Kwa hiyo ninaomba muweke mchanganuo vizuri wasije wakachanganya tu gari kubwa na dogo likawa na kodi moja. Lakini na hiyo nayo tunaomba angalau ipungue, kwa sababu 3,500,000 ni kubwa, angalau ingekuja 2,500,000 au hata 3,000,000.
Halafu ya mafuta kuchukua ile faida ya mwenye kituo cha rejareja shilingi 20 katika faida yake ya shilingi 100 ikumbukwe kwamba kuna wengine wana faida ya shilingi 70, kwa hiyo ukishamchukulia tena shilingi 20, ni sawa, hiyo itaondoa milolongo mingi, lakini sasa iwe ndiyo inafaa lakini iwe imekwisha, siyo tena baadaye mnaanza tena hesabu, kunakuwa tena kuna usumbufu ambao si wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kingine, kuhusu magari. Katika bajeti yako umezungumza kwamba sasa hivi watumishi wa Serikali mtawakopesha magari, lakini sasa hapa hujaliweka sawa au tunaomba ukija uliweke sawa; unawakopesha magari, magari yale ukishawakopesha yanakuwa ni ya kwao, na gari likishakuwa mtu ya kwake huwezi tena ukampangia kwamba hili gari sasa hivi labda mtu Mkurugenzi wa Dodoma ukamwambia nenda kijiji fulani. Kitakachotokea ni kwamba watakuwa wanayachunga sana magari yao, kwa hiyo na zile safari za kiserikali au za kwenda kutembelea wananchi zitapungua, huo ndio ukweli. Kwa sababu hawatayatumia kama wanavyoyatumia magari mengine kwa sababu watakuwa wanayaonea huruma na watapunguza safari. Au kuna mpango, je, mtakuwa mnawalipa? maana gari nimeshaikopa, ni yangu, sasa una nilazimisha tena niende nikafanyie kazi nyingine ambayo si yangu. Hiyo nayo tunataka ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ushauri wangu ni kwamba kwenye magari mimi nilikuwa nafikiri tu Serikali mjaribu kudhibiti na mjaribu kutoa miongozo. Nakumbuka kuna Mbunge mmoja Musukuma, aliwahi kulalamika kuhusu Mkurugenzi wake kanunua VX V8. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge; lakini ni kweli hamna mwongozo wa Serikali kuonesha kwamba hapa Wakurugenzi labda wa wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri si watumie tu Land cruiser tu na double cabin? Wekeni miongozo kama hii; yaani pawe level ya watu kutumia magari ya V8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali mnataka mwende na fashion, leo hii kuna watu tayari hapa wana LC300 hizi new model Land cruiser za milioni 500, zipo. Sasa muwe mnaangalia; kama Serikali mnataka kwenda na fashion ninyi ndio mnaleta hasara kwenye hii nchi; muangalie. Kuna watu kama Mawaziri, Rais Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na watu wengine sawa wakitumia magari kama hayo; lakini kuna sehemu zingine huku muwapangie magari gani ya kutumia, double cabin, watumie labda level nyingine, watumie gari hizi prado ndogo, wengine watumie hata crown kama sisi Wabunge; mbona sisi hela mnazotupa ni za crown?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba hela anayopewa Mbunge anapewa hela ya kununua crown mpya, lakini huko nje watu wanajua Wabunge wanakopeshwa ma-V8. Ukimuona Mbunge ana V8 ujue hela kaongeza ya kwake mwenyewe, ndio ukweli huo. Piga hesabu, hela unayompa Mbunge haifiki milioni 100, ananunua gari gani mpya kama siyo crown new model? Ndio ukweli. Sasa huko Serikalini mjibane. Sisi hatuna TEMESA Mbunge unatengeneza gari mwenyewe kila kitu mwenyewe, hupeleki TEMESA. Mtu wa Serikali anapeleka TEMESA anapeleka wapi na bado unataka kumpa gari la gharama; ndiyo maana mnaibiwa. Nataka nikuambie Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu, fanya uchunguzi, hata hii kampuni ya Toyota spare zingine zinazouzwa siyo original; na mimi nilimwambia Mheshimiwa Mbarawa kwenye kamati ya Miundombinu; kwamba hata spare siyo original; fanyeni uchunguzi ninazo huku. Kwa hiyo mnapigwa sehemu nyingi sana.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa
T A A R I F A
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa anayechangia katika kubana matumizi ya Serikali lakini cha ajabu kwenye sensa wameleta mwongozo wa kununua Rover Four kwa milioni 129 ilhali tofauti na Land cruiser ni milioni mbili naomba nichangie tu hivyo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ahmed Shabiby unaipokea hiyo taarifa?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Naipokea kwa mikono miwili. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunajua kabisa wewe na watu wako wote ambao mko mnapanga hiki kitu, mnalitakia Taifa hili mambo mazuri; tunaomba muangalie, wekeni mwongozo wa magari namna ya kufanya, au kama mna mpango wa kuwakopesha basi mtatuletea tutaujua vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine amezungumzia habari ya interest. Tunaona kwenye kila hotuba za kila kiongozi anazungumza interest ni kubwa kwenye benki. Benki zijitahidi kupunguza interest; lakini sielewi. Yaani ni vipi mnakuwa mnafumba macho? Hivyo fedha zote za Serikali, na nyinyi Serikali ndio wenye mtaji mkubwa, zote mnapeleka BOT? Kwa mfano kuna fedha za bandari, TANAPA, TANESCO na za mashirika mengi tu; na hata haya mashirika ya mifuko wa jamii sasa hivi mmeachia kidogo, lakini nusu ziko BOT nusu ziko huku. Kuna baadhi ya taasisi zina hela zao ziko kule BOT zaidi ya miaka mitano hazizalishi wala hazifanyi chochote. Kama mnadhibiti hizi fedha lakini mjue kabisa kwamba fedha yoyote inayokwenda kwenye benki za nje ni Commercial Bank peke yake, ndizo zinasambaza fedha kwa watu, na ndivyo fedha zinakuwa nyingi kwa wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunalalamika fedha hamna lakini fedha mmeziweka wenyewe kule halafu hapo hapo tena mnakuja tena mnakopa kwenye benki hizo hizo, lakini fedha mnaziweka kwenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mkichukua hela zenu zile mnazoweka BOT ambazo hazizai ukiweka kwenye benki za biashara hata kama unazitumia kila siku, unatoa na kuingiza lakini unapata asilimia 3.5. Ukiziweka fixed account unaweza ukapata asilimia sita mpaka saba; kwa hiyo wewe utamkopesha mtu kwa asilimia kumi au tisa, zile benki za biashara zitayakopesha kwa asilimia tisa au kumi. Lakini leo wenye pesa nyingi mnazikumbatia; sasa hivi mnatisha hata wafanyabiashara. Kama ninyi watu wa Serikali hamuamini hizi benki, mna wasi wasi nazo na hata sisi sasa itabidi tutengeneze makabati nyumbani tuwe tunaficha hela zetu, na huo ndiyo ukweli. Yaani lazima mbadilishe hii sera yenu, kwamba kwenda kuweka mabilioni na fedha zote hazikai kwenye mzunguko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu wajiangalie, kwenye treasury bond kuna watu wanaweka pesa wanapata asilimia 15, sasa nani atakayefanya kazi? Sasa hivi mmeshusha mmeweka asilimia 12, mnamwambia mtu aweke miaka 25 mpaka miaka 20 mtampa asilimia 12.5, tena mmeshusha juzi, lakini ziko mlikuwa mnawapa mpaka 15%. Sasa mtu akishaweka hela pale zinakaa kule mtu anakula interest, ana haja ya kuzungusha hiyo fedha? Na ninyi mnawaambia benki washushe, watashushaje hiyo interest kwetu haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mlivyo wafanyakazi, wafanyakazi leo mnatumia Benki ya CRDB na NMB. Ile payroll mnatayarisha Wizara ya Fedha, check list Utumishi. Mnapeleka fedha kule wana-charge service charge, si mbaya ni ki-benki. Lakini angalia mfanyakazi wa umma, huku CRDB ana 13% imeshushwa juzi huku NMB sijui 15%; na hawezi ku-negotiate kwenye kupata mkopo. Lakini mfanyakazi wa mtu binafsi atakwenda benki atafanya negotiations, kwamba tunatakiwa hapa tufanye hivi hivi itakuja hata 12% hata 11%. Sasa, ili kuwasaidia watumishi wetu bora Wizara ya Utumishi ingekuwa inaweka tu kama tender. Kwamba, jamani watumishi wetu mwaka huu wanataka kukopa, benki zijitokeze zilete interest yake, na atakayeonekana ana interest ndogo ndiye aruhusiwe kukopesha watumishi wa umma lakini msiwabane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Shabiby
MHE. AHMED M. SHABIBY:… nilikuwa bado naendelea; basi ahsante, naunga hoja mkono.