Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuanza mchango wangu wa jioni hii ya leo. Kwanza nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyofanya kazi vizuri ya kutuletea maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara na Naibu Waheshimiwa Mawaziri na Watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Kipekee naomba nichukue nafasi hii kukupongeza sana kwa kuendelea kuaminiwa, umetoka kwenye Uwenyekiti wa Kamati na sasa umekuwa Mwenyekiti wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nimepata nafasi hii ya kwanza kuchangia, nichukue nafasi hii kukupongeza sana, tuna imani na wewe, chapa kazi, najua unaweza. Kipekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Katika miaka mitatu ya uongozi wake tumeona kazi kubwa aliyoifanya, alisema kazi iendelee na kweli tumeona kazi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ujenzi wa reli ya kati ya kilometa 1,219, Serikali ikiwa imetoa shilingi trilioni 10.6 tunaona kazi inaendelea. Mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, kazi inaendelea, tumeona tayari Megawatt 2,115 zinazalishwa na tayari utekelezaji umefikia 96.8% katika mitambo tisa, mmoja tayari umewashwa na tayari Megawatt 235 zimeingia kwenye gridi ya Taifa na tunaona tatizo la umeme tayari limepunguzwa, kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania kazi kubwa imefanyika, Mheshimiwa Rais tayari amelipa kiasi cha shilingi bilioni 753, ndege tatu zilizoagizwa, tayari mbili zimefika, moja itafika mwezi huu. Sasa tunakuwa na ndege 16 katika Shirika letu la Ndege la Tanzania. Kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Mheshimiwa Rais ameendelea kufanya kazi kubwa, mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima - Uganda mpaka Chongoleani – Tanga kilometa 1,443, Serikali katika ushirika wake tayari imechangia katika mradi huo kiasi cha dola 268.7. Kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kazi inaendelea kufanyika Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi, kimekamilika kwa 99%. Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 320.5, tayari kiwanda kimeanza kuzalisha na mpaka sasa kimezalisha tani 1,851, kinaenda kupunguza uhaba wa sukari nchini. Siyo hivyo tu, imeongeza ajira 1,996, kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizofanyika ni nyingi sana, hata nikisema hapa nitandelea kusema kwa muda mrefu, lakini nashukuru hata wenzangu wamechangia na kusema ni namna gani Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende moja kwa moja kwenye jimbo langu la Mkoa wa Kilimanjaro. Katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro shughuli za kiuchumi zinazofanyika ni pamoja na kilimo, biashara na utalii. Tunamshukuru sana Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya kilimo. Leo nitaenda kuzungumza zaidi kwenye kilimo kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wanalima ndizi, kahawa na parachichi, lakini wana changamoto zinazowakabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa iliyofanywa, na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti na kuwapatia Maafisa Ugani pikipiki, bado kuna changamoto zinazowakabili wananchi wetu, hasa wakulima wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro. Katika changamoto hizo, ya kwanza ninayoweza kwenda kuisemea siku ya leo ni changamoto ya mbegu bora au miche bora. Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa wakulima wetu. Kwa kuwa hawapati mbegu bora au hiyo miche bora, wanaenda kufanya kilimo ambacho kinakuwa hakina mazao yanayokidhi vigezo, wanakosa thamani kubwa au faida kutokana na kile wanacholima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninashauri, kwa kazi kubwa iliyofanyika, Maafisa Ugani waweze kuwatembelea wakulima wetu, waweze kufanya utafiti, waweze kujua afya ya udongo na kuwashauri akinamama na wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao wanafanya kilimo ili waweze kulima kilimo cha kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kuishauri Serikali ambayo ni changamoto kwa wakulima wetu wa Kilimanjaro ni utegemezi wa mvua za msimu. Mpaka leo sisi tunategemea mvua za msimu. Ina maana kama mvua za msimu hazipo, watu wanakuwa hawapati mavuno yale ambayo walikuwa wanategemea, wanayostahili. Nilikuwa nashauri, Serikali sasa ifuatilie kwenye suala la kilimo cha umwagiliaji, waweke mabwawa ya kutosha. Mvua zinanyesha na kuleta athari kwa wananchi na wakati mingine mpaka mafuriko. Kwa nini basi Serikali isione namna ya kutumia maji haya kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji na wananchi wetu wakaweza kupata faida ya kutosha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni elimu kwa wananchi, hawa wakulima ya namna ya kuongeza thamani ya ubora wa mazao yao. Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa wakulima wetu kwa sababu, unakuta katika mazao wanayolima hasa zao la kahawa, wakulima wale wanauza kahawa ghafi na wanaenda kuuzia nchi ambazo hazina hata mti mmoja wa kahawa katika nchi yao. Nao wanachofanya ni kwenda kuongeza thamani kidogo tu, lakini wanapata faida mara tatu mpaka mara tano ya faida anayopata mkulima ambaye anateseka tangu anapoanza kupanda mti huu mpaka anapovuna. Kwa hiyo, Serikali iweke jicho lake kwenye sehemu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kusema jambo lingine ambalo linawakwamisha wananchi au wakulima wa Kilimanjaro ambalo ni soko la ndani na nje. Bado tumekuwa na shida kubwa sana ya kupata masoko kwa ajili ya bidhaa zetu. Kama ndizi zetu akina mama wa Kilimanjaro tunataka kuona zinaenda nje ya nchi, zisiishie kupelekwa Mabibo, zisiishie kutengeneza mtori, ziweze kwenda mbali zaidi ili kuwaletea wananchi wetu mafanikio makubwa. Tumeona Mheshimiwa Mama Samia Suluhu ameleta ndege za mizigo, ndege hizo basi zikatumike kwenda kuchukua mazao yetu kutoka Kilimanjaro na kupeleka nje ya nchi na sisi tuweze kujipatia faida na fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linawakwamisha wakulima wetu ni kutokana na kutokuwa na takwimu sahihi za idadi ya wakulima. Leo ukitaka kuwahudumia watu ni lazima ujue idadi yao. Kama ambavyo nchi inataka kuwahudumia wananchi hawa inafanya sensa, lakini leo hawajui wakulima wapo kiasi gani? Wakulima hawa wanalima kwa kiasi gani? Wakulima hawa wana mashamba kiasi gani? Je, kama tunahitaji mbolea, pembejeo na miche, wanawezaje kujua kama hawajui idadi ya hawa wakulima? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali iangalie ni namna gani itapata takwimu sahihi za wakulima wa kahawa, wakulima wa ndizi, wakulima wa parachichi, wakulima wa maua ili kuweza kuwapa stahiki zao pale wanapokuwa wanahitaji pembejeo na mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie na suala la 4:4:2,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kidogo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa hitimisha kidogo muda wako umeisha, tafadhali.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wa Kilimanjaro wanataka kusikia Serikali inasema nini juu ya fedha inayotoka halmashauri ile ya 10%, kwani wamekaa wakisubiri kwa muda mrefu. Tunajua Serikali inafanya mikakati na mipango ya kuweza kuboresha, lakini basi waweze kupewa taarifa ni lini fedha hiyo inatoka na Serikali itoe tamko ili akina mama wa Kilimanjaro nao waweze kufaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)