Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Santiel Eric Kirumba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Fedha. Awali ya yote ningependa kuipongeza Serikali kwa bajeti hii ambayo imekuja mahsusi kuweza kubana bajeti katika matumizi ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuipongeza bajeti hii imetua mzigo mkubwa kwa wananchi hususan kwenye suala la ada, kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha tano watoto wetu wanasoma bure. Bajeti hii pia naipongeza katika Wizara ya Afya na Sekta ya Maji, tumeweza kupata mitambo ya kisasa kwenye Sekta ya Afya na yote inaonekana kwamba imeshafika. Katika suala la maji pia mitambo ya kuchimba visima ambayo itaenda katika mikoa yote imeshafika, ningependa kuipongeza Serikali kwa hatua hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maoni machache sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameomba atoe asilimia tano, katika asilimia 10 zile za mapato ya halmashauri. Tunavyopita kwenye kampeni wenyewe tumeandika Ilani wenyewe, tukasema hizi asilimia 10 tutazitoa kwa makundi maalum. Leo tena tunarudi hapa kutengua kauli zetu kwamba tuzipunguze kutoka asilimia 10, kwenda kwenye asilimia tano ilhali tukiwa tunajua asilimia 10 yenyewe haitoshelezi, hii si sawa. Haya makundi maalum yana uhitaji mkubwa, ukiangalia kwamba si watu wote wataajiriwa kwenye Serikali, lakini hii ni namna moja Serikali imetenga fedha hii katika Halmashauri ili wananchi wale ambao hawajapata ajira waweze kujikomboa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano mmoja katika Mkoa wangu wa Shinyanga ambao pesa hii ya asilimia tano imeambiwa ikaende kwenye miundombinu. Natoa mfano wangu katika Mkoa wangu wa Shinyanga, TANROADS kwa mwaka huu wa fedha 2022 kwenda 2023 wameomba bilioni 13 kwa ajili ya barabara na kwa mwaka Mkoa wetu wa Shinyanga unakusanya mapato ya ndani bilioni 27. Wakitenga ile asilimia 10 tunapata bilioni mbili, hii hela hata tukipeleka kwenye hiyo miundombinu ambayo tumepanga haina tija. Ningependelea hii hela hii ibaki kwa sababu Mkoa wetu wa Shinyanga una kilomita 600 ambazo ni changarawe, ambazo mvua ikinyesha barabara hizi zinakuwa hazifai. Kwa hii bilioni haiwezi kutosheleza. Kwa hiyo nimwombe Waziri wa fedha hii asilimia 10 aiche kama ilivyo, kwa mfano tu kwa Mkoa wetu haina tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuongelea suala zima la kuhusu Waziri Mkuu. Mwaka jana niliuliza swali hapa, ile Mifuko 18 iweze kuchanganywa ili iweze kuleta tija kwa watu ambao wako Mikoani. Kuna halmashauri nyingine makusanyo yao ni madogo, nichukulie tu mfano katika Mkoa wangu, Halmashauri ya Shinyanga Vijijini, Kishapu makusanyo yao ni madogo sana. Kwa hiyo tungeomba ile Mifuko, 18 huu ni mwaka wa pili tunaelekeza najua Mheshimiwa Waziri Mkuu ni msikivu. Mheshimiwa Katambi mwenyewe hapa alikiri mwaka jana kwenye bajeti, anaenda kuichanganya, lakini naona mchakato umekuwa ni mrefu. Kwa mwaka huu pesa hizi zichanganywe na hii mifuko 18 mingi ime-base mijini. Tungeomba Mifuko hii sasa hivi ikishamaliza kuchanganywa ikawa Mfuko mmoja, mikoa, halmashauri zetu zigawanyiwe pesa hizi. Ukiangalia uhitaji wa pesa hizi ni mkubwa sana kwa watu ambao wapo Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameelezea hapa wanawake ni walipaji wakubwa wa mikopo na wameonyesha jinsi gani ni waaminifu katika mikopo hii. Nimwombe Waziri wa Fedha atupandishie hizi asilimia, wanawake wapate kutoka asilimia nne twende kwenye asilimia sita. Nahisi italeta tija kwa sababu tunahitaji kujikomboa kiuchumi na nina uhakika kwamba hizi pesa tukipewa itawasaidia wananchi wengi sana kufanya biashara ndogondogo ambazo tutaongeza pato la Taifa na wananchi watajikomboa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)