Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge lako hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nichukue fursa hii adhimu kabisa kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Mkuranga katika Mkoa wa Pwani, naomba niwahakikishie ya kwamba kazi yao walionituma ya kuwawakilisha nitaifanya kwa weledi, uaminifu, juhudi na maarifa yangu yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizi, nami kwa kuwa sikupata fursa ya kujadili hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa hapa katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nichukue fursa hii pia kusema kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais ilimaliza kazi yote, nami binafsi baada ya pale nilifanya ziara katika Jimbo langu la Mkuranga kwa ajili ya kutoa shukrani na Wanamkuranga wana imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Wanasema Mheshimiwa Rais aendelee na kazi yake na imani yetu ya kuiona Tanzania ikielekea katika uchumi wa kati ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niendelee katika hoja hii inayohusu Mpango wa Maendeleo ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa Bungeni. Kwanza kabisa ningeenda kugusa katika eneo la viwanda. Mkakati wa Serikali yetu ni mzuri, na mimi binafsi nauunga mkono kwa asilimia 100. Hata hivyo, yapo mambo ambayo ningefikiri kwamba hatuna budi kujielekeza kuona ni namna gani tunajipanga nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la viwanda, pale Mkuranga, neema ya viwanda imeshaanza kuonekana. Tunavyo viwanda vingi sana sasa ambavyo vinajengwa kila kukicha. Sababu yake kubwa ni pamoja na kwamba Dar es Salaam imeshajaa na sasa inapumulia katika Wilaya ya Mkuranga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwetu imekuwa ni faraja kubwa sana na tungeomba jambo hili liendelee na hata Serikali iendelee kutusaidia kuhamasisha kuhakikisha kwamba wawekezaji wa viwanda mbalimbali wanaendelea kumiminika pale katika Jimbo letu hili la Mkuranga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango mkakati wa maendeleo uliopita, wakati tunaujadili utekelezaji wake, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alisema neno, kwamba katika mambo yaliyotufanya tushindwe katika uwekezaji wa viwanda hapo nyuma ni pamoja na fidia za ardhi. Fidia ya ardhi ipo kwa mujibu wa Sheria namba 4 ya mwaka 1999, lakini ninalo jambo ambalo nilikuwa nikilifikiri sana na nilikuwa nafikiri kwamba wataalam walichukue wakalijadili, waone ni namna gani tunaweza tukaboresha kitu cha namna hii. Hizi fidia za ardhi zimekuwa zikifanywa kila mara, lakini kama fidia ya ardhi inayohusu biashara, hasa ya viwanda na sisi tunataka uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati umilikiwe na Watanzania wenyewe, nafikiri tuanze kubadilisha mtazamo wetu. (Makofi)
Watanzania wamekuwa wakipewa fidia, si jambo baya, ni haki ya kisheria, lakini wakishapewa ile fidia, wanaelekea wapi. Tumeona watu wakipewa fidia Dar es Salaam, kule Kibada, Kigamboni watu wanalipwa fidia vizuri sana tu wanakwenda na sisi pale Mkuranga tutalipwa fidia, lakini baada ya hapo tunasogezwa, tunaondoka. Sasa tutasogea mpaka tutafika Rufiji, tukitoka Rufiji tutakwenda mahali pegine, ardhi ile tumepoteza na uchumi ule hatutaendelea kuumiliki. (Makofi)
Wazo langu nililokuwa nafikiri ni kwamba, ni lazima itafutwe mbinu nzuri zaidi ya kuwafanya Watanzania hawa wawe ni sehemu ya umiliki wa vile viwanda, wao mchango wao uwe ni ile ardhi yao. Tuliweke jambo hili vizuri badala ya kuja kuwapa fidia ya 1,500,000. Anaondoka Mtanzania yule wa pale Mkuranga, ameacha kiwanda kimetengenezwa pale, ile haitamsaidia. Kama ungetengenezwa mpango madhubuti na mzuri, maana yake ni kwamba eneo lake linakuwa ni mchango katika kiwanda kile atakula yeye, watoto wake, wajukuu wake na mpaka vitukuu vyake! Nadhani hii itakuwa ni namna bora zaidi ya kuwafanya Watanzania wamiliki uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo la viwanda, nimewahi kuzungumza kwamba pale sisi tunavyo viwanda vingi lakini viwanda hivi lipo tatizo la ajira, ajira zile zinazotolewa tunasema kwamba sio decent. Hazina staha! Vijana wetu wako wengi kweli wanapata vibarua mule ndani, ajira zile ndani ya saa kumi na mbili hawapumziki hata kidogo. Baada ya hapo analipwa 4,500, lakini ni ajira hatarishi kwelikweli. Naomba jambo hili wakati tunaendelea kuomba hivi viwanda tuliangalie vizuri ili tujiandae nalo lisije likatuletea matatizo hapo mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wa maji ambao umesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kwamba maji ni uhai na Mbunge mwenzangu wa Rufiji amesema vizuri sana hapa mchana huu wa leo juu ya suala la maji. Kutoka Rufiji, Mto Rufiji mpaka Mkuranga, hazizidi kilometa 100. Maji kule yamekuwa ni mengi mno yanaleta hata mafuriko! Tusaidieni tuondokane na tatizo la maji na liwe ni historia. Yatoeni maji kutoka Mto Rufiji, yafike Mkuranga, yapite Kibiti, Ikwiriri, Bungu na maeneo mengine ya Wilaya zetu hizi. Mkifanya hivi mtakuwa mmetusaidia sana. (Makofi)
Vilevile upo mkakati wa maji mkubwa pale katika Kijiji cha Kisemvule, ningeomba maji ya pale Mpera yasiondoke kwenda Dar es Salaam mpaka kwanza na sisi watu wa Mkuranga tuwe na faida nayo maji yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaendelea kuangalia namna ya kuboresha uchumi wetu, naomba nizungumzie miundombinu. Wilaya ya Mkuranga kama tulivyosema, Jimbo letu hili lipo kabisa kimkakati kwamba ni sehemu ya kupumulia katika Jiji la Dar es Salaam. Ombi langu hapa ni kuhakikisha kwamba pesa katika Mfuko wa Barabara ziongezeke. Ziongezeke ili tuweze kutengeneza miundombinu yetu. Sisi pale tuna uchumi mzuri, lakini uchumi ule umekwama kwa sababu miundombinu ya barabara katika Jimbo hilo ni mibaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenzangu wa Rufiji alisema kwamba Rufiji katika umri wake wote toka iwe Wilaya hata nusu kilometa ya lami hakuna, sisi hata robo kilometa ya lami haipo katika Wilaya yetu ya Mkuranga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja hii ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja. Ahsante sana. (Makofi)