Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii ya bajeti ambayo inaenda kuakisi maisha ya mtanzania hasa kwenye mwaka wa fedha huu ambao unakuja. Kwanza niipongeze Serikali ya awamu ya sita kutuletea bajeti hii nzuri lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam wake wote wa wizara kuweza kuleta hii bajeti ambayo sisi kama Wabunge tunaona inaenda kwenda kumkomboa mwananchi wa Tanzania na kukuza uchumi wa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona bajeti hii namna ambavyo inaakisi hali ya ukuaji wetu wa uchumi. Nilikuwa napitia taarifa aliyopewa hapa tuaona ukuaji wetu wa bajeti namna ambavyo unazidi kwenda mwaka hadi mwaka. Tukipitia kwenye hii taarifa, tangu mwaka 1999/2000 bajeti kuu ilikuwa ni trioni 1.3; lakini mwaka 2022/2023 bajeti kuu imekuwa ni trioni 41. Lakini kwenye taarifa zao zilikuwa zinaonyesha kwamba kufikia trioni 42 itakuwa mwaka 2025/2026; sasa hivi tumeweza kwenda vizuri zaidi Serikali ya awamu ya sita kabla ya 2025/2026 kufikia trioni 42 sisi 2022/2023 tumefikia trioni 41 tuipongeza sana Serikali na Mheshimiwa Waziri na wataalam wake kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchango wangu mimi nitajikita kwenye mambo makubwa matatu; nitazungumza habari ya kilimo nitazungumza habari ya miundombinu na barabara lakini pia nitazungumza habari ya makaa ya mawe pamoja na chuma kule Liganga na Mchuchuma, na muda ukiwepo nitazungumza habari ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona Serikali awamu ya sita namna ambavyo imeamua kumkomba mkulima wa nchi hii. Kama tunavyojua wakulima wa nchi hii takribani asilimia 70 tunategemea kilimo. Hawa wananchi ni wengi zaidi; na kwa kuwekeza kwenye kilimo maana yake tunakwenda kupiga hatua kubwa sana. Tunaona namna Serikali imeongeza bajeti toka bilioni 294 mpaka zaidi ya bilioni 900, kuna ongezeko ya zaidi ya milioni 700 kwenye kilimo. Hii ni hatua kubwa sana kumkomboa mkulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuishukuru pia Serikali, sisi wakulima wa tumbaku tunaona namna juhudi kubwa ambazo Serikali ya awamu sita imeweza kufanya. Kutoka kuwa na mnunuzi mmoja sasa tunaenda kupata wanunuzi wengi zaidi, tayari kwenye upande wa tumbaku tumeweza kupata Kampuni ya Amiworld Company Limited ambao tayari mwaka huu wameshaanza kununua tumbaku. Lakini bado tunaendelea, kuna kampuni nyingine pia imeshajitokeza na sisi Wilaya yetu ya Chunya imekuja kujitambulisha jana inaitwa Voedsel Tobacco Tanzania Limited; maana yake sasa tunakwenda kuwa na kampuni nyingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hizi tunazikaribisha sana sisi wakulima wa tumbaku, na sisi watu wa Chunya Tarafa la Kipambalwe tunaomba ziweze kufika haraka zaidi, ziweze kuongea na vyama vya misingi tuweze kukubaliana tuongeze makisio ili mwaka ujao wa kilimo tuweze kulima kwa makisio makubwa zaidi na baadaye tupate bei iliyokuwa nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri haya ambao Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwenye kilimo; tunaona dhamira nzuri zaidi; lakini je, tuangalie huku kwenye kilimo tulikowekeza hivi watu wakishalima msimu ujao wakishavuna je, tumejiandaa kwa masoko yakutosha? je tumejiandaa kwa viwanda vya kuweza kupokea malighafi zinazotoka shambani huko vya kutosha? tulikuwa tunaona kwenye tv takribani wiki moja iliyopita maeneo ya Tanga kule wakulima wa mihogo wamelima mihogo yao vizuri zaidi lakini wamekosa soko na mihogo ile imeharibika sasa ikawa inamwagwa. Hili ni funzo kubwa sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ni mihogo kidogo tu, tani chache, sasa sisi sasa hivi tunakwenda kuwekeza vya kutosha kwenye kilimo. Je, uwekezaji huu utaenda sambamba na masoko pamoja na viwanda hili viweze kutusaidia? Mimi niishauri Serikali, pamoja tumewekeza kwenye kilimo sasa nguvu kubwa twende tukaielekeze kwenye masoko pamoja na viwanda vidogodogo. Viwanda hivi tutahakikisha kwamba malighafi inayotoka tunaweza kusindika hapa kabla hatujauza nje, na tukiweza kusindika hizi kuanza kuziongezea thamani hizi mali zinatoka kwenye kilimo maana yake, tutatengeneza ajira za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajira hizi vijana wetu hawa wataweza kuajiriwa kwenye hivi viwanda vidogovidogo. Maana yake sasa huyo mnyororo wa thamani kutoka kwenye kilimo, kule mazao tunakoyapata kule, itaenda sambamba sasa kwenye masoko, na baadaye kwenye viwanda hivi na baadaye wananchi wetu wakipata ajira hivi uchumi utakuwa zaidi lakini pia kwa Tanzania tutakuwa tumepiga hatua kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo sasa nizungumzie habari ya miundombinu. Tumewekeza vizuri kwenye kilimo, sawa, lakini, je, miundombinu yetu hii ambayo tunayo inaakisi uwekezaji huu ambao umepelekwa kwenye kilimo? Je, pembejeo hizi zitaweza kufika vizuri kule kwa wakati? Zitaweza kuwafikia kule vijijini ambako kuna barabara zisizo rafiki kwa wakati? Tuangalie vizuri sana, kwenye miundombinu pia tuongeze bajeti. Tuone namna ambayo tuangalie kwa jicho la pekee miundombinu hii ili iweze kujengwa kwa haraka zaidi ili haya mazuri ambayo yanajitunza kwenye kilimo tuweze kuhakikisha kwamba yanaleta tija kwa wananchi wetu lakini kwenye uchumi wetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme kwamba moja kati ya sera kwenye upande wa barabara ni kuunganisha mikoa kwa mikoa. Tumeona kazi kubwa inafanyika miradi ya barabara inaendelea karibu kila kona ya nchi hii na mimi niseme tu….

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niseme tu, ndani ya Mkoa wetu wa Mbeya tuone kazi kubwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita inaenda kufanya. Barabara yetu ile ya kuanzia Igawa mpaka Tunduma ipo kwenye mipango, sasa inaenda kutekelezeka. Hii barabara inaenda kugawiwa kwa maana ya vipande vipande, na tayari tender imeshatangazwa, kipande cha kutoka Uyole mpaka Ifisi karibu kilometa 29 itaenda kujengwa kwa njia nne. Tunaishukuru sana Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kufanya hivi, bado barabara yetu ya kuunganisha Mkoa wa Mbeya pamoja na Mkoa wa Tabora na Singida imekuwa inaahidiwa mara nyingi kwenye mipango ya Serikali na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi imekuwa inawekwa. Barabara hii inaanzia Makongorosi mpaka Mkiwa. Tunaiomba sana Serikali ya Awamu ya Sita. Mheshimiwa Waziri Fedha, najua kwamba barabara hii na wewe pia inakugusa, tuiangalie kwa jicho la kipekee ili barabara hii iweze kujengwa haraka sana iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoyasema haya, sisi tayari Wilaya ya Chunya kule kutokana na ziara za mama ambazo anazifanya kwenda kufungua nchi, tayari tumeshapata wawekezaji kuja kulima kwenye kilimo cha Soya. Mwekezaji huyu anakuja na tayari ameshafika kule, sisi tayari tumeshampatia eneo lenye zaidi ya ekari 17,000 aweze kuwekeza kule. Sasa kwa miundombinu hii ya barabara ambayo siyo rafiki, barabara ya vumbi, tuone namna nzuri ili tusimkatishe tamaa na hii kazi iweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa Habari ya chuma pamoja na makaa ya mawe. Tanzania tuna chuma cha kutosha na makaa ya mawe. Duniani sasa hivi kuna vita kati ya Ukraine na Urusi. Hizi ni nchi ambazo zinaongoza kwa uzalishaji mkubwa sana wa makaa ya mawe pamoja na chuma na tayari hizi nchi zimeshawekewa vikwazo kwenye Mataifa makubwa sana kule Ulaya na Amerika. Sisi hii ndiyo nafasi pekee ya kutumia vita hii kuweza kujiimarisha kiuchumi, kuweza kuchimba makaa yetu ya mawe na kuchimba chuma chetu ili sasa na tuweze kuuza nje ya nchi. Tukiuza nje, maana yake hii ni fursa kwetu kwamba uchumi wetu tuweze kuupandisha. (Makofi
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa ya mchambuzi mmoja alikuwa anaongelea kwamba mwaka 2021 sisi Tanzania tuliagiza chuma kutoka nje chenye thamani ya Dola milioni 700.6. Hizi ni fedha nyingi sana ambazo tunaagiza kutoka nje. Je, Tanzania kwa hizi fedha ambazo tunaagiza chuma kutoka nje, tukizitumia hizi fedha Dola 700.6 kuwekeza kwenye chuma chetu hapa na makaa yetu ya mawe, tutapata faida kiasi gani? Naomba sana Serikali tuone kwa udharura wake, tuangalie kwenye haya makaa ya mawe pamoja na chuma hiki, namna gani ambavyo vitaweza kutusaidia kuhakikisha uchumi wetu unakwenda mbali zaidi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mengine nitaleta mchango wangu kwa maandishi, nami naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)