Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya Serikali. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri ambayo inaakisi dira, malengo, dhamira na nia njema ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama muda utaruhusu vizuri nina mchango kwenye maeneo mawili, eneo la kwanza ni kilimo na eneo la pili ni maliasili na utalii. Kwenye eneo la kilimo ninayo mambo mawili, jambo la kwanza Mheshimiwa Waziri mwaka jana tulizungumza sana hapa kuhusu crop cess na ukakubali ukaenda uka-withdraw kwenye Finance Bill. Mwaka huu wataalam wako wameiweka kwa lugha nyingine lakini jambo ni lile lile tutakutana huko kwenye Finance Bill. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili mwaka 2005 Serikali yetu kupitia Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 31 wa mwaka 2005 iliita Kampuni ya Katani Limited kuendesha mashine za kuchakata mkonge kwenye mashamba matano yaliyoko Korogwe. Shamba la Mwelya, Shamba la Magoma, Shamba la Magunga, Shamba la Hale na Shamba la Ngombezi, lakini kwenye waraka ule kulikuwa na masharti kwamba kampuni hii kwenye kila shamba iwe na hisa asilimia 60 na wakulima wadogo wadogo wapewe hisa asilimia 40. Jambo hili halikufanyika kwa miaka yote na kampuni hii ilikuwa ikijiendesha kwa kukopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2003 ilikopa Dola Milioni Tatu kutoka NSSF, mwaka 2005 ilipopewa viwanda hivi ilikopa Dola Milioni 3.7 kutoka NSSF, mwaka 2006 walipoona uwezekano wa kulipa madeni ni mgumu NSSF akaingia akapewa hisa kwenye Katani Limited akawa mbia akapewa hisa asilimia 49. Maana yake ni kwamba NSSF na Katani Limited wanamiliki kwa pamoja Kampuni hii ya Katani Limited. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichokuja kutokea ni nini? mwaka 2012 wakachukua mkopo mwingine tena na fedha zote hizi hazikwenda kufanya kazi iliyotakiwa. Baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali yetu kupitia Waziri Mkuu, maelekezo ya Rais mwaka juzi na mwaka jana tumeona Katani Limited ikinyang’anywa mashamba na ikinyang’anywa viwanda, lakini baada ya kunyang’anywa wamerudi NSSF kinyumenyume ambaye ni sehemu ya Katani Limited wamekuja kupewa viwanda vya kuchakata mkonge, wameanzisha Kampuni tanzu inaitwa Sisalana inachakata mkonge wa wakulima. Matokeo yake ni kwamba Sisalana inachofanya sasa imejikita kuona ni namna gani ina-recover gharama ambazo NSSF aliingia kumpa Katani Limited. (Makofi)

Mheshimiiwa Mwenyekiti, huu ni wizi wa mchana kweupe, kwanza hisa za wananchi wetu wakulima wadogo wadogo hazikuwahi kupatikana, wananchi wetu wakulima wadogo wadogo hawakuwahi kufaidika, lakini mwisho wa siku tena anakuja huyu huyu ambaye ni sehemu ya huu wizi wa kuzuia hizi hisa za wakulima wetu, anakuja kutoa makorona yale, anajikita kukusanya madeni. Kasi ya kuchakata mkonge wakulima wetu imekuwa ni ndogo, badala ya kuchakata mita 100 kwa sita utachakata mita 30, mkonge wa wakulima unaozea shambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tutashusha kiwango cha uzalishaji wa mkonge tutawaumiza wakulima wetu, tunaiomba Serikali na wakulima hawa kupitia taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor General) wanaidai hiyo Kampuni ya Katani karibu Bilioni 29. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama NSSF wanapewa mashine ku-recover madeni yake wakulima wetu wanapewa nini? Nani analipa madeni ya wakulima wetu? Ninakuomba Waziri wa Fedha kupitia kwa Msajili wa Hazina tunaomba hisa za wakulima wetu zipatikane, kama haiwezekani hii mitambo ya kuchakata mkonge tuliyonayo sasa, wapewe wakulima wadogo kupitia AMCOS zao ili wachakate wenyewe wachakate kwa kasi mkonge wao usiharibike. Tuthaminishe hizi mashine wapewe waendeshe kwa muda maalum wakimaliza wakirudisha gharama, zile mashine zibaki kuwa mali ya wakulima wadogo wadogo kwenye AMCOS zao. Kuna hatari kubwa ya kutenganisha mashamba ya mkonge na mashine za uchakataji kwa kuwa mchakataji hana uchungu wala maumivu na mkonge wa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba niseme kwenye upande wa maliasili na utalii. Utalii una faida kubwa sana kwa nchi yetu, zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni tunapata kutoka kwenye utalii. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 67(a) inayotuelekeza kuongeza idadi ya watalii mpaka kufikia watalii Milioni Tano ifikapo mwaka 2025. Kazi aliyoifanya kwenye Royal Tour inakwenda kutupa matokeo hayo na kwenda kutekeleza Ilani hii ya Uchaguzi kwa vitendo. Pamoja na hilo yako mambo mawili nilikuwa nataka na mimi nichangie kama sehemu ya Watanzania wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mambo yanaendelea kule Ngorongoro na watu wanachanganya, Ngorongoro kuna mambo mawili tofauti, kuna jambo la Ngorongoro, Tarafa ya Ngorongoro kuna jambo la Loliondo na nimeshuhudia jana nilikuwa nasikia mjadala mahali Serikali inalaumiwa sana, wamekwenda mbali wanaanza kulaumu mpaka na Bunge letu kwa kutetea na kuiunga mkono Serikali kwenye jambo la Ngorongoro. Wapo waliomshambulia binafsi Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hili niseme tu hasa kwa wenzetu wanaharakati, tatizo la wanaharakati wetu ni kutokuwa na kumbukumbu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mambo ambayo wanaharakati wanatumia kukosoa mfumo wa kuendesha nchi yetu hasa wanapokuwa wanazungumza Katiba mpya, ndiyo wanapozungumzia effectiveness ya utendaji kazi wa Bunge letu hili. Jambo linalofanyika Ngorongoro kwa upande wa Ngorongoro peke yake ni utekelezaji wa maelekezo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na siyo Bunge hili ni kuanzia Bunge la Kumi kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, kwenye Bunge la Kumi na Moja Serikali ya Awamu ya Tano na Bunge hili tunaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kusoma taarifa za Bunge ukisoma taarifa ya utendaji kazi za Kamati kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013 Kamati ya Kudumu ya Bunge iliishauri Serikali kwenye ukurasa wa 45, kuchukua hatua mahsusi kuipitia na kuitafakari sheria iliyoanzisha na kuendesha Mamlaka ya Ngorongoro ili kuona namna ya kuinusuru hifadhi ile. Hatukuishia hapo ukienda kusoma taarifa ya Kamati ya Bunge, taarifa iliyotolewa kwa shughuli za Kamati kwa kipindi cha Januari, 2017 mpaka Januari, 2018, Bunge hili linasema Kamati inashauri kwamba pamoja na changamoto nyingine zote hatua ya kwanza ya kuinusuru Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni kuhuisha sheria ya kuanzishwa kwake ili iendane na hali halisi ya sasa. Aidha, Serikali ifanye tafiti ya kina wa tathmini ya mfumo wa matumizi mseto ya ardhi katika hifadhi na kutoa mapendekezo yenye tija. Kamati inaishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia wafugaji mashamba na maeneo mengine nje ya hifadhi ili kupunguza mzigo mkubwa uliopo kwa mamlaka. Haya ni maelekezo ya Bunge, ninazo taarifa nyingine za Kamati zaidi ya tatu wakati wa kupitisha bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba tu wanaharakati, ninawaomba wenzetu watuachie tujenge nchi, Ngorongoro ni ya kwetu wote kila mmoja anaihitaji, faida zake zinajulikana, watuache tufanye kazi ya kujenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kwa Wizara ya Maliasili nimesema kwa eneo la Ngorongoro pia kuna Loliondo, hapa napo kumekuwa na maneno mengi na mengine ya upotoshaji. Eneo la Loliondo wasiolijua liko Kaskazini mwa Hifadhi ya Ngorongoro, lakini eneo hili liko Mashariki mwa Hifadhi ya Serengeti na mpaka wa Kaskazini wake ni mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili lina square meter 4,000 limetajwa kwenye tafiti mbalimbali kwamba ni critical part of the Serengeti ecosystem ni eneo muhimu sana. Ni eneo muhimu sana kwa nyumbu na pundamilia wanapofanya migration, ni eneo muhimu sana kwa mazalia, ni eneo muhimu sana kwa maji, ni eneo muhimu sana kwa uoto na ecosystem ya Serengeti kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika sasa kule kwenye lile eneo letu la Loliondo siyo jambo jipya halikujulikana leo, mimi nimeenda kusoma ninayo hapa mkononi mwangu taarifa wakati mwaka 1994 Serikali ikifikiria kufanya matumizi mazuri ya eneo la Loliondo, walienda wakaandika taarifa wataalam naomba nisome ninukuu kwa kifupi tu: “for solidarize Loliondo has been seen by the Masai and their heads of livestock hand in hand with the wildlife, other tribe such as Wasonjo wanaitumia hilo eneo, lakini mwisho wanasema hivi wanaizungumzia encroachments sasa: “these encroachments have forced the wildlife to occupy small area to the detriment, the excessive use of the land has further laid to the destruction of the natural habits that is in detail and desirable forces such as soil erosion, vegetation cleared na cut-off ya wanyama wengine”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu mwaka 1994 Tanzania Wildlife Conservation Monitoring ilifanya utafiti kwa kushirikiana na Serengeti Wildlife Research Institute, kwa kushirikiana na Wildlife Division, kwa kushirikiana na Tanzania National Parks, kwa kushirikiana na Frankfurt Zoological Society, taarifa ninayo. Moja ya madhara iliyoonekana yanasababishwa na muingiliano mkubwa wa watu kukaribia eneo lile ni kusababisha kupungua kwa nyumbu kwenye eneo lile. Eneo hili ni muhimu usipotunza zile square meter 1,500 maana yake uta-destruct Serengeti Ecosystem na pale ndipo kwenye kiini chake. Uki-destruct hiyo maana yake Serengeti National Park iko kwenye shida, Ngorongoro National Park iko kwenye shida na wenzetu jirani ile hifadhi yao nao iko kwenye shida ni eneo muhimu sana kwa utalii na ni eneo muhimu sana kwa uhifadhi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali ya Rais Mama Samia tunashukuru na kupongeza utashi wa kisiasa uliokuja nao kwenye kutekeleza jambo hili, tusirudi nyuma hapa tulipo. Najua yako maumivu na uzuri eneo la Loliondo hakuna anayeishi, ni eneo ambalo hata wenzetu huwa wanalitumia kwa kuchunga na kunywesha hasa wakati wa kiangazi, lakini hili eneo tunalihitaji zaidi kwa manufaa ya nchi hii. Tusirudi nyuma kwenye kutekeleza jambo hili. Nasema twende mbele tulitekeleze kwa faida na manufaa ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho niwaombe wenzetu wa maliasili…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kutoa taarifa kwa rafiki yangu mpendwa na Youth League wa Chama chetu, Mbunge, kumpa taarifa kwamba katika eneo hilo analolizungumza la kilometa za mraba 1,500 ni eneo linalogusa Kata Nane za Tarafa ya Loliondo na Tarafa ya Sale. Kuna vijiji vilivyoandikishwa hiyo ni village land, ni ardhi ya vijiji ambayo sheria tuliyonayo inakataa kabisa kuchukua ardhi ya vijiji na kujumuisha katika eneo la pori tengefu, huo ndio msimamo wa sheria ilivyo na kuna vijiji vilivyosajiliwa katika mpaka wa Serengeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu nimpe taarifa ndugu yangu ili ajue kwamba pale kuna watu na kuna shughuli za binadamu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Timotheo unaipokea taarifa?

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwanasheria, ninasema ninachokijua, siipokei taarifa yake na nimhakikishie bahati nzuri pia mimi ni Mjumbe wa Kamati yako ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, vikao vyote alivyofanya Waziri Mkuu mimi na Mwenyekiti wangu kwa niaba ya Kamati tulishiriki, nazungumza ninachokijua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo linalosemwa hapa ni eneo ambalo ni sehemu ya eneo la pori tengefu la Loliondo, kuwa karibu na vijiji, kupakana na vijiji hakuondoi hakujawahi kushusha hiyo hadhi na sheria anayoisema ilipobadilishwa ilipitiwa na pori liliendelea kuwa pori na tunalo pori tengefu la Loliondo. Taarifa yake siipokei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ili tuendelee kufurahia utalii huu tuwaombe Wizara ya Fedha, wapeni fedha ya kutosha watu wa maliasili na utalii watuletee mikakati mizuri ya kukabiliana na wanyama waharibifu kwenye maeneo yetu. Tusipofanya hivyo tutatengeneza jamii yenye njaa, tutatengeneza Taifa lenye njaa kwa kuwa mazao yanaharibiwa na wanyama, watu wetu wanapoteza maisha baadhi ya maeneo kwa sababu ya wanyama. Tunahitaji mkakati wa namna gani tupambane na kuzuia wanyama hawa lakini pia kwa yale maeneo ambayo tayari yameathirika tunaomba muda mrefu tumesema kile kifuta jasho ni fedha ndogo sana, haiwezekani mtu akapata ulemavu wa kudumu akapewa Shilingi 500,000, mtu kapoteza maisha anapewa shilingi 1,000,000; lakini mashamba yanaharibika heka moja mtu anapewa shilingi 100,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza Taifa lenye njaa, Taifa lenye njaa halitawaliki, Taifa lenye njaa halina amani, Taifa lenye njaa watu wake hawana furaha. Tunaomba tuongeze kifuta machozi, lakini pia madhara yakitokea tusichukue muda mrefu kufika kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni Wizara ya Maliasili na Utalii kwa muda mrefu Bunge hili limewashauri kuleta Bungeni Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA). TAWA tuliyonayo sasa imeanzishwa kwa amri ya Serikali (Establishment Order) ambayo imetokana na kifungu cha Nane cha Wildlife Conservation Act. Kwa sheria ile na utaratibu huo uanzishwaji wake TAWA haina Bodi ya kufanya maamuzi, TAWA ina Bodi ya ushauri, yako mambo ambayo yanashindwa kwenda vizuri kwa sababu haina mamlaka makubwa ya kufanyakazi mpaka kila kitu iende ikazungumze na Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema la mwisho lakini nilisahau jambo moja, mlimpa Mheshimiwa Rais wakati mgumu sana kwenye sherehe za Mei Mosi mmeanzisha Jeshi USU, tuleteeni hapa sheria, wakati tunaanzisha Jeshi USU inawezekana tulijisahau hatukufanya consequential amendments kwenye Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ili kama wale ni Wanajeshi tuwajumuishe kuwa wanajeshi waende kijeshi, wasiwepo kwenye vyama vya wafanyakazi wawe na utaratibu tofauti wa mafao, lakini kwa sasa sheria haisemi kitu. Kwa kuwa tumeanzisha Jeshi USU kwa sheria, leteni mabadiliko ya sheria turekebishe kifungu kwenye Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, tuwajumuishe Jeshi USU kwenye ajira ambazo hazilazimiki kuunda vyama vya wafanyakazi na hazilazimiki kufuata utaratibu ule wa kawaida wa mafao ambao tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)