Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, kwanza kabisa niungane na wenzangu waliompongeza kiongozi wetu wa Serikali na nchi yetu Mheshimiwa Rais. Niungane pia na wote waliompongeza Waziri mwenye dhamana ya fedha, Naibu wake, Katibu Mkuu na wote wanaowasaidia katika Wizara hii ambayo kwa kweli ndio imebeba matumaini makubwa ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni Wizara mbili ndani ya Wizara moja na leo kwa bahati mbaya tunachangia mambo mawili katika moja, maana hapa leo tunachangia Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo na wakati huo huo tunachangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa 2022/2023. Sasa nataka niliombe kwanza Bunge lako katika utaratibu mzuri kwa uzito wa mambo haya, ndio maana wakati mwingine utakuta hapa tunasimama Wabunge tunajielekeza kwenye jambo moja tu linalohusu matumizi, lakini jambo linalohusu mapato na mpango wa maendeleo tunaliacha kwa sababu tunaona muda ni finyu na shughuli yenyewe ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ilani ya CCM ya toka mwaka wa 1995, 2000, 2005, 2010, kuna jambo moja ambalo CCM imeliweka kama dira katika kuongoza nchi yetu. Jambo lenyewe linasemaje? Linasema kwamba katika kipindi hiki CCM inataka tujenge Taifa lenye uchumi wa kisasa, linalojitegemea na kuondokana na Taifa duni na tegemezi lakini ukiangalia Bajeti zetu bado hazijajibu dira hii ya chama ya kujenga Taifa lenye uchumi wa kisasa linalojitegemea na kuondokana na uchumi duni na tegemezi. Bajeti zetu kwa sehemu kubwa bado ni tegemezi.
Mheshimiwa Mweyekiti, hata leo tunapofurahia hapa tunafurahia mambo mengine ambayo tunafurahia matarajio kwa sababu makadirio ya mapato na matumizi, maana yake ni makadirio. Unaweza ukapata kile unachotaka kukikusanya au usikipate. Leo asilimia 14 ya bajeti hii ambayo ni trilioni 5.78 ni mikopo, unaweza ukapata mkopo au unaweza usipate mkopo. Sasa hapa ndipo ninapotaka tujielekeze vizuri na kwa nini nataka tujielekeze hapa? Tuongeze nguvu zetu katika mapato ya ndani ili tupunguze fikra za kutegemea mikopo na uwezekano huo upo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesimama hapa ndugu yangu Mheshimiwa Tabasam, akaeleza njia za kupata fedha. Amesimama hapa pia Mheshimiwa Kunambi pamoja na kwamba mengine hawakumwelewa, lakini amezungumzia kuongeza wigo wa kodi katika kupima ardhi, unafanya kitu gani? Unachukua darubini, unapima, halafu unatoa karatasi kumpa mwananchi, yeye anakupa fedha kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nasimama kusema jambo moja la masikitiko, nalo ni kodi kwenye biashara ya vitenge. Hili nataka Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri sana. Hili jambo linanisikitisha kidogo na linanisikitisha kwa sababu naona kuna kitu ambacho kinawezekana. Sisi tuna viwanda vya nguo 33 hapa nchini, lakini kati ya viwanda hivyo ni viwanda tisa tu ndio vinavyofanya kazi. Uzalishaji wa vitenge kwa mwezi mmoja ni kati ya kontena sita mpaka nane. Mahitaji ya vitenge nchini kwa tafiti zilizofanywa ni kati ya kontena 38 mpaka 40. Kwa hiyo tuna mambo mawili, tuna production ambayo haijibu demand, lakini wakati huohuo tuna tatizo la quality, maana hata kama tunazalisha vitenge Tanzania, lakini bado quality inaweza ikawa ni mgogoro. Huwezi kumlazimisha kila mtu avae quality tunayozalisha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo baadhi ya Watanzania ni kwamba ni lazima wavae vitenge. Serikali ikiweka kodi kubwa watavivaa kwa magendo na Serikali itakosa kodi, ikiwekwa kodi inayolipika, Serikali itapata mapato na wananchi watavaa. Nataka kuonesha mfano mmoja tu wa Kigoma. Mkoa mzima wa Kigoma, ushuru wa forodha ulikuwa hauzidi milioni 15 kwa mwezi, lakini akaja Meneja wa TRA mmoja anaitwa Bwana Gabriel Mwangosi, ndio Meneja wa Mkoa, pale, sasa hivi amesimamishwa kazi na nitaeleza kwa nini kasimamishwa kazi. Akaleta harmony kwenye suala la kukusanya kodi ya forodha, akawataka wafanyabiashara wasipite njia za pembeni na akawataka watu wake kuachana na habari ya kuchukua hela kuweka mfukoni badala ya kuingia Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwezi mmoja, mwezi wa Oktoba 2021, wakakusanya milioni 155 kutoka milioni 15. Mwezi Novemba wakakusanya shilingi milini 380 kutoka milioni 15. Mwezi Desemba akakusanya milioni 550 kutoka kwenye milioni 15. Nini ninachokusudia kusema? Ninachokusudia kusema ni kwamba, eneo hili tunaweza tukapata kodi, lakini kasimamishwa kazi na Kamishna Mkuu wa TRA, sababu ame-charge chini ya kiwango, kwamba afadhali watu wapige hela mfukoni kuliko kuingia kwenye Mamlaka ya Serikali. Nasikitika sana, nasikitika sana na jambo hili. Yule Bwana Gabriel Mwangosi siyo shemeji yangu, siyo mjomba wangu, sina unasaba naye lakini nimemuhurumia sana, uzalendo wake leo unamfikisha mahali anasimamishwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vitenge…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Mheshimiwa Tabasam Taarifa.
TAARIFA
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazalendo katika nchi hii hawatakiwi, wanatafutwa kwa tochi, wazalendo katika nchi hii wanaitwa kizabizabina, wanawekewa majina ya kila namna, huyo Kamishna ni miongoni mwa watu mashujaa katika nchi hii, anatakiwa kupigiwa makofi. Ahsanteni sana. (Kicheko/Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiumbe una…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Meneja, Meneja, Meneja wa Kigoma.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe unaipokea hiyo taarifa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.
MHE. KIUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.
MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Kilumbe naomba usubiri.
KUHUSU UTARATIBU
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamheshimu sana Mheshimiwa Tabasam pia nilikuwa nanogewa na mchango mzuri aliokuwa anautoa Mheshimiwa Ng’enda. Neno aliloliweka Mheshimiwa Tabasam kwamba wazalendo nchi hii wanaitwa majina mabaya mabaya tu, wanoko sijui vizabizabina na maneno mengine aliyoyatumia siyo maneno ya Kibunge pia Kanuni zetu zinakataza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 71(1)(a) kwamba Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli. Sasa hayo maneno yeye ameyafanyia utafiti ana ukweli nayo? Pia ni maneno yanayochochea na kuzidisha chuki dhidi ya wale ambao wanafanya mambo mazuri na makubwa kwa nchi hii, kwamba wote wanaofanya mazuri kwa nchi hii ni wabaya, siyo neno zuri sana hili.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam tumepokea huo utaratibu kutoka kwa Mheshimiwa Chief Whip Kanuni ya 71(1) inakataza kuzungumza neno lolote ambalo huna ushahidi nalo, siyo la kweli na hilo neno ulilotumia la kwamba wazalendo wanatafutwa nchi hii na labda maneno mengine mabaya, naomba uyafute.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, neno alilolitamka Mheshimiwa Simbachawene namheshimu sana, neno ‘mnoko’ sijalisema mimi. Yeye ndiyo anatakiwa aombe radhi katika hilo. Lakini Mheshimiwa kusema wazalendo wanaitwa kwa majina mabaya na kwamba wazalendo sasa hivi katika nchi hii ni wakuwatafuta kwa tochi, siombi msamaha katika hilo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachosema ni kwamba kauli hii kama imekataliwa iondoke katika Hansard. Ahsanteni sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam, Mheshimiwa Tabasam taarifa yako yote kwa Mheshimiwa Kilumbe naomba iondoke kwenye Hansard. Mheshimiwa Kilumbe naomba uendelee.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nakushukuru kwa busara za kuutunza muda wangu ili niendelee pale nilipokuwa nimeishia. Bado nipo kwenye vitenge, sikusudii kumlaumu Mheshimiwa Waziri wala Mamlaka ya Kukusanya Mapato ya TRA, nakusudia kuzungumza namna ya kuleta harmony kwenye ukusanyaji wa kodi na kama kuna mahala kuna tatizo tunarudi hapa kama ni sheria turekebishe sheria ili iendane na mahitaji ya sasa. Hiyo ndiyo hoja yangu kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi sheria tulizitunga kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu vya ndani na sheria hizo tulizozitunga kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu vya ndani, kama viwanda vyenyewe haviwezi kukidhi mahitaji……
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe subiri kidogo, taarifa Mheshimiwa Musukuma.
T A A R I F A
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji anayechangia vizuri sana kwenye biashara ya vitenge. Pamoja na Serikali kupandisha kodi, kuweka vizuizi vingi bado vitenge vimejaa Kariakoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia nyepesi inayotumika, wafanyabiashara walewale wameenda kufungua maduka Tunduma, kwa hiyo, makontena yanaandikwa transit Malawi wakifika pale mpakani kuna maduka halafu vinarudi vitenge na malori. Sasa ninaunga mkono kwamba tunapoteza fedha kwa sababu ya ukiritimba na watu wanaofanya biashara wapo wanajulikana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda unapokea hiyo taarifa?
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hiyo kwa mikono miwili na ninaendelea kupitia taarifa hiyo kwamba nchi ya Zambia jirani zetu, kontena moja la vitenge kodi yake ni kati ya shilingi milioni 18 mpaka shilingi milioni 24 za Kitanzania. Zanzibar ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kontena kama hilohilo ni shilingi milioni 35 za Kitanzania. Nchi ya Kenya, kontena hilohilo ni shilingi milioni 35 lakini Tanzania Bara kontena hilo ni shilingi milioni 397! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kutafuta fedha za kukopa, tunaacha tunazoweza kukusanya wenyewe bila matatizo. Ninataka Waziri atakapokuja hapa, atueleze bahati nzuri sana Mheshimiwa Mwigulu mimi amekuwa Kiongozi wangu wa kazi, ni mtu msikivu, mtu mwadilifu, mtu mwaminifu kwa Taifa. Naomba atakapokuja hapa atuambie tunatokaje hapa kwa faida ya nchi yetu. Kwamba tukusanye kodi isaidie Taifa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Malizia sentensi yako muda umeisha.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda uliobakia niseme neno moja, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye Kiongozi Mkuu mwenye imani na wananchi anasisitiza kukusanya kodi kistaarabu, kuleta harmony kwenye kodi, watu wasibambikiwe kodi, wasikusanyishwe kodi za miaka 10 iliyopita. Nauliza, kuna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa TRA? Kwa nini TRA hawasikii? Kwa nini wanaendelea na vitendo hivi? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe muda wako umeisha. Ahsante.
WABUNGE: Aendelee.