Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu iliyopo mbele yetu. Kwanza nitumie nafasi hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Tunaamini uzoefu wako kwenye mambo ya sheria na uzoefu wako wa kibinadamu wa mahusiano yako na Wabunge wenzako utakuwa ni chachu ya kuweza kumsaidia Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wenzako katika kuongoza shughuli za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama na wasaidizi wake, vilevile Mheshimiwa Ndejembi na msaidizi wake kwa kazi kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Sisi Wabunge wote ni mashuhuda, Waziri Mkuu kupitia Ofisi yake na ninyi wasaidizi wake, mmekuwa ni wasaidizi wazuri kwa Mheshimiwa Rais kwa kutimiza majukumu yenu ambayo ni dhamira ya Mheshimiwa Rais kutupeleka Watanzania katika maisha safi, maisha yenye hadhi na ubora katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa Watanzania. Sisi Wabunge wote ni mashuhuda, kila Mbunge anayesimama anampongeza Mheshimiwa Rais. Wako watu wanaona wivu, ni kwa nini tunampongeza? Kwa uhalisia sisi tulioko ndani ndio tunajua ni yapi Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya kwa Watanzania katika majimbo yetu na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la elimu, kule jimboni kwangu mambo ni mazuri. Tuna shule ya vipaji maalum imejengwa kwa thamani ya karibu shilingi 3,700,000,000 madarasa yamekuwa mengi kwenye shule ya msingi na shule ya sekondari. Kwenye masuala ya umeme, vijiji vyote vimepata umeme na sasa hivi tunaelekea kwenye vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye barabara, kazi imeendelea kufanyika. Juzi, tarehe 5 mwezi wa pili, barabara ya Bigwa – Kisaki yenye urefu wa kilometa 78 imetiwa saini kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 134. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo kwa Mheshimiwa Rais, nitumie nafasi hii kuishauri Serikali yangu. Kuna suala hapa la utalii, yaani ongezeko la watalii, na kubwa zaidi ni kutokana na jitihada za dhati za Mheshimiwa Rais kupitia Royal Tour. Mwaka 2022 tumeona watalii walikuwa ni 1,459,920 lakini mwaka 2023 watalii wameongezeka mpaka kufikia 1,808,205 ni ongezeko almost la asilimia nane. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini vilevile ukiangalia mapato ya utalii mwaka 2022 yalikuwa ni dola bilioni 2.53, lakini mwaka 2023 yamekuwa ni dola bilioni 3.37. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tumeambiwa kwamba pamoja na jitihada hizi zote za dhati zinazofanywa na Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, bado kupitia filamu ya Jing Dong tunatarajia kupata watalii wengi kutoka China. Sasa ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, ukijaribu kuangalia mapato haya ya utalii yanatoka Ukanda wa Kaskazini, lakini bado kuna Ukanda wa Kusini na maeneo mengine ya nchi yetu ambayo yana vivutio vikubwa vya utalii. Mfano, Morogoro tuna Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, Mikumi na Udizungwa, ukienda Iringa kuna Ruaha, ukienda Katavi kuna Hifadhi ya Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa fupi kwamba kupitia Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, mwaka 2022/2023 kulikuwa na wageni karibu 34,189 wa kutoka nje ambao walifika kufanya utalii kwenye hifadhi yetu, lakini wageni wa kazi walikuwa ni karibu 19,800 na wageni wazawa walikuwa 900 na almost watalii 54,000 walifika kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere ambapo mapato ya shilingi bilioni 11 yalipatikana. Ukijaribu kuangalia ongezeko la watalii, halafu ukiangalia sehemu moja ya Kusini utaona kwamba, bado Wizara ya Maliasili ina wajibu wa kuendelea kutangaza utalii wa Nyanda za Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nitoe pongezi kupitia Mradi wa E-Grow, ambao ni uboreshaji wa utalii upande wa Kusini. Tumeona kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere kuna ujenzi wa uwanja wa ndege. Ninakumbuka katika bajeti iliyopita nilipiga kelele kwenye hili, ujenzi wa uwanja wa ndege, lakini kupitia Mradi wa E-Grow safari hii uwanja wa ndege umejengwa kwenye lango la kutokea Matemere. Vilevile, kuna ujenzi wa campsite yenye uwezo wa watu 100, rest house yenye uwezo wa kulaza wageni 20, vilevile kuna ujenzi wa kambi za askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwako kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, bado kuna changamoto kwenye lango la kupitia Matambwe – Kisaki ambayo ni Morogoro DC. Tunaomba Uwanja wa Ndege wa Matambwe uboreshwe ili kuruhusu watalii wengi waje na kuweza kutuletea fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna ujenzi wa madarasa. Katika kuunganisha hifadhi, bado kuna hiyo changamoto kwa hiyo, naomba kupitia Wizara ya Maliasili na Ofisi ya Waziri Mkuu, tuangalie ni jinsi gani tunaweza tukafanya jambo hili likamilike na ndiyo maana nimetangulia kusema tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kujua umuhimu wa utalii kwenye Nyanda za Kusini, na hasa Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, ameweza kuidhinisha kujengwa kwa kiwango cha lami kilometa 78. Hiki ni kichocheo cha kutaka tupate watalii wengi na tupate fedha nyingi za kigeni ili tuweze kuendeleza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie suala la kilimo; mwaka 2023 nilizungumza na mwaka huu ninaomba nizungumze tena, watu wa Morogoro Mungu ametupa bahati, kuna zao la karafuu. Zao la karafuu kwa Zanzibar ndiyo limekuwa zao kuu la biashara, lakini Mungu ni mwema, sisi watu wa Morogoro vilevile tumepata bahati ya kuwa na zao la karafuu ambalo ninaamini mpaka tulipofika ni jitihada za uongozi wa Halmashauri ya Morogoro Vijijini na uongozi wa Mkoa na mwaka 2023 tuliweza kuvuna tani 2,200 ambazo ziliwapatia wananchi wa Morogoro zaidi ya shilingi bilioni 39.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, kupitia zao hili kama Taifa upande wa Tanzania Bara, na lenyewe linaweza likaleta fedha nyingi za kigeni ambazo zitaingia kwenye shughuli za kuleta maendeleo kwa Taifa letu. Naiomba Wizara isimame, iungane na viongozi wa Mkoa ili ikiwezakana zao la karafuu nalo litangazwe kwamba ni zao la kimkakati katika kuleta mapato kwa wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nichangie ni suala la kodi. Mimi ni mfanyabiashara na ninaamini watu wengi wanaamini wafanyabiashara ni wezi au wanatamani sana kupata fedha ambayo siyo stahiki. Naipongeza Serikali yangu katika mwelekeo ambao imekujanao katika mwaka huu kuondoa kodi ambazo zimekuwa ni mzigo na zimekuwa ni sumbufu kwa wafanyabiashara kiasi cha kuwafanya washindwe kwenda mbele na kuweza kusaidia kuongeza pato kwenye Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa katikati ya Julai mpaka Januari mwaka huu kwenye mapato ya Serikali za Mitaa yamefikia shilingi bilioni 17, almost 95.9%, lakini kwenye TRA kuna asilimia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, hitimisha hoja yako, ahsante.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)