Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuchangia. Kama ilivyo kawaida yetu, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, amefanya kazi iliyotukuka. Ni wajibu wa Chama cha Mapinduzi kulinda masilahi yote yanayofanyika ya Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi, na tutamlinda kwa yote mazuri atakayokuwa anayafanya, nasi wenyewe tutaendelea kufanya hizo kazi nzuri. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu; kawaida yangu huwa nikichangia hoja nzito, huwa naangalia mtu ametoka wapi? Nilikuwa nakuchunguza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ulisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na ulipa first class. Ulisoma miaka 20 tu baada ya kuhitimu degree yako ya Kwanza ya Fedha, ukapelekwa Hazina, wakakuchukua Benki Kuu. Wakakununulia gari ya kwanza ukiwa mdogo ukawa unafundishwa pale kuendesha.
MBUNGE FULANI: Haaa!
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Sasa baadaye wakakurudisha kufanya kazi. Sasa waliokuteua hapo, wanaangalia uwezo wako. Siyo kwamba wewe unapendeza, hapana. Wameangalia uwezo wako. Kwa hiyo, nakushukuru sana kwa kazi hiyo. Pia bajeti uliyotupa ni nzuri sana na wote tumeikubali. Ni bajeti ya matumaini, tunategemea huko mbele itakuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo linaitwa tembo. Nianze na tembo. Kwakweli nitoe pole kwa ndugu yangu Kitawita Ginanani aliyefiwa na mke wake akiwa na mtoto mgongoni hivi karibuni tarehe 11/6/2022. Mama alikuwa anasindikiza mtoto mwingine akiwa na mtoto wake wa miezi saba mgongoni, akauawa na tembo juzi tarehe 11. Kwa kweli tembo ni tishio kwa watu wetu. Ni tishio kwa watu wote wanaoishi kwenye maeneo yetu. Hata hivyo, kwa hilo namshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, amefanya kazi kubwa sana, yule mama akazikwa kwa wakati muafaka na vyombo vyote vinavyohusika vilihusika pale, wakamzika. Wamemtendea haki kwa kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana tembo atamaliza watu wetu. Hili la tembo tusipoliangalia, mtamaliza Mawaziri wote kwenye Wizara hiyo. Kwa sababu gani? Nataka niwaambie ukweli Waheshimiwa Wabunge, TANAPA na TAWA vilipoanzishwa kwa miaka hiyo, toka Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere, ikaja ya Rais Mwinyi, ikaja ya Mkapa, akaja Mheshimiwa Kikwete, akaja Mheshimiwa Magufuli. Sasa kutokana na Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli, hapa Awamu ya Tano hii, kutokana na Corona fedha za TANAPA na TAWA wakapeleka Hazina. Hili jambo tusipolichukulia makini, watu wetu watamalizika na mbuga zitamalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu anaandika fedha, anaenda kuomba fedha Hazina, zirudi ziende kulinda tembo. Kwa hiyo, ni wakati muafaka sasa fedha za tembo, fedha za TANAPA na fedha za TAWA warudishe wenyewe walipokuwa wanazitumia toka awali. Tutaua mbuga zetu na mtawafukuza Mawaziri wote kama hizi fedha haziwezi kurudi kwa wenyewe. Huwezi kuandika fedha eti uende ulinde tembo ulipe askari, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Serikali, katika hili la tembo mfanye mambo mawili; la kwanza, lazima tuendeleze ule mtindo wa kujenga fence kwenye maeneo yanayozunguka watu. Kama fence imesaidia Botswana, inaweza kutusaidia na sisi. La pili, ni muda muafaka sasa Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha uzazi wa mpango kwa tembo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekti, haiwezekani sasa! Kama tembo mwenyewe hamwezi kuwavuna, wanaendelea kuua watu, tuanzishe uzazi wa mpango kwa tembo wale ili wasizae zaidi. Vinginevyo tutaua watu. Ni tembo wangapi wanahitajika kwenye nchi hii ili watalii waone? Tembo wangapi wanaohitajika sasa, tujue? Haiwezekani watu wanakufa kila siku tupo tunaangalia. Tunalinda watu kwanza, wanyama baadaye. Haya mambo yamezungumzwa muda mrefu na tunaendelea kuyaona. (Kicheko/Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Boniphace, kuna taarifa.
T A A R I F A
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji, anachosema ni kweli kwamba inatakiwa kufanyika mkakati wa juu zaidi, kwa sababu katika Wilaya yetu ya Ikungi nilisema mtoto alikanyagwa na tembo mwezi wa Tano, na juzi mzee mmoja wa miaka 82 pale Mlumbi naye amekanyagwa tena na tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hali hii ya tembo lazima Serikali ichukue hatua stahiki ili kusaidia hali hii ambayo inaendelea, kwa sababu wananchi hawawezi kuwafanyia chochote tembo kwa sababu ni nyara ya Serikali, lakini nyara hii Serikali isiwe ni tatizo kuwamaliza wananchi wetu. Mwananchi ana umuhimu zaidi kuliko tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea hiyo taarifa?
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza hili suala la tembo tusipolichukulia kwa umakini, kwa kweli hata hiyo Royal Tour tunayoizungumza hapa itakuwa ni kikwazo, kwa sababu watu hawawezi kufurahia Royal Tour kama wanakufa, haiwezekani. Kwa hiyo, nadhani Serikali imesikia vizuri hili jambo, italifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za TANAPA na TAWA warudishieni wenyewe wahudumie, kwa sababu tuna mbuga 22, lakini zinazozalisha ni mbuga tano tu, watatoa wapi fedha za kutunza mbunga nyingine? Tuna hifadhi hizi za game reserve 27 na kitu, wanatoa wapi fedha? Tuwape fedha zao washughulike na hizo mbuga nyingine. Hata na sisi tukitaka semina au makongamano kwenye maeneo yetu, watuletee fedha wananchi wapewe semina na kufanya makongamano. Watatoa wapi fedha? Kwa hiyo, nafikiri kwamba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu umesikia hilo na Serikali imelisikia, itafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kuzungumza ni suala la Machinga. Wabunge wamezungumza humu sana hili, naliangalia, nasoma nchi nyingine huku nyuma, naangalia mambo wanavyofanya. Hivi nchi yetu tukoje? Wenzetu wa Ulaya wanatengeneza incentive, wanatengeneza mazingira mazuri ya kubakiza watu vijijini, vijana wakae vijijini wasihamie mjini. Kazi yetu sisi ni kurekebisha majiji watu wahamie mjini. Hivi watu wakoje hawa? Hivi maneno gani haya? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani badala ya kutunza vijana wakae kule vijijini walime, tunabakiza wazee, tunasema kilimo, kilimo, kilimo; kitalimwa na nani? Watoto wetu wote watakuja kuwajengea majumba humu ndani, watakaa nani huku ndani? Hilo suala la Machinga, kwanza tuliangalie vizuri. Machinga tafsiri yake ni nini? Si vijana wanaofanya kazi! Vijijini hawapo, wameenda wapi? Yaani tubebe hela kutoka vijijini, tulete mjini. Sisi tutaishi na nani sasa? Wazee wabaki na nani? Kwa hiyo, nafikiri Wabunge, wamezungumza vizuri, ile asilimia 10 haiwezekani. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kulizungumza hapa, mtu mwingine alikuwa ananikumbusha hapa kwamba sasa wanataka TASAF itunze wazee kule vijana waje machinga mjini, kazi ngumu sana hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu pesa ya miamala, sisi Wabunge tulikabiliana na hiyo adha kubwa sana huko mitaani pesa ya miamala. Tukaitetea kwamba hiyo fedha itakwenda kujenga vituo vya afya na maboma yetu. Fedha hii ilipokuja Mheshimiwa Ummy akiwa Wizara ya TAMISEMI akaanza kuitangaza leo tuna milioni nne, bilioni nne, leo tuna bilioni ngapi, tutapeleka kwenye vituo, tutapeleka kwenye Tarafa, tukasikia. Leo nauliza, siku moja nagombana na mwenzangu wa Mwibara anasema mimi bwana napewa sekondari mbili, nikamwambia mwenzangu hivi hela za miamala zikiisha mimi nitasemaje, acha na mimi nipate hizo hela za miamala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangisha, wananchi wanachanga hela za miamala tulikuwa tunazitangaza, sasa ziko wapi? Mbona hawazitangazi, walituambia hela zitakuwa zinakuja hapa tunatangaza, zinaenda kwenye vituo vya afya, zinaenda kwenye maboma, zinaenda kwingine, ziko wapi, zinatangazwa wapi? Isije ikawa makusanyo ya TRA ndiyo fedha za miamala. Hapana, hiyo hatuwezi kukubali. Kwa hiyo Mheshimiwa Mwigulu atuambie fedha za miamala mpaka sasa zimekusanywa ngapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia tena fedha ya majengo. Fedha ya majengo, Serikali imechukua vyanzo vya halmashauri, fedha ya majengo wakasema TRA ikusanye, na fedha ile inakusanywa kupitia TANESCO. Maana yake ni fedha moja kwa moja, hizo fedha za majengo, ziko wapi? Mheshimiwa Mwigulu akija hapa atuambie, fedha ya majengo ni ngapi, isichanganywe na fedha ya TRA. Kwa hiyo, Waziri atuambie fedha ya majengo iko wapi? Waheshimiwa Wabunge nilikuwa nafikiri sasa hii fedha ya majengo na hii fedha ya miamala tungepeleka moja kwa moja kwa wananchi wetu itusaidie maboma, vituo vya afya, tuna hali mbaya vijijini. Fedha ambayo inakusanywa moja kwa moja tunaiona, iende vijijini.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Hiyo kengele ya kwanza. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere, kengele ya pili, Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana ya kwanza.
MWENYEKITI: Ya pili hiyo, Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza.
MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ya pili, Makatibu wako makini sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, lakini naomba fedha ya miamala na fedha ya majengo ijulikane inafanya kazi gani, ahsante. (Makofi)