Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niungane na Wabunge wote ambao wameendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anazozifanya. Maana hata mimi kule Ludewa nimeshuhudia mambo yakienda kwa kasi. Tunapata fedha za miradi mbalimbali, wananchi kila mahali wako busy. Nami mwaka 2021 nilifanya ziara katika vijiji vyangu vyote 77 na changamoto kubwa ilikuwa ni madarasa ya shule za msingi yalikuwa yamechakaa sana. Nashukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia kwa Waziri wa TAMISEMI tumepata madarasa mengi sana. Kwa hiyo, wananchi watakuwa busy sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri wa Fedha, naye anafanya kazi nzuri na bajeti yake nzuri. Kwa sababu nimepata nafasi hii, namwomba, kule Ludewa kuna barabara moja inaanzia Lugarawa, inaunganisha kata nne; Lugarawa, Mkongobaki, inakwenda Kata ya Ludende kwa Mheshimiwa Vasko Mgimba, Diwani inakwenda mpaka Kata ya Luwana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana kwa sababu ni eneo la uzalishaji. Tulikuwa tumepata mkandarasi pale Boimanda, amefanya kazi, ameshamwaga vile vifusi, lakini kwa bahati mbaya tokea mwezi wa Tano, Mheshimiwa Waziri naomba kule Hazina angalia angalia, Wakandarasi wale wanaofanya kazi za TARURA kuna kama mwezi hivi malipo yao yame-stuck. Kwa hiyo, naomba sana ili wananchi waendelee kufurahia Serikali hii ya Awamu ya Sita, utawala wa Mama Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi, barabara ile kwa kweli iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kumekuwa na changamoto nyingine ambayo wananchi wamekuwa wakinikumbusha mara nyingi, kwa sababu nimesoma ukurasa wa tisa, naona kwamba Serikali imejitahidi sana kukusanya mapato. Hongera sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, umefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia takwimu hapa kwa mwaka uliopita, ukurasa wa tisa, umeainisha pale kwamba hadi kufikia mwezi Aprili, 2022 Serikali ilikuwa imekusanya Shilingi trilioni 19.99 ambayo ni sawa sawa na asilimia 93 ya makadirio. Kwa hiyo, ni pongezi nyingi kwa usimamizi mzuri, lakini wananchi wanaomba kwamba fedha hizi sasa ziweze kuonekana na kule Majimboni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nikikumbusha hapa hoja ya meli Ziwa Nyasa. Nashukuru Naibu Waziri wa Uchukuzi ameahidi tarehe 1/7/2022 meli ile inaweza kuanza kufanya kazi. Wananchi wanaomba sana meli ile ifanye safari zake, ikifika pale Manda au ikifika Wilaya ya Nyasa kwa Mheshimiwa Eng. Manyanya iweze kuunganisha safari na nchi jirani ya Malawi ili kuwapa fursa wananchi kuweza kupata biashara na nchi Jirani; na sasa hivi Diplomasia ya kiuchumi naona imekaa vizuri, kwa hiyo, kutakuwa na fursa sana. Maafisa Uhamiaji wapo, Mheshimiwa Masauni ametuletea, na Maafisa wa TRA wapo. Kwa hiyo, itakuwa rahisi zaidi wakiweka pale One Stock Center, biashara kati ya Tanzania na Malawi inaweza ikawa rahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna eneo wananchi wanaliita Chilumba, Malawi. Wanasema pale ni kilometa 40 tu hadi 45. Kwa hiyo, hata maboti wananchi wakiruhusiwa tunaweza tukaongeza fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Malawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wananchi wamekuwa wakinikumbusha mara kwa mara ni wale wakandarasi. Namwona Naibu Waziri wa Nishati, wale wa REA, kwenye zile Kata za Lumbila, Kilondo na baadhi ya Vijiji vya Makonde, bado Mkandarasi hajafika site na nguzo hazijapelekwa. Kwa hiyo, tunaomba muweze kumkumbusha, wananchi hao nao waweze kuona kwamba wapo sehemu ya Tanzania, wapate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile yule mkandarasi aliyepewa Mkwimbili, Makonde na Kata ya Lifuma naye bado hajawasha umeme kwa muda mrefu, wananchi wanaona wananyimwa fursa za kupata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia Serikali kwa kuongeza bajeti ya uvuvi. Nasi kule Ludewa tuna Ziwa Nyasa, tuna kata nane zipo kando kando ya ziwa. Kwa hiyo, fedha hii niliomba tuweze kupewa kituo tujengewe soko lile la ule Mwalo, kwa ajili ya kuuzia bidhaa za Samaki, na watusaidie teknolojia ya kuhifadhi dagaa wa ziwa Nyasa. Ziwa Nyasa lina dagaa wengi wazuri, lakini ninaamini Wizara kwa fedha hiyo wanaweza wakaja na teknolojia mpya ya kuhifadhi wale dagaa ili tuweze kutoa ajira zaidi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaishukuru Wizara tumeweza kushirikiana nao kufanya utafiti na kuona athari zipi za kimazingira iwapo tutaanzisha ufugaji wa samaki kwenye Ziwa Nyasa. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, atusaidie upatikanaji wa vifaranga bora vya samaki na Wizara iendelee kufuatilia ubora wa vifaranga vyao, kwa sababu baadhi ya wafugaji wanapata hasara wakati mwingine. Kwa hiyo, watusaidie pia upatikanaji wa chakula cha samaki, hili ni eneo ambalo limeajiri Watanzania wengi sana. Vilevile waziangalie vizuri hizi sera, sheria na miongozo. Sheria nyingi zinazotumika ni za uvuvi kumbe kungekuwa na sera za ufugaji wa samaki na sheria ya ufugaji wa samaki na tungepunguza urasimu, tungeweza kutengeneza ajira nyingi sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia sekta ya uvuvi nije sasa nipongeze pia Serikali kwa kutoa kipaumbele kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo, ila naomba tu hii mbolea ya ambayo imewekewa ruzuku, katika mikoa yetu iweze kufika mapema sana kwa sababu wananchi wanaitumia kwenye kilimo cha viazi. Kwa hiyo ikifika mapema inaweza kusaidia. Vilevile soko la mahindi kwa sababu wananchi wameumia sana kwa bei ya mbolea, kwa hiyo tuangalie mahindi yaweze kununuliwa kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimtake Waziri wa Fedha anapofanya majumuisho, atueleze maana yake Wizara ya Ardhi ni nyeti sana, tunapozungumzia maboresho ya kilimo, tunapozungumzia umwagiliaji lazima watu wa ardhi watangulie kwenda kufanya upimaji na mipango ya matumizi bora ya ardhi, lakini bajeti ambayo wametengewa Wizara ya Ardhi ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi wanafanya kazi nzuri sana na wameanzisha mifumo ambayo inarahisisha sana utendaji kazi. Kuna mfumo unaitwa ILMIS, mfumo huu ni mzuri sana. Unaunganisha taarifa zote za ardhi hata maeneo ambayo hayajapimwa unaweza kutambua, lakini hii inasaidia sana kupunguza muda wa kumhudumia mwananchi, kurahisisha ukusanyaji wa mapato, lakini hata kuepusha migogoro ya matumizi mbalimbali ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sekta hii ina vifaa ambavyo ni gharama sana ili waweze kupeleka, kwa sababu mfumo huu wa ILMIS unatumika Dodoma na Dar es Salaam pekee. Sasa Jiji la Mwanza nalo lina viwanja vingi, Arusha, Mbeya, Tanga na Manispaa nyingine kama Morogoro. Kwa hiyo ili Wizara ya Ardhi iweze kufika maeneo haya na kuweka hii mifumo, Serikali haina budi kuwaongezea fedha, zitolewe fedha za kutosha ili wafunge mifumo hii ili tupunguze kuwalaumu kwa migogoro ya ardhi na vilevile tuwaongezee wataalam. Hapa Jiji la Dodoma kwa mfano, kuna upungufu mkubwa wa wataalam, kweli Wizara inajitahidi na wengi wamehamishwa, lakini hakuna replacement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wananchi wanalisikitikia kwa muda mrefu ni issue ya Mchuchuma na Liganga. Miradi hii imegunduliwa miaka mingi sana, mwaka 1898 na mwaka 1860. Kwa maslahi ya muda na kwa sababu ya vita vya kiuchumi, nitachangia mradi huu kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. (Makofi)